Wednesday, July 24, 2019

MUUNGANO ULIKUWA NI WA NYERERE NA KARUME SASA NI WA SHEIN NA MAGUVULI SIO WANANCHI

Afbeeldingsresultaat voor shein na magufuliDawa pekee ya kumaliza Kero za Muungano, Wananchi wa sehemu zote mbili Tanganyika na Zanzibar, waulizwe swali moja tu kuwa: Je, wanautaka au la.
Taifa lolote duniani linafanikiwa kutokana na raia wake kuishi kwa furaha, kusikilizwa matakwa yao, siyo kuongoza kwa kulazimisha kwa mabavu na vitisho.
Miaka 55 ya Muungano ni muda mwafaka wa kuwasikiliza wananchi kuhusu Muungano, kama wanauhitaji au laa. Muungano ni hoja ya wananchi. Viongozi wanapaswa kuacha kiburi na hofu.
Picha na maelezo yalipo juu ni sehemu ya maoni kulingana na habari iliyopo chini kuhusu Kero za Muungano, amabzo sasa ni kidondandugu kisichopoa.
Imetimia miaka 55 tangu Tanganyika na Zanzibar zilipoungana, lakini muungano huo bado umekuwa na kero nyingi zinazoibua mijadala mara kwa mara.
Tangu Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume walipounganisha nchi hizi bado kulikuwa na masuala mengi yaliyohitaji ufafanuzi au kuwekwa sawa, lakini fursa hiyo haikupatikana, wala hata mijadala ya wananchi kuhusu jambo hilo haikuruhusiwa.
Ili kuthibitisha kuwepo kwa nyufa katika muungano huo, Tume kadhaa zilizoundwa na serikali ilionyesha kasoro kwenye muundo wa muungano wenye Serikali mbili. (Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar)
Tume ya Jaji Francis Nyalali iliyoundwa kuwahoji wananchi kuhusu mfumo wa vyama vingi, katika mapendekezo yake iligusia suala la muungano ikijenga hoja kwamba muundo wa serikali mbili hautekelezeki kwa mfumo wa vyama vingi.
Ilitaja masuala ya uraia, milki ya fedha za kigeni, ukusanyaji na mgawanyo wa mapato kutokana na kodi na ushuru wa forodha, tatizo la kanuni ya kuchangia gharama za uendeshaji Serikali ya Muungano.
Hata hivyo, mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali hayakufanyiwa kazi.
Mbali na Tume ya Nyalali, mwaka 1998, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa aliunde tume iliyoongozwa na Jaji Robert Kisanga, ikapeleka kwa wananchi waraka wa serikali, maarufu ‘Whitepaper’, kama ilivyokuwa kwa Tume ya Nyalali, tume hii nayo ikarudia yaleyale kuwa muundo wa serikali mbili haufai.
Ripoti ya Jaji Kisanga ilitaja kasoro za muungano zilizobaki hazirekebishiki. Maana yake ni kwamba kunahitajika mfumo wa muundo wenye kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye utakaokuwa tiba ya matatizo mbalimbali. Vilevile mapendekezo hayo hayakufanyiwa kazi.
Mbali na tume hizo mbili, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba iliibua suala la muungano kwa kupendekeza Serikali ya Shrikisho la Serikali tatu, yaani ya Shirikisho, ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku mambo ya muungano yakipunguzwa kutoka 22 hadi kubaki saba.
Sura ya kwanza ya Rasimu ya Katiba mpya iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inasema:
“1(1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo limetokana na muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, zilikuwa nchi huru. Inaendelea,
“(2) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na lisilofungamana na dini.”
“(3) Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyorejewa katika ibara ndogo ya (1), ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba hii, kwa kadri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa makubaliano hayo.”
Mvutano wa muundo wa muungano haupo kwenye muundo pekee, bali pia kero zake. Hayo ni mambo ambayo yamekuwa yakileta mijadala mikali hata bungeni.
Hivi karibuni tu mjadala huo umeibuka tena bungeni ambapo, Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea alitoa hoja bungeni akihoji lini serikali itabadilisha katiba ili kutoa ufumbuzi wa kudumu.
“Hii ni moja ya kero za muda mrefu za muungano. Sasa ninavyotaka, waseme lini huo mchakato wa kubadilisha katiba, lakini waziri anasema tutaleta, tuko kwenye majadiliano kwenye Baraza la Mawaziri,” alisema Kubenea.
Hoja ya Kubenea iliungwa mkono na Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu akisema wakati Muungano ukitimiza miaka 55 serikali imeshindwa pamoja na mambo mengine kuiruhusu Zanzibar kukopa kwenye vyombo vya kimataifa ili kutekeleza masuala ya msingi kama kufanya upanuzi wa uwanja wa ndege na bandari.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alifafanua kuhusu suala hilo akisema serikali haitekelezi ahadi zake kuhusu muungano na hivyo kuifanya isiaminike.
“Mwaka 1977, katiba ibara ya 134 ilianzisha Tume ya pamoja ya fedha. Ilichukua mpaka mwaka 1996 Serikali ya CCM kuandaa muswada wa tume hiyo ya fedha.
“Ilichukua tena muda mpaka mwaka 2013 Serikali ya CCM kuleta kanuni ya kutekeleza hiyo sheria. Mpaka sasa tume haijaanza kazi,” anasema Zitto.
Amedai kuwa uchambuzi uliofanywa na Tume ya pamoja ya Fedha, inaonyesha mapato ya muungano yanayopaswa kugawanywa kwa pande zote mbili za Muungano yanatumiwa na Tanzania Bara, Zanzibar haipati chochote.
Hata hivyo, Mbunge wa Uyui (CCM), Almasi Maige anapinga hoja hiyo akisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijazuiliwa kukopa bali hutoa tu taarifa kwa Serikali ya Muungano.
Kwa nini?
Miongoni mwa waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Awadhi Said anasema sababu ya mvutano huo kuendelea kuwepo licha ya tume zote kubainisha kasoro za Muungano, ni hofu ya CCM kushindwa uchaguzi.
“Ni matokeo ya hofu ya CCM, kwa sababu wanataka kutawala serikali zote. Wanahofu ya kushindwa uchaguzi Zanzibar,” anasema Awadhi.
Anaongeza kuwa hofu hiyo ndiyo ilisababisha ikaundwa kamati ya Jaji Mark Bomani, mwaka 1994 ambayo ilibadili muundo wa vyeo vya Muungano ambapo Rais wa Zanzibar aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais akabadilishwa na kuwekwa cheo cha mgombea mwenza ambaye huwa Makamu wa Rais, huku Rais wa Zanzibar akibaki huru.
“Waliona ingekuwaje endapo Rais wa Zanzibar atakuwa wa upinzani? Wamechukua mfumo wa Marekani wa mgombea mwenza,” anasema Awadh.
Hata hivyo, alisema Rais wa Zanzibar amefanywa kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Muungano. Lakini bado wanadhibiti uchaguzi wa Zanzibar, kwa sababu akishinda mpinzani atalazimika kuingia kwenye Baraza la Mawaziri jambo ambalo kwao ni tatizo.
“Muungano una matatizo mengi, lakini yanafichwa kwa kuhakikisha upande huu anatawala mkubwa na mwingine unatawaliwa na mdogo,” anasema Awadh.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Hebron Mwakagenda anasema suluhisho la kero za Muungano ni wananchi kudai katiba mpya.
“Suluhisho ni wananchi kudai katiba mpya. Kwa sababu katiba ni ya wananchi wenyewe. Hata Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuruhusu mchakato wa katiba ilitokana na msukumo wa wananchi na hata katiba ya sasa inasema serikali inapata mamlaka kutoka kwa wananchi,” anasema Mwakagenda.
Ameendelea kusisitiza umuhimu wananchi kudai katiba akisema viongozi wamekuwa na tabia ya kuweka katiba zinazolinda masilahi yao na si ya wananchi kwa jumla.
“Sisi wananchi ndiyo tunataka katiba mpya. Katiba siyo ya kiongozi, kwa hiyo tuendelee kudai mpaka ipatikane,” anasema Mwakagenda.

No comments:

Post a Comment