Hayo si maneno yangu. Ni maneno yaliyotoka kinywani mwa mmoja wa rafiki zangu wa kambi ya ''walioufyata'' ndani ya Bunge Maalumu la Katiba Dodoma. Nilimuuliza sahibu yangu huyu: ''Ilikuwaje nyinyi mliokuwa mkitoa cheche za moto vinywani na kunguruma kama Simba hapa Zanzibar kulalamikia mfumo uliopo wa Muungano, lakini mara mlipofika Dodoma mkageuka vipanya vilivyojikunyata kwa hofu ya mlio tu wa paka?''
Jibu alilonipa ni hili: ''Sikiliza bwana, sisi hatuko tayari kurudia kosa lililofanywa na waliotutangulia.'' Nikamuuliza kwa udadisi mkubwa: ''Kosa gani hilo?'' Akasema: ''Ni kosa la kuchonga mdomo mbele ya Watanganyika kwa kujifanya watetezi wa Zanzibar na wapinzani wa Muungano uliopo.Umesahau wewe yaliyomfika Aboud Jumbe mwaka 1984 na waliomuunga mkono akina Brigedia Ramadhan Haji, Aboud Talib na Hafidh Suleiman (Sancho) ambao wote walilazimika kujiuzulu baada ya yeye kupelekwa machinjioni na kusulubiwa Dodoma? Umeyasahau yaliyomfika huyo Seif Sharif mwaka 1988 huko huko Dodoma na wenzake kadhaa, akiwemo marehemu Shaaban Khamis Mloo, Ali Haji Pandu, Hamad Rashid Mohammed, marehemu Sudi Yusuf Mgeni, marehemu Maulid Makame na wengineo? Ya karibuni tena ya kina UAMSHO na Mansour nadhani umeyaona mwenyewe,'' aliendelea sahibu yangu huyo na kumalizia kwa kunambia: ''Kwa hivyo sisi hatuko tayari kupoteza ulua wetu.''
Nikamwambia: ''Ina maana nyinyi mko radhi muendelee kuwa watumwa wa Tanganyika na kuiacha Zanzibar iendelee kuwa koloni lake?'' Akacheka na kusema: ''Watumwa tu? Haidhuru na tuwe hata watwana kwa Watanganyika, la muhimu kwetu ni kuendelea kuwa mabwana kwa Wazanzibari. Tukiwaridhisha hao unaosema mabwana zetu wa Tanganyika na kuendelea kuwa hewalla bwana kwao, tutaendelea milele kutawala na kubaki madarakani Zanzibar na kuwa mabwana kwa Wazanzibari. Na tukiondoka sisi watarithi watoto wetu, na ndio maana hatuko tayari kuukubali mfumo wa serikali tatu kwa sababu ingawa ni kweli utakuwa na maslahi kwa Zanzibar, lakini unahatarisha ulua wetu.''
Mimi sikukomea hapo nikaendelea kumhoji: ''Sasa huku kuitwa wasaliti wa Zanzibar, wasakatonge na vibaraka wa Tanganyika hakuziumizi wala kuzisononesha nyoyo zenu?'' Akaniambia:''Wacha watuite watakavyo, ni maneno tu hayo, sawa na kelele za mlango.'' Nikajaribu kumbana zaidi kwa kumwambia: ''Lakini hata wanaokuungeni mkono nao pia wamejua kuwa mnachojali zaidi ni matumbo yenu, kwa hivyo na wao pia washaamka, mnaweza mkapoteza nafasi zenu au hata kushindwa katika uchaguzi wa mwakani.''
Nilitarajia hilo litamgusa na kumshtusha, lakini badala yake alicheka sana na kunambia: ''Watu wetu sisi wanahitaji dozi ndogo tu kuwaweka sawa na kuwarejesha kwenye msimamo. Nikamhoji: ''Dozi gani hiyo?'' Sahibu yangu akanambia: ''Ni ileile ya kasumba ya ''Usultani wa Waarabu utarudi na Mpemba hatawali. Tukishawapa dozi hiyo hawaelewi chochote, watakuwa radhi sisi tuendelee kuvimbisha matumbo yetu na wao waendelee kula dongo. Isitoshe madamu tumewatii hao unaosema mabwana zetu wa Tanganyika, hatuna hofu tena kwa ajili ya uchaguzi wa mwakani. Wewe mwenyewe si unajua, wakati ukiwadia, mbali na Polisi ya Muungano, ikilazimu hata jeshi la JWTZ litatinga hapa Zanzibar kuja kulinda ushindi wetu.'' Kwa kweli jibu lake liliniacha kinywa wazi nikabaki nayatafakari na kuyawaza yote aliyonieleza.
KILA MZANZIBARI ATAULIZWA SIKU YA KIYAMA NA MWENYEZI MUNGU ULIPOSIKIA WAZANZIBARI WENZIO WANADHALILISHWA NA KULAWITIWA NA HAWA JE ULIFANYA NINI TAFUTA JIBU LAKO MAPEMA KWA SIKU HIYO YA KIYAMA SIKU AMBAYO MALI NA WATOTO WAKO WALA CHEO CHAKO HAVITAKUFAA SIKU HIYO.
No comments:
Post a Comment