Monday, October 8, 2012

MAALIM AJA JUU NA KUMUWEKA SAWA BALOZI WA TANGANYIKA NCHINI Z,BAR BALOZI SEIF ALI IDDI

UN
Mimi sitafuni maneno kwamba ni muumini wa Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na mashirikiano kati yake na Tanganyika kupitia Muungano wa Mkataba. Namshangaa leo anakuja kiongozi wa Zanzibar anasema tuna bendera na muhuri na wimbo wa taifa, hayo yanatosha. Hivi huyu anajua anachokisema au anatumikia maslahi ya waliomtuma? Una bendera gani hii ambayo mwisho wake Chumbe? Mimi nataka niione bendera ya Dola ya Zanzibar inapepea Umoja wa Mataifa, New York pale. Nataka tuwe na Paspoti ya Zanzibar, nikisafiri nitoe Paspoti ya nchi yangu. Nataka tuwe na Ofisi za Kibalozi za Zanzibar katika nchi za nje.
Leo hata mamlaka ya kiuchumi hatuna. Tumeamua rasilimali yetu ya mafuta na gesi asilia yasiwe mambo ya Muungano, mpaka leo Tanganyika wamekwamisha, wanatuzuia tusinufaike na rasilimali zetu tukajenga uchumi wetu. Wanasema tuna viwango na mfumo mmoja wa kodi lakini bidhaa zikitoka Zanzibar wanazitoza ushuru tena. Lengo ni kuua uchumi wetu ili hatimaye tudhoofike na tusalimu amri kwao. Yaguju! Wasahau hilo. Leo hata katika mikutano ya kimataifa, viongozi wetu wa Zanzibar hawapewi heshima ya uwakilishi wa nchi yetu.
Inafika mahala hata Naibu Waziri tu wa Bara anaongoza ujumbe wa Tanzania wakati kuna Waziri kamili kutoka Zanzibar lakini haheshimiwi. Tutarejesha mamlaka yetu kamili. Tuwe na Benki Kuu, tuwe na sarafu yetu ya Zanzibar, tupange uchumi wetu kwa maslahi ya watu wetu. Tunataka tuwe na uanachama katika jumuiya na mashirika yote ya kimataifa. Tuwe na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zanzibar. Tuwe na uwezo wa kuingia mikataba na nchi za kigeni. Hayo ndiyo tunayoyataka. Tukisema hivi hatuna maana tunataka ugomvi na Tanganyika. Hapana! Tunataka tuwe majirani wema na Tanganyika kama tutakavyokuwa na ujirani mwema na Kenya. Hayo yatafikiwa kupitia Muungano wa Mkataba wa Madola mawili huru kamili.”

No comments:

Post a Comment