Timu ya Sayari iliibuka mshindi wa kombe hilo la Jihadi na kukabidhiwa pamoja na mambo mengine Kombe na shilingi laki nne taslim, baada ya kumshinda mpinzani wake timu ya Taifa Jipya kwa mikwaju ya penalty.
Dakika 90 za mchezo zilimalizika kwa timu hizo kuwa na nguvu sawa ya kufungana na (mabao 2-2) na ndipo sheria ya kupiana mikwaju ilipochukua nafasi yake ambapo Sayari ilishinda mikwaju yote 5 dhidi ya Taifa Jipya iliyopoteza mkwaju mmoja na mwisho kuugomea ikijua kuwa tayari imeshashindwa.
Akizungumza baada ya mtanange huo uliomalizika wakati wa magharibi na kuonekana kupata mashabiki wengi na kuyapiku hata mapambano ya ligi kuu ya Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alisema Serikali ya Awamu ya Saba imedhamiria kurejesha hadhi ya soka Zanzibar.Amesema mashindano hayo yameonakana kupata mafanikio makubwa hasa ikizingatiwa kuwa timu zilikuwa na nidhamu ya hali ya juu huku zikiwaunganisha vijana bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Ametoa changamoto kwa timu za Zanzibar kudhamiria kuwa washindi wakati wanapoingia kwenye mashindano mbali mbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa na kuachana na mtazamo finyu wa kuingia kwenye mashindano hayo kama washiriki au wasindikizaji.Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Magogoni ambaye ndiye mlengwa wa mashindano hayo Mheshimiwa Abdillahi Jihadi Hassan alisema lengo la mashindano hayo yaliyozishirikisha timu 9 za daraja la pili na tatu katika Wilaya ya Mjini ni kuibuwa vipaji vya vijana kwenye soka na hatimaye kuviendeleza.Alisema michezo ni ajira na afya, hivyo vijana hawanabudi kushiriki katika michezo mbali mbali hasa wa soka ili kujijinga kiafya na kujiandalia mazingira ya ajira.Katika risala ya kamati ya michezo hiyo ya “Jihadi Cup” iliyosomwa na afisa habari wake Ali Cheupe, walisifu mafanikio yaliyopatikana na kumpongeza Waziri Jihadi kwa jitihada zake za kutafuta wadhamini wa ligi kuu ya Zanzibar alizozichukua ambazo zimezaa matunda kwa kampuni ya vinywaji ya “Grand Malti” kukubali kuidhamini ligi hiyo.Wamewashauri viongozi wa kitaifa na soka kutobeza udhamini huo ambao ni muhimu katika kuendeleza soka la Zanzibar.
No comments:
Post a Comment