TUNAAMBIWA kuwa hapa nyumbani na nje katika mfumo wa utawala bora wa haki na sheria dhamana kwa mshitakiwa ni haki, japokuwa mahakama ndiyo yenye uamuzi wa mwisho juu ya suala hili.
Nchi nyingi zenye utawala wa demokrasia zimeweka utaratibu unaojaribu kwa kiasi fulani kuhakikisha mahakama hazitumii vibaya mamlaka yake katika suala la dhamana.
Hii ni kwa sababu ipo dhana yenye nguvu inayosema kumuwekea mshitakiwa masharti magumu ya dhamana yanatoa tafsiri ya kuwa sawa na kumnyima dhamana au kuanza kumuadhibu mtu hata kabla hajatiwa hatiani.
Katika baadhi ya kesi zinazoendelea Zanzibar hivi, hasa zile zenye harufu ya kisiasa, kuchimba almasi au dhahabu ni rahisi kuliko kupata dhamana. Hali hii imesababisha baadhi ya watu,Visiwani na nje, kuuliza kwa kiasi gani mahakama za Zanzibar zipo huru? Mimi ukiniuliza jibu langu ni kwamba nasikia kuwa zipo huru, lakini sizioni kuwa huru.
Baadhi ya watu Visiwani, hasa wanasheria, wanasema panapokuwepo kesi zenye mashiko ya kisiasa ya aina moja au nyingine mahakama za Zanzibar huwa zinendeshwa kwa kitufe cha mbali (remote control).
Maelezo haya yamepata nguvu kutokana na mahakimu na majaji kueleza mara nyingi kuwa wamekuwa wakipewa amri na wakubwa, baadhi ya wakati kwa kutumiwa vikaratasi, juu ya namna wanavyotakiwa kuendesha kesi.
Unapokuwa na mtindo wa aina hii, hata ikiwa kwa kesi chache sana, basi majumuisho unayopata ni kuwa mahakama hazipo huru na kwamba zimegeuzwa kuwa sehemu ya utawala badala ya kuwa eneo lililo huru na linalotoa na kulinda haki.
Mahakama za Zanzibar hivi sasa zimekuwa zikitoa masharti ya dhamana ambayo unaweza kusema magumu sana au hayatekelezeki na hali hii imezusha wasi wasi juu ya huo uhuru wa mahakama unazungumzwa.
Zanzibar imekuwa na sifa ya kuweka masharti magumu ya mtuhumiwa kupewa dhamana na baadhi ya masharti haya ni ya aina yake na ya kipekee ambayo husikii kuwekwa Tanzania Bara au katika nchi yoyote ile inayojinadi kuwa na mazingira ya utawala wa haki na sheria.
Baadhi ya masharti haya, kama nilivyoeleza siku za nyuma, yana sura chafu ya kuwabagua raia na kuwaweka katika madaraja mawili, moja la watukufu na lingine ni la watu ambao mahakama haitaki kuwaamini.
Hawa watukufu ni wale wanaofanya kazi serikalini na wasiostahiki kuaminiwa na kuheshimiwa ni wale ambao sio wafanyakazi wa serikali.
Siku hizi imekuwa kawaida kusikia mshitakiwa anaambiwa kwamba wadhamini wake lazima wawe watumishi wa serikali wakati inajulikana wazi kuwa mtumishi wa serikali hawezi kuhatarisha ajira yake kwa kukubali kuwa mdhamini katika kesi ambayo watuhumiwa wake wamekuwa wakizungumzwa na viongozi wakuu wa nchi.
Mfano mmoja ni wa kesi inayowakabili viongozi wa jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho. Hivi mfanyakazi gani wa serikali atajitokeza kuwawekea dhamana? Tusidanganyane, huu sio mchezo mzuri na ndio maana wananchi wengi na hata hao tunaowaita washirika wetu wa maendeleo wanauona hauonyeshi haki kutendeka.
Au vipi kijana ambaye hana hata kiwanja utamtaka aweke dhamana waraka wa nyumba wakati hata hivyo viwanja hugawiana wakubwa na watu wanaohusika na ugawaji hujigawia wao, watoto, wake zao na hata wajukuu? (angalia ripoti ya tume ya uchunguzi juu ya ugawaji wa viwanja). Kama majina ya kweli na sio ya bandia ya watu waliopewa viwanja yatawekwa hadharani utaona watu hoe hae kama akina Salim Said Salim ambao hawapo tayari kuwaabudu viongozi kwa ajili ya kutaka vyeo au kulinda urafiki hutayaona.
Majina ya waliopewa viwanja yatawekwa hadharani. Sasa vipi mtu masikini utamtaka aweke kaburi la mzee wake. Jamani zama za kuifanya Zanzibar kuwa na haki ya kufanya tutakalo, licha ya kutia saini mikataba ya kimataifa ya kuheshimu haki za binaadamu, ikiwa pamoja na za washitakiwa, zimepita. Siku hizi nchi haziruhusiwi na hzivumiliwi ukiukaji wa haki za binaadamu au za washitakiwa.
Mtindo huu wa kuwabagua watu wa Zanzibar kwa mafungu ni wa hatari na utaiathiri Zanzibar.
Fikiria serikali itahisi vipi kama watatokea watu na kusema wanaoruhusiwa kuingia katika hoteli au maduka wanayoyamiliki ni wale tu ambao sio watumishi wa serikali? Kama serikali kupitia mahakama, ina wabagua watu kwanini na wananchi nao wasiwe na haki ya kuendeleza sera hii ya ubaguzi kwa kutumia mali zao?
Lakini kama serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar inataka kurejea tulikotoka ambapo kulikuwepo mahakama za wananchi (mahakimu wazee wanaosinzia hovyo) na kutojali uhuru wa mtu na hata kutoa hukumu kabla ya kesi kusikilizwa basi serikali isione aibu kutamka hivyo.
Kinachosikitisha ni kuona haya yanafanyika wakati Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ile ya Mkurugenzi wa Mashitaka inaongozwa na watu wenye kuheshimika katika fani ya sheria, lakini wamekaa kimya kama vile kutoa masharti magumu au kumnyima mshitakiwa dhamana ni jambo zuri na linalofaa kupongezwa.
Nilitegemea wanasheria wenye kuheshimika kama hawa wawili wanaoongoza taasisi hizi muhimu za serikali, wangejitokeza kupinga mwenendo huu wa kibaguzi, lakini inaonekana wameweka maslahi yao mbele kuliko yale ya kulinda haki na sheria.
Wazanzibari waache utamaduni wa kulindana kwa maovu. Watu anaojiita waungwana hulindana kwa mambo mazuri na sio mabaya, hasa yale yanayoitia nchi dosari. Lakini hata jumuiya za kiraia zimekaa kimya, labda kwa kuhofia msajili kuzifuta, lakini ukweli lazima usemwe, potelea mbali liwalo na liwe.
Wazanzibari wanataka kuwa na utawala wa haki na sheria za kweli na sio bandia kama inavyojitokeza sasa. Wazanzibari wengi walikuwa na imani na matumaini makubwa na serikali ya umoja wa kitaifa katika kusimamia haki na sheria, lakini kinachoonekana hivi sasa ni kwamba ndoto yao haikuwa ya asubuhi, mchana wala usiku.
Hakuna kitu kibaya katika nchi inayojigamba kuwa na utawala wa kidemokrasia, halafu zikaweopo dalili za vyombo vya dola na mahakama kutumika vibaya na hasa kuridhia kile kinachoonekana kama utashi wa kisiasa.
Mpaka sasa viongozi wa Uamsho hawana kosa mpaka pale itapothibitishwa bila ya wasi wasi wowote na mahakamani kuwa shutuma zinazowakabili ni za kweli na sio za kusingiziwa au kubunia.
Watu waliokabiliwa na mashitaka ya kuingiza dawa za kulevya ambazo zinaathiri maisha ya mamia ya watu, waliodaiwa kuiba mabilioni ya fedha, waliodaiwa kufanya uzemba wa meli kuzama na watu wengi kufa na wanaosemekana wameajiri wafanyakazi hewa na kuitia hasara serikali wamepata dhamana.
Ni muhimu kuelewa kwamba dunia ina tuangalia na kutucheka. Tufanye mambo mezani na kutumia hekima na busara. Vile vile tuelewe kwamba dunia inatuangalia na hapo tutakapolaumiwa kwamba tuliziendesha mahakama zetu hovyo tusije tukasema tunaonewa. Tujuwe kuwa hatimaye tutapanda tunachovuna, lakini historia itatukumbuka baadhi yetu kuwa tulikataa kupalilia mbegu mbaya.