Wednesday, April 18, 2012

WASOMI NA VIONGOZI MUHIMU ALIYO WAUWA MZEE KARUME NA KUFA KWAKE.

MZEE KARUMA NA MAUWAJI YAKE YA VIONGOZI NA WASOME NCHINI Z,BAR NA KULAZIMISHA KUOLEWA BINTI ZA WATU KWA LAZIMA ATI ANAONDOSHA UBAGUZI

Miaka 40 iliyopita, Aprili 7, 1972; Rais wa Serikali ya awamu ya kwanza ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abeid Amani Karume, aliuawa kwa kupigwa risasi katika mazingira na sababu za kutatanisha.
Risasi nane zilitolewa mwilini kwake mwili wake ulipofikishwa kwenye Hospitali ya V. I. Lemin, mjini Unguja kwa uchunguzi, sawa na idadi ya miaka minane ya utawala wake tangu 1964 hadi kifo chake.
Ilikuwa hivi: Rais Karume na Makomredi wenzake wa Chama cha Afro-Shirazi (ASP) alikuwa na mazoea ya kucheza karata, damma au dhumuna kwenye ukumbi wa ofisi za makao makuu ya Chama hicho Kisiwandui, kila jioni kama sehemu ya mapumziko. Siku hiyo alifika saa 11.00 jioni akiwa na walinzi wake, akaingia ndani nao wakabaki nje kulinda.Ikafika zamu yake kucheza; akawa anacheza na Mzee Maalim Shaha Kombo ambaye alionekana kulemewa. Ndipo Karume akamwita Mzee Mtoro Rehani ajitayarishe baada ya Kombo, naye akaitikia kwa kuaga kwanza aende msalani kujisaidia.Sekunde chache baada ya hapo na kabla Mzee Mtoro Rehani hajarejea kutoka msalani, ghafla watu wawili wenye silaha walivamia chumba alimokuwa Karume na wenzake na kumimina risasi wakimlenga; na kufumba na kufumbua, akawa katika dimbwi la damu kimya, amepoteza uhai. Hakuna mtu mwingine aliyeuawa mbali na kujeruhiwa tu, mmoja wao akiwa Katibu Mkuu wa ASP, (sasa) Hayati Thabit Kombo Jecha.Risasi uaji (the fatal bullet), mbali ya risasi zote, iliyochukua uhai wa Karume ilitoka kwenye bunduki ya Luteni Hamoud Mohammed Hamoud wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT), ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa uvamizi huu na aliyefyatua risasi ya kwanza wakati Karume akicheza na wenzake. Inasemekana, Hamoud aliuawa papo hapo na mlinzi wa Karume.Wauaji wengine waliofuatana na Hamoud katika uvamizi huo ni Kapteni Ahmada Mohamed, Koplo mmoja wa jeshi ambaye jina lake halijafahamika hadi leo, na raia mmoja aliyekwenda kwa jina la Ali Khatibu Chwaya, ambao inaelezwa wote hao waliuawa kwenye mapambano ya silaha nje ya eneo la tukio.Dakika chache baada ya mauaji kutokea, alifika Kanali Ali Mahfoudhi na askari mwingine, Kapteni Makame Hamis, wakauchukua mwili wa Karume na kuukimbiza hospitali.Itakumbukwa, Kanali Mahfoudhi ni mmoja wa vijana wa Umma Party (UP) cha Abdulrahman Mohamed Babu, kilichoungana na ASP baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kuunda Serikali ya mseto. Ni kati ya vijana waliopelekwa Cuba kwa mafunzo ya kijeshi, na ni mmoja wa wapiganaji walioendesha mapambano ya kisayansi usiku wa Mapinduzi na kukamata uwanja wa ndege mchana Aprili, 1972.Ni mmoja wa wanaharakati wa siasa za mrengo wa Kikomunisti ambao hawakutakiwa Zanzibar wakati wa utawala wa Karume, hivi kwamba kufuatia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, 1964, Karume alishinikiza kwa Nyerere wapewe kazi Tanzania Bara aweze “kupumua” ambapo Mahfoudhi alipewa cheo cha Mkurugenzi wa Operesheni katika JWT.Wengine ambao hawakutakiwa ni pamoja na Babu mwenyewe aliyepewa Uwaziri wa Mipango ya Uchumi, na kama tulivyoona makala zilizopita, hasimu mwingine wa Karume, Othman Sharrif, ambaye alifanywa Afisa Mifugo wa Mkoa, Mtwara au Mbeya, na Balozi Salim Ahmed Salim wakati huo Balozi wa Zanzibar nchini Misri ikaridhiwa aendelee kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano nchini humo.
Tuache hayo, lakini hapa swali linazuka: Kwa kuwa Kanali Mahfoudh hakuwa kipenzi cha utawala wa Karume tangu mwaka 1964, ilikuwaje akawa Afisa wa kwanza kuwa kwenye tukio kabla ya maafisa wengine vipenzi, kama vile Kanali Seif Bakari ambaye alikuwa pia Mkuu wa Usalama wa Taifa Zanzibar ambalo halikuwa jambo la Muungano, na wengineo?Je, alikuwa katika ziara ya kikazi wakati mkasa huu ukitokea au alijua kilichotarajiwa kutokea? Kwa nini alikuwa mmoja wa washitakiwa zaidi ya 100 kwa tuhuma za mauaji hayo, na mmoja wa watuhumiwa 18 miongoni mwa hao walioshitakiwa wakiwa Tanzania Bara, Abdulrahman Babu akiwa mmoja wao.Kuna dhana mbili kinzani kuhusu jinsi Karume alivyouawa na hatima ya wauaji. Dhana moja inadai kwamba, watu wanne walivamia mahali alipokuwa Karume na wenzake, wakamimina risasi mara nne au mara tano hivi, risasi ya kifo ikampata Karume shingoni akafa, huku zingine zikiendelea kumiminwa kulenga meza walipokuwa.Inadaiwa kuwa Hamoud aliuawa kwenye eneo la tukio, ambapo wawili waliuawa baadaye na vyombo vya usalama (kwa mapambano?) na mmoja alijiua.Dhana ya pili inadai kwamba Hamoud alikufa kwenye eneo la tukio katika mazingira ya kutatanisha, ama kwa kujipiga risasi kuepuka kukamatwa hai na kuteswa baada ya kuona asingeweza kutoroka; au alijeruhiwa vibaya na walinzi wa Karume, kisha Ahmada akampiga risasi na kumuua kumwepusha kuteswa na kutoa siri kama angekamatwa hai, kisha (Ahmada) akaweza kutoroka kwenye eneo la tukio.
Juu ya utata huu kuhusu hatima ya wauaji, ni ukweli kwamba ni Luteni Hamoud pekee aliyeuawa kwenye eneo la tukio na washiriki wengine katika mauaji waliweza kutoroka eneo la tukio na baadaye kuuawa katika mazingira yasiyofahamika.Kufuatia mauaji hayo, watu 1,100 walikamatwa na kuhojiwa juu ya kuhusika au kutohusika kwao na mauaji, wengi wakiwa viongozi na wanachama wa zamani wa Umma Party, chama cha Babu na wanachama mashuhuri wa ASP wenye siasa za mrengo wa kikomunisti.Yote haya yanaturejesha kwenye swali letu la awali: je, kuuawa kwa Karume kulikuwa na lengo la kulipiza kisasi kwa chuki binafsi, kama baadhi ya watu wanavyodai, au lilikuwa jaribio la Mapinduzi lililoshindwa kwa Serikali ya Mapinduzi? Ni nani huyu Luteni Hamoud Hamoud aliyeongoza mauaji na kwa nini?Je, lengo lilikuwa ni mauaji hayo pekee au kulikuwa na mpango mkubwa zaidi nyuma? Ukiongozwa na nani?Kupata majibu ya maswali haya, hatuna budi kuiangalia hali ya kisiasa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na baada ya Muungano na Tanganyika, Aprili 26, 1964.Kama nilivyoeleza katika mfululizo wa makala nne hivi karibuni katika gazeti hili kuhusu jinsi “Field Marshal” John Okello alivyoongoza Mapinduzi ya 1964, na kuundwa kwa Serikali ya Mseto kati ya vyama vya ASP na Umma, lengo kuu la Karume lilikuwa ni kuzivunja nguvu za wanaharakati wa Umma Party na za wakomunisti wa ASP walioshabihiana kimawazo na kimtazamo wa kitaifa na wana-Umma Party na kumnyima Karume usingizi.Lakini tofauti na matarajio ya Karume, hatua hiyo iliwaleta karibu zaidi wanamapinduzi hao na kumnyima zaidi usingizi kwa hofu ya kupinduliwa, wakimtuhumu kushindwa kuongoza na kusimamia madhumuni ya Mapinduzi Visiwani.Mungu bariki kwa Karume, ukatokea Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika mwaka huo, akaona vyema awasambaratishe kwa kuwatafutia nafasi Tanzania Bara ambako wasingeweza kufurukuta.Waliokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na Abdulrahman Babu (Umma) na aliyepewa Uwaziri wa Mipango na Uchumi kwenye Serikali ya Muungano; Kassim Hanga (ASP) aliyeteuliwa Waziri katika Ofisi ya Rais wa Jamhuri, Mambo ya Muungano; Salim Ahmed Salim (Umma) aliyeteuliwa Balozi nchini Misri.Wengine ni Othman Sharrif (ASP) aliyeteuliwa Balozi nchini Marekani, lakini Karume akampinga Nyerere akidai hastahili, uteuzi ukafutwa; badala yake akateuliwa kuwa afisa mifugo katika moja ya mikoa ya Kusini Tanzania, Mbeya au Mtwara, na Kanali Ali Mahfoudh (Umma) aliyeteuliwa Mkurugenzi wa Operesheni katika Jeshi la Wananchi (JWT), na wengineo.Kwa wale wenye maoni tofauti na ya kukosoa Serikali waliobaki Visiwani, hasira ya Karume aliyetawala kwa mkono wa damu iliwashukia, wengi walikamatwa na kutiwa kizuizini na pengine kupoteza au kuuwawa kikatili na katika mazingira ya kutatanisha. Mmoja ya waliouawa kikatili kizuizini ni Mzee (mwanaharakati) Mohamed Hamoud, baba yake Luteni Hamoud Mohamed muuaji wa Karume.Tangu Mapinduzi ya Januari 12, 1964, Zanzibar haikuwa na Katiba wala Sheria; iliongozwa kwa Amri za Rais (Presidential Decrees) kadri alivyoona inafaa. Na kwa mujibu wa Gazeti la “The Tanganyika Standard” la March 9, 1968, Karume aliapa kutofanya uchaguzi wala kuwa na Katiba Kisiwani kwa miaka 50 tangu 1964 – 2014 Kwa madai kwamba “chaguzi zote ni vyombo vya mabeberu kuwakandamiza wananchi”.Na kadiri kalamu ya Karume ya wino wa damu ilipozidi kuandika historia ya ukatili, udikteta na umwagaji damu kwenye kurasa ngumu za kukwaruza ndivyo alivyojichongea na kujiongezea upinzani na uadui kwa jamii ya Kizanzibari.Kufikia mwaka 1967 hofu ya Karume dhidi ya wenzake na kwa nafasi yake ilitia fora kiasi cha kuogopa kivuli chake mwenyewe. Na ili kuendelea kuwamaliza wenzake, mwaka huo zilitungwa tuhuma za uongo dhidi ya watu 14 makada wa ASP katika kumpindua, zikiwalenga hasa wenye fikra za kikomunisti.Walioingizwa kwenye tuhuma hizo ni pamoja na mawaziri wa Serikali yake mabwana Abdallah Kassim Hanga, Salehe Saadallah Akida, Abdul Aziz Twala na makatibu wakuu wa wizara, Aboud Nadhif na Mdungi Ussi na baadaye Othman Sharrif.Wote waliokuwa Visiwani walikamatwa, kisha Karume akamwomba Nyerere kuwarejesha Zanzibar kutoka Bara, Othman Sharrif na Hanga ili “wakahojiwe” lakini wote wakaishia kuuawa kikatili bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.Mmoja wa mashahidi wa uongo walioandaliwa dhidi ya “watuhumiwa” kwa vyombo vya Karume, alikuwa Ahmada ambaye kwa uongo wake, watu wanne akiwamo Hanga, Twala, Saadallah na Othman, walinyongwa mwaka 1969. Kwa uongo huo, Ahmada alizawadiwa cheo cha kapteni jeshini. Ni Kapteni Ahmada huyu, aliyeshiriki kwenye mauaji ya Karume miaka mitatu baadaye.Kwa hofu ya jamii ya Kizanzibari kufikiwa na fikra na mawazo mapya ya kimaendeleo, Karume alipiga marufuku vijana wa Kizanzibari kwenda nje kwa masomo ya juu ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam; alipiga marufuku pia ujenzi wa Chuo Kikuu Visiwani.Mbali na kutokuwapo kwa utawala wa sheria enzi za Karume, unyanyasaji wa kijinsia na ubaguzi kwa misingi ya historia na kisiasa ulitia fora. Kwa mfano, mwaka 1966, alitoa amri (decree) kuwanyima wazazi haki ya kuwakataa wanaume walioposa binti zao kama njia ya kuondoa ubaguzi wa rangi.Kwa sababu hii, wasichana, hasa wale wa Kiarabu walilazimishwa kwa nguvu ya Serikali kuolewa kwa nguvu. Karume mwenyewe, wakati huo akiwa na umri wa miaka 65, aliwania kuoa kwa nguvu, wasichana wanne wa Kiajemi, na alipokataliwa, aliamrisha wazazi wao watiwe kizuizini na kuchapwa viboko kwa kosa la kuzuia mpango wa ndoa mchanganyiko, na baadaye kutimuliwa Zanzibar.
Chini ya mpango huo, raia wa kigeni waliotaka kuchumbia wasichana wa Kizanzibari walitakiwa kuilipa Serikali Sh. 64,000,000, bila hivyo hawakuruhusiwa kuwaoa.Karume alikuwa ameanza kuwa mwiba kwa Mwalimu Nyerere pia juu ya Muungano. Kwa mfano, alimkatalia Nyerere kwa lugha ya dharau na kejeli juu ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha kutumika Zanzibar.Na kuhusu akiba ya fedha za kigeni ya Zanzibar iliyofikia dola milioni 80 mwaka 1972, alimuonya asithubutu kuitolea macho,akamwambia: “Fedha ya kichwa cha Malkia si yako na usiniulize, labda niulize juu ya hii (sh.) yenye picha ya kichwa chako”.Na kuhusu Muungano, Karume alikuwa ameanza kuchoka nao. Siku moja alisema, “Muungano ni kama koti tu; likikubana unalivua”.Ufa huu kati ya viongozi hao wawili juu ya Muungano, ndio uliosababisha kamati ya kupendekeza Katiba (Constitutional Committee) isiundwe na Bunge la Katiba (Constitutional assembly) lisiteuliwe ndani ya muda wa mwaka mmoja tangu Muungano, kama ilivyotakiwa chini ya Mkataba wa Muungano wa Sheria ya Muungano ya 1964.Wadadisi wa mambo ya siasa wanakubaliana kuwa, kama Karume angeendelea kutawala miaka kadhaa baada ya 1972, Muungano ungefikia kikomo kwa njia ya kutisha na kusikitisha.Kufikia mwaka 1972, upinzani kwa Serikali ya Karume ulikuwa umechukua harakati za uasi wa umma, chini kwa chini kwa mara ya kwanza tangu Hanga na wenzake wanyongwe mwaka 1969.

No comments:

Post a Comment