Juzi, tarehe 27 Septemba, 2015 wakati anahutubia mkutano wa kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) huko Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho, Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa matamko ambayo ni dhahiri yanaashiria kwamba yeye na chama chake hawako tayari kwa uchaguzi huru, wa haki na wa amani na badala yake wanajiandaa kusababisha shari na kutibua hali ya amani na utulivu uliopo.
Katika hotuba yake, Dk. Ali Mohamed Shein amenukuliwa akisema mambo mawili ambayo hayapaswi kuachiwa bila ya kutolewa kauli na chama chetu. Mambo hayo ni:
1. Kwamba eti CCM wanazo taarifa kuwa CUF inaandaa wafuasi wake kufanya fujo kuanzia tarehe 24, 25 na 26 Oktoba, 2015 na kwamba Jeshi la Polisi limejizatiti kukabiliana na hali hiyo. Kauli hiiyo imekuwa ikirudiwa rudiwa kwa namna tofauti na Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya CCM, Balozi Seif Ali Iddi.
2. Kwamba CUF mara hii kimekuwa kikisisitiza katika mikutano yake ya kampeni kwamba kitashinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa vyovyote vile, kwamba CCM wakitaka wasitake watatoa Serikali, na kwamba CCM wataipeleka weneywe Serikali Mtendeni (yaliko Makao Makuu ya CUF). Akasema kwa kauli hizo CUF kinaonekana wazi kwamba hakitokuwa tayari kukubali matokeo endapo kitashindwa.
Ni vyema tuweke bayana kwamba hatukustaajabishwa na matamko hayo ijapokuwa tumesikitishwa kumuona Mgombea huyo anatumia nafasi yake kuleta hali ya taharuki katika nchi na miongoni mwa raia pasina sababu yoyote. Tunaamini kauli hizo zinatokana na taarifa zisizo sahihi na ushauri mbaya anaopewa na wasaidizi wake ambao ndiyo wanaoonekana wana nia ya kusababisha vurugu pasina sababu wakati nchi yetu kwa kiasi kikubwa imetulia. Tunasema hatukustaajabishwa kwa sababu zifuatazo:
1. Tamko kwamba eti CUF inaandaa wafuasi wake kufanya fujo kuanzia tarehe 24, 25 na 26 Oktoba, 2015 na kwamba Jeshi la Polisi limejizatiti kukabiliana na hali hiyo, sambamba na kauli za Balozi Seif Ali Iddi za kutisha watu mara kwa mara kupitia hotuba zake, linaonekana lina lengo la kuficha mipango miovu inayopangwa na viongozi wa Kamati ya Kampeni ya CCM la kutaka kuitia nchi katika taharuki katika siku za wiki ya mwisho ya kampeni kwa lengo la kuwatisha raia wema wasijitokeze kwenda kupiga kura tarehe 25 Oktoba.
Tunazo taarifa kwamba miongoni mwa mambo yanayopangwa kwenye vikao vyao vya mikakati ni kwamba vikundi vya vijana wa CCM waliowekwa katika makambi maalum na kupewa mafunzo ya kufanya hujuma dhidi ya raia wema wanaandaliwa kufanya fujo katika siku za mwishoni za kampeni wakisaidiwa na kile kikundi cha baadhi ya askari wa Vikosi Maalum vya SMZ wanaojifunika nyuso na kuvaa makachara. Lengo la mkakati huu ni kuwajaza hofu raia wema wasijitokeze kwenda kupiga kura. Ziko taarifa kuwa vijana hawa wanatafutiwa sare za CUF ili ionekane ni CUF wanaofanya fujo hizo. Kwa tamko hili la Dk. Ali Mohamed Shein ni wazi sasa kwamba mazingira yanaandaliwa ya kutafuta visingizio ili kuhalalisha mipango hiyo miovu.
2. Sambamba na mkakati huo wa kutaka kuzua taharuki, tunazo taarifa pia kwamba kutokana na CCM kufikwa na maji ya shingo na kuonekana kuelemewa na uwezo wa Timu ya Kampeni ya CUF ambayo imepelekea mafanikio makubwa katika kampeni za CUF na mgombea wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kuna mpango mwengine unaopangwa wa kutaka kuwakamata na kuwabambikizia kesi viongozi wa Timu ya Kampeni ya CUF na baadhi ya wagombea wa CUF wanaoonekana kuwa ndiyo wanaofanikisha kampeni za CUF zinazokimaliza CCM.
Miongoni mwa wanaotajwa katika orodha ya kutaka kubambikiziwa kesi na kukamatwa ni Mwenyekiti wa Timu hiyo, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, na wajumbe wengine Mhe. Mansoor Yussuf Himid, Mhe. Ismail Jussa, na Mhe. Mohamed Ahmed Mugheiry (Eddy Riyami). Katika orodha hiyo, pia wanatajwa wagombea na wanaharakati kadhaa hususan wale waliohama CCM na kujiunga na CUF hivi karibuni ambao wanaonekana kukiweka CCM katika wakati mgumu kwenye majimbo yao. Wapo baadhi yao ambao tayari wamekamatwa katika siku za karibuni na kuhusishwa na tuhuma ambazo mtu anashangaa wakati wote walipokuwa CCM hawakuwahi kuhusishwa nazo.
Miongoni mwa hao ni Khamis Jabu Mohamedambaye ni Mgombea wetu wa Udiwani katika Wadi ya Chumbuni, Abdi Seif ambaye ni Mgombea wetu wa Ubunge wa Jimbo la Shaurimoyo, na Ramadhani Abdulsatar Salehe ambaye ni Mgombea wetu wa Udiwani katika Wadi ya Kwahani.
3. CUF inamtaka Dk. Ali Mohamed Shein, iwapo kweli anataka wananchi wa Zanzibar wamuamini kwamba ana dhati ya kuhakikisha amani na utulivu, awaeleze wananchi kwa nini hadi leo hajachukua hatua zozote za kuyafunga makambi ya vijana wa CCM yanayoendesha mafunzo ya kiharamia ambayo Maalim Seif Sharif Hamad alimuandikia rasmi na hata kumueleza ana kwa ana juu ya taarifa za kuwepo kwake. Makambi hayo ni pamoja na ile ya Tunguu (iliyopewa jina la SCENARIO ambayo ina vijana wapatao 900), Dunga (ina vijana 150), Welezo (ina vijana 200), na Amani CCM Mkoa (yenye vijana 300) huku kukitajwa mipango ya kufungua kambi nyengine kama hizo katika maeneo ya Kilombero, Pangatupu, Bumbwini na Makunduchi. Maalim Seif pia aliliarifu Jeshi la Polisi kuhusu taarifa za kuwepo makambi haya. CUF pia imechukua hatua ya kuiarifu jumuiya ya kimataifa juu kuwepo kwa makambi haya.
4. CUF pia inataka ielezwe iwapo kweli Dk. Ali Mohamed Shein ana nia ya kuhakikisha amani na utulivu katika nchi yetu amechukua hatua gani dhidi ya matukio ambayo yamekuwa yakifanyika hadharani na yameandikwa kwenye magazeti mbali mbali na hata kuwepo kwa picha zake za video ya kuwepo kwa kikundi maalum kinachohusisha baadhi ya askari wa Vikosi vya SMZ ambavyo viko chini yake na ambao wamekuwa wakivaa makachara na kujifunika nyuso na kuhujumu watu mitaani hususan wakati wa uandikishaji wa wapiga kura wapya katika miezi ya Juni na Julai, mwaka huu.
Matukio haya pia yameripotiwa na Maalim Seif kwake Dk. Shein na kwa Rais Jakaya Kikwete na pia CUF ikamuandikia rasmi Kamishna wa Polisi Zanzibar lakini hadi leo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa. Matukio hayo yalifikia hatua mbaya tarehe 4 Julai, mwaka huu, kijijini Makunduchi pale watu wawili, Kheri Makame Hassan na Ramadhani Hija Hassan, walipopigwa risasi na kujeruhiwa vibaya. Tunashukuru kwamba jumuiya ya kimataifa imetuhakikishia kuwa inafuatilia matendo haya yote na kwamba wahusika watabeba dhima kwa yatakayotokea kulingana na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia.
5. CUF inataka Dk. Ali Mohamed Shein pia aeleze iwapo yeye ni msimamizi wa amani na utulivu na anapenda uchaguzi huru na wa haki, ni kwa nini anakaa kimya wakati kikundi maalum cha askari wa Vikosi vya SMZ ambavyo viko chini yake wamekuwa wakiendesha zoezi maalum la kupita mitaani na barabarani, mjini na mashamba na kuzipachua na kuzichana picha za mgombea Urais wa CUF na wakati mwengine kubandika picha za Dk. Shein juu ya picha za Maalim Seif kinyume na Mwongozo wa Maadili ya Uchaguzi ambayo vyama vyote vya siasa, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vilisaini kwa pamoja? Haya yanafanyika huku askari wenyewe wa Vikosi wakikerwa na kutumiwa kisiasa kinyume na maadili ya kazi zao.
6. Kuhusu kauli kwamba CUF mara hii kimekuwa kikisisitiza katika mikutano yake ya kampeni kwamba kitashinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa vyovyote vile, kwamba CCM wakitaka wasitake watatoa Serikali, na kwamba CCM wataipeleka weneywe Serikali Mtendeni na kwamba kwa kauli hizo CUF kinaonekana wazi kwamba hakitokuwa tayari kukubali matokeo endapo kitashindwa, hili ndiyo linavunja hadhi na muruwa wa Mgombea Urais wa CCM kuliko jambo jengine lolote na kumuonesha udhaifu wake. Waandishi wa habari na wananchi watakumbuka kuwa tarehe 23 Agosti, 2015 wakati Mgombea Urais kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alipokuwa anazungumza baada ya kuchukua fomu za uteuzi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) alitamka bayana kwamba iwapo uchaguzi utakuwa huru, wa haki na wazi, na yeye ikatokezea akashindwa basi atakubali matokeo na kumpongeza mshindi. Akatumia fursa hiyo kumtaka na Dk. Ali Mohamed Shein na yeye atoe kauli kama hiyo. Siku iliyofuata, tarehe 24 Agosti, Dk. Shein alichukua fomu na kuulizwa swali hilo, lakini waandishi wa habari na wananchi wote wakamsikia akisema kwamba, “Bado ni mapema kutoa kauli kama hiyo”. Hadi leo hajatoa kauli kwamba iwapo atashindwa ataheshimu na kukubali matokeo ya uchaguzi, atampongeza mshindi halali na atakabidhi madaraka kwa atakayepewa ridhaa na wananchi. Sasa hapo ni nani ambaye anaonesha dalili za kutokuwa tayari kukubali matokeo?
Hizi ni hoja za msingi ambazo tunamtarajia Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, azitolee ufafanuzi na nyengine zinahitaji hatua madhubuti kuchukuliwa ili tujue iwapo kweli anayoyasema kuhusu amani na utulivu yanatoka katika dhati ya nafsi yake au ni kauli zinazoficha dhamira nyengine ambayo hataki kuisema.
Kwa upande wetu, Chama Cha Wananchi (CUF) tunazichukulia kauli hizi kuwa ni dalili za kutapatapa kwa Mgombea Urais huyo na chama chake baada ya kubaini kwamba mambo yanawaendea kombo kutokana na mwamko mkubwa unaooneshwa na wananchi wa Zanzibar kumkataa yeye na chama chake. Wananchi wa Zanzibar wameamua kukipa talaka chama cha CCM baada ya kuchoshwa na ahadi za chama hicho zisizotimizwa miaka nenda miaka rudi. Sasa wameamua kuikumbatia fursa ya mabadiliko yanayowakilishwa na CUF na mgombea wake Maalim Seif Sharif Hamad.
Tunapenda kukinasihi Chama Cha Mapinduzi kwamba kisiwaingize Jeshi la Polisi katika mipango yao miovu wanayoipanga. Kwa hakika, hadi sasa Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kazi nzuri ya kuhakikisha amani na utulivu katika kipindi chote cha kampeni. Na sisi CUF tumekuwa tukitoa mashirikiano ya hali ya juu ili kwa pamoja tuhakikishe nchi yetu inabaki salama na kwamba tunavuka katika kipindi hichi cha uchaguzi katika hali ya amani na utulivu. Hatudhani ni busara kwa viongozi wa CCM kula njama za kutaka kuturudisha kwenye vurugu na fujo.
CUF tunatoa wito kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama hapa nchini kuendelea kusimamia amani na utulivu wa nchi yetu pasina kuegemea upande wowote wa kisiasa na kuendelea kuwajengea imani wananchi wote kwa kukataa kuingizwa katika ubishani wa kisiasa wakati huu wa harakati za kampeni na hatua nyengine za uchaguzi. Sisi katika CUF tunawahakikishia mashirikiano yetu katika kufanikisha dhamira hiyo kama ambavyo tumekuwa tukifanya wakati wote.
Mwisho, tunamkumbusha Mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kwamba alikabidhiwa uongozi wa nchi mwaka 2010 katika hali ya usalama wa hali ya juu na umoja wa kupigiwa mfano wa wananchi wa Zanzibar kutokana na kazi kubwa ya kuleta na kusimamia maridhiano iliyofanywa na mtangulizi wake, Dk. Amani Karume, akishirikiana na Maalim Seif Sharif Hamad.
Tunamuomba na kumnasihi na yeye awe muungwana kwa kusimamia uchaguzi ulio huru na wa haki na utakaofanyika katika mazingira ya amani, usalama na maelewano, na pale wananchi wa Zanzibar watakapofanya maamuzi yao tarehe 25 Oktoba, 2015 basi ayaheshimu maamuzi hayo. Bila shaka, muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa utaendelea na unavihakikishia vyama vyote vya siasa vitakavyopata uwakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi kuwa sehemu ya Serikali hiyo.
CUF tunalihakikishia Jeshi la Polisi na vyombo vyote vya ulinzi na usalama hapa nchini kwamba tutaendelea kuwa mfano katika kufuata sheria bila shuruti na kwamba tutaendelea kutoa mashirikiano kwao katika kuendelea kuitunza tunu ya amani na usalama katika nchi yetu. Tunawaomba na wao wasisite kuwasiliana na sisi kama ambavyo wamekuwa wakifanya kila inapoonekana kuna haja hiyo ili kwa pamoja tushirikiane kufanikisha uchaguzi huru, wa haki na wa amani. CUF tunaendelea kutoa wito kwa wanachama na wafuasi wetu na wananchi wote kwa ujumla kufuata sheria na pia maelekezo ya viongozi wetu katika kutunza amani na utulivu wakati wote wakijua kwamba tunaelekea katika ushindi mkubwa kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
MKURUGENZI WA MAWASILIANO – TIMU YA KAMPENI YA CUF
ZANZIBAR – 29 SEPTEMBA, 2015
KILA MZANZIBARI ATAKAE IPIGIA KURA CCM ILI IBAKI MADARAKANI AJUWE NA YEYE ANACHANGIA KUFUNGWA KWA MASHEIKH NA KUTHALILISHWA KWAO NA KUENDELEZA DHULMA KATIKA NCHI YA ZANZIBAR UKAE UKIJUWA UTAULIZWA SIKU YA KIYAMA NA MWENYEZI MUNGU ULIPOSIKIA WAZANZIBARI WENZIO WANADHALILISHWA,KUDHULUMIWA NA KULAWITIWA NA HAWA JE ULIFANYA NINI TAFUTA JIBU LAKO MAPEMA KWA SIKU HIYO YA KIYAMA SIKU AMBAYO MALI NA WATOTO WAKO WALA CHEO CHAKO HAVITAKUFAA SIKU HIYO.