KUNA uhalifu umefanywa Zanzibar. Ni katika matukio mabaya yaliyoanza usiku wa tarehe 26 Mei 2012. Watu wamechochewa kupambana na dola. Hili halijaelezwa na serikali.
Polisi wamevamia nyumba za viongozi wa Uamsho na kuvunja milango huku wakiwatukana matusi ya nguoni viongozi na familia zao sambamba na kuwatishia maisha. Polisi hawajalieleza hili.
Amir (kiongozi) wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI), Sheikh Farid Ahmed Hadi anasema usiku wa Jumamosi hiyo, akiwa kwake, alipata taarifa anafuatwa na polisi wa kuzuia fujo (FFU).
Akajiandaa. Mnamo saa 7.30 kweli wakafika. Wakataka mlango ufunguliwe. Hakuna aliyewatii. Wakarusha risasi hewani. Hakuna aliyetoka. Hakuna aliyepiga kelele kutokea ndani.
Lakini, baada ya kuona vishindo vimezidi, Sheikh Farid akasema kwa sauti, “Nipo ndani na familia yangu tumepumzika. Kama mpo tayari, fanyeni chochote nje ila, ninaapa kwa jina la Allah, anayekuja ndani, tutakabiliana mimi sina bunduki.â€
Polisi hawakujali. Wakafyatua mabomu. Wakavunja mlango na kuvuruga walivyovikuta nje. Wakataka kuingia ndani. Wakakatazana, “hapana. Mnajua nani wamo ndani? Tuondokeni.â€
Wakaondoka, anasimulia Sheikh Farid. Amepata simulizi kama hizo kwa viongozi wenzake wa Uamsho. Lakini sokomoko kama lililomkuta, lilitokea nyumbani kwa naibu wake, Sheikh Azzan Khalid Hamdan, wakati mwenyewe akiwa nje ya nchi kwa matibabu.
Sheikh Azzan aliporudi Ijumaa, akapewa taarifa na familia yake kuwa walifika polisi wa FFU na kufanya fujo. Walifyatua risasi nje, wakavunja mlango. Wakapiga mayowe ya kumtukana matusi yeye na familia. Wakaondoka.
Hakutulia. Alikwenda kupiga ripoti kituo cha polisi Mfenesini, karibu na anapoishi. Wakuu wakakana kufika kwake. Wakasema askari waliomfuata walitoka Mwembemadema.
Mwembemadema ni makao makuu ya polisi mkoa wa Mjini Magharibi. Hawa ndio waliotuma makachero Jumamosi ile wakamshike Ustadhi Mussa Juma Issa, mmoja wa wahadhir wakuu wa Uamsho, kipenzi cha wahudhuriaji wa mihadhara ya jumuiya hii inayohamasisha Wazanzibari kuukataa muungano.
Wapo watu wamejitokeza kutoa ushahidi wa walivyoona polisi wanalipua nyumba na mali za vitegauchumi za raia wema, zikiwemo gari zilizoegeshwa Kisiwandui na Michenzani.
Mwanamke anayefanya kazi shirika la ndege la Kenya Airways, gari yake iliteketezwa kwa bomu lililorushwa na polisi. Matukio yote hayo katika siku mbili – Jumamosi na Jumapili.
Leo, taarifa zimepatikana za uhalifu wa Polisi uliofanywa Jumatatu, 28 Mei, muda mfupi baada ya watuhumiwa 30 wa fujo, walipoachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Mwanakwerekwe, mjini Zanzibar. Kati yao wapo viongozi wawili, akiwemo Ustadhi Mussa, wa Uamsho.
Wakati wakili wao, Abdalla Juma akiwa Mahakama ya Ardhi, Vuga, vijana wa FFU walivamia ofisi zake Amani, yapata kilomita tano kutoka Vuga. Wakapitisha mitutu ya bunduki madirishani na kufyatua risasi na mabomu ya machozi.
Hawakujali wafanyakazi waliokuwa ndani. Ni mchana kweupe. Hapana, ni mchana wa mola muumba mbingu na ardhi siku ya kazi, Jumatatu.
Ipo taarifa ya Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS) kulalamikia kitendo hicho. Wamemtumia barua Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa, na kumtaka asake wahusika na kuwashitaki.
ZLS wamekiita kitendo hicho cha makusudi kilicholenga kutisha mawakili wasiwe imara katika kazi yao ya kutetea wananchi wanaposhitakiwa. Polisi wanatuhumiwa sasa kushiriki vitendo vya uhalifu katika kipindi kilekile ambacho wao wanatuhumu Uamsho kuzusha ghasia mjini Zanzibar.
Ninayaeleza haya ili kukumbusha historia ya kisiasa Zanzibar inayochefua. Siasa za maridhiano zilizoanza kustawi tangu 2010 mwishoni, zinachafuliwa kwa nguvu.
Ni kama zilivyokuwa zikipandikizwa na kustawishwa siku zile za giza, mara tu mfumo wa siasa za vyama vingi, siasa za ushindani, uliporudishwa chini ya sheria ya Tanzania.
Sasa wapo wasiotaka amani Zanzibar idumu. Wapo. Pengine wanampenda Amani Abeid Karume, kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, ambao walizijenga, bali wanachukia matunda ya maridhiano.
Polisi. Polisi. Polisi. Polisi. Polisi. Polisi. Polisi. Polisi. Polisi. Hapana; si peke yao. Kwa jumla, vyombo vya
dola, vya dola, vya dola. Dola, dola, dola, dola, dola, dola, dola, dola, dola.
Vyote vilitajwa kupandikiza chuki kwa wananchi, mgongo ukiwa vyama vingi na uimara wa CUF. Visima vikapakwa kinyesi, ofisi za umma zikawashwa kwa viberiti na makanisa yakachomwa kiajizi. Kanisa linawashwa, dakika mbili tu hao walinzi wamefika.
Ushetani ule ukakoma pale wananchi wa Shengejuu, kaskazini Pemba, walipovizia usiku kutafuta nani hasa wakihusika na vitendo vile vya kiharamia. Waliokutwa mpaka leo Polisi hawajawataja.
Ni askari polisi na mashushushu ndani ya Landrover iliyosheheni madumu ya petroli, mapipa ya kinyesi na viberiti vya kuwashia mabomu ya chupa.
Kutaka kuzubaisha umma wa Watanzania na ulimwengu, IGP Omari Mahita akaunda kikosi kuchunguza. Akamteua Robert Manumba, kachero aliyekuwa msaidizi mkuu wa DCI Adadi Rajabu, kukiongoza.
Alitaka wachunguze chimbuko, sababu na wahusika wa milipuko ile ya kishetani pamoja na vitendo haramu vya kupaka kinyesi madarasa na kukimwaga kwenye visima vya maji wanayotumia wananchi.
Tangu wakati ule, karibu miaka kumi sasa, si DCI Manumba ambaye sasa ndiye DCI, si IGP Mahita wala serikali iliyotoa ripoti ya uchunguzi huo. Wananchi waseme nini hapo? Lakini kwa sababu wahusika walijulikana na kufikia kukamatwa Shengejuu, zile fitna kuwa CUF walikuwa wahusika, zilifutika.
Tungalinao wakorofi wasiopenda maridhiano. Wahafidhina ndani ya CCM wameibuka upya wakitaka kuharibu amani na utulivu. Hawawezi kuitaja CUF moja kwa moja maana wanashirikiana nacho kuendesha serikali.
Wametafuta pa kuingilia – Uamsho. Kwa kuwa taasisi hii imechukua jukumu la kupigania haki za wananchi wasioridhishwa na mwenendo wa muungano, wanawapakazia kuwa wanavunja amani.
Kumbe bado kuujadili Muungano wa Tanzania ni uhaini. Pamoja na serikali kuruhusu Watanzania watoe maoni yatakayotumika kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watawala hawapendi watu wafikiri tofauti na wao.
Tunaona kila viongozi wa polisi wanavyojitahidi kupotosha ukweli wa kilichotendeka mjini Zanzibar, ile dhamira yao ya kupotosha inawarudia. Wanatajwa baada ya kuonekana wazi wakivamia na kuharibu mali ikiwemo ofisi za wanasheria.
Mpanga ubaya mwisho humrudia. Hawajajisafisha, wamejiumbua. Na ndiyo matokeo ya polisi nchini kushabikia siasa. Wanasubiriwa watamshika nani mchoma makanisa. Bado watafute ushahidi kuthibitisha kesi ya watu 30, pamoja na wafadhili wa Uamsho.
No comments:
Post a Comment