Ahmed Rajab
JUMAPILI, Novemba 9, 1975, siku mbili kabla ya Ureno kusalimu amri na kuipa Angola uhuru wake, Radio Tanzania, Dar es Salaam, ilinguruma ikiwapasha Watanzania habari motomoto wasizozitarajia siku hiyo ya mapumziko.
Habari hizo ziliihusu serikali yao. Rais Julius Nyerere aliibadili serikali yake kwa kuliteua Baraza jipya la Mawaziri. Majina ya mawaziri na wizara zao zilipotangazwa, ilibainika kwamba baada ya miaka mingi Nyerere aliona bora abadili mtindo na awe na waziri kamili wa sheria.
Chaguo lake la waziri wa kuiongoza wizara mpya lilikuwa Julie Manning. Manning alikwishapata umaarufu kwa kuwa mwanamke pekee katika kundi la mwanzo la wanafunzi waliohitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kuingia chuoni humo 1963. Kadhalika, yeye ni mwanasheria wa kwanza wa kike na jaji wa kwanza wa kike nchini Tanzania.
Mara ya mwisho Nyerere alipokuwa na waziri wa sheria ilikuwa kabla ya kuundwa Tanzania alipokuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika. Waziri wake wa sheria alikuwa Chifu Abdalla Said Fundikira.
Nyerere na Fundikira walitoka mbali. Wote walikuwa watoto wa machifu, waliosomea Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda. Muhimu zaidi walikuwa wapiganiaji uhuru wa Tanganyika. Juu ya yote hayo, miaka michache tu baada ya uhuru walikorofishana na mwaka 1963 Fundikira alijiuzulu uwaziri.
Nyerere hakuona haja ya kumteua waziri mwingine wa sheria hadi 1975 alipomteua Manning. Kwa muda wa miaka 12 mambo yaliyohusiana na sheria yalikuwa yakisimamiwa na waziri wa mambo ya ndani ya nchi. Watanzania walikwishaizoea hali hiyo ya ‘sheria kutokuwa na wizara mahususi.’
Kipindi hicho kilikuwa kipindi kigumu kwa sheria na kwa haki za binadamu Tanzania, hasa Zanzibar ambayo ilikuwa na mfumo wake wenyewe wa kisheria uliokuwa wa ajabu ajabu.
Huko, watu wengi walifungwa jela bila ya kushtakiwa. Kuna waliokamatwa na vyombo vya dola na ambao hadi leo hawajulikani walipo na kuna walioteswa mateso ya kila aina hadi wakafariki. Kuna waliokamatwa kwa visingizio vya kisiasa na kuna waliokamatwa kwa sababu za wivu.
Yaliyokuwa yakitendeka katika Gereza Kuu la Zanzibar yameelezewa vizuri kwenye riwaya “Haini” ya Adam Shafi, aliyewahi kuwa mfungwa wa kisiasa gerezani humo.
Nyerere alipoamua kumteua waziri kamili wa sheria, magereza ya Tanzania yalikuwa yamesaki wafungwa waliokuwa wamehukumiwa kwa kuhalifu sheria.
Walikuwako pia chungu ya watu waliokuwa wamewekwa kizuizini kwa sababu za kisiasa. Wafungwa hao walikuwa wametiwa korokoroni bila ya kufikishwa mahakamani. Huko jela walikuwa ‘wageni wa Nyerere.’
Mnamo mwaka 1962, Bunge la Tanganyika liliidhinisha Sheria maalumu iliyompa Rais haki ya kuamrisha mtu akamatwe na afungwe endapo atahisi kwamba mtu huyo ni kitisho kwa usalama wa taifa. Sheria hiyo ilitumiwa pia dhidi ya mafisadi, wahujumu uchumi na wahalifu wengine.
Iliainisha kwamba mtu anaweza kukamatwa kwa amri ya Rais na kuzuiwa gerezani kwa muda usiozidi siku 15 bila ya kushtakiwa au kufikishwa mahakamani.
Hayo ni madaraka makubwa aliyopewa Rais. Aliwaumiza wengi kwa kuyatumia kwani sheria hiyo ilikuwa kama wavu uliowakumba waliokuwamo na wasiokuwamo.
Ingawa sheria ilisema kwamba mtu anaweza kushikwa kwa muda usiozidi siku 15, hata hivyo, shirika la haki za binadamu la Amnesty International liliwahi kusema kuwa kulikuwako watu waliokuwa wamewekwa ndani kwa muda uliofikia hata miaka 10 bila ya kujuwa walituhumiwa kwa kosa gani.
Wakati hali ilikuwa mbaya hivyo katika magereza ya Tanzania Bara, hali katika magereza ya Zanzibar ilikuwa mbaya zaidi kwa sababu ilikuwa kawaida wafungwa kuteswa.
Megereza ya Tanzania yana historia ndefu. Yale ya Tanganyika yalijengwa toka nchi hiyo ilipokuwa chini ya utawala wa Wajerumani kabla ya mwaka 1914. Ya Zanzibar yalijengwa miaka mia moja iliyopita Waingereza walipojenga gereza la mwanzo la kisasa visiwani. Waingereza walipoitawala Tanganyika waliyajenga mengine na baada ya uhuru serikali ya Tanganyika ikayaongeza.
Moja kati ya magereza ya mwanzo yaliyojengwa Tanganyika baada ya uhuru ni lile la Ukonga, jijini Dar es Salaam. Ukonga ni gereza lenye sifa mbaya. Lina historia ya kuwa na idadi kubwa ya wafungwa kushinda nafasi iliyo nayo, chakula chake kibovu na huduma zake za afya pia ni duni.
Kwa sasa Tanzania ina magereza yasiyopungua 120 kwa wafungwa wasiopungua 45,000. Wafungwa hao hubanana utadhani kuku waliotiwa susuni, au katika tenga, kupelekwa mnadani.
Nimeambiwa kwamba siku hizi takriban nusu ya wafungwa hao ni washtumiwa wanaozuiliwa kusubiri kesi zao au wafungwa waliowekwa rumande.
Zaidi ya watu elfu moja walikamatwa na kuwekwa kizuizini Zanzibar baada ya kuuliwa Sheikh Abeid Karume Aprili 7, 1972 na mwaka mmoja baada ya tukio hilo, 81 miongoni mwao walishtakiwa. Kumi na saba kati yao wakiwa pamoja na Abdul Rahman Babu, waziri wa zamani katika Serikali ya Muungano, walishtakiwa ilhali wenyewe wakiwa hawapo Zanzibar.
Kama alivyoeleza karibuni Bibi Ashura Hilal, aliyekuwa mkewe Babu, katika kurasa za gazeti hili, Nyerere alikataa kuwapeleka Zanzibar ambako hamna shaka wangeliuliwa. Badala yake aliwafunga bila ya mashtaka yoyote katika magereza mbalimbali ya Bara.
Aliitumia ile sheria iliyompa nguvu za kuwaweka watu kizuizini bila ya kuwafikisha mahakamani. Akina Babu waliselelea wakisota gerezani kwa muda wa miaka sita hadi Aprili, 1978. Siku Julie Manning alipoteuliwa awe waziri wa sheria Babu na baadhi ya wenzake walikuwa wamefungwa Ukonga. Hawakuwa wakisubiri kesi wala hawakuwekwa rumande.
Siku 12 baadaye, mnamo Disemba 21, Babu alishika kalamu na kumuandikia barua Manning iliyokuwa na maneno takriban 1,300. Baada ya kumpongeza kwa kuteuliwa kushika nyadhifa hiyo muhimu, Babu alilitoa dukuduku lake na la wenzake kuhusu hali zao za gerezani akitumai kwamba hatimaye waziri atachukuwa hatua za kuwatoa Watanzania kutoka kwenye aibu hiyo.
Halafu humo humo Babu alimpa Manning darsa za kisiasa, maadili, sheria na za historia. Kwa mfano, alimnukuu Fidel Castro aliyewahi kusema kwamba hakuna kazi iliyo ngumu “kushinda kumshtaki mtu asiye na hatia.” Babu alimuelezea Castro kuwa “mpiganiaji thabiti, adhimu na shujaa wa haki za umma.”
Kadhalika, Babu alimwandikia Manning hivi: ““Tatizo la kijamii, naliwe kubwa vipi na lenye kutisha vipi, linaweza tu kutanzuliwa kwa njia za kijamii na siyo kwa ukandamizaji.” Halafu Babu akamtajia Manning Jenerali Francisco Franco, aliyekuwa dikteta wa Hispania tangu 1939 hadi alipofariki 1975. Babu aliandika: “Franco alijaribu kukandamiza, na tazama mchirizo wa damu na uvundo aliouacha.”
Barua hii inaonyesha kwamba ijapokuwa Babu alikuwa ndani gerezani akishikiliwa na vyombo vya dola asiweze kufurukuta, hata hivyo, bado alikuwa akiyajuwa vyema yaliyokuwa yakijiri nje ya kuta za gereza la Ukonga.
Alimueleza Manning, kwa mfano, kuhusu jinsi wafuasi wake waliokuwa wameshtakiwa kwenye kesi ya uhange huko Zanzibar walivyokuwa wakiteswa ili wakubali kwamba kulikuwa na mpango wa kuipindua serikali ya Afro-Shirazi Party.
“Inajulikana kwamba watu wanne wamekufa kwa kuteswa. Wawili walipigwa risasi ili wenzao watishike na wakiri [kwamba kulikuwa mpango wa kupindua].”
Aliwataja watu hao kuwa ni Luteni Mikidadi Abdulla Ali, maarufu kwa jina la ‘Meki’ na Luteni Ali Othman. Aliongeza kwamba wengine wawili, aliowataja kuwa ni Abbas Muhammadiya na Muhammed Saghir, walifariki baadaye baada ya kuteswa na kunyimwa huduma za afya.
Kwa hivyo, watawala na vyombo vyao vya dola vilishindwa kumzuia Babu aliyekuwa gerezani asiwe na mawasiliano na walio nje na kuyajuwa yanayotendeka mitaani hadi serikalini.
Na hayo yasingeliwezekana lau pasingekuwako ushirikiano kati ya baadhi ya askari jela wakizalendo na wafungwa wao.
Walikuwepo bila ya shaka ‘mabwana jela’ waliowasaidia wafungwa kwa kuhongwa lakini walikuwako wengine waliouweka uzalendo mbele na wakawasaidia wafungwa kama kina Babu kwa sababu wakiziamini fikra zao.
Walikuwepo bila ya shaka ‘mabwana jela’ waliowasaidia wafungwa kwa kuhongwa lakini walikuwako wengine waliouweka uzalendo mbele na wakawasaidia wafungwa kama kina Babu kwa sababu wakiziamini fikra zao.
Halafu kuna mianya hata katika udhibiti wa dola ambayo humwezesha anayethubutu akaweza kuipenya. Bila ya kueleza mengi niseme tu kwamba binafsi niliweza kuipenya mianya hiyo mara mbili nikaingia Ukonga kwa njia ya ‘halali isiyo halali.’ Mara moja kumtembelea Babu na mara ya pili kumtembelea jamaa yangu, Badru Said, aliyekuwa amefungwa naye.
Mara ya mwanzo ‘bwana gereza’ aliniruhusu nizungumze naye Babu kwa muda mrefu sana kuliko uliokuwa ukiruhusiwa kisheria. Ulikuwa mrefu mno hata aliyenishindikiza gerezani aliingiwa na wasiwasi nje ya jela akidhania kwamba labda na mimi pia nimeshikwa. Hakuna mwingine ila mkewe Babu, Ashura.
Kwa hakika, bibi huyu katika mahojiano yake yaliyopita na Raia Mwema hajaeleza hata chembe ya mchango wake katika juhudi za kuwapigania akina Babu na wafungwa wenzake wa kisiasa.
Pengine Watanzania watashangaa kusikia kwamba watu watatu waliokuwa muhimu katika kampeni ya kuwapigania wafungwa hao walikuwa wanawake: yeye mwenyewe Ashura pamoja na Shirin Hassanali aliyewahi kuwa katibu muhtasi wa Babu na bibi mwengine ambaye kwa sasa sitotaka kumtaja kwa vile sikupata bado ridhaa yake.
Wao, kwa njia zao wazijuwazo wenyewe, ndio walioanzisha mawasiliano na wafungwa na kuwezesha barua zao zitoke nje. Si barua tu bali hata muswada wa kitabu cha Babu cha “African Socialism or Socialist Africa?” na miswada miwili mifupi ya Kanali Ali Mahfoudh. Mmoja ulihusu mapambano ya ukombozi wa Angola na mwengine ulimhusu Sheikh Abeid Amani Karume.
Ule wa Babu waliniletea London na nikaupatia mchapishaji na ile ya Mahfoudh niliondoka nayo mwenyewe baada ya kuizuru London.
Katika barua yake kwa Manning, Babu alisikitika kwamba sumu ya mateso ya Zanzibar ilikuwa inanyemelea Tanzania Bara. Aliandika hivyo kwa sababu Tahariri ya gazeti la Daily News la Novemba 18, 1975 ilitaka “maharamia’ wateswe ili wakiri makosa yao.
Babu alimwandikia hivi Manning: “Mwandishi wa tahariri haelewi kwamba ikiwa leo tutakubali maharamia wateswe, kesho itakuwa ni zamu ya wahariri kuteswa…”
Baada kushukuru kwamba Nyerere “mwenye kukirihishwa na umwagaji wa damu” ndiye aliyekuwa Rais wa Tanzania Babu alitahadharisha kwamba “Nyerere ni binadamu na akija akarithiwa na mtu mwenye maadili ya paka shume, basi maadili yote ya kisiasa na ya kijamii yatakuwa ya kipaka shume, ikiwa atarithi taasisi zilizopotoka kimaadili.”
Babu aliihitimisha hivi barua yake: “Tunatumai kwa dhati kwamba kwa vile sasa sheria imepata Waziri, haki itatendeka. Hatudai zaidi ya haki yetu ya kutendewa kwa mujibu wa sheria za nchi, na tufunguliwe kutoka maisha haya ya usumbufu, kwa mujibu wa sheria. Usiifanye historia ikaja kusema (kutuhusu) kwamba: “Waligonga kwa nguvu mara kwa mara kwenye kwenye lango la haki lenye nuru, lakini hawakujibiwa.”
Barua ambayo mahabusi Babu alimwandikia waziri Manning ni yenye kusisimua na ni muhimu kwa historia. Kwa hakika, sikuitendea haki kwa kuidokoadokoa hapa na pale. La kushangaza ni kwamba ina mengi ya kimsingi kuhusu dhana nzima ya haki ambayo bado yanaikabili Tanzania.
Juu ya muda wote uliopita tangu iandikwe na mageuzi yaliyotokea nchini, mengi anayoyalalamikia Babu humo bado tungali nayo. Sio katika magereza tu bali katika jamii nzima ya Tanzania kwa jumla.
Wafaransa wana usemi wao unaoielezea vizuri hali kama hiyo. Wao husema: “plus ça change, plus c’est la même chose.” Yaani, kila mambo yanavyozidi kubadilika, ndipo yanavyozidi kubaki yalivyo.
Imekuwa kama watawala wetu hawajajifunza chochote kutoka historia.
Wanasahau kwamba ni muhimu kujifunza kutokana na yaliyopita. Wasipofanya hivyo watazidi kutuhasiri na kutuumiza kwani watarejelea kufanya makosa yale kwa yale na dhunubu hizo kwa hizo, mara baada ya mara.
No comments:
Post a Comment