Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maaalim Seif Sharif Hamad amesema Muungano wa Tanzania uliyopo sasa tayari ume-’expire’ na ufumbuzi wake ni Muungano mpya, utakaotoa mamlaka kamili kwa Zanzibar.
Maalim Seif ambaye amekuwa akipinga wazi wazi muundo wa Muungano huo tangu akiwa Waziri Kiongozi, mwishoni mwa miaka ya 1980, akiwa nje ya Serikali na sasa akiwa kiongozi wa pili Mkuu wa Serikali ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein hivi karibuni katika mabadiliko ya Baraza la mawaziri alimuacha nje aliyekuwa Waziri bila wizara Mansour Yussuf Himid kwa tuhuma za kuwa muwazi katika madai ya Zanzibar yenye mamlaka kamili.
Akihutubia mkutano wa hadhara Mwanakwerekwe, Unguja leo jioni Maalim Seif alisema Muungano wa Zanzibar na Tanganyika hauna ufumbuzi bali Zanzibar, inahitaji Muungano mpya:
“Muungano huu hauna ufumbuzi bali tunataka muungano mpya kabisa wenye mamlaka kamili…Zanzibar iwe na mamlaka kamili na Tanganyika iwe na mamlaka kamili huo ndio muungano tuutakao,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema Zanzibar inadidimia kutokana na udhibiti wa Muungano kwa kukosa mawasiliano ya moja kwa moja na mataifa ya nje na mashirika ya kimtaifa:
“Kiti chetu tunacho Umoja wa Mataifa na mpaka leo hakijaondolewa, lakini kiliwekwa kando kidogo kwa hiyo barua iliyotoka Dar es Salaam, na sisi kwa bahati mbaya hatukuiuliza,” alisema na kufafanua zaidi:
“Sisi hatuna mamlaka ya kuzungumza na nchi yoyote wala shirika lolote la nje na halikuwa katika Katiba ya Muungano lililowekwa katika Muungano ni mambo ya nje…Mashiriano ya Kimataifa katika ‘article of union’ hilo halimo,” alisema Maalim Seif.
Akizungumza kwa kujiamini Maalim Seif, alisema suala la Ushirikiano wa Kimataifa halikuwapo katika Mkataba wa Muungano, na kuungizwa kwake kulisababisha kuipotezea Zanzibar mawasialino na Mataifa ya nje:
“Serikali ya Muungano wenzetu walibadilisha wakaita ‘Wizara ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa’ hilo ushirikiano wa kimataifa halimo katika ‘article of union’ wamelipenyeza,” alisema na kuendelea:
“Kwa hivyo wametukata miguu na unapeleka nyaraka za kusaidiwa zinaganda kwao, kwa hivyo Muungano huu hautufai Wazanzibari, hao wenye kusema Serikali hizi lazima tunawaambia lazima ni Mwenyezi Mungu tu, hilo unalisema wewe tu nani kakutuma ukaseme hivyo,” alisema maalim Seif.
Maalim Seif, alisema Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda, amekuwa akitoa vitisho dhidi ya watu wanaohitaji mabadiliko ya Muungano ili Zanzibar iwe na mamlaka yake kamili:
“Mhe Pinda, anatoa vitisho anasema Muungano wetu umeshakomaa…kukomaa kwa maana ya kupea sio kama ukoma…sasa anasema laa Mtanganyika awe Mtanganyika, Wazanzibari warudi kwao…kakwambia nani Pindaaaa, au ndiyo vitisho?,” alihoji Maalim Seif.
Alisema kwa sasa Mzanzibari hatishiki tena, wakati wa vitisho umekwisha: “Mimi nawambia wananchi sababu za Muungano huu ni kuunganisha nchi za Afrika, hebu nambieni nani amekuja kujiunga?,” aliuliza na kuendelea:
“Kuna wakati baadhi ya viongozi wa Afrika walitaka kujiunga, wala haji. Maana kuna wakati Mzee kaunda, alikuja akachungulia, lakini akasema aaaa sitaki,” alisema Maalim Seif.
Kuhusu wafanyakzi katika Balozi za Tanzania nchi za nje, alisema hakuna uwiano wa kuridhisha baina ya wafanyakazi katika ofisi hizo na wote wanatoka upande mmoja wa Muungano:
“Nilikuwa huko Ulaya kuna maofisa 23 Mzanzibari mmoja tu na Umoja wa Mataifa ndiyo kwanza kapelekwa juzi Muombwa, ukenda Uingereza kati ya 19 wote Mzanzibari mmoja, jee hiyo ni haki? aliuliza na kuendela:
“Lakini watu wameshika Serikali mbili…yagujuuu!!tunasema tunadai na kudai haki sio vibaya na niwaambie kuna nchi ya Misri na Syria na Syria walipoona mambo hayendi vizuri wakajitoa wala hawakujitoa juzi nilishangaa mheshimiwa Pinda anatoa vitisho,” alisema Maalim Seif..
No comments:
Post a Comment