Sunday, August 12, 2012

MAALIM ANZAA KULIKORONGA NA KUHIMIZA WATU KUIKUBALI SENSA AHH MAALIM WEE AH MAALIM WEE BADO TU HUJAMKAA..?


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika sensa ya watu na makaazi, ili kuirahishia serikali kupanga mipango yake ya maendeleo kwa uhakika.
Maalim Seif ametoa wito huo leo katika ukumbi wa chuo cha Benjamin Mkapa Wete Pemba alipokuwa akizungumza na viongozi wa CUF kwa ngazi za Wilaya na Majimbo.
Amesema Sensa ya watu na Makaazi ni muhimu kwa wananchi na serikali kwa ujumla katika kutathmini na kuandaa mipango yake ya maendeleo kwa wananchi, na kuwataka kuachana na mtazamo kuwa suala hilo linaihusu serikali pekee.
Makamu wa Kwanza wa Rais ametoa msimamo huo kufuatia wananchi wengi wa Kisiwa cha Pemba kuwa na mtazamo wa kutaka kususia suala la sensa kwa madai kuwa hawakushirikishwa ipasavyo katika suala hilo.
Sababu nyengine iliyowafanya wananchi hao kutaka kususia suala hilo ni kwa madai kuwa hawawezi kushiriki suala la sensa, huku wakiwa bado hawajatekelezewa haki zao za kisheria ikiwemo kutopewa vitambulisho vya uzanzibari ukaazi.
Amewataka wananchi kupima faida na hasara za kushiriki kwenye zoezi hilo la sensa, na hatimaye waweze kushiriki kikamilifu kwa maslahi ya maendeleo ya nchi.
Akizungumzia kuhusu mchakato wa ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya mabadiliko ya katiba, Maalim Seif amewataka wananchi kuwa huru kutoa maoni yao, na kwamba hakuna atakayeadhibiwa kwa sababu ya kutoa maoni. “Mimi najua wapo wanaotaka serikali moja, wengine mbili, tatu, nne, na muungano wa mkataba, lakini wengine wanataka waachiwe wapumuwe.
Yote hayo ni maoni na kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake bila ya kulazimishwa, kwa hivyo wakati wenu ukifika nendeni mkatiwe maoni hayo kwa uwazi”, alisisitiza Maalim Seif.
Amesema lengo la serikali ya Tanzania ni kuwa na katiba mpya ifikapo April mwaka 2014, na kufahamisha kuwa kwa Wazanzibari suala kubwa linalowagusa kwenye mabadiliko hayo ni suala la Muungano. “Zanzibar tunayo katiba yetu ambayo imejitosheleza kwa mambo yetu ya Zanzibar, lakini suala kubwa kwenye mabadiliko hayo kwetu sisi litakuwa ni la Muungano, na hili haliwezi kuepukwa”, alibainisha.
Amesema Zanzibar kabla ya Muungano ilikuwa nchi huru iliyokuwa na kiti chake katika Umoja wa Mataifa, na kuelezea haja ya kuwepo kwa Mamlaka kamili ya Zanzibar ili iweze kurejesha kiti chake kwenye umoja huo.
Amewataka wananchi kuangalia maslahi ya nchi yao kwanza katika mchakato wa kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba, na kuachana na misimamo ya vyama katika suala hili linalohusu maslahi ya nchi. “Katiba ya nchi ni mali ya wananchi sio ya chama chochote, lakini najua kila chama kina katiba yake na hiyo ndio itabakia kuwa katiba na muongozo wa chama husika, kwa hivyo ndugu zangu naomba tulifahamu hili na tuangalie maslahi ya nchi yetu kwanza”, alifahamisha.
Makamu wa Kwanza wa Rais alitumia fursa hiyo kutoa mkono wa pole kwa wananchi walioathirika kutokana na ajali mbaya ya boti ya Mv. Skagit ilisababisha vifo vya watu kadhaa.
Amewataka wananchi kuweka imani zao kuwa suala hilo limetokana na mipango ya Mwenyezi Mungu, na kwamba hakuna mtu angeweza kulizuia lisitokee. Katika hatua nyengine Maalim Seif amempongeza aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasilino Mhe. Hamad Massoud Hamad kutokana na kitendo chake cha kijasiri cha kuamua kujiuzulu nafasi hiyo.
Amesema kitendo hicho cha kuwajibika kisiasa kimemjengea heshima yeye mwenyewe, chama chake na taifa kwa ujumla, kitendo ambacho linapaswa kuingwa na viongozi wengine wa nchi iwapo litatokea jambo lolote linalogusa maslahi ya wananchi. “Mhe. Hamad amekuwa mwalimu wa viongozi wa Afrika, kwani viongozi wa Afrika hawana utamauni huo hata likitokea jambo gani, lakini yeye ameamua kujisafisha licha ya kuwa hakuwa na kosa kwa sababu safari ili haikuanzia Zanzibar”, alifahamisha Maalim Seif
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Ole Mhe. Hamad Massoud Hamad ambaye alikuwa akishikilia nafasi hiyo ya uwaziri, amesema aliamua kuachia nafasi hiyo siku chache baada ya tukio, ili kujijengea heshima kisiasa. “Niliamua kujiuzulu nafasi ile kwa nia njema, sikulazimishwa wala kupokea shinikizo kutoka kwa mtu yoyote”, alisema Hamad Massoud.
Alisema kwa sasa akiwa Mwakilishi wa wananchi na kiongozi wa chama hicho, ataendelea kushirikiana na viongozi na wanachama katika kukijenga zaidi chama hicho ili kiweze kufikia malengo yake iliyojiwekea.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais aliwataka wananchi wa kisiwa cha Pemba kuendeleza utamaduni wa kufutari kwa pamoja ili kuongeza upendo miongoni mwao.
Maalim Seif alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti baada ya kushiriki katika futari ya pamoja aliyoiandaa kwa wananchi wa mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba iliyofanyika Ukumbi wa kiwanda cha makonyo Wawi na viwanja vya Ikulu ya Wete.

No comments:

Post a Comment