UROHO na UTAPIA fedha unawafanywa na watawala wetu wacheze na moto. Tunachoshuhudia siku hizi ni jinsi watawala wetu na matajiri wetu wanavyosaidiana kujitajirisha bila ya kikomo huku mamilioni ya wananchi wenzao wakizidi kuwa mafukara,masiki,mayatima ndani ya nchi yao wasijuwe wapi paa kukimbilia.
Utajiri, tena utajiri mkubwa, umeangukia kwa njia za haramu katika mikono ya watu wachache sana nchini humu. Si dhamiri yangu kuwazungumza wafanyabiashara waliotumia ubunifu wao wa kibiashara kujipatia utajiri mkubwa kwa njia za halali. Hawa tunaweza kuwatia kwenye kiganja kimoja.
Wala siwazungumzi wafanyabiashara wa kawaida wanaohangaika usiku na mchana kujipatia faida katika biashara zao wakiwa, kwa mfano, ama na maduka au magari ya kusafirisha abiria,wauza mitumba,nyanya,mama ntilia n.k.
Ninaowakusudia ni ile mitajiri, iliyo mijivi au ni ite majizi mengwegwe, inayotumia ulaghai kulighilibu taifa kwa manufaa yao wenyewe bila ya kujali madhara makubwa wanayowasababishia walio chini katika jamii.
Ufisadi wote huu unarahisishwa na mfumo wa uchumi tulionao. Huu ni mfumo unaotumia kisingizio cha utandawazi na uchumi wa soko huru ili kuwapururia majambazi waweze kulinyonya taifa hili. Mfumo huu ni mfumo mwovu.
Tumeona katika miaka na miezi ya hivi karibuni jinsi mfumo huo ulivyozusha taharuki na mahaniko katika nchi mbalimbali zikiwa pamoja na zile zinazotajwa kuwa ziko safu ya mbele miongoni mwa nchi zilizoendelea.
Chumi za nchi hizo zimetikiswa na zikatikisika kwa sababu mwingi wa utajiri wao umo mikononi mwa waroho wachache katika nchi hizo. Na wao ndio wenye kuzusha mfarakano na mpambano baina ya matajiri na wafanyakazi.
Ukweli wa mambo kwa sasa wanauhisi zaidi walio maskini na hata walio katika tabaka la kati katika nchi za Ulaya ya Magharibi na Marekani. Wanaoishi katika nchi hizo wanaona jinsi hali za uchumi katika nchi hizo zilivyodidimia, jinsi wasio na ajira wanavyohangaika bila ya mafanikio ya kupata ajira, jinsi bei za bidhaa zilivyoruka, jinsi huduma za afya na za kijamii zilivyoanguka na jinsi maisha kwa jumla yalivyo magumu.
Mwezi Septemba mwaka jana taasisi moja ya kiuchumi mjini Washington iitwayo Economic Policy Institute ilichapisha takwimu za mapato ya wafanyakazi wa Marekani. Kwa mujibu wa takwimu hizo mapato ya wastani ya mfanyakazi wa kiume wa Marekani aliyeajiriwa kikamilifu mwaka 2011 yalikuwa madogo yakilinganishwa na mapato aliyokuwa akipata mfanyakazi kama huyo mwaka 1973.
Takwimu hizo pia zimeonyesha kwamba asilimia 74 ya mwongezeko wa utajiri baina ya mwaka 1983 na 2010 uliwanufaisha asilimia 5 tu ya Wamarekani ambao ndio matajiri wakubwa kabisa. Hali za asilimia 60 ya wasiojiweza zilizidi kudidimia.
Hali kama hiyo haina budi ila kuzusha mapambano. Huo huwa ni mpambano wa kitabaka, baina ya maskini na wafanyakazi wanaonyonywa na matajiri wachache wanaoishi kama kupe kwa kuwanyonya walio wengi.
Mpambano huo wa kitabaka ndio moto wanaouchezea waroho wetu. Tuliacha kuzungumzia kuhusu mapambano ya kitabaka katika miaka ya mwisho ya 1980 pale Ukuta wa Berlin ulipoporomoka na Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti ulipo sambaratika.
Lakini ni dhahiri kwamba mapambano hayo bado tungali nayo. Na yana hatarisha hata uthabiti wa kisiasa nchini China ambako wafanyakazi, hasa katika sehemu za kusini mwa nchi hiyo, wanakabiliana na matajiri wao wakidai mishahara zaidi na hali bora za kufanyia kazi.
Wenye kutunga sera zetu za uchumi wanafaa wakumbuke kwamba kuna majeshi ya wasio na ajira na majeshi ya wenye vipato vya chini — walio kwenye majeshi yote hayo wanaghadhibika wakiwaona wachache katika jamii yetu wakiichezea rasilimali ya taifa hili.
Wanaghadhibika wakisikia jinsi mabilioni ya fedha yalivyohaulishwa na kufichwa katika akaunti za nje zilizo kwenye benki za ama huko Uswisi au Jersey au Bahamas. Wanaghadhibika wakiona kwamba serikali na taasisi zake zinazohusika ama zimelala au zimekhiyari kuvifungia macho vitimbi hivyo vya kifisadi kwa kuwa na wao wanakula humo humo.
Wanaghadhibika zaidi na kukirihishwa wakisikia, kwamba miongoni mwa wanao ukorofesha uchumi wa taifa kwa vitendo vyao vya kifisadi ni aliyekuwa Mkuu wa Majeshi, waziri wa zamani wa nishati na madini pamoja na waziri wa zamani wa ulinzi. Wote hao walitajwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ambaye ameyavalia njuga mas’ala haya ya waroho wetu wenye kutorosha mabilioni kwa matrillioni ya fedha nje ya nchi na kwenda kuyaficha nchi hizo nilizozitaja na kwengenako.
Kwa sasa hakuna vuguvugu linalowaunganisha wananchi kuupinga mfumo uliopo wa kiuchumi na sera zake. Lakini watawala wetu wasifikiri kwamba walio chini katika jamii wataendelea kuvumilia wakinyonywa na kunyanyaswa bila ya kuchukuliwa hatua dhidi ya wanyonyaji na wanyanyasaji au bila ya hatua kuchukuliwa kurekebisha hali za walio chini, ambao ndio wengi wa wananchi wa taifa hili wanao umia.
Yote hayo yanaweza yakachukuliwa hatua endapo wakuu wa serikali kweli wamejizatiti kuung’oa ufisadi katika jamii sambamba na misingi ya utawala bora. Ni muhimu kwamba tuna yatafakari haya sasa wakati nchi yetu ya Zanzibar iko mbioni kudai mamlaka kamili na Tanganyika wakiwa mbioni katika mchakato wa kulipatia taifa lao Katiba mpya.
Lazima watawala na sisi watawaliwa tujikumbushe kwamba mamlaka kamili hayatoshi sasa na nchi ya Tanganyika kupata Katiba pekee haitoshi na kwamba tunapaswa tuwe na utamaduni wa kisiasa utaowazuia mafisadi kutorosha mabilioni ya fedha kutoka nchini. Ikiwa utamaduni huo wa kisiasa hatunao basi Katiba kwa nchi ya Tanganyika na mamlaka kamili kwa nchi ya Zanzibar hata yawe mamlaka kamili ya utamu namna gani haitoweza kuhakikisha kwamba vitendo vya kifisadi kama hivyo havitoweza kutokea tena., kwa Tanganyika ndio hivyo hivyo katiba na iwe nzuri namna gani, haitoweza kuhakikisha kwamba vitendo vya kifisadi kama hivyo havitoweza kutokea tena.
Ugumu uliopo ni kwamba inachukua muda mrefu kuulea utamaduni wa kisiasa utaotuwezesha tuutumie kuimarisha demokrasia na utawala bora ili ufisadi usiwe na nguvu ya kutuvurugia uchumi.
Inatupasa tutafakari na tujiulize iwapo ni siasa au utamaduni wa kisiasa utaotuwezesha tufanikiwe kuung’oa ufisadi wa hali ya juu wa akina huyo Mkuu wa Jeshi mstaafu, aliyetajwa bila ya kutajwa jina na Kabwe.
Iwapo tunataka maendeleo hatuwezi kuwaachia watawala wetu waendelee na utamaduni wao wa kuvumiliana na kulindana. Lazima wajirekebishe. Wazitumie siasa kuubadili utamaduni wao. Demokrasia wanayosema kuwa wanaijenga haiwezi kuwa kitu iwapo haitoandamana na utawala wa sheria.
Na ni huo utawala wa sheria tu utaoweza kuwazuia mafisadi wasiendelee na ufisadi wao unaozusha mpasuko mkubwa wa mapato katika jamii baina ya matajiri wachache na mamilioni ya wananchi wenzao wanaozidi kusononeka kwa hali zao duni. Wasipo usimamisha huo utawala wa sheria basi watawala wetu wataendelea kucheza na moto. Kuna siku utakuja waunguza haba dunia bado kwenye kaburi wakifukiwa na siku ya kiyama wala musijidanganye kuwa ni mbali hata sio mbali Nyerere yuko wapi..? Mzee Karume yuko wapi..? Mabutu yuko wapi..? Mzee Kinyata yuko wapi..? Iddi Amini yuko wapi..? Kabila yuko wapi..? Savimbi yuko wapi..? Said Baree na Jeneral Aidid wako wapi..? Gaddafi yuko wapi n.k. n.k. basi na nyinyi mtakwenda mtaziwacha hapa hapa.