ADHABU YA ALLAH INAMSTAHILIA ALOMTUKANA MTUME (S.A.W) KAMA ZINAVYOMSTAHILIA MWENYE KUUWA WASIOKUWA NA HATIA
Kila sifa njema zinamstahikia Allah (S.W.) Muumba Mbingu na Ardhi Mfalme wa wafalme asiyeshindwa na kitu; sala na salamu zimuendee kipenzi cha Umma, Mtume Muhammad (s.a.w). Aliyeletwa kuwa ni Rehma kwa walimwengu wote na aliyekuwa kasifiwa na Mola wetu kuwa ameshikamana na sifa nzuri na vitendo vizuri kabisa.Kwa utukufu alopewa Mtume (s.a.w) ni muujiza wa kutosha kwa mwenye kuzingatia kiasi ambacho hauathiriki utukufu wake kwa maneno ya wajinga bali hudhalilika msemaji na kuzidi kutukuka mtukufu wa daraja Mtume (s.a.w) na kwanini asitukuke wakati ametukuzwa na yeye Allah (S.W.) utukufu usio kifani pale alipomwambia:
“..Kwa hakika wewe Muhammad una Tabiya ADHIYM..”
Ndugu wa Kiislaam,
Inasikitisha sana kuona kuwa kuna baadhi ya Waislaam ambao ni watu wepesi kiasi cha kuweza kuchokozwa na wajinga wasio na thamani wakajiingiza katika mitego na vitendo vyao vikawashirikisha pia Waislam wasiokubaliana na vitendo vyao viovu. Daima Mwislamu anatakiwa awe katika haki; asimuasi Mwenyezi Mungu ili kuepukana na ghadhabu zake Allah (S.W.).
Uislaam ni dini ilokamilika kwa kumdhaminia mwanaadamu ufumbuzi na miongozo ya mambo yote katika maisha yake ya Dunia na ndio maana Allah (S.W.) kakitukuza Kitabu chake kwa kusema:
“…hatujaacha kitu katika kitabu hichi…”
Tukizingatia tutaona kuwa watu waovu kuibuka kila baada ya muda na kumtukana Mtume (s.a.w) au kuutukana Uislaam si jambo geni ni ukafiri wa wazi na uadui ulioanza tokea siku ya mwanzo ya kupewa Utume na kuanza kuufikisha kwa watu wake yeye mwenyewe Mtume (s.a.w) na kwa bahati, aliyeanza hujuma na dharau hizo alikuwa mtu wa karibu wa damu kabisa na Mtume (s.a.w) na haikuwa kumkanusha tu bali alifikia hadi kumuombea maangamizo kwa maneno mashhuri aliposema Abuulahab:
“..maangamizo yakufike, hili ndio ulotukusanyia…!”
Mbali ya kupigwa mawe na mengine mengi tu, la umuhimu ni kujifunza kutoka kwake (s.a.w.) na vile vile maandiko ya Qur-aan.
Ni sahihi kabisa kuwa amelaanika na kuangamia yule mwenye kumtusi Mtume (s.a.w.) ndio tukaona hakusalimika jamaa yake Mtume (s.a.w) wa damu, bwana Abuulahab, Allah akashusha sura nzima ya maangamizo akaanza kwa kusema:
“Imeangamia mikono ya Abulahab na kuangamia na yeye mwenyewe…”
Lakini je! ni sahihi kuuwawa maquraysh wa makka kwa kosa lake? Jawabu: aya hazikushuka kuwalaani Makuraysh wote, si wa ndani hapo Makka, seuze waliokuweko nje seuze wale ambao wamo katika dhimma na hifadhi za Waislamu; ikiwa kosa la Abulahab hakuadhibiwa mwengine basi ni wazi kuwa hakuna uhalali wa Waislamu kwa kosa la watu kumkejeli Mtume (s.a.w) kuwahujumu wasiohusika na wasiokuwa na hatia.
Kuvamia Ubalozi wa Marekani hukoBenghazi nchini Libya ni kosa kwa pande nyingi tu kwani Allah (S.W.) anasema:
“…wala hatobeba mkosaji dhambi ya mwengine…”
Kosa la kumkejeli Mtume (s.a.w) haijawa halali kufanya ndio sababu ya kutenda vitendo vya uadui.
Allah (S.W.) ametufunza hayo ndani ya Qur-aani kwa kusema:
“… wala makosa ya watu ya kukuzuiyeni msiingie masjidi ‘lharami yasikufanyeni mkatenda uadui na kuchupa mipaka…”
Ubaya mkubwa zaidi ni kuhatarisha roho za watu ambao wako chini ya dhimma zetu kwani kila balozi na wafanya kazi wake huwa katika hifadhi ya nchi waliokuweko. Hivo leo tutafurahia kusikia balozi wa Libya nae anavamiwa na kuuwawa na familia yake nchi yoyote aliko?
TUNALAANI TUNALAANI NA KUKEMEA KWA NGUVU ZOTE KWA KEJELI DHIDI YA MTUME MUHAMMAD S.A.W. ILOFANYWA NA MAKUNDI YANAYOTAKA KUPANDIKIZA MBEGU ZA FITNA NA UCHOCHEZI WA VITA, PIA TUNAKEMEA KITENDO CHA KUULIWA BALOZI NA WATENDAJI WAKE WASIO NA HATIA, NA PAMOJA NA MATENDO YOTE YA UHARIBIFU YANAYOFANYWA DUNIANI KOTE KISHA KUNASIBISHWA NA UISLAMU AMBAO UKO MBALI NA DHULMA NA UADUI HUO.
Pia tunamuomba Allah (s.w) awaangamize na kuwadhalilisha wale wote walochangia kwa njia moja au nyengine kutengeneza Fitna hiyo.
Hakika Mtume (s.a.w) ni Rehma ilioletwa hapa ulimwenguni akishushiwa ndani ya Qur-ani:
“…na hatukukupeleka wewe Muhammad illa uwe ni rehma kwa walimwengu…”
Rehma hii ni mafunzo alotuachia Mtume (s.a.w) yatakayowavutia wasiokuwa Waislamu kutaka kuujuwa Uislamu wala hatutokuwa rehma kwa matendo maovu acha mauwaji. Tufuate sira yake Mtume ya kuwa na sifa nzuri na vitendo vizuri.
Tunamshukuru Mola kwa neema Zake na ulinzi Wake.
Sh. FARID HADI AHMED
MSEMAJI MKUU WA UMOJA WA JUMUIYA
NA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR 18/9/2012
No comments:
Post a Comment