NITAMHESHIMU vilivyo Mwajuma Ali Khamis, mwanamke pekee aliyeingia kuwania wadhifa wa urais Zanzibar, lakini akakiri ufukara umemuangusha. Bi Mwajuma, ambaye sijajua ametokea wapi, amekua vipi, aliingia lini katika siasa mpaka kuthubutu kugombea, nitamheshimu kwa sababu nataka kuamini ni mkweli na muungwana. Huyu mama amesubiriwa kurudisha fomu za kuomba idhini ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kugombea urais, lakini mpaka inatimia saa 10 alasiri, Jumapili, Septemba 6, hakutokea. Alipopigiwa simu na rafiki yangu kikazi kueleza sababu za kutorudisha fomu aliyoichukua mara tu kipenga kilipopulizwa na Tume tarehe 22 Agosti, akasema, “Nilidhani ningetimiza masharti (ya kisheria), lakini baada ya kusafiri nchi kutafuta wadhamini, fedha zikaniishia kabla ya kutimiza.”
“Na kwa bahati mbaya sana, chama changu kimeshindwa kuniunga mkono,” anasema kwa kusikitika.
Naam, mwanamke pekee aliyejaribu kimo cha maji katika bahari nzito ya kutafuta urais Zanzibar ambako ni nyumbani kwa maajabu, vituko na visa, visivyoweza kufanyika kwingineko duniani. Kila nikitafakari maelezo yake, nazidi kuongeza mapenzi yangu kwa wanawake, mama zangu, dada zangu, binti zangu. Ingawa kimaumbile wanawake ni mtihani, wanaaminika. Imani ninayowapa, ni kumudu kusema ukweli unaotoka nafsini. Wana uadilifu wa kiwango kisichofanana na cha wanaume. Wanawake waadilifu zaidi ya walivyo wanaume.
Si wanawake wengi wanaoshiriki vitendo vya ujambazi, si wa kutumia silaha wala kalamu maofisini.
Roho zao huwa nzito kujiingiza penye batili. Mtaalamu wa masuala ya saikolojia, anasema wengi wa wanawake wanaokutwa katika maovu, huwa wamesukumwa na wanaume. Sasa Bi Mwajuma ameonesha uadilifu. Alijaribu, akajitahidi kutimiza masharti, akashindwa. Kasamehe, hata kule alikotarajiwa kufika kuirudisha fomu, hakutia mguu.
Tume ikamtangaza Bi Mwajuma wa United People’s Democratic Party (UPDP) ameshindwa mbio.
Kwa hivyo, mama huyu shupavu, akasababisha orodha ya wagombea urais Zanzibar, ibakie na watu 14, kwa kuwa waliochukua fomu kuomba kuteuliwa, walikuwa 15. Zanzibar kwa mara ya kwanza maishani, inapata wagombea wengi wa urais haijapata kutokea. Idadi hii imenishangaza. Naona kama nchi inaongeza maumivu ya utawala mbaya. Naangalia hapo kwa sababu kama si kwamba nchi inaongozwa vibaya, ni kwanini basi waibuke wananchi wengi wawanie kushika hatamu? Tena wameingia wananchi 14 akiwemo Dk. Ali Mohamed Shein, Rais aliyeingia madarakani Novemba 2010, kutokana na uchaguzi mkuu wa Oktoba 31? Anatetea kiti hicho kwa sababu Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inamruhusu. Mchambuzi mmoja wa masuala ya sheria na haki za binadamu amekataa mtizamo wangu huu. Anasema hadhani kama hiyo ndio sababu, japo anasisitiza, kasoro ya uongozi ameishuhudia. Yeye anasema anachokiona ni kwamba kumebuniwa mpango wa kifisadi wa kuwepo wagombea wengi ili kuzubaisha wananchi wakati wa kupiga kura, kuhesabu na kujumlisha kura, ili matokeo nayo yachezewe.
Harakaharaka nilimbishia. Nikamwambia utawala uliopo hauna ubavu wa kuendeleza ujinga huo.
Kwamba watawala wapange wahuni kuingilia taratibu na kuvuruga uchaguzi, lengo lao likiwa kulazimisha ushindi na kung’ang’ania madarakani, sikuamini haraka. Lakini sasa, taratibu napata hofu. Wakiwepo wawaniaji wengi, maana yake ndani ya chumba cha uchaguzi, kutakuwa na watu wengi. Mawakala wa wagombea watakuwa 14. Kwa mazingira ya uchaguzi unavyoendeshwa Zanzibar, idadi hii ni kubwa inayoweza kuvutia shutuma na hisia za hila. Wapo mawakala waweza kuhadaika wakakubali kutumika. Ndio, watakubali kuhadaiwa na kuridhia kutumika kubeba watawala. Huyu mchambuzi ananiambia kwa fikra zake na anayoyasikia chini kwa chini, wagombea wengi wamefadhiliwa. Si rahisi kuchunguza dhana hii ukaja na jawabu la uhakika wa mia kwa mia. Lakini, mbona baadhi ya wagombea hawajulikani kwa wananchi..? Inakuaje mtu kufika kugombea urais, asijulikane? Sitaji hata mmoja katika hawa wanaotajwa kuwa ni wageni. Hapana, sitaji majina. Nataka kueleza upo mchezo unachezwa katika uchaguzi huu. Wachezaji hawa, wanataka kuhakikisha mambo yao yanakaa vilevile, pasina kubadilika. Kama wao ni mafukara, waongeze mtaji wa shughuli zao, kama wanazo fedha, basi nyongeza siku zote huwa juu ya fungu. Aliyenacho kitu, ndiye huongezewa.
Bi Mwajuma huenda ikawa alipoambiwa na kushawishiwa, alikataa kutumwa. Uungwana. Uadilifu. Nitapokutana naye, nitakuwa na mengi ya kumuuliza. Angalieni: Jahazi Asilia, chama kilichoanzishwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005, harakaharaka kilimsimamisha mama muanzilishi, Jamila Abeid kuwania urais. Uchaguzi uliofuata, 2010, akasimama Haji Kitole, ambaye alipata kura 803, ikiwa ni asilimia 0.2 ya kura zote za urais zilizopigwa. Akashika nafasi ya tatu katika wagombea sita. Safari hii, kimemsimamisha Khamis Bakari Ali. Tatizo kwangu ni kutoshuhudia tukio hata moja la kuimarisha chama hiki tangu uchaguzi ule. Kimepata wapi nguvu ya kushiriki tena? Kikapata wadhamini na Sh. milioni 2. Maswali hayo nayauliza kwa wagombea wengine waliobakia isipokuwa gwiji wa siasa nchini, Hamad Rashid Mohamed, anayegombea kupitia Alliance for Democratic Change (ADC). Huyu siulizi uwezo wake kifedha, anazo. Mbunge wa miaka mingi, kiongozi mkubwa katika Chama cha Wananchi (CUF) kabla ya kufukuzwa Disemba 2012 na mfanyabiashara wa kiasi chake. Ameingia kupima upepo kama ni kweli Wazanzibari wamemtupa, baada ya kunyanyasika jimboni kwao Wawi, Chake Chake Pemba, kwa kumkataa kwenye kura za maoni tangu 2005 aliporudi kuomba kuteuliwa kugombea ubunge. Mara zote mbili, kwa taarifa za ndani ya CUF, aliteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi (BKU) kwa kupuuzwa maoni ya wananchi jimboni.
Lawama nyingi za maamuzi ya BKU alitupiwa Maalim Seif Shariff Hamad, katibu mkuu na swahiba wake mkubwa wakiwa waliotemwa CCM mwaka 1987, wakaanzisha kundi la kuchochea mageuzi, hatimaye chama cha CUF mwaka 1992. Vipindi tofauti wote walifungwa gerezani kwa hujuma. Maswali yale yanawagusa Juma Ali Khatib anayegombea kupitia TADEA, Said Soud Said (AFP), Mohammed Masoud Rashid (CHAUMMA), Abdalla Kombo Khamis (DP), Tabu Mussa Juma wa Demokrasia Makini na Issa Mohamed Zonga wa Sauti ya Umma (SAU). Mgombea Khamis Iddi Lila wa ACT-Wazalendo, najua amepata nguvu ya kubebwa na chama hiki kilichopata mtaji mkubwa wa kuanzishwa baada ya wanasiasa watatu akiwemo Zitto Kabwe, kufukuzwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa tuhuma za usaliti. Kama Jahazi Asilia, TADEA waliopata kura 497 (0.1) hawakujishughulisha kwa lolote hadharani katika kuimarisha chama. Rafiki yangu Soud Said Soud (AFP) ni shujaa wa mageuzi ambaye hajavuna kura ya maana popote pale, ameipata wapi milioni mbili? Masoud wa CHAUMMA, Kombo wa DP, Tabu wa Demokrasia Makini na Zonga wa SAU ubavu wamepata wapi?
KILA MZANZIBARI ATAKAE IPIGIA KURA CCM ILI IBAKI MADARAKANI AJUWE NA YEYE ANACHANGIA KUFUNGWA KWA MASHEIKH NA KUTHALILISHWA KWAO NA KUENDELEZA DHULMA KATIKA NCHI YA ZANZIBAR UKAE UKIJUWA UTAULIZWA SIKU YA KIYAMA NA MWENYEZI MUNGU ULIPOSIKIA WAZANZIBARI WENZIO WANADHALILISHWA,KUDHULUMIWA NA KULAWITIWA NA HAWA JE ULIFANYA NINI TAFUTA JIBU LAKO MAPEMA KWA SIKU HIYO YA KIYAMA SIKU AMBAYO MALI NA WATOTO WAKO WALA CHEO CHAKO HAVITAKUFAA SIKU HIYO.
No comments:
Post a Comment