KAMA kimya kinasema basi hichi kilichotanda miongoni mwa baadhi ya vigogo vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinasema mengi, tena kwa sauti kubwa. Hichi ni kimya chao kuhusu hatua ambazo Dkt. John Magufuli amejaaliwa kuzichukua katika kipindi cha siku thelathini ushei tangu aapishwe awe Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika kwa tiketi ya CCM. Hadi sasa miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho ni Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye, pekee aliyejitokeza akionekana kuwa yuko upande wa Magufuli. Nnauye, ambaye naye alichaguliwa mbunge kwa mara ya mwanzo katika uchaguzi uliopita, amejigamba kwa kusema kwamba Magufuli anachofanya ni kutekeleza atii ilani ya CCM. Juu ya hayo, hata naye pia amethubutu kuonya kwamba chama chake cha CCM kitaingilia kati endapo Magufuli atatenda mambo kinyume na chama hicho. Hilo ni onyo na tishio kwa Magufuli licha ya kuwa Nnauye hajawadhihirishia ni kwa njia gani chama cha CCM kitaingilia kati pindi akikikiuka chama chao. Jumapili hii iliyopita Ramadhan Madabida, mwenyekiti wa wenyeviti wa mikoa wa CCM alisema kwamba wenyeviti hao wanampongeza Magufuli kwa kasi yake ya kuwachukulia hatua watendaji wanaoshindwa kuyatekeleza majukumu yao. Wakuu wengine wa CCM wamejikunyata kama paka aliye rovyowa na maji ya mvua. Ama wamepigwa na muhuma kwa mshtuko walioupata, na wasioutarajia, kutoka kwa Magufuli. Kama si hivyo, basi wamepigwa na bumbuwazi na hawajui Magufuli ana mizungu gani mingine ambayo baadaye atawaonyesha Watanganyika na Wazanzibari haswa hao MaCCM walio zoe kula rushwa kwa miaka zaidi ya 50 sasa na ushaiyaa.
Ala kuli hali, hatua alizochukua mpaka sasa zimewatikisa walio karibu na hao vigogo na pia baadhi ya vigogo vyenyewe.
Sitoshangaa waathirika hao wakimwagia Magufuli maganda ya ndizi ili ateleze akiwa njiani kupigana na ufisadi, ubadhirifu pamoja na uzembe uliozagaa serikalini. Au huenda wakamwekea vizingiti ili ajikwae, wakitaraji kwamba ataanguka ili wamcheke na kumuumbuwa.Uzuri wa Magufuli ni kwamba yeye pamoja na waziri mkuu wake, Majaliwa Kassim Majaliwa, wanaonekana kuwa wanayajali maisha ya Rai wote kwa ujumla zaidi kuliko walivyo viongozi wengini wenye maradhi BT. Hilo halina shaka. Pili, wamekuwa wakichukua hatua bunifu, hatua tusizowahi kuziona zikichukuliwa na marais waliopita wa taifa hili baada ya Julius Nyerere. Tatu, kila moja ya hatua walizochukua ni kama yenye kumsuta au kumpiga kigongo Rais wa Awamu ya Nne, J Mrisho Kikwete. Tunaweza labda kuzimithilisha hatua hizo na yale maneno ya Nyerere dhidi ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi. Mwaka 1994, Nyerere aliandika kijitabu alichokiita “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanganyika na Zanzibar”. Kijitabu hicho kilikuwa na mengi ya kuukaripia na kuukosoa uongozi wa serikali ya wakati huo iliyokuwa chini ya Mwinyi na Waziri Mkuu wake, John Malecela, pamoja na Katibu Mkuu wa CCM wa wakati huo, Horace Kolimba. Kwa vile Nyerere wa siku hizo hakuwa na madaraka serikalini hakuweza kufanya lolote ila kukemea. Magufuli mwenye madaraka serikali hana haja sana ya maneno. Kwa vile anao uwezo wa kikatiba wa kuchukua hatua basi amekemea kwa vitendo shabash.Wakati maneno ya Nyerere yalikuwa yakikinzana na uongozi wa aliyemfuatia kwenye madaraka, vitendo vya Magufuli vinakinzana na uongozi wa aliyemtangulia kwenye madaraka.Katika nchi nyingi Rais anayeondoka madarakani aghalabu hupendelea anayemrithi awe dhaifu kushinda yeye au asiwe mtu mwenye kung’ara kumpita yeye. Bahati mbaya tena nasema tena Bahati mbaya ya Kikwete ni kwamba amerithiwa kwenye madaraka na kiongozi anayeonekana kuwa mshupavu zaidi yake na ambaye, hadi sasa, kila hatua aliyoichukua imezidi kumnawirisha na kumfanya azidi kuwa kipenzi cha umma isipokuwa hapa juzi ameanza kulikoroga baada ya kumrudisha Profesa Sospeter Muhongo na Dk. Harison Mwakyembe katika madaraka watu wameanza kusema aha CCM ni CCM tu na rushwa haitakwisha kwa hiyo Magufuli anatakiwa awe makini zaidi kuliko alivyo fikiri kwani hao hao CCM ndio wamwanzo wao msuburi ajikwae ili wamzome kwa sababu washajuwa anapendwa na wananchi.
Kwa mujibu wa wananchi, Magufuli ni Rais mwenye kujiamini, mwenye uchungu na nchi yake na mwenye ari ya kizalendo. Hivyo ndivyo wamuonavyo wananchi. Zaidi ya hayo, wanaamini kwamba anajuwa anasema nini na anajuwa anafanya nini. Juu ya hayo yote, ameonyesha unyenyekevu kwa kusema, bila ya kubania, kwamba yuko tayari kujifunza asiyoyajuwa, kama alivyowaambia wafanya biashara aliokutana nao wiki iliyopita. Mara kwa mara amekuwa akisisitiza kwamba serikali iliyopo sasa ni serikali yake yeye John Pombe Magufuli. Haitaji kuwa ni ya CCM, ingawa ulimwengu mzima unajuwa kwamba yeye ndiye aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho. Tusisahau kwamba mara mbili tatu wakati wa kampeni ya uchaguzi wa urais alisikika akitamka hadharani kwamba CCM ni chama chenye wanafiki na kinachohitaji kusafishwa. Kwa kusema hayo akimaanisha kwamba hicho chama ni kichafu, yaani uongozi wake wa juu ni mchafu na akijuwa kwamba chanuka kwa wengi wa wananchi. Yote hayo yamewatia kiwewe wajionao kuwa ndio wenyewe wa kuiendesha nchi watakavyo kufanya watakavyo kwa kuwatesa wanyonge kwa kutumia madara yao sasa wameigiwa na kiwewe tafrani ndani ya nyoyo zao na roho zao hawapati usingizi tena, hata kama ni kwa kuzipinda sheria wao wako tayari. Ndio maana vigogo vya juu ndani ya CCM vimekaa kimya vikimkodolea macho tu Magufuli badala ya kumshajiisha katika bidii zake za kizalendo na kufurahi nae au hata kumuunga mkono hapa wako kimya wanatafakari. Tunayahifadhi majina ya wawili watatu, mmoja akiwa katika ngazi ya juu kabisa, ambao tunasikia kwamba faraghani wanamkebehi na hata kumcheka wakimfanya kuwa kama ni mwehu. Wanaikebehi kauli yake ya “kupasua majipu” na wanazifanyia dhihaka ahadi alizotoa.Ninazisikiliza hotuba zake, naiangalia ile iitwayo “lugha ya mwili” wake inavyosema na moyo unaridhika, unafarijika kwamba kweli huyu ni kiongozi mwenye kuyaweka mbele maslahi ya taifa na wananchi kwa ujumla na si ya chama chake au ya viongozi wa chama hicho walio zoea kuona kama hii nchi wamerithishwa kutoka kwa baba na babu zao na wengine wote ni watumwa wao.Huyu ni mtu ambaye unaamini kwamba atakifanya anachosema atakifanya kwa sababu unahisi ya kuwa anakikusudia kwa dhati yake. Haonyeshi kuwa na ajizi wala muhali.Magufuli ana sifa nyingine inayomzidishia haiba: anaweza kuyalainisha magumu kwa mizaha lakini katu si mcheka ovyo. Ukimsikiliza tu utajuwa kwamba kiongozi huyu hana mchezo. Hii ndiyo sababu inayowafanya wenye nguvu ndani ya CCM wawe wanamcha na kutafuta paa kujificha na makucha yao wameyarudisha ndani ya nyama zao za vidole wakisubiri wakati muafaka wamalize kiaina, wakati huohuo, kumchukia.Wameingiwa na wasiwasi mkubwa kwa sababu wanachelea asije akaamua kuyageukia na kuyafufua madudu yao waliyoyazika yakazikika. Kwa sasa hawawezi kumgusa kwani hagusiki kwa vile wananchi wengi wanamuunga mkono kwa hatua alizochukuwa.
Habari tunazozisikia ni kwamba wapinzani wake ndani ya uongozi wa CCM-Taifa wanaungwa mkono, chini kwa chini, na baadhi ya viongozi wa CCM-Zanzibar walio wahafidhina na wanaong’ang’ania madaraka kwa kukataa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar isiyatangaze matokeo yaliyosalia ya Uchaguzi Mkuu huko nchini Zanzibar. Pande la viongozi hao linaongozwa na Balozi Seif Ali Iddi,Vuai ali Vuai,Ameir Kificho,Nahodha N.K. na mpaka sasa hakuna hata mmojawao aliyejitokeza kuiunga mkono kasi ya Magufuli na hatua anazozichukuwa au hata kumpogeza wote kimya kama majini ya baharini. Pale ambapo kasi za Magufuli hazijaonekana bado ni katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi ya Zanzibar. Mgogoro huo umesababishwa na hatua ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Firauni Jecha, kukataa kumaliza kuyatangaza matokeo yaliyosalia ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wa Urais wa nchi ya Zanzibar. Pamoja na hayo aliubatilisha uchaguzi Mkuu wa nchi ya Zanzibar isipokuwa ule wa wabunge na wa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika huo hakubatilisha kuwachama kama ulivyo. Hatua hiyo imeipelekea Marekani kuonya kwamba itainyima Tanganyika msaada wa dola za Marekani milioni 472 lau mgogoro huo wa kisiasa wa nchi ya Zanzibar usipotanzuliwa. Marekani, pamoja na mataifa mengine yaliyo wafadhili wa Tanganyika, yanataka mgogoro huo umalizwe kwa kukamilisha zoezi la kutangaza matokeo yaliyoyabaki ya uchaguzi na kutangazwa kwa aliyeshinda urais wa nchi ya Zanzibar.Tuna taarifa kwamba Muungano wa Ulaya (EU) umekwishaanza kufikiria ni hatua gani za kiuchumi unazoweza kuchukuwa dhidi ya Tanganyika pindi ZEC isiporejelea zoezi la kutangaza matokeo ya uchaguzi wa nchi ya Zanzibar.Kasi ya Magufuli pia imepwaya kwa kutowaondosha nchini Zanzibar wanajeshi wa nchi ya Tanganyika waliopelekwa huko kutoka Tanganyika tangu siku za uchaguzi na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo ya Tanganyika J.R.Kikwete na Kutawanywa wanajeshi hao mitaani na hili ni kuwatia watu hofu kubwa hasa kwa vile nchi ya Zanzibar haimo vitani wala hakuna hata fujo. Watu wanajiuliza kwa nini....?? au kunani.....?? Wanajeshi hao wametawanywa mitaani ilhali huko kwao nchini Tanganyika wanajeshi wameondoshwa mitaani baada ya kumalizika uchaguzi mkuu kwa nini iwe hivyo...?? Mwenye kuweza kuwatuliza wananchi wa Zanzibar kuhusu suala hilo ni yeye Magufuli akiwa Amiri Jeshi wa majeshi yote nchini kwa kuamrisha kwamba vikosi vilivyopelekwa nchini Zanzibar virudishwe huko nchini kwake Tanganyika. Asipochukuwa hatua za kuyatatua matatizo hayo ya nchi ya Zanzibar japo kuwa anaona ni nchi ndogo sana Magufuli atakuwa anajitafutia uhasama wa bure na wengi wa Wazanzibari wanaotaka utawala wa kisheria uheshimiwa kote ikiwa unahishimiwa nchini Tanganyika basi na nchini Zanzibar pia uheshimike sio nchini Tanganyika uheshimike nchini Zanzibar unaviringwaviringwa Magufuli atajiharibia jina lako la utendaji haki kwa wote. Huu si wakati wa kujipatia maadui zaidi ya wale walio katika uongozi wa CCM ambao wanakusubiri kwa hamu ufeli ili wakucheke na kukutukana. Hao viongozi wa CCM waliokaa kimya na wanaokerwa na miondoko yake ya uongozi ambayo ni miondoko iliyo safi sana mpaka wananchi wacheza mziki huu wa miondoko yako lakini hawa CCM hawana hila ila waendelee na kimya chao na labda waendelee pia kukuperemba Magufuli na kutamani ujikwae. Magufuli atafanya kosa kubwa akikipuuza kimya cha wasiomtakia yeye, na taifa, mema. Kimya chao ni cha shari na ni cha hatari. Ajue namna ya kupambana na wenye kimya hicho. Kwa sadfa, Nyerere alitanguliza kijitabu chake kilichoushambulia uongozi wa Mwinyi kwa shairi kuhusu ukimya lililoandikwa na malenga wa mwambao wa Kenya, Muyaka bin Haji Ghassany (1776-1840). Inafaa Magufuli ayakumbuke maneno ya ubeti wa mwanzo wa shairi hilo:
“Kimya mshindo mkuu, ndivyo wambavyo wavyele
Kimya chataka kumbuu, viunoni mtatile
Kimya msikidharau, nami sikidharawile
Kimya kina mambo mbele, tahadharini na kimya!”
KILA MZANZIBARI ALIYE IPIGIA KURA CCM AU MPAKA WAKATI HUU BADO ANAISAPOTI CCM ILI IBAKI MADARAKANI JAPO KUWA CCM IMESHINDWA UCHAGUZI AJUWE NA YEYE ANACHANGIA KUENDELEZA DHULMA NA KUFUNGWA KWA MASHEIKH NA KUTHALILISHWA KWAO NA KUENDELEZA DHULMA KATIKA NCHI YA ZANZIBAR UKAE UKIJUWA UTAULIZWA SIKU YA KIYAMA NA MWENYEZI MUNGU ULIPOSIKIA WAZANZIBARI WENZIO WANADHALILISHWA,KUDHULUMIWA NA KULAWITIWA NA HAWA JE ULIFANYA NINI TAFUTA JIBU LAKO MAPEMA KWA SIKU HIYO YA KIYAMA SIKU AMBAYO MALI NA WATOTO WAKO WALA CHEO CHAKO HAVITAKUFAA SIKU HIYO.