KAMPENI ZA KWETU NA USHUKU WA AKILI ZETU VISIWANI
Na: Mwandishi Maalum
Kuna watu hadi leo bado wanashangaa kwa nini Zanzibar imeshindwa kujikwamua na makucha ya ukoloni mpya uliojengwa kwa misingi ya hadaa iitwayo Muungano. Kwa lugha nyepesi Zanzibar haijapata kuwa huru, tusidanganyane. Lakini hali hii pamoja na kuwa inachangiwa na mataifa makubwa ya magharibi, mchango wetu sisi wananchi wa Zanzibar kama Zanzibar ni mkubwa mno katika kujihakikishia kuwa tunabakia kuwa watumwa wa ukoloni usiokwisha wa Mkoloni Mweusi Tanganyika.
Nina kila aina ya ushahidi kuwa Wazanzibari wenyewe wanapenda kutawaliwa dumu daima. Kwa mfano, Zanzibar ilitawaliwa na Mwarabu kwa miaka karibu mia mbili. Hakukuwa na lolote la maendeleo tulilofanyiwa zaidi ya lile la kuchanganya damu baadhi yetu na kisha kuishi katika dhambi ya kubaguana kwa makabila. Dhambi ambayo bado ipo baina ya Wazanzibari wenyewe, ilhali wote au tuseme asilimia 99 tukiwa Waislamu. Na juu ya madhila yote tuliyofanyiwa, najua wengine watapinga lakini hakuna mkoloni mwema ingawa kuna watu wengi Zanzibar wanaojitanibu na Uarabu na hata wanatamani bado nchi hii ingekuwa chini ya Utawala wa OMAN. Hili moja tu.
Ushahidi wa pili kuwa sisi ni watumwa wa akili zetu, ni pale mwenyezi Mungu anaposema kuwa hatabadilisha katika watu jambo mpaka wao watakapotaka libadilike. Sasa hapa utaona, kwa vile hadi leo tunasifia na kuutamani ukoloni wa Mwarabu, wenzetu wenye nguvu ya mataifa yenye nguvu zaidi ya Waarabu, wakaitumia fursa hiyo kututawala. Wametutawala sio kwa lazima, bali kwa akili na mapenzi yetu. Hapa namaanisha kuwa akili ya Mzanzibari haijawahi kuwa huru na kwa maana hiyo, akili isiyo kuwa huru haina haja ya kupewa uhuru. Itabakia kuwa akili ya kiutumwa tu!
Sababu kubwa ya kuwa tunabakia kifungoni kama nilivyotangulia kusema, ni akili zetu. Ni uhakika kuwa wengi wetu tumenyimwa elimu ya kujitambua lakini pia hata baada ya zama za ukweli na uwazi kufika, bado inakuwa vigumu sana kwa Mzanzibari kujikwamua na makucha ama ya ukoloni mweusi na ule ukoloni wa Viongozi ambao hawana la kuwapa wananchi zaidi ya lugha chafu kila ifikapo siku za kampeni za uchaguzi na kuwadanganya tutafanya hivi na vile na hakuna moja walilo fanya zaidi ya nusu karne sasa.
Mfano mwingine ulio hai, ukitaka kujua kwa kiasi gani akili zetu na zile za viongozi wetu zimefilisika, sikiliza kampeni zetu za siasa hasa majira au tuseme msimu kama huu wa uchaguzi. Nijuavyo, na uzoefu wangu unaonyesha kuwa, watu huenda kampeni kusikiliza mipango ya wagombea juu ya murua wao na wa nchi yao. Kwa kuwa muwazi na fasaha zaidi, watu huenda kwenye kampeni kusikiliza ni kiongozi au chama gani kina sera na ilani nzuri ya maendeleo kwao ili wapate waamue nani wamchague. Hivi ndivyo kampeni za watu wenye akili timamu zinavyofanywa. Kwetu sisi hali haiko hivyo!
Ukitaka kuthibitisha fuatilia mikutano yote ya vyama vya siasa inayofanyika hapa kwetu. Tena hasa hasa mikutano ya chama fulani hivi. Utakutia mkutano wa kampeni wa masaa matatu mazima unahutubiwa na viongozi wasiopungua kumi, na hakuna hata mmoja anayezungumza la maana zaidi ya matusi. Tena matusi ambayo wale wanaoyazungumza, hawathubutu hata kuyazungumza majumbani mwao lakini ktk jukwa la kampeni wanatukana kama hawana akili vizuri hiyo ndio barabara,viwanda,hospitali,umeme,maji,skuli,elimu wanao wahidi wananchi matusi.
Kinachoshangaza sana ni kuwa, ikiwa huwezi kutumia matusi ya namna ile nyumbani kwenu au kwako, kuna haja gani uyaseme hadharani kwenye uwanja uliojaa watu – wazee, watu wenye heshima zao na hata viongozi wa dini, achilia mbali mastuhu zako na mastuhu wa wenzako?
Kampeni za kwetu visiwani, tangu kuanza kwa vyama vingi, imekuwa matusi ndio ilani ya vyama na sera zao. Na cha kushangaza wananchi, wengi wao wakiwa watu wazima waliojistiri vizuri, husafiri masafa marefu kufuatilia kampeni kama hizi kusikiliza matusi ya nguoni tu nakuchekelea!
Hili kwa kweli linanifanya nizihakiki upya akili za watu wetu hapa visiwani. Pia hali hii inanipa bishara kuwa kwa akili zetu zilivyo, maendeleo yatabakia kuwa ndoto kwani hakuna maendeleo kwa watu waliotawaliwa na wakoloni. Hakuna maendeleo pia kwa watu ambao ni watumwa wa akili zao mbovu. Na kwa maana hii, tutabakia kuwa hivi milele iwapo hatukubadilika.
Kampeni za vyama vya siasa za visiwani siku hizi ni zaidi ya kashfa. Tena kashfa ambazo hazina sitaha wala hazijali nani yupo na nani hayupo. Nani namstahi na nani simstahi. Awepo mkubwa awepo mdogo, matusi ndiyo ilani na sera ya vyama vyetu vya siasa. Kampeni zetu badala ya kutuambia kuhusu sera za kilimo, uvuvi, na maendeleo kwa ujumla zinatumia historia ya watu waliopata vyeo kwa kupiga ama kucheza Sunsumia.
Badala ya kampeni zetu kutuambia vipi ilani zao zitaboresha elimu ambayo kwa hakika inakufa kibudu kila uchao, tunaambiwa habari za vipi kiongozi fulani alipatikana ndani ya ndoa ya mama yake na baba yake. Kwa mfano, Kiongozi wa siasa anayetaka chama chake tukipigie kura, anathubutu kumsema mtu mzima mwenzake kuwa mama yake asingemzaa kama hakutoka nje ya ndoa ya baba yake. Maneno kama haya na mengine, tumeyazoea kuyasikia katika kampeni za kwetu na cha aibu zaidi, waliopo wote wanafurahia kusikia hivyo.
Nilitarajia kuwa kampeni zetu zitazungumzia namna gani zitaboresha huduma za afya kwa wananchi. Hilo sijalisikia kamwe kwa kweli. Badala yake, nasikia kuwa kiongozi fulani anataja msururu wa viongozi anaodai ni mashoga na wengine waliouza kaburi za baba zao. Haya kweli tuseme yametendeka, lakini yanatuhusu nini sisi kama wananchi ambao tunataka maendeleo yetu na ya nchi yetu?
Itatusaidia nini sisi kujua kuwa kiongozi fulani ni shoga au alikuwa mwanachama wa Sunsumia? Hii ina mshabaha gani na maendeleo yetu? Inatusaidia nini Wazanzibari kujua eti fulani mama yake kaolewa kwa mahari ya shilingi 500 alizogaiwa na kiongozi fulani na kisha akauza kaburi la baba au mama yake?
Ukweli, yote haya hayatusaidii kitu na wala si maneno ambayo watu wenye akili timamu wanaweza kuyajadili hadharani. Pia si maneno ambayo watu wenye akili timamu wanaweza kuyafuatilia kwenye kila mikutano tena kwa kusafiri masafa kuyapigia ngoma na kofi kwa kuyafurahia, ilhali huko makwao hakuna waliloacha kutokana na nchi yao kufilisika kimaendeleo. Inashangaza sana kwa kweli kuona watu wetu bado wanashabikia vyama ambavyo vimekuwa vikipata kura kwa umahiri wao wa kutukana na sio sera za maendeleo ya kweli.
Kwa hali hivi iendavyo, sasa natilia mashaka kwa kuhoji iwapo akili zetu Wazanzibari ziko sawa ama kwa lugha nyepesi naweza kusema inaonyesha hatujatulia. Na kwa hali hii hatuwezi kupata maendeleo wala kufika popote! Tutabakia kwenda katika kampeni kufurahia matusi ya viongozi ambao wapo kwa ajili ya neema zao tu na hawana cha kutupa sisi wanyonge isipokuwa lugha ya matusi iliyotokana na kufilisika kwao kisiasa. Kufilisika ambako kunazifilisi akili zetu pia na kutufanya tuamini kuwa viongozi wajuzi wa kutukana tu ndio wanaoweza kutuletea maendeleo katika visiwa vyetu. Tubadilike wananchi.
No comments:
Post a Comment