Kamanda Simon Sirro
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema Mwandishi wa Habari wa DW na Mwananchi, Salma Said anayedaiwa kutekwa alisema alipita lango namba mbili, huku kamera za CCTV zikionyesha kuwa alipita lango namba moja. Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa kauli ya mwandishi huyo inakinzana na taarifa iliyorekodiwa katika kamera. Alisema kamera hiyo ilionyesha kwamba baada ya mwandishi huyo kufika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), alikuwa akitembea katika maeneo mbalimbali ya uwanja huo.
“Kwa sasa tunaendelea na upelelezi kujua mwenendo mzima wa tukio hilo na ukikamilika tutatoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa sababu hatutaki kumuonea mtu tunapenda kila mwananchi apate haki yake,” alisema Kamanda Sirro. Salma alitekwa Machi 18, mwaka huu katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam baada ya kuwasili akitokea Zanzibar na siku tatu baadaye alikutwa katika Hospitali ya Regency, mjini Dar es Salaam. Hivi karibuni, Salma alipohojiwa na vyombo vya habari, alidai kwamba alitekwa na wanaume wawili baada ya kumkamata na kumuingiza kwenye gari na kuondoka naye kusikojulikana. Alieleza kuwa watu hao walimfunga mtandio wake mweusi usoni ili kumbambaisha asitambue mahali walikokuwa wakimpeleka.
No comments:
Post a Comment