NILIONA ni vyema kwenda nchini Zanzibar kuwatembelea baada ya siku nyingi sana. Matumaini yangu yalikuwa pia kupata wasaa wa kutathmini hali ya hewa baada ya Uchaguzi wa Marejeo uliofanyika tarehe 20 Machi 2016. Huenda nilikuwa nimeshawishika na mijadala iliyokuwa ikifanyika nchini na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) hivyo nilipopata fursa ya kuzungumza na watu kadhaa waliojipambanua kuwa ni Wazanzibari nikaona vyema niwadadisi juu ya mategemeo waliyonayo juu ya awamu ya pili ya Shein. Wazungumzaji wenzangu walikuwa saba; wanaume wanne na wanawake watatu. Bila ya kupoteza muda wakaniweka sawa. Aliyeonekana kama ndiye ‘nahodha’ wao akataka kuweka jambo moja sawa. “Tumekuwa tunasikiliza vyombo vya habari na kusoma makala nyingi. Tunashangazwa kuwa wengi wametekwa na hii dhana kuwa Zanzibar ni mfungwa wa historia yake. “Eti kuwa siasa za vyama ambavyo vimekuwa muflisi karibu nusu karne bado vimegubika mioyo na fikra ya kizazi kikubwa cha wapiga kura ambao wamekulia chini ya mfumo wa chama kimoja au vyama vilivyoanizshwa miaka ya tisini. Mtizamo huu si sahihi”, alitahadharisha. Mchangiaji mwengine wa makamo alikubaliana na kauli yake na akaongezea, “Chama Cha Mapinduzi na Chama cha Wananchi wametufikisha hapa. Leo siasa za Zanzibar ni sawa na ushabiki wa vyama vya mpira au ushabiki uliokuwepo kati ya vikundi vya taarabu enzi za nyuma. “Utaifa ama utambulisho wa Uzanzibari umefifia, umewekwa pembeni kabisa”, alilalama. Nikataka kujua baada ya kipindi kirefu cha utata juu ya mustakabali wa Zanzibar kisiasa wana matarajio gani kwa serikali inayoingia madarakani?
Wakizungumza kwa hamasa kubwa walikaribisha fursa ya kumpelekea Rais wa Zanzibar salamu juu ya masuala ya kuyazingatia atakapounda serikali mpya. Mzungumzaji niliyemtambua kama nahodha wa kundi akataka suala la uongozi wa nchi uwekwe bayana na hususani wananchi wafafanuliwe nani ndiye Rais wa Zanzibar? Nikamuomba ajieleze zaidi tuweze kumuelewa. Akaeleza, “Wakati wa mkwamo wa kisiasa baada ya kufutwa kwa uchaguzi Oktoba 2015, Rais aliyesalia kwa kiasi kikubwa alikua haonekani wala kusikika. Tumeona huko Bara kuwa mara nyingi anayetoa taarifa za Rais au Nchi ni Katibu Mkuu Kiongozi au Kurugenzi ya Mawasiliano. “Hapa Zanzibar tunasikia makada wa chama ndio wasemaji wakuu juu ya masuala ya nchi. Mwisho juzi Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM ndiye katoa kauli juu ya siasa ‘kumalizika rasmi’ Zanzibar baada kwisha uchaguzi. Huu ni mfano dhahiri wa kubakwa kwa demokrasia kwani serikali ni ya Wazanzibari wote si ya chama chochote. “Hata kama matokeo ya uchaguzi yameturudishia serikali ya chama kimoja, mipaka kati ya serikali na chama lazima ipambanuliwe. Sisi wananchi tunataka uhakika serikali yetu inaongozwa na nani? Nani ndiye msemaji wake mkuu?” Alikazia. Mchangiaji yule wa makamo bila ya kupoteza muda akadakia. Yeye alitaka wizara zitakazoundwa ziakisi mwelekeo wa watawala. Alifafanua, “Kuna sura zimeselelea serikalini na katika Baraza la Wawakilishi miaka nenda miaka rudi. Mimi naona haja kuwepo ‘wizara ya wenye nchi, wano nafasi maalumu na za kudumu!” Akasita kidogo iniingie halafu akauliza, “Kuna haja gani ya kuteua mawaziri wasio na wizara maalumu kwa kipindi kizima cha miaka mitano wakati kuteuliwa kwao kunaashiria kuwa mtu huyo anayo nafasi maalumu na ndio maana hajaachwa?”
Wakati natafakari mantiki ya pendekezo nilolisikia, mchangiaji wa kwanza wa kike alizungumza. Yeye alikosoa tabia ya kuunda wizara kwa mazoea. Alimtaka Rais wa Zanzibar ajifunze kutoka kwa Magufuli ambaye kaparaganya wizara kwa mujibu anavyohisi mambo yanafaa kushughulikiwa. “Hapa Zanzibar kuwe na wizara tu ambazo zitasimamia yale ambayo watawala wetu wanayaona ni muhimu”, alipendekeza. Nikataka anipe mfano wa wizara hizo. Mchangiaji akajibu bila kusita, “Tusipoteze muda kuunda wizara hewani wakati serikali na wapambe wake wana sera zao wanazotaka kuziendeleza. Kwa mfano, bora tuundiwe ‘wizara ya ubaguzi, maudhi na unyanyasaji dhidi ya wananchi badala ya kuwa eti na Wizara ya Katiba na Utawala Bora. “Wizara mpya itahalalisha kisheria tabia ya serikali kuonea watu wake, na pia kubagua baadhi ya watu wake kuliko kudai kuwa ‘tutaheshimu haki za binadamu’ wakati nchi haiendeshi kwa mujibu wa katiba, sheria au haki!” Mzungumzaji wa kiume aliyebaki naye akajimwaga katika mjadala. “Mimi napendekeza kuwepo wizara ya kuimarisha ubabe, ukiukaji sheria, uafiriti na tashtiti, ili tujue kuwa hivi ndivyo vigezo vya utawala si katiba wala sheria!” Kauli yake ilinishangaza sana nikahoji “Sasa tuuondoe mfumo wa kikatiba na kisheria?” Akanijibu kwa sauti ya chini, “Utawala wa Kisheria labda upo kwenye karatasi maana kwa uhalisia kila anayejikuta kileleni anafanya anavyoona yeye. Kungekuwa na utawala wa sheria basi tusingevurugana kiasi hiki!”
Mwanamke kijana miongoni mwa wazungumzaji naye akaongeza, “Tusikome katika kupendekeza wizara tu lakini pia tushauri sura za mamlaka mbalimbali zifanyiwe marekebisho ya msingi”. Nikapata tumaini kuwa labda sasa nitapata picha timamu juu ya muundo wa serikali unaotakiwa. Akaendelea, “Binafsi naona haja ya kuwa na mamlaka maalumu ya kukwamisha mambo maana tunaambiwa hakuna kilichobadilika toka tumepata Uhuru na Mapinduzi, na kwa minajili ya siasa zetu hatutaki kubadilika!” Mwana mama mwengine akarukia, “Hakika tunahitaji mamlaka si ya mambo ya kale lakini ya mambo yaleyale!” Nahodha wa kikundi naye akaongeza, “Umeiona jinsi Nyumba ya Ajabu ilivyomegeka-megeka na kuporomoka? leo paa, kesho kuta ili hali ndio sehemu ya urithi wa mambo ya kale ambao unaouweka Zanzibar katika ramani ya dunia. “Badala ya kuenzi urithi wetu vitega uchumi vya Mji Mkongwe vimehodhiwa na kuwaneemesha watumishi katika mazingira yanayoashiria wazi Maslahi Kinzani (conflict of interest). Lakini nani anajali hilo?” Hakika nilichokuwa nakisikia sikikutarajia kabisa. Nikamgeukia mmoja wa mshiriki aliyekuwa hajasema kitu muda mrefu. “Naam, una la kuongeza?” nilimuuliza. Akacheka na kujibu akiwa katika tafakuri nzito, “Hata sijui niongeze nini” alianza. “Utamaduni uliotawala na kuzoeleka visiwani kwetu ni kukataa fikra chanya. Hapa wanafurahiwa wapika majungu si watengeneza mambo na waleta maendeleo” akaendelea. Yule mzungumzaji wa makamo alionesha kukunwa na hoja za mwenzake kiasi cha kumeza maneno yake na kuzungumza yeye. Alipendekeza kuundwe wizara au mamlaka maalumu inayotukuza ‘ukawaida’ au ‘ugando’.
Akifafanua pendekezo lake alisema, “hapa kwetu umahiri na umaridadi ni dhana ngeni. Hivyo, tujue sisi ni watu wa kiwango cha chini ya wastani na turidhike hivyo. Kioo chetu ni Sauti ya Utangazaji ya Zanzibar. Wale walioshindwa kuiendeleza kipindi chote hicho ndio tutegemee watafanya miujiza leo?” Alihoji na kuendelea, “Bora tukubali tu kuwa sisi ni watu wa chini ya viwango na tuunde taasisi itakayohakikisha kuwa tunabaki katika ‘ubora’ wetu huo badala ya kutupotezea muda wetu kutafuta ‘maisha bora’ na ‘maendeleo’ wakati haya ni mambo mageni kwetu”. Mmoja wa mchangiaji wa kike akasisitiza, “viongozi waache kusema kuwa hii ni nchi ya kidemokrasia, maana viashiria vyote ni kuwa ni nchi inayoendeshwa kwa mabavu. Zanzibar na wakazi wake hawafurukuti. “Majeshi kila mahala. Vikosi vinabughudhi badala ya kulinda raia. Kuna kila dalili za nchi kudhibitiwa na nguvu ya jeshi lakini hapohapo tunadanganyana kuna amani, hali shwari na kuna demokrasia”. Akahitimisha kwa kusisitiza, “Uhuru si kupiga kura tu. Uhuru ni kuwa na chaguo na imani kuwa chaguo lako litaheshimiwa na kuzingatiwa kwa usawa na uzito unaostahili siku ya kura na katika kipindi chote cha utumishi wake. Awamu hii unafiki uwe basi. Tujipambanue namna tulivyo watu wote waelewe na waridhike kuwa hivi ndivyo tulivyo. Hata hivyo ningependa kuwakumbusha walio ihodhi nchi kuwa Zanzibar si ya CCM au ya CUF bali ni ya Wazanzibari wote, wenye vyama na wasio na vyama. Kuwashurutisha raia kujiunga na mitizamo finyu na yasiyo na tija ya kichama ni uhaini wa aina yake”, mchangiaji akamalizia.
Bila ya shaka ujumbe mzito wa raia hawa wa nchi ya zanzibar utazingatiwa.