Thursday, April 5, 2012

WAZANZIBAR TUSHIKANE SOTE NA JUMUIA YA UAMSHO NDIO NCHI YETU ITAKUWA HURU SOTE TUSIGAWIKE VIKUNDI VIKUNDI SOTE TUWE KTK UAMSHO


Wazanzibari wana haki ya kuujadili Muungano



Viongozi wa dini wakiwa katika kongamano la kujadili khatma ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Labda leo makala hii ivunje ukimya juu ya hali ya kisiasa inayoendelea hivi sasa hapa Zanzibar, maana vyombo vya habari vyote vya Tanzania vimefanya kama kwamba hakuna kilichopo, yaani mambo kama kawaida. Kwa hakika mambo si kama kawaida. Kuna harakati nyingi na ziko wazi kabisa ambazo zinafaa kuandikiwa kwa sababu ni kwa kuandikiwa ndio zitajulikana lakini si kujulikana tu ila hata kufanyiwa uchambuzi.
Hali ya kisiasa ya sasa ya Zanzibar inatokana na kukaribia au kuelekea kwenye mchakato wa Katiba ya Muungano ya Tanzania kuridhi matakwa ya Sheria Namba 8 ya 2011 ambapo imetandika misingi ya Watanzania kujadili Muungano ikiwa ni miaka 48 tokea ulipoasisiwa.
Harakati zinazoendelea zimo au zinatarajiwa kuwemo ndani ya wigo wa kuelimisha umma juu ya mchakato ujao, lakini kwa kiasi kikubwa zimechukua mkondo mkubwa zaidi pengine hata ambao haukuwa ukitarajiwa.
Kwa busara kubwa Serikali ya Zanzibar imeruhusu mjadala huo kuendelea ili kutoa fursa ya Kikatiba kwa watu kutoa maoni yao, na kwa sababu hakuna fujo zozote zilizotokea hadi sasa, ukitoa kauli zisopendeza, basi mambo yamekuwa yakishika kasi.
Kuna taasisi tatu ambazo zimekuwa zikiendesha elimu ya umma kuhusu mchakato huo ujao, ambazo zote zina mitizamo tofauti, zina hadhira tofauti na kwa hivyo zina mbinu tofauti na zina malengo ya mwisho tofauti.
Kuna Jumuia ya Taasisi Ziso za Serikali za Mkoa Mjini Magharibi UWECSONET ambayo wao wanatoa elimu ya uraia kama ilivyo katika kitabu kwa kuwapitisha wadau wake kwenye vipengele vya sheria na hawafiki kutoa suluhisho lolote juu ya Muugano.
Pili ni Jumuia ya Taasisi za Kiislamu, lakini wakiongozwa na Jumuia ya Uamsho na Jumuia ya Maimamu ambao wao mtizamo wa ni kuwa miaka 48 ya Muungano imetosha na hakuna haja ya kuendelea nao na uvunjike halan, kwa msimamo wao.
Kisha kuna Baraza la Katiba ambalo linachukulia suala zima katika mizani ya Sheria na Katiba na wao mtizamo wao ni kuelekea kujaribu kutoa suluhu ya nne kwa kuona kuwa mfumo wa sasa wa Serikali mbili haukuuvusha Muungano, wa Serikali moja hautakiwi na wa Serikali Tatu hautaweza kuipatia Zanzibar utaifa (sovereignty) na kwa hivyo wamekuja na dhana ya Muungano wa Mkataba ( Treaty Union) badala ya Muungano wa Katiba ( Constitutional Union) kama ilivyo hivi sasa.
Pia lipo kundi la vijana wengi wakiwa ni wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wao pia ni kama Uamsho wanataka Muungano uvunjike kama leo, na wito wao unabebwa na bango lenye anuani ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Kwanza.
Mjadala unaokuja unataka wananchi wajadili kuimarisha Muungano, kama zilivyo hadidu rejea katika Sheria Namba 8, ambayo itaunda Tume ya Kukusanya Maoni, na kwa sababu ya hilo ndipo harakati za kisiasa za Zanzibar zimejikita katika nukta hiyo.
Hoja iliyopo kwa walioingia katika mjadala na wafuasi wao hasa Uamsho, ni kuwa si haki wala si vyema kabisa kubana mjadala wa Katiba kuwa ujikite kwenye kuimarisha Muungano, ambapo hadi sasa kuimairisha kumekuwa ni kuongeza mambo ya Muungano na sio kupunguza.
Hadi leo, wanadai kuna maeneo mengi ambayo yamo kwenye Muungano lakini hayatekelezeki au yamemaliza kazi yake na kwa hivyo yanapaswa kutolewa katika Mambo ya Muungano na kurudishwa ndani ya mamlaka ya Zanzibar, lakini hilo halijawahi kufanywa wala jaribio lake halijatokea.
Baraza la Katiba na Uamsho wameeleza kuwa wanaelewa vipengele vinavyofunga kuwepo mjadala wa aina hiyo na pia vipengele vinavyobana Tume ya Maoni ijayo kwa vile hadidu rejea ziliopo hazitatoa nafasi ya kubadili mfumo wa Muungano seuze mabadiliko makubwa kama wanayotizama Uamsho ya kuvunja Muungano au ya Baraza la Katiba ya Muugano wa Mkataba ambao utaiwezesha Zanzibar kuwa mwanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki na jumuia nyengine zote za kimataifa.
Pia wadau wa mtizamo huo wameeleza wasiwasi wao iwapo Tume ya Maoni itaruhusu kuwepo maoni aina hiyo katika vikao vyake na wananchi hapa Zanzibar. Wanasema itawezekana kabisa mambo mawili kutokea watu watapoenda katika kutoa maoni yao.
Ama watafukuzwa katika kikao kwa kuwa watakuwa wakisema kitu ambacho Tume haikutumwa kukisikiliza kwa kuwa itasema haina mamlaka ya kufanya hivyo, lakini pili inawezekana kabisa ikasikiliza lakini hatimae maoni kama hayo yasiwemo kwenye majumuisho yao.
Baya zaidi wanasema ni kuwa inawezekana Tume ikajumuisha maoni hayo ya kutaka ama Muungano uvunjike au usonge mbele katika mfumo mpya, lakini maoni hayo yakifika kwa Rais yatapuuzwa kama yalivyopuuzwa majumuisho ya Jaji Robert Kisanga kwa kuambiwa kuwa amefanya jambo nje ya hadidu rejea ilizopewa kamati yake.
Kwa sababu hiyo basi Jumuia ya Uamsho ina msimamo kuwa hakuna haja ya kuingia katika mchakato wa katiba kwa sababu ni maoni yanayohitajika tu ndio ambayo yatolewe lakini mengine yote yakiwemo ya kutaka Muungano usite, iwapo kutakuwa na ridhaa, yasizingatiwe kabisa.
Pia kuna wasi wasi unaolezwa kuwa kumekuwa na utamaduni mdogo wa Serikali za Kiafrika, Tanzania ikiwemo kuheshimu maoni ya Tume kama hizi na kwa hivyo fikra iliopo kuwa mchakato mzima ni upotezaji wa fedha na wakati.
Hoja nyengine mbili zinatolewa. Moja ni ile ya kuwa ili kuepuka gharama na kupoteza muda basi ingekuwa vyema kwa kwanza kutishwa Kura ya Maoni kwa Wazanzibari, ambayo wanayo sheria hiyo, kuulizwa iwapo wanaotaka au la Muungano uliopo hivi sasa halafu ndio kuendelea na mchakato.
Hilo wanataka lifanywe na Serikali ya Zanzibar lakini hapana dalili kuwa litaweza kutokea maana kimya kimetanda na kura kama hiyo inaweza kuitishwa na Rais au Baraza la Wawakilishi kumshauri Rais.
Kuna hoja pia Sheria Namba 8 kama ilivyo hivi sasa ikianza kazi basi ni batili na haramu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar. Imeelezwa wazi kuwa Sheria yoyote inayotengenezwa na Bunge kwa maeneo ya Muungano ili ifanye kazi Zanzibar lazima iwasilishwe katika Baraza la Wawakilishi na Waziri anaehusika, lakini hadi leo jambo hilo halijafanywa.
Kwa sababu hiyo basi pia Uamsho imekuwa ikipiga vita ushiriki wa Wazanzibari katika Tume ya Maoni ijayo ikisema wasiingie humo kwa ajili ya kutafuta kipato ilhali wanajua kuwa Tume hiyo haitaweza kwa hakika kulinda maslahi ya Wazanzibari.
Kama kawaida ya Zanzibar kuna kundi kubwa la Wazanzibari ambalo limenyamaza kimya likitizama hali inakwendaje. Kundi hili ni muhimu ingawa kwa sasa halisemi chochote lakini naamini kila mtu kwenye kundi hili yumo kutafakari na baada ya muda mitizamo na misimamo yao itajulikana.
Kwa sasa pongezi kwa Serikali ya Zanzibar kuachia kushamiri mawazo huru ambayo baadae yatajichuja na kutulia na kujua wapi yanaelekea. Naamini mchakato wa katiba ujao utaendelezwa kwa njia ambayo kila wazo litachukuliwa, kila wazo litapewa nafasi ya ushawishi na hatimae wengi watakubaliwa, wachache wataheshimiwa na matakwa ya umma yatakuwa ndio mbele na maslahi ya nchi yatajikita katika mizani.

No comments:

Post a Comment