Wednesday, July 24, 2019

HISTORIA YA BABU

ashura bilal 2
KAMA ndiyo mara yako ya kwanza kusikia jina la Abdulrahman Mohamed Babu, ngoja nikurahisishie kazi kidogo. Nitakueleza machache kumhusu ili ufahamu alikuwa mtu wa namna gani.
Mwaka 1959, miaka minne kabla nchi ya Zanzibar na miaka miwili kabla nchi ya Tanganyika na nchi yoyote ya Afrika Mashariki haijapata Uhuru, yeye tayari alikuwa mtu wa kwanza kutoka nchi ya Zanzibar au eneo hili Afrika Mashariki kwenda nchini China na kufanya mawasiliano na Chama cha Kikomunisti.
Katika safari hiyo, mwenyeji wake alikuwa Chou En Lai na yeye ndiye alikuwa mwananchi wa kwanza kutokea nchi ya Zanzibar na Afrika Mashariki kukutana na kuzungumza na Mwenyekiti Mao Ze Dong.
Kabla ya Baba wa Taifa la nchi ya Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, hajajiingiza katika masuala ya Umajumui wa Afrika, Babu akiwa Mzanzibari alikuwa miongoni mwa Waafrika mashuhuri waliohudhuria mkutano wa All African People Congress uliofanyika Novemba 1958 nchini Ghana na kuhudhuriwa na wanasiasa kama Kwame Nkrumah, Kenneth Kaunda, Nnamdi Azikiwe, Patrice Lumumba na Frantz Fannon.
Ndiye mwanasiasa maarufu wa nchi ya Zanzibar anayeweza kuwataja watu kama Ernesto Che Guevarra na Malcolm X kama marafiki zake. Kimsingi, katika baadhi ya duru za kimataifa, Babu alikuwa maarufu kuliko Mzanzibari yeyote Kiongozi yoyote wa nchi hizi za Afrika Mashariki yani Kenya,Uganda na Tanganyika kwenye miaka ya 1960. Na hapo najumlisha na Nyerere.
“Kusema ukweli, kama leo tunasema kuna uhusiano wa kihistoria baina ya China na Nchi ya Zanzibar au nchi ya Tanganyika, ni lazima tuseme kwamba Babu ndiye aliyeziunganisha nchi hizi Tatu. Kuna mtu anaitwa Ali Sultani, Mzanzibari, aliwahi kwenda China lakini akitokea Uingereza kwa masuala ya kupigania Harakati za Wafanyakazi lakini ni Babu ndiye alikwenda China na kuitambulisha nchi ya Zanzibar na nchi ya Tanganyika,” anasema Mama Ashura Hilal maarufu kama Ashura Babu, aliyekuwa mke wa mwanasiasa huyo kwa zaidi ya miaka 30.
Bi Ashura kwa sasa anaishi nchini Marekani. Amekuja nchini Zanzibar na atatembelea nchi ya Tanganyika pia kushuhudia ndoa ya mmoja wa wajukuu zake na ilikuwa bahati tu kwamba Muandishi wetu kuarifiwa mapema kuhusu ujio wake huwo.
Akiwa amezaliwa katika eneo la Mwembeladu, nchini Zanzibar, mwaka 1942, mama huyu sasa ni mtu mzima mwenye umri wa miaka 73. Hata hivyo, ana udongo mzuri na utaweza kuamini hata akikwambia ana umri wa miaka 55 Mashaa Allah.
Wakati nilipokutana naye,Bi  Ashura hakuwa na sura ya kinyongo wala huzuni kutokana na madhila ya kisiasa yaliyomkumba mumewe huyo wa zamani pamoja na familia yake kutokana na harakati zake za kisiasa.
“Miye sizeeki kwa sababu sina kinyongo na mtu. Kama ningeamua kuwekea watu vinyongo ningekuwa naumwa na presha kila siku. Ninachoshukuru ni kwamba Babu mwenyewe alikuwa amewasamehe waliomfanyia mabaya na aliendelea na maisha yake,” anasema.
Kwa mara ya kwanza, walikutana na Babu kwenye miaka ya 1950 wakati yeye akiwa mwanafunzi na Babu akiwa Katibu Mkuu wa chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP).
Bi Ashura alikuwa mmoja wa wasichana wachache waliokuwa wakivutiwa na siasa wakati huo. Ni mapenzi yake yaliyomfanya ajiunge na Umoja huo wa Vijana na kisha kukutana na Babu ambaye alikuwa ameshawishiwa kuhama kutoka Uingereza alikokuwa akishiriki katika harakati za Wafanyakazi.
Kwa mujibu wa Bi Ashura, aliyemshawishi Babu kurejea nchini Zanzibar ni Ali Muhsin Barwani, ambaye pia alihudhuria mkutano ule wa Ghana wa mwaka 1958 pamoja na Abeid Amani Karume aliyekuja kuwa Rais wa kwanza wa nchi ya Zanzibar bila ya kupigiwa kura wala wananchi wa Zanzibar kulizwa baada ya Mapinduzi ya mwaka mauwaji ya hali ya juu ya Wazanzibari walio uliwa bila ya hatia yoyote na wakuri walima makonge 1964 wakitokea nchini Tanganyika walio andaliwa katika mji wa Tanga.
“Babu aliporejea aliomba kuiona ilani ya ZNP. Akaifanyia marekebisho kwa mujibu wa alivyoona inafaa. Yeye ndiye aliyeweka utaratibu wa vijana kufundishwa Elimu ya Siasa (Political Education) kila Jumamosi ambayo alikuwa akifundisha yeye Mwenyewe.
“Ndiyo maana baadaye vijana wa ZNP wakawa wana uelewa mkubwa sana wa siasa kuliko wa vyama vingine vyote. Katika miaka hiyo ya 1950, Babu tayari alikuwa anajua kila kinachoendelea duniani kote kuhusu siasa na Ukomunisti.
“Ni wakati huo ndipo ZNP kilipoanza kupiga na miziki na kuwaruhusu vijana wake wa kike kuanza kuvaa sketi za khaki na kofia zenye nyota. Muziki na mavazi haya yakasaidia sana kuongeza idadi ya vijana na ZNP. Katika vijana waliokuwapo ZNP wakati huo, namkumbuka zaidi huyu Salim Ahmed Salim ambaye baadaye alikuja kushika nyadhifa nyingi za juu hapa nchini Zanzibar na hata nchini Tanganyika na duniani,”
Nilifanya mazungumzo na Bi Ashura kwenye bustani nje ya nyumba yake jijini Dar es Salaam nchini Tanganyika. Ilikuwa jioni na jua halikuwa kali. Ingawa sasa ameingia kwenye umri wa uzee, alikuwa nadhifu katika gauni lake la marinda.
Walianza uhusiano na Babu wakati huo. Hatimaye,Bi  Ashura alipotimiza umri wa miaka 18 mwaka 1960, wakafunga ndoa na mwanasiasa huyo ambaye tayari wakati huo serikali ya kikoloni ilikuwa imemuona kama mtu hatari hapa nchini Zanzibar.
Katika mazungumzo yangu naye,Bi  Ashura ananipa ukweli kuhusu jambo moja ambalo bila shaka lilikuwa halifahamiki kwa wengi. Kwamba akiwa nchini Uganda mwaka 1963, Babu alipiga simu kwa Salim Ahmed Salim na kumweleza kuwa aanze mipango ya kuunda chama cha Umma Party.
Babu alikuwa amekorofishana na wenzake ndani wa ZNP kuhusu mwelekeo wa chama hicho kwenye nchi ya Zanzibar Mpya yenye mamlaka kamili kutoka mikononi mwa Mkoloni wa Kiengereza. Wenzake, akina Ali Muhsin walikuwa na Mrengo wa Kibepari lakini yeye alikuwa na Mrengo wa Kijamaa. Tofauti hizo, ambazo zilichochewa pia na wakoloni, ndizo zilizosababisha Babu hatimaye ahame kutoka chama hicho na kuanzisha Umma Party.
“Baada ya Babu kuhama, asilimia kubwa ya vijana walihama kutoka ZNP na kujiunga na Umma Party kwa sababu walikuwa wanamuelewa kiongozi wao huyo. Wengine, baadhi yao, ni wale ambao walikwenda kufanya mafunzo ya kijeshi Cuba,” anasema Bi  Ashura.
Ni vijana hao, anasema mama huyu, ambao ndiyo waliotoa mchango mkubwa kwenye Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, wakitumia vema mafunzo ya kijeshi kwenye mapigano ya Guerrilla waliyoyapata nchini Cuba.
“Historia ya Mapinduzi inapotoshwa sana. Yale Mapinduzi ya mwaka 1964 yalifanikishwa kwa kiasi kikubwa na wapiganaji wa Umma ambao ndio waliokuwa na mafunzo ya kijeshi na waliojua mbinu za mapigano.
“Ukumbuke kuwa kwenye mkesha wa Mapinduzi, viongozi wote wa juu wa chama cha Afro-Shiraz na Umma hawakuwapo Zanzibar. Akina Karume, Babu, Kassim Hanga na wengine wote walikuwa Dar es Salaam. Wananchi wengine hawakuwa na mafunzo yoyote ya kijeshi lakini wakawa wamepewa silaha.
“Bila kutumia mbinu wasingeweza kuiteka Kambi ya Malindi ya Polisi. Hii ni kwa sababu ilikuwa imezungukwa na ukuta ambao ulikuwa na matundu ya kupitishia risasi. Mbele ya kambi kulikuwa na eneo la uwanda wa wazi kabisa. Kusogelea pale ilikuwa ni kujitakia kifo maana wangeonekana na wangepigwa risasi.
“Ni wapiganaji wa Umma ndio waliokuja na mbinu ya kuvamia kambi ile usiku tena kwa kutambaa kwa kutumia matumbo. Askari wa kambi wanakuja kushituka watu tayari wako kambini. Ile ndiyo ilikuwa namna pekee ya Mapinduzi kufanikiwa,” anasema mwanamamamapinduzi huyu.
Babu alitakiwa akamatwe siku chache kabla ya Mapinduzi hayo. Bi Ashura anasema ilikuwa bahati kwamba mmoja wa askari anayemkumbuka kwa jina moja la Barnabas, ndiye aliyekwenda kwao na kuwapa taarifa kuwa aondoke kwani atakamatwa.
“Babu alitoroka Zanzibar kwa kutumia usafiri wa ngalawa iliyokuwa nyuma ya eneo la Ngazimia, Unguja na ndiyo iliyompeleka Dar es Salaam. Mimi sikuondoka naye kwa sababu nilikuwa na watoto wadogo watatu na wasingeweza kusafiri baharini na ngarawa. Nikabaki lakini vijana wa Umma Party walikuwa wakilinda.
“Baada ya Mapinduzi, ndipo akina Babu wakarudi kwa kutumia usafiri wa boti iliyotolewa na Myahudi mmoja aliyekuwa akimiliki Hoteli ya Silversands anayefahamika kwa jina la Mischa. Hivyo hapo utaona mchango mkubwa wa vijana na chama cha Umma Party kwenye Mapinduzi,” anasema.
Mama huyu anayakumbuka Mapinduzi hayo kwa sababu nyingine ya kibinafsi. Baada ya Babu kutoroka Visiwani, binti yao mkubwa aliyekuwa akicheza nje ya nyumba yao aligongwa na gari na dereva mwanafunzi na kufariki dunia.
Babu asingeweza kurudi Zanzibar kwa sababu angekamatwa na Mapinduzi yasingefanyika kama yalivyopangwa. Ikabidi mtoto yule azikwe pasipo baba yake ingawa Babu alipewa taarifa. Bi. Ashura anasema askari walitanda makaburini wakifikiri kuwa huenda Babu angekuwepo lakini hakujitokeza.
Malcolm X na Che Guevarra
Katika matukio ya kihistoria ambayo Bi Ashura anayakumbuka; hakosi kusahau mikutano ya Babu na wanamapinduzi maarufu duniani; Ernesto Che Guevarra na Malcolm X. Hawa walikuwa marafiki wa mumewe huyo wa zamani ambao naye alikutana nao.
Mara ya kwanza walikutana na Malcolm X kwenye mojawapo ya ziara za kikazi za Babu nchini Marekani. Aliyewakutanisha alikuwa ni Mzanzibari Ali Foum ambaye baada ya Muungano alipangiwa kituo cha kazi New York, Marekani. Huyu alikuwa ni mmoja wa vijana waliolelewa kisiasa na Babu.
“ Siku moja Foum alitualika chakula cha usiku nyumbani kwake na tukakutana na Che Guevarra. Yeye ndiye akatuambia kwamba alitakiwa kuhutubia kwenye mkutano wa Malcolm X uliopangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Audubon Ballroom, Manhattan, New York.
“ Alitusimulia kwamba ilikuwa yeye aende kuhutubia pale Audubon lakini Rais wa Cuba, Fidel Castro, alikuwa amemkataza asiende kwa sababu za kislamu. Hivyo Che akamuomba Babu akatoe salamu zake kwenye mkutano ule.
“Mimi na Babu tukaenda kwenye ule mkutano. Babu akakaa jukwaani na Malcolm, huku mimi na mke wa X, Betty Shabazz, tukikaa kwenye mstari wa mbele kushuhudia. Babu alipewa nafasi ya kuzungumza na alipoeleza kuhusu salama za Komredi Che, ukumbi mzima ulisimama na kulipuka kwa nderemo na vifijo.
“Mwaka huohuo wa 1964, kwenye mwezi wa kumi hivi, Malcolm alialikwa na Babu na akaja Zanzibar na Tanganyika. Alikwenda kwanza Zanzibar na kisha akaja Dar es Salaam. Alipangiwa hoteli lakini alikuwa akishinda nyumbani kwetu pale Mtaa wa Luthuli jirani na Ikulu.
“Malcolm X alikuwa mtu mzuri na mwenye bashasha. Alikuwa na uchungu kutokana na mateso ambayo mtu mweusi wa Afrika na Marekani alikuwa akiyapata. Alikuwa akipenda sana vyakula vya Kiafrika kama vile samaki wa kupaka (samaki wa kupikwa chukuchuku, bila kuwekewa mafuta wala viungo vingi).
“Alipokuwa Dar es Salaam, nyumba ilikuwa inatembelewa na wageni wengi. Marafiki wa Babu waliopo nchini na wapigania Uhuru wa nchi mbalimbali waliokuwa wakiishi Zanzibar na Tanganyika wakati huo.
“Walikuwa wanajifungia chumbani na kuzungumza mpaka usiku mkubwa. Mimi kazi yangu ilikuwa ni kupeleka chakula na kahawa. Wanazungumza mpaka asubuhi na ajenda kubwa ilikuwa masuala ya ukombozi, hadhi ya mtu mweusi na mapinduzi duniani kote.
“Che Guevarra na Malcolm X wote walikuwa watu wazuri. Lakini Malcolm X ilikuwa zaidi kwa sababu Betty alikuja kuwa rafiki yangu mkubwa. Nilikuwa siwezi kwenda Marekani pasipo kukutana na Betty na rafiki yetu mwingine aliyeitwa Ann.
“Watu wote hao watatu sasa hawapo tena duniani; Che, X na Babu. Wakati Malcolm alipouawa kwa kupigwa risasi, nilijisikia kama nimefiwa na mwanafamilia. bayaa zaidi aliuawa palepale Audubon. Betty alinisimulia kuwa alikuwa amekaa kwenye kiti kilekile alichokaa wakati nilipoenda. Ule msiba uliniuma sana,” alisema.
Sababu za Babu kutofautiana na akina Karume
Bi. Ashura hapepesi maneno linapokuja suala la kiini hasa cha ugomvi baina ya Babu na kundi la wanamapinduzi waliokuja kufahamika kwa jina la Liberators (Wakombozi) ambao kimsingi ni wahafidhina wa Mapinduzi ya mwaka 1964.
“Mara baada ya Mapinduzi, Rais Karume aliamua kuongeza mshahara wa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi kufikia kiasi cha shilingi 25,000 wakati huo. Pamoja na mshahara huo, mkubwa kwa wakati huo, Karume pia aliwakopesha wajumbe hao kiasi cha shilingi 75,000 kama mkopo wa nyumba.
“Babu alipinga suala hilo. Alisema lifanyike jambo moja; ama watu waongezwe mshahara na wasipewe mkopo au wapewe mkopo na wasiongezwe mshahara. Alisema jambo hilo ni ufisadi na yeye hatochukua mkopo huo.
“Wenzake wote walikubali. Yeye alikataa. Sasa kuna watu wakaenda kwa Karume na kumweleza umbea kwamba eti Babu anamsema vibaya kwa watu kuwa wao ni wezi kwa sababu ya kujiongezea fedha hizo. Karume akachukia sana.
“Pamoja na kuombwa sana achukue, Babu akakataa. Nakumbuka mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1970 wakati tulipoenda Japan kwenye Maonyesho ya Afro 70. Mzee Thabit Kombo alinifuata na kuniomba nimwambie Babu aache maneno na achukue zile fedha.
“Unajua Kombo alilelewa na baba mzazi wa Babu. Wazazi wa Babu walichelewa sana kupata mtoto wa kiume na wakamchukua Kombo na kumlea. Baba mzazi wa Abdulrahman alifariki dunia wakati mwanaye ndiyo kwanza akiwa na umri wa miaka miwili. Kwa hiyo, kwa Kombo, wazazi wale walikuwa kama wazazi wake.
“Watoto wangu wawili; Salma na Mohamed waliyapata majina yao kutoka kwa baba na mama wa Babu. Sasa Thabit Kombo alikuja na kuniambia; ‘Sasa Babu anataka ugomvi wa nini na watu...? Basi achukue tu mkopo ili mama yangu Salma na baba yangu Mohamed wapate mahali pa kukaa. Watoto hawa wataishi wapi akipata matatizo....’?
“Nilijua msimamo wa Babu kwenye hili lakini nikamuahidi Kombo kuwa nitajitahidi. Kweli nikamuambia lakini akanipa jibu moja; ‘Naomba hii iwe mara yako ya mwisho kuniambia kuhusu jambo hilo. Nimesema sitaki kuchukua mkopo,’. Babu akakataa. Mpaka anafariki dunia, Babu hakuacha nyumba, shamba wala mti wa mkarafuu. Hakuwa na chochote.
“Hakuamini katika utajiri wa mali. Ninachoshukuru Mungu ni kwamba hakuna mtu yeyote ndani au nje ya nchi ambaye anaweza kunyooshea kidole familia yangu na kusema tuliiba hiki au kile. Na hili si jambo dogo maana limetufanya tuishi kwa amani. Kama angetaka, Babu angeweza kuwa tajiri mkubwa maana yeye ndiye aliyekuwa anafahamika na watu wazito nje ya nchi yetu,” anasema Mama huyu.
Dalili za tofauti hizi alianza kuziona awali. Bi  Ashura anasema Karume alianza kutofautiana na wanasiasa wasomi na wenye mtazamo wa kuona mbali.
Miongoni mwa wasomi hao walikuwa ni akina Babu, Kassim Hanga na Sultani. Wote hao Karume hakuelewana nao vizuri na badala yake akajiweka jirani na akina Juma Washoto, Edington Kisasi, Brigedia Yusuf Himidi, Said Natepe na Seif Bakari.
Ndiyo maana, anasema Bi Ashura, akina Babu na Hanga walikuja kufanya kazi Tanganyika ambako usomi wao na changamoto zao zilikuwa zinavumilika kwa Mwalimu Nyerere.
Makala hii itaendelea wiki ijayo ambapo Ashura ataeleza kuhusu matukio yaliyofuata baada ya kifo cha Karume, uhusiano wa Babu na Mwalimu Nyerere na maisha yake baada ya kuwekwa kizuizini kwa Abdulrahman Mohamed Babu.

No comments:

Post a Comment