Saturday, April 2, 2016

MNALAZIMISHA TUUNGANE KUENDELEZA HARAMU KWENYE MGAWANYIKO


Na Julius Mtatiro.
Kuna mambo mengine yanakera na kuudhi sana, tumeendelea kushuhudia wapiga PROPAGANDA wa dola wakiendelea na kampeni mitandaoni, ati watanzania waungane kupinga udhalimu wa nchi za Magharibi dhidi ya taifa letu. Nikakaa na kujiuliza udhalimu upi wametutendea...? Nilitegemea wapiga PROPAGANDA hao wasimame kidete kupinga udhalimu mkubwa uliofanywa na dola pale Zanzibar, wakakaa kimya na wakaunga mkono NGUVU YA DOLA dhidi ya DEMOKRASIA! Leo wanakuja kifua mbele kututaka sote tuungane kwenda kubembeleza misaada kwa wakubwa, upuuzi! Yaliyotokea Zanzibar ni aibu kubwa mwa Mwafrika, ni mfano wa wazi wa namna mwafrika anavyotengeneza matabaka, ubaguzi na kudharau mamlaka na maamuzi ya wananchi. Hakuna dhambi kubwa katika utawala wowote kama ile ya kudharau maamuzi ya wananchi. Hii ya nchi za magharibi ni “mzizi wa dhambi tu!” na ni ndogo sana! Kwa tulio na akili tunajua kuwa nchi za Magharibi haziwajibiki kunyanyua uchumi wa nchi yetu. Lakini tunatambua kuwa uongozi wa Tanzania kwa miaka 50 iliyopita na hadi leo unaendelea kuwa tegemezi kwa nchi hizo kiuchumi na unahubiri dhana ya “kujitegemea” majukwaani huku unaomba misaada kwa mlango wa nyuma.
Wengine tunaziona sababu za wafadhili hao kukata misaada yao kama ZA MSINGI SANA! Na hatuoni ni wapi mnataka tuungane kama taifa kuwapinga? Tukiingia kwenye mtego wa kuungana nanyi kuwapinga wafadhili wenu, tutakuwa tunakubali kuwa yaliyojiri Zanzibar ni halali! Kwa sababu wengine tulishasema ni HARAMU, hata hatua za wazungu kuwarudisha kwenye mstari tutaziunga mkono. Baada ya uhuru ilitegemewa waafrika wajifanyie mambo yao wenyewe, watendeane haki wao kwa wao, wautumie uhuru wao vizuri. Badala yake, wanashughulikiana wao kwa wao, wanatwezana wao kwa wao, wanaumizana wao kwa wao na wako tayari kuuana wao kwa wao kwa ajili ya kung’ang’ania madaraka. Kwamba leo tunashindwa kusimamia chaguzi zetu kwa kujali utu wetu, tukatangaza washindi halali na kuacha maamuzi ya wananchi yachukue mkondo wake, hadi wafadhili waje kutuonesha wamechukizwa!!!! Halafu wakionesha hasira zao juu ya nchi yetu, tunaanzisha kampeni ya kutaka tuungane! Mimi siwezi kuingia kwenye muungano wa kipuuzi kabisa huo!
Mtatiro J.

No comments:

Post a Comment