Friday, July 10, 2015

NCHINI ZANZIBAR WANA SIASA WAMEGOMA KUSAINI WAARAKA WA MADILI YA UCHAGUZI

Wadau wa vyama vya siasa wamekataa kusaini maadili ya uchaguzi mpaka kiingizwe kipengele cha jeshi la polisi
Nchini Zanzibar: Wadau wa vyama vya Siasa wamekataa kwa sauti moja kusaini maadili ya vyama vya siasa mbele ya uongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Kikao hicho kilichohuduriwa na wajumbe wa vyama vyote vya siasa  kilifanyika jana katika ukumbi wa hoteli ya Grand Palace na kushuhudiwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Ferauni Jecha, Mkurugenzi Salum Kassim Ali na maafisa wengine wakiwemo Makamishna wa tume hiyo pamoja na maafisa wa Shirika la UNDP.

Maadili hayo yalipangwa kutumika wakati wote wa uchaguzi mkuu ambapo wadau hao walitakiwa kuyazingatia na kuyafuata ili kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi ya kufanyika kwa haki na uhuru. Akizungumza kwa niaba ya wenzake Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa alisema hawatasaini waraka wa maadili hayo hadi kitakapoingizwa kipengele kitakachoeleza wazi majukumu ya jeshi la polisi na vikosi vya Serikali ya Zanzibar ambavyo vimeonesha ishara mbaya hivi karibuni. Jussa alisema licha ya kuwa vikosi vya SMZ havitakiwi kisheria kusimamia uchaguzi lakini vimeshuhudiwa vikiingilia uandikishaji wazi wazi na kufanya ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu, kukiuka sheria, kanuni na taratibu za uandikishaji jambo ambalo limezusha malalamiko makubwa kwa wananchi na wadau hao. Alisema bila ya kuwekewa kipengele mahsusi jeshi la polisi na vikosi vya SMZ maadili hayo yatakuwa hayana maana yoyote kwa kuwa hivi karibuni Wazanzibari wameshuhudia vikosi vya SMZ vilivyopita njiani na kuvaa soksi usoni huku vikiwa vimebeba silaha nzito nzito pamoja na silaha za kienyeji kama mapanga, nondo na misumeno ya kukatia miti wakiwatisha wananchi na kuwatishia maisha waandishi wa habari.
“Mwenyekiti mimi na chama changu hatukubaliani na kusaini maadili haya na ninawashawishi wenzangu wakatae hadi hapo kitakapoingizwa kipengele ambacho kitaeleza bayana majukumu ya jeshi la polisi, majukumu ya vikosi vya SMZ kwa sababu hivi juzi tu vimeonesha mfano mbaya sana kwa vikosi hivi kuvaa masoksi usoni kuwavamia na kuwapiga watu kuvamia vituo vya radio na kufanya uhuni mkubwa kwa hivyo kama hawajaingizwa hawa kwenye muongozo huu wa maadili hatuwezi kutia saini kikao kivunjike mkaingize tena kisha tuitane tena kuja kusaini” alisema. Kauli ya Jussa iliungwa mkono na wadau wengine huku wakipiga makofi kuonesha kuunga mono hoja hiyo wajumbe hao wamesema ni kweli kuna kila sababu ya jeshi la polisi na vikosi vya SMZ kuwekewa utaratibu wa maadili kwa kuwa wao ndio waribifu wakubwa tena sana na kila mara wao huharibu uchaguzi namba moja hivyo sio vyema maadili yakawaacha nyuma.
Suleiman Mohammed Abdallah kutoka chama cha NRA ambaye amesema anashangazwa kuona serikali ikikaa kimya licha ya kelele zote zilizopigwa za ukiukwaji mkubwa wa sheria na haki wa kuingilia uandikishaji huku jeshi la polisi likiwakana watu wao na kusema hawawajui wenye kuendesha vitendo hivyo. “Mimi nashangaa ikiwa serikali inaona vitendo vilivyokuwa vikifanyika njiani watu wamebeba silaha za moto, wamebeba mapanga, wamebeba misumeno ya kukatia miti wanatumia magari ya polisi na wengine wamevaa sare sasa hawa kama hawajawekewa utaratibu maalumu au hawajaingizwa kwenye haya maadili watakuja kutuletea maafa baadae” alisema Mohammed. Akitaja kipengele cha kuongeza katika maadili hayo Jussa alisema kifungu cha 15 kwenye wajibu wa serikali na wajibu wa tume ya uchaguzi kuongezwe wajibu wa jeshi la polisi na wajibu wa vikosi vya SMZ mbapo iwe wajibu wa jeshi la polisi ni kuhakikisha wanalinda usalama wa raia na mali zao, wanalinda wapiga kura maafisa wa tume lakini pia kuhakikisha wanalinda Amani na usalama na hawaingiliwi na taasisi nyengine ya ulinzi kwa kuwa wao ndio wenye mamlaka ya ulinzi.
Aidha katika kipengele hicho jeshi la polisi lihakikishe linafuata sheria na katiba na kwenye idara maalumu za SMZ zina sheria na jukumu na sheria iliyoanzishwa idara hizo na zijikubalishe kuwa hazitaingilia kwa hali yoyote katika uchaguzi. Juma Said Sanani kutoka Chama cha ACT Wazalendo, amesema kuwekwa maadili ya uchaguzi ni vizuri kwa kuwa yatakuwa ni muongozo wa kuipelekea nchi kwenye amani na kufanyika uchaguzi huru na wa haki. “Maadili haya tunayokuja kuyaweka basi yawe yanafuatwa ili tuvuke katika uchaguzi kwa salama bila ya hivyo tutakuwa na uchaguzi usio huru wala haki na matokeo yake tutashuhudia machafuko kama nchi nyengine kwa hivyo mimi nashauri maadili haya yatupeleke kwenye ukweli atakayeshinda apewe ushindi wake na alokuwa hajashinda akubaliane na matokeo” alihimiza Sanani. Makamo mwenyekiti wa baraza la vijana Chadema, Zeudi Mavamo Abdillahi alisema matumizi ya nguvu ya vikosi vya SMZ yaliotumika ni makubwa hivyo haiwezekani vikosi kuwekwa nyuma kutokana na kuonesha mfano mbaya hivi karibuni.
“Hatuwezi kusaini bila ya vikosi na wao kuingizwa humu kwa sababu wao wanajulikana namna gani wanavyoingilia chaguzi zetu na kwa kuwa tumeshatafunwa mara moja hatukubali kutafunwa tena juzi tu hapa wamefanya uhuni mkubwa kwa kuingilia watu na kuwapiga ovyo vipi tukubali tu hilo haliwezekani” alisema Zeudi. Mohammed Noor kutoka CUF naye alipendekeza kwenye kifungu cha 13 kuongezwa kifungu chengine kidogo kushughulikia kwa wepesi malalamiko yanayotolewa kwani kumeonekana malalamiko yanapotolewa tume huchukua muda kuyashughulikia. Aidha amesema katika kifungu cha 18 badala ya vyama vya siasa kuahidi kuyakubali matokeo  ya uchaguzi bali kuwepo neno halali “Mimi hapo kwenye neno kuyakubali matokeo kuongezwe neno halali hivyo isomeke vyama vya siasa tunaahidi kutakubali matokeo halali ya uchaguzi kwa mujibu wa fomu za uchaguzi yaliosainiwa kwenye vituo vya upigaji kura” alisema Noor. Peter Magwira wa UDP amesema kuna kila sababu ya kuwekwa maadili ya vyama vya siasa ili yaweze kuwaongoza wakati wote wa uchaguzi na baada ya kutoka matokeo ya uchaguzi ili nchi iwe salama na uchaguzi ufanyike kwa Amani.
“Watu wengine hawapendi kuyaheshimu haya maadili wakati sisi wenyewe ndio tunaoyatengeza lakini mimi nawashauri wanasiasa wenzangu tuyaheshimu haya maadili tunayoyatengeneza” alisisitiza Peter. Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya vyama vya siasa, Kamishna Nassor Khamis Mohammed kutoka ZEC alikubaliana na wadau hao kwamba maadili hayo yasisainiwe lakini akawaomba wafanye marekebisho ya vifungu ambavyo wanataka kuviongeza ili waende sambamba na dhana ya kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki. Khamis alisema maadili hayo ni yao wao kwa pamoja na sio ZEC peke yao hivyo wana kila sababu ya kuwasikiliza wadau hao hadi hapo watakapowafikiana kwani mwisho wa siku muongozo huo ndio utakaotumika kwa wote wakati wa uchaguzi hivyo sio busara wao kama ZEC kushikilia wanavyotaka wao tu bila ya kuridhiwa na wadau wote. Hata hivyo Chama Cha Mapinduzi hakikuhudhuria katika kikao hicho, akiomba radhi kwa kutoshirikia Mwenyekiti wa maadili hayo alisema kwamba aliwasiliana nao wamesema hawakuhudhuria kutokana na viongozi ambao walipaswa kuwepo kwenye kikao hicho wamekwenda Giningi Dodoma kwenye shughuli za kumtafuta mgombea urais wa nchi ya Tanganyika Masultani Weusi Tanganyika lakini wanakubaliana na mabadiliko na maamuzi yeyote yatakayofanyika katika kikao hicho.

KILA MZANZIBARI ATAULIZWA SIKU YA KIYAMA NA MWENYEZI MUNGU ULIPOSIKIA WAZANZIBARI WENZIO WANADHALILISHWA NA KULAWITIWA NA HAWA JE ULIFANYA NINI TAFUTA JIBU LAKO MAPEMA KWA SIKU HIYO YA KIYAMA SIKU AMBAYO MALI NA WATOTO WAKO WALA CHEO CHAKO HAVITAKUFAA SIKU HIYO.

No comments:

Post a Comment