Wakati umefika kwa vijana wa Kizanzibar wenye uchungu wa Nchi yao kujitolea kwa hali na mali kupigania Visiwa vyao kutoka katika makucha ya Wakoloni. Ni dhahiri kwamba Zanzibar kama Zanzibar kwa kupitia Serikali yake ya Mapinduzi imeshindwa kuwaongoza Wazanzibar na matokeo yake kila siku Zanzibar inapoteza kila kilicho chake, na huku Wazanzibar wakizidi kudidimia na hali ya maisha kuzidi kuwa ngumu kila uchao. Hii yote inatokana na sisi Wazanzibar kuvishwa koti bovu la kaniki na Watanganyika, huku baadhi ya vibaraka Zanzibar wakivishwa vilemba vya ukoka vyenye madaraka ya uongo kupitia mwavuli wa Muungano.
Zanzibar sio Nchi tena ya kuongozwa na Baraza la Mapinduzi, kwani hata hao wanaojiita Wanamapinduzi basi hawapo tena na hao waliobakia basi hoi bin taaban na hawana muelekeo wowote ule wa kimaendeleo isipokuwa hisia zao ni zakibaguzi, umimi,uonevu na muelekeo wao ni ule ule kwamba tumepindua au wazee wetu walipindua. Kimsingi Zanzibar inahitaji damu mpya ya vijana wenye uchungu, hisia na ”vision” ya kuongoza Taifa lao.Vijana hao tunao lakini Wanamapinduzi hawa wanashindwa kuwapa nafasi kwa kuogopea maslahi yao. Hawana budi kuelewa kwamba kwa sasa itikadi zao zimeshapitiwa na wakati hawana budi kulijua hilo na kulifanyia kazi.
Leo hii Wazanzibar wengi wamekuwa wakitowa lawama kila kona na pembe ya dunia, lakini ukiangalia utagundua kwamba kelele za mlango hazimfanyi mwenye nyumba yake ashindwe kupata usingizi. Jee sisi kama Wazanzibar hatua gani tumezichukua ambazo watawala wetu watatuelewa kwamba tumechoshwa na utawala na ubeberu wao ? Sisi hatuishi kwa raha takriban nusu karne sasa, kama ni hivyo kwa nini na wao waishi kwa raha huku tulio Wengi kwenye Nchi yetu tukiumia ! hilo haliwezekani hapana budi kukaa kitako na tukalifanyia kazi suala hili.
Watawala wetu wana kila mbinu za kuzima kelele zetu kwani wao wanafaidi matunda ya nchi yetu kwa maana hiyo kuitoa keki midomoni mwao hicho sio kitu rahisi, kunahitajika mbinu na ikibidi hata vita basi wako tayari kwa hilo.Kiufupi watawala wetu hawajali hali zetu wala matatizo yetu, maslahi yao ndio kitu wanachojali na sivyenginevyo.Na usifikiriwe ya kwamba kama hatukujitolea kwa hali na mali Wanamapinduzi hawa watabadilika la hasha, hawa lazima tuwapindue kama walivyoipindua Zanzibar lakini kwa njia ya demokrasia sio ile fitna ya mauaji.
Wanamapinduzi hawa wameshindwa kuongoza Serikali kwani hawa ni vibaraka ambao wanafanya kazi ya kuikandamiza Zanzibar chini ya mwevuli wa Muungano unaongozwa na Serikali ya Tanganyika. Ukiangalia na kulifanyia uchunguzi suala hili utagundua hawa wote wanaojitia umapinduzi basi ni watu wenye asili ya kutoka bara, ama wazee wao walikuja hapa Zanzibar kutafuta maisha au ni mashushushu ambao walipandikizwa na Mwalim Julius Nyerere kuja Zanzibar kwa kazi maalum. Ndio hawa sasa hivi wanaojiita Wazanzibar halisi lakini kama hilo halitoshi basi watu hawa ndio wanaojifanya kwamba wana haki zaidi Zanzibar kuliko mtu yeyote hapa Visiwani.
Sasa wakati umefika kwa Wazanzibar kuacha porojo na malumbano kwenye mitandao na magazeti ya mitaani. Chamsingi kabisa ni kwa vijana wa Kizanzibar popote pale walipo duniani kujikusanya pamoja na kuunda makundi maalum ambayo yatandaa mikakati ya kudai Nchi yetu kwa njia yeyote ile.Kinyume na hapo tutakuwa tunajidanganya na vilio vyetu vitaishia kwenye kapu Dodoma. Wazanzibar tusidanganyike sana na Katiba kwani hawa Watanganyika sio wapumbavu kama Wazanzibar, tayari wameshajipanga vyakutosha ni vipi wataipitisha katiba hii na wapi watawamaliza Wazanzibar, katika hili lazima tuwe wa kweli na mipango madhubuti ipangwe ili tupambane kuipigania Nchi yetu, ikumbukwe kwamba siku zote umoja ni nguvu.
Hatuna budi tuangalie kwa undani kabisa, hivi inaingia akilini kwa Jumuia ambayo sio ya kiserikali kulivalia njuga suala la katiba huku Serikali ya Mapinduzi ambayo ndio mdau mkubwa wa suala hili ikiwa kimya, Wazalendo wenzengu hapo pana Katiba au tunadanganyana ? Nilifikiria kwamba Serikali ya Mapinduzi ndio itowe muongozo na Elimu kwa Wananchi wake lakini hilo halionekani kila mmoja analinda maslahi yake asije akabadilishwa Wizara, sasa kweli tutafika na tupate Katiba itakayotukomboa Wazanzibar ?
No comments:
Post a Comment