MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Saleh Mohammed Saleh, anashikiliwa na polisi mjini Zanzibar kwa madai ya kuhusika kulipua nyumba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame. Mhadhiri huyo ambaye ni Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF)Zoni ya Magharibi A Unguja na aliyekuwa mgombea wa ubunge wa Jimbo la Welezo, alikamatwa na saa nane za usiku wa kumkia jana. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na Uenezi, Pavu Juma Abdalla alisema polisi walivamia nyumbani kwa mhadhiri huyo na kuvunja mlango. Alisema kiongozi mwingine aliyekamatwa ni Mwenyekiti wa chama hicho Zoni ya Mfenesini, Omar Hassan Issa. Alisema kutokana na hali hiyo, jana kutwa nzima walizunguka vituo vingi ya polisi lakini hawakuwaona.“Polisi walivamia nyumbani kwao saa nane usiku, wakavunja milango na kuwapiga na kuondoa nao.
“Tumewatafuta vituoni hatukuwaona,tumeambiwa ni miongoni mwa watu wanaoshutumiwa kwa kulipua nyumba ya Kamishna Hamdani,” alisema Pavu.Alisema CUF wanaendelea na jitihada za kuwatafuta viongozi hao waweze kujua hatima yao. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alikiri kushikiliwa kwa viongozi hao. Alisema hakuwa tayari kutaja majina ya watu wengine waliowakamatwa akisema wanaendelea na upelelezi. Bado tunaendelea na upelelezi, tukiwa tayari tutatoa kila kitu, kwa sasa hatuko tayari kuwataja majina yao,” alisema Kamanda Mkadam. Alisema polisi wanaendelea na msako mkali dhidi ya watu wote wanaotuhumiwa kuhusika na ulipuaji wa nyumba hiyo. Kutokana na uchunguzi wetu tuliofanya, tunayo orodha ya washukiwa wote na tutaendelea kuwakamata na ikithibitika tutawachukulia hatua,” aliongeza
No comments:
Post a Comment