Saturday, June 16, 2012

BARUA YA WAZI KWA UMMA WA WAZANZIBARI WALIO NDANI YA NCHI NA WALIO NJE YA NCHI NA WALIMWENGU KWA UJUMLA.

HII NI BARUA YA JUMUIA NA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR. Na Masoud Ali
Kwa ndugu waislamu na wote wapenda haki na wanaoipendelea maslahi mema zanzibar.
Umoja  wa Jumuiya na taasisi za kiislamu Zanzibar umeamua kuandika barua hii ya wazi kwa ummma wa Wazanzibar, viongozi na wananchi kutokana na tuhuma kadhaa zilizoelekezwa kwa jumuiya ya Uamsho.
Awali tunapenda ifahamike kuwa harakati za kuikomboa Zanzibar ili ipate mamlaka yake kamili na kuirejeshea heshima yake ni harakati zinazosimamiwa na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu si jumuiya ya Uamsho peke yake kama wanavyojaribu kwa makusudi vyombo vya habari kupotosha ukweli ili kudhoofisha harakati hizo za ukombozi kuipelekea Zanzibar kupata mamlaka kamili (sovereign state).
Kumejitokeza maadui wengi wa harakati hizi kwa kuituhumu jumuiya hiyo ina uhusiano na makundi yenye msimamo mkali wa kiislamu na wengineo wamekua wakisema wazi kuwa Uamsho ina uhusiano na makundi ya Al-Qaeda, Alshabab, Boko haramu na mengineyo. Uvumi mwengine ni kua jumuiya ya Uamsho inashirikiana na Marekani katika kuendesha harakati zake, vile vile ina uhusiano na chama cha Hizbu Tahrir na Chama Cha Wananchi – CUF.
Tuhuma hizo zimetolewa na viongozi wa makanisa sambamba na viongozi wa CCM kama NAPE pamoja Mh. ALI HASSAN MWINYI na wenziwe pamoja na watu wanaoheshimika na wenye dhamana kubwa katika jamii na kwa hamasa kubwa sana, hayo yametamkwa hadharani bila ya kuwa na ushahidi wowote. Tuhuma hizo zimetolewa ili kuwapoteza malengo Wazanzibar na kuvuruga umoja wao katika kudai haki zao za msingi ambazo ni kudai utaifa wa nchi yao. Njama za kuvuruga umoja wa Zazanzibar hazikumalizia katika tuhma tu bali hivi sasa zinaandaliwa nama za kughushi  Account katika mabenki ambazo zitaihusisha jumuiya ya Uamsho kuwa inapokea misaada kutoka makundi ya Al-qaeda, Al-shabab na mengineyo na njama nyengine ambazo hazijatajwa kwenye maelezo haya. Zaidi kuliko hayo viongozi wa kanisa wameanza harakati za kuziburuza serikali zote mbili na kutumia vyombo vya dola kwa lengo la kuvunja katiba na amani ya nchi kwa kuzitaka serikali kuingilia uhuru wa kuabudu na uhuru wa maoni kwa kuwanyima waislamu  na kuwapiga marufuku haki yao ya kuabudu na uhuru wa maoni kupitia mihadhara, dua, itikafu, nk. Ifahamike kwamba katiba zote mbili zinalinda haki hiyo ibara ya 19. ya katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema (1,2) kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo ,imani na uchaguzi katika mambo ya dini…..kazi ya kutangaza dini kufanya ibada na kueneza dini ni huru na jambo la hiari….shughuli na uendeshaji wa jumuiya za kidini zitaka nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.(rejea ibara ya 18,19,20 ya katiba ya zanzibar).
Hivyo umoja wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu inapenda kuwataarifu wananchi wa Zanzibar, wanaoipendelea mema Zanzibar na wapenda haki kote duniani kuwa Jumuiya ya Uamsho haina uhusiano wowote na makundi yaliyotajwa hapo juu kwani hakuna haja wala hoja ya kutaka misaada yeyote kutoka kwao. Pia inasisitiza kuwa Junuiya ya Uamsho ni vuguvugu la umma la Wazanzibar ambao hawajajiambatanisha na makundi yoyote yenye kufanya mapambano na tawala zao kwa njia ya silaha, wala haijajiambatanisha na nchi au taasisi yeyote ya nje ya nchi na ndani kwani hakuna haja wala hoja ya kufanya hivyo.
Jumuiya ya Uamsho inafanya kazi hiyo kwa kushirikiana kikamilifu na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu tofauti nchini Zanzibar kwa kutetea maslahi ya kupatikana kwa mamlaka kamili ya Serikali ya Zanzibar kutokana na kushindwa kwa vyama vya siasa kutetea utaifa wa Zanzibar kwa sababu vyama vya kisiasa vimezingirwa na katiba  ya Jamhuri ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika.
Katika hali hiyo ni nani angejitolea kulizungumza jambo hilo? Chombo pekee ambacho ndicho kinawakilisha umma wa Zanzibar ni Jumuiya na Taasisi za Kiislamu na kukabidhiwa jukumu la mambo tofauti. Jumuiya ya Uamsho ambayo ndio yenye sauti pekee katika jamii na kwasababu hiyo imelazimika kutoa sauti ambayo hakuna mwengine angeliweza kutoa.
Watu wa Zanzibar wajuwe kuwa wachache wasioipendelea mema Zanzibar hawatasita kuunda kila njama za kuharibu vuguvugu la kudai mamlaka kamili ya Zanzibar. Viongzi wa jumuiya wanawataka Wazanzibar watambue njama hizo na wasiyumbishwe katika msimamo wao.
Jumuiya ya Uamsho si kundi la magaidi, wala si kundi la wachoma  moto makanisa au waporaji wa mali za umma. Jumuiya  ya Uamsho inatoa sauti kwa njia za amani bila ya kutumia nguvu za silaha bali kwa kutumia nguvu za hoja na inaendesha harakati zake juu ya misingi ya sheria za nchi  na katiba.
Wananchi wa Zanzibar kudai uhuru wa kujiamulia mambo yetu ni haki yetu ya msingi na kwa hilo HATUNA MJADALA MPAKA KIELEWEKE, tutaendelea kudai haki zetu kwa kila hali bila ya kuvunja sheria za nchi.
Tunasisitiza kuendelea na kudai Zanzibar huru ingawa tunaelewa gharama ya kufanya hivyo ni kubwa ikiwemo kupoteza roho zetu kwa mfano aliekua Rais wetu wa kwanza Almarhum Abeid Aman Karume alipoteza uhai wake baada ya kuanza kuugusa muungano pale alipopiga marufuku azimio la Arusha kutumika Zanzibar na kusema mwisho wake Chumbe pia na kusema muungano ni kama koti likikubana unalivua haukupita muda alipoteza uhai wake.
Mzee wetu mheshimiwa Aboud Jumbe alipotengeneza mazingira ya muungano wa haki alikwenda Dodoma akiwa RAIS alirudi akiwa raia wa kawaida aliuzuliwa urais. Hayo ndio  matokeo ya kuugusa muungano. Watu walipoteza mali zao, heshima zao na roho zao eti kwa sababu ya kuugusa muungano.
Wazanzibar tutaendelea kudai Zanzibar yetu huru. Kama sheria zinavyoelekeza ikiwemo kudai kuwepo kwa KURA YA MAONI kwa njia ya amani.
                                           TUWACHENI TUPUMUE!!!!!!!
WABILLAHI TAUFIQ….

No comments:

Post a Comment