Wednesday, July 24, 2019

KATIKA MAKUNDI MANNE YALIOTAKA KUIPINDUWA NCHI YA ZANZIBAR NILIPI LILILOFYATUWA RISASI KWANZA


Afbeeldingsresultaat voor john  okello

Jemedari kutoka Uganda alivyoongoza Mapinduzi ya kuikomboa Zanzibar


NA JOSEPH MIHANGWA
WAKATI Abdallah Kassim Hanga na wenzake wakipanga Mapinduzi dhidi ya utawala wa Sultani visiwani Zanzibar kwa msaada wa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere mapema mwaka 1963, hawakuelewa kwamba, Mwanamapinduzi mwingine, ‘Field Marshal’ John Gideon Okello, naye alikuwa akipanga Mapinduzi kama hayo.
Hanga, mwanasiasa wa mrengo wa kushoto na mfuasi wa harakati wa aina za Mapinduzi ya Oktoba 1917 ya Urusi, alijua chuki waliyokuwa nayo baadhi ya vijana wa Chama cha Afro-Shirazi (ASP) dhidi ya utawala wa kikoloni na Serikali ya Kisultani visiwani; lakini walikosa ari ya Mapinduzi kwa sababu kiongozi wa ASP, Sheikh Abeid Amani Karume, hakupendelea njia ya umwagaji damu kutafuta uhuru badala ya sanduku la kura.
Lakini Hanga alielewa nguvu ya wanaharakati wa Kikomunisti wa chama kipya cha Umma Party (UP) cha Abdulrahman Mohamed Babu; akatamani ‘ushirika’ wa siri nao bila Karume na vijana wake kujua. Akajihoji, kama ASP ilizuia ukombozi kwa njia ya Mapinduzi, kwa nini asikubali kuitwa ‘msaliti wa ASP’ na kuleta uhuru kwa njia hiyo?
Wengine wa kundi la Hanga kutoka ASP wenye itikadi za Ki-Marx waliopanga Mapinduzi kwa msaada wa Mwalimu, huku aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Tanganyika, Oscar Kambona, akiwa kiungo chao, ni Abdul Aziz Twala, Saleh Sadallah, Akida Athuman na Othman Sharrif Mussa.
Katika kipindi hicho, Mwanaharakati mwingine, ‘Field Marshal’ Okello, mzaliwa wa Lang’o, Uganda na mhamiaji Zanzibar, alikutana pia na Mwalimu Nyerere miezi michache kabla ya Uhuru wa Zanzibar, wakajadili uwezekano wa Mapinduzi dhidi ya Serikali iliyotarajiwa kuingia madarakani.
Inasemekana, Mwalimu alimpa Okello jukumu la kuisoma hali ya kisiasa na kiulinzi visiwani humo kwa maandalizi ya Mapinduzi siku itakapowadia.
Kwa nini Mwalimu alitaka Mapinduzi visiwani?
Akizungumza kwenye hafla moja ya jioni mjini Dar es Salaam kabla ya Uhuru wa Zanzibar, Mwalimu akionekana kutofurahia hali ya kisiasa visiwani humo enzi hizo, alisema:
“Kama ningeweza kukikokota kisiwa kile (Zanzibar) hadi katikati ya Bahari ya Hindi (kiwe mbali na Tanganyika), ningefanya hivyo. Sitanii! Ninaogopa huko mbele (baadaye) Zanzibar itakuwa tatizo kubwa kwetu lenye kuumiza kichwa.”
Kwa tamko hilo pekee, ni dhahiri Mwalimu hakutaka kuwa na ‘jirani’ huyo ila kama kungefanyika Mapinduzi chanya. Kwa hilo, kwa nini asifikirie kuwatumia Hanga na Okello kufanya Mapinduzi kipindi ambacho Wazanzibar wengi hawakuyawazia?
Waingereza ambao ndio waliokabidhi Uhuru kwa Serikali ya Mseto ya Zanzibar National Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) kwa sharti la nchi kubakia chini ya himaya ya Sultani, nao waliamini kwamba Mwalimu alisimamia na kuwezesha Mapinduzi hayo; na hivyo kumfanya akane kwa kujitetea baadaye (kisiasa), akisema:
“Nilitabiri machafuko yangetokea muda si mrefu; na tazama, ndani ya mwezi mmoja Mapinduzi yakatokea… Na wote waliamini kwamba nilikuwa sehemu ya mpango wa Mapinduzi hayo. Kwa sababu tu nilitabiri matatizo, walidhani nimeshiriki!”
Lakini mtafiti na mwanahistoria mahiri wa Kizanzibari, Dk. Harith Ghassany, anaweka bayana ushiriki huo wa Mwalimu, katika kitabu chake ‘Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru’, akisema: “Maandalizi ya Mapinduzi yaliratibiwa vizuri na Mwalimu Nyerere mwenyewe, Wamakonde na wapiganaji wengine waliandaliwa katika kambi ya Sakura, Tanga.
“Alimteua Kambona na kumtuma huku na huko ili kufanikisha hilo. Ile siri (ilikuwa) ni yake na hakutaka itoke.”
Ikumbukwe, Julai 25 hadi 28, 1963, Mwalimu Nyerere alifanya ziara nchini Algeria ya Kimapinduzi, ya Rais Ahmed Ben Bella na miezi mitano baadaye kufuatia ziara hiyo; Januari 2, 1964, meli yenye shehena ya silaha, MV Ibn Khaldun, ilitia nanga Dar es Salaam na kushusha silaha nyingi kama sehemu ya maandalizi ya Mapinduzi.
Hanga kwa upande wake, alinukuliwa baadaye akisema, yeye na Abdul Twala, walikaa Tanganyika kwa miezi miwili wakifunzwa na Jeshi la Polisi namna ya kutumia silaha na kwamba, mwanzoni Mapinduzi yalipangwa kufanyika mwishoni mwa Desemba 1963, yakaahirishwa hadi Januari 7, 1964, lakini tarehe zote mbili hazikuwa nzuri.
Hanga alisema pia kwamba, siku moja kabla ya Mapinduzi, alikwenda Dar es Salaam kuchukua silaha lakini hakuweza kurejea hadi Januari 13, 1964 wakati Mapinduzi yamekwishafanyika.
Kundi la pili la Wana-ASP linalodhaniwa kupanga Mapinduzi lakini lenye siasa baridi, chini ya uongozi wa Seif Bakari, lilikuwa na Saidi Washoto, Abdullah Natepe, Khamis Hemed, Saidi Ali Bavuai, Yusuf Himid na Pili Hamis.
Wengine ni Mohamed Abdallah, Hafidh Suleiman, Hamad Ameir, Ramadhan Haji, Hamis Darwesh na Said Mfaranyaki.
Kundi hili tiifu kwa Sheikh Karume na ASP, halikuwa na programu ya Mapinduzi ya kueleweka na kwa sehemu kubwa, lilizingatia msimamo wa Karume wa kutoichokoza serikali kwa hofu ya ASP kufutwa na viongozi wake kuingia matatani.
Karume alielekeza wafuasi wake wawe watulivu hadi Uchaguzi Mkuu mwingine miaka mitatu baadaye, ambapo alikuwa na hakika ASP ingeshinda.
Septemba 1963, Field Marshal Okello kama mwanachama wa ASP, alionana na Seif Bakari, wakazungumza juu ya Mapinduzi na kubaliana, lakini dhamira ya Bakari ilikuwa dhaifu juu ya hilo.
Kwa kuchukizwa na uratibu dhaifu usio na malengo wa ASP, Okelo alianzisha kivyake mafunzo ya kijeshi ya siri kwa vijana kutoka Tanganyika, Kenya na Msumbiji kwa ‘baraka’ za Tanganyika na kushirikisha baadhi ya Wazanzibari shupavu.
Mafunzo hayo, yaliyojumuisha ‘manamba’ waliofukuzwa mashambani na Mamwinyi wa Kiarabu, pamoja na baadhi ya Askari Polisi waliofukuzwa kazi na Serikali mpya ya ZNP/ZPPP kwa kutoviunga mkono vyama hivyo wakati wa kampeni, yalifanyika vichakani chini ya minazi kwa kutumia silaha za jadi na bunduki bandia za miti.
Lengo la Okello na wapiganaji wake lilikuwa si kunyakua dola, bali kuchoma moto na kuteketeza kabisa mji wa Unguja.
Julai 1963 kuelekea Uhuru, aliyekuwa Katibu Mkuu wa ZNP, Abdulrahman Babu, alijiengua kutoka chama hicho baada ya kutofautiana kiitikadi na Rais wa ZNP, Ali Muhsin, aliyetaka Zanzibar huru ifuate siasa za Kiliberali (ubepari), wakati Babu (pamoja na Hanga wa ASP) alitaka Zanzibar iwe ya Kikomunisti.
Waliojiengua pamoja na Babu kutoka ZNP na kuunda UP ni Salim Ahmed Salim, Ali Sultan Issa, Mohamed Ali Foum na Ali Mahfoudh ambaye ndiye aliyeunda na kuongoza Jeshi la Ukombozi la Zanzibar (Zanzibar Peoples Liberation Army – ZPLA) baada ya Mapinduzi.
Akiwa Katibu Mkuu wa ZNP, Babu aliwezesha chama hicho kuanzisha ushirikiano wa kikazi na kiitikadi na nchi za harakati za ukombozi kama Misri ya Abdel Gamal Nasser, Cuba ya Fidel Castro na China ya Chou Enlai.
Kwa sababu hiyo, aliweza kupeleka huko vijana kwa mafunzo ya kijeshi mwaka 1961 ambapo miezi miwili kabla ya Mapinduzi, vijana hao ndio tu walikuwa wamerejea kutoka mafunzoni.
Dhamira kuu ya Umma Party ilikuwa ni kuanzisha mapambano kwa kushirikiana na ASP dhidi ya Serikali ya Kisultani Visiwani.
Na katika salaamu zake siku ya ‘Uhuru’, Desemba 10, 1963; Babu hakuficha dhamira yake, alisema: “Salaam! Watu wa Zanzibar na chama chao cha Umma Party, wanasubiri kunyakua madaraka na kuyaweka mikononi mwao siku na saa itakapowadia.”
Kwa mujibu wa Babu, saa na siku iliyosubiriwa ni ile ya kupinduliwa kwa Serikali ya ZNP/ZPPP na makada wa Umma Party, pengine kwa kushirikiana na kundi la Hanga.
Kufikia hapo, ni dhahiri kulikuwa na mipango ya Mapinduzi ya makundi manne yasiyofahamiana.
Kundi la kwanza ni lile la ASP la Hanga kwa kuungwa mkono na Tanganyika; kundi la pili lilikuwa la Field Marshal Okello, la walalahoi wa ASP na wasio na vyama; kundi la tatu lilikuwa la vijana butu wa ASP wakiongozwa na Seif Bakari na kundi la nne la harakati za Ki-Karl Marx, lililoongozwa na Babu.
Ni kundi lipi kati ya hayo manne, lililofyatua risasi ya kwanza ya Mapinduzi?
Jumamosi ya Januari 11, 1964, ilianza kushuhudia isivyo kawaida, mitaa myembamba ya Mji wa Unguja ikifurika nyuso ngeni zisizo za kimjini, tangu mchana hadi giza; lakini kila mtu alichukulia mambo kirahisi tu kama sehemu ya pilikapilika za maandalizi ya Sikukuu ya Ramadhani iliyotarajiwa.
Ukweli, vikosi vya Mapinduzi vilianza kuingia mjini tangu saa 10 jioni na kuendelea hadi usiku.  Sultani Jamshid bin Abdullah Khalfa Harub, alianza kuamini ule uvumi ulioripotiwa na Karume na Aboud Jumbe kwa Kamishna wa Polisi (Superintendent) J. M. Sullivan, siku mbili zilizopita, juu ya uwezekano wa kutokea machafuko.
Kama tahadhari kwa yawayo yote, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia cha Mtoni na polisi wa Kituo cha Ziwani, walipewa amri kwenda kulinda mjini, umbali wa kilometa tano hivi ambako kulikuwa kukichezwa dansi (fete) na kubakia askari wachache tu vituoni.
Nitamke mapema hapa kwamba, wakati haya yakiendelea, Karume, Hanga na Babu walikuwa Dar es Salaam.
Karume, inadaiwa alikimbilia huko siku moja kabla, pengine kwa kuhofia yale ambayo yangeweza kutokea, Hanga alidai baadaye kwamba alikwenda kuchukua silaha wakati Babu alitorokea huko Januari 8, baada ya kutafutwa ili akamatwe na Serikali kwa tuhuma za uhaini.
Yapata saa 7.00 hivi usiku Januari 12, Field Marshal Okello, akiongoza kikosi cha wapiganaji 400, alivamia Kituo cha Polisi Ziwani kilichokuwa chini ya Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Derham, baada ya kukata waya wa uzio. Akawazidi nguvu askari na baadhi kuwaua na kuteka silaha nyingi.
Kutoka Ziwani, Jemedari Okello alishambulia na kuteka Kituo cha Polisi Mtoni na kujipatia silaha nyingi zaidi.  Vijana wa Babu (Umma Party), walijitupa uwanjani kuungana na Okello wakati kituo kikiwaka moto, huku Okello akiwa amejitosheleza kwa silaha alizoteka, tayari kuuteketeza kwa moto Mji wa Unguja.
Kuingia kwa ‘vijana wa Babu’ wenye mbinu za juu za kijeshi na Mapinduzi walizosomea China, kulibadili madhumuni ya ‘maasi’, kutoka kuuteketeza kabisa mji wa Unguja, kuwa ya kushika dola, wazo ambalo lilitolewa na Qualletin Badawi wa Umma Party.
Mbali na kuteka vituo vya polisi, ikawa pia sasa ni kukamata Uwanja wa Ndege na Ikulu ya Sultani, bila hivyo, Okello pekee angepigwa, kwani Sultani alikuwa ametuma ndege Pemba kuleta silaha nyingi, lakini wakati ndege hiyo ikirejea, tayari vijana wa Babu walikuwa wamekamata uwanja wa ndege.
Gerelateerde afbeelding
Kwa kifupi, kuanzia kutekwa kwa Mtoni na kuendelea, mapambano yaliendeshwa na kuratibiwa kwa mbinu za Vita vya Msituni (Guerrilla Warfare) chini ya uratibu thabiti wa makamandoo wa Umma Party.
Hadi saa 12.00 asubuhi, upinzani pekee ulitoka Kituo cha Polisi Malindi, karibu na Bandari ya Unguja na makazi ya Sultani; na kufikia saa 2.30 asubuhi, Malindi nayo ikawa mikononi mwa Wanamapinduzi; Sultani Jamshid na familia yake, akatimka kuelekea Mombasa ndani ya Meli yake ‘Seyyid Khalfa’ iliyokuwa ikisubiri Pwani.
Jioni hiyo, Field Marshal John Okello akatangaza kupitia Redio Zanzibar kukamilika kwa Mapinduzi, akisema: “Mimi ni Field Marshal; Enyi mabeberu, hakuna tena Serikali ya Mabeberu katika visiwa hivi; Chama cha Afro-Shirazi na Chama cha Umma vitaunda Serikali mpya; Zanzibar sasa ni Jamhuri ya Zanzibar na Pemba; Rais wake atakuwa Sheikh Karume.”
Kisha akamwamuru Karume arudi haraka Zanzibar kuja kuchukua madaraka, akisema kwa sauti ya mamlaka: “Karume, popote ulipo. Rudi haraka kuchukua kazi yako.”
Januari 13, 1964, ambayo ndiyo siku Karume, Hanga na Babu waliporejea kutoka mafichoni Dar es Salaam, Okello alitangaza Baraza lake la Mawaziri likiwa na: Abdallah Kassim Hanga (Makamu wa Rais), Abdulrahman Babu (ambo ya Nje na Biashara); Aboud Jumbe (Afya na Huduma za Jamii); Othman Sharrif (Elimu na Utamaduni); Idris Abdul Wakil (Mawasiliano na Ujenzi), Hasnu Makame (Fedha) na Salehe Saadallah (Kilimo).
Manaibu Waziri walikuwa ni Hassan Nassoro Moyo (Mawasiliano) na Abdul Aziz Twala (Ofisi ya Rais) huku yeye ‘Field Marshal’ akijitangaza kuwa Waziri wa Ulinzi na Utangazaji na Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi, akisema:  “Serikali sasa inaendeshwa na sisi – Jeshi; ni juu ya kila raia kutii amri zetu.”
Hapana shaka kufikia hapo, kwamba John Okello, ndiye aliyeongoza Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964; na si Karume, Hanga wala Babu. Hata kama watu hao walikuwa na mipango ya kufanya hivyo, basi, Okelo aliwazidi kete na fikra kwa kutenda kabla yao.
Vyombo vya habari na taasisi za Kimataifa zinakiri hivyo. Gazeti la Tanganyika, The Standard la Januari 13, 1964 liliandika:  “Wapigania Uhuru waliokuwa na silaha wamekiteka Kisiwa cha Zanzibar; wamekamata majengo yote muhimu ya Serikali kwa muda usiozidi saa 24; usiku, Kiongozi wa Mapinduzi (Okello), alitangaza Muundo wa Serikali mpya ya Jamhuri ya Zanzibar na Pemba.”
Keith Kyle, wa Gazeti la ‘The Spector’, aliyekuwa Zanzibar siku ya Mapinduzi, naye aliandika: “Baada ya kukidhibiti Kisiwa cha Zanzibar, Okello alimwalika Abeid Karume kurudi Zanzibar kuchukua nafasi ya Rais asiye Mtendaji.”
Profesa Othman, Mwanazuoni mahiri wa Kizanzibari na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, naye alikiri hilo katika ‘The Influence of Nyerere [1999]’, kwamba: “Uhuru wa Zanzibar ulipatikana Desemba 10, 1963.
“Sultani akiwa mkuu wa nchi, ndani ya majuma matano tu Serikali hiyo ilipinduliwa na ‘Masiha’ mjinga, kiongozi wa wanaharakati, John Okello. Baada ya kipindi kifupi alisimika Baraza la Mapinduzi.”
Jumapili, Januari 19, 1964; Jemedari Okello, akiwa kiongozi halali wa Serikali ya Mapinduzi, aliamua kwenda Dar es Salaam kwa mapumziko na mazungumzo ya kikazi na kiongozi mwenzake, Rais wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere, yaliyodumu hadi usiku wa manane; na katika mazungumzo hayo, Mwalimu alimsihi Okello afanye kazi kwa amani na Rais Karume.

Na haikuwa hivyo bali Okello na alizidiwa kete na Mzee Karume na kujikuta katika wimbi la maji ya bahari asio weza kuyaonga maana alijikuta Zanzibar hayupo tena na Tanganyika Nyerere alimtimuwa Uganda ambako ndiko kwao hakukumuweka maana Iddi Amin Dada hataki mchezo akaishia Kenya akiwa kama mtu wa kawaida tu au kigaragosi tu asiye na lolote wala chochote.

No comments:

Post a Comment