Wednesday, December 5, 2012

HATUTAIPATA NCHI YETU YA ZANZIBAR MPAKA TUACHE KUCHEZA NGOMA NA TUSHIKANI TUWO WAMOJA NDIO TUTAIPATA ZANZIBAR


kazi ndio hii kweli sisi tutaikombowa nchi yetu ya zanzibar......?
Kwa wale waliokuwa wakifuatilia mihadhara ya UAMSHO hapa Zanzibar wanakiri kuwa moja kati ya malengo makuu ya jumuiya ile ni kuwaamsha Wazanzibari juu ya athari zisizotibika wala kurekebishika tena za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Hivi ndivyo ninavyoifahamu hasa kokwa ya kiini cha mihadhara ya uamsho.
Lengo la uamsho limefanikiwa kiasi Fulani kwani kila mzanzibari ameweza kujua hasa nafasi ya Zanzibar katika Muungano, na jinsi Muungano huo unavyoiumiza Zanzibar bila kuipa pumzi. Lakini kama hili ndio lengo, bado kunabakia hatua gani Wazanzibari wachukuwe kujikwamua na hili.
Nasema kazi ya uamsho imekwisha, na sio kwa sababu wahusika wako Rumande kwa sasa laa hashaa, bali ni kuwa walifanikiwa kutuamsha. Hofu yangu ni kuwa sisi tulioamshwa tumeamka na tuko tayari kujitutumua katika vitanda vyetu na kutoka na seja za vikowi na kanga kupambana...? Kwa hili naona bado.
Naamini kuwa Wazanzibari hawajawa tayari, na wala hawatakuwa tayari kuukataa Muungano kwani kimaumbile sisi Wazanzibari, ‘Hatujui tunalolitaka wala tusilolitaka’.pia ni majoga kweli kweli  Nasema hivi kwamba leo hii akija Sheikh Farid akituambia ‘Mnautakaaaa!’ Tutajibu huku tukitokwa na vipovu vya midomo kwa jazba ‘Hatuutaki’ na wengine watasema ‘Hatuwebuuuu’. Akishuka jukwaani tu, maneno haya haya hukauka na mate na vipovu vyetu vya midomo, hatunayo tena, tunayasahau yote.
Akija Warioba tunaanza kujikanyaga kanyaga weee kama wenye maradhi ya kifafa. Mara Muundo mkataba, mara Serikali tatu, mara zibaki mbili lakini upigiwe pigiwe mtomo, yaani uzibwe nyufa, alimradi vurugu mechi. Wazanzibari hatusomeki kabisa. Leo hii tunakaa baraza la waakilishi kauli moja. Akija ‘Kijichwa’ cha kokochi hapa kila mtu na lake jinsi tulivyo majoga makubwa. Hivi tushakuwa tayari..? Mie nasema bado, na wala hatuthubutu kuukataa Muungano kwa sababu kama hizo na nyenginezo zijazo hapa chini.
Kabla sijaendelea na sababu za kwamba hatuthubutu kuukataa hata chembe Muungano nataka niseme kuwa hakuna suluhuisho mbadala la Muungano huu ila uvunjwe kila mtu awe kwake. Kama kuna mazungumzo mengine yatakuja usoni tena kwa kuwa na umakini mkubwa na wenzetu hawa. Nasema lazima uvunjike kwa sababu wenzetu wa Tanganyika wametuzoea kwa miaka 48 na wanatujua kope na jicho udhaifu wetu hasa juu ya ile asili yetu ya kuwa ‘Hatujui tukitakacho, wala tusichokitaka’.zaidi ya kucheza ngoma.

Pili wezetu wanatujua asili , utandu na ukoko kuwa ili watuweze wachukuwe katika sisi kwa sisi wawape tonge wanyamaze kimya hata wakiona nchi hii inauzwa kiasi gani. Ndio hao tena. Tuna viongozi lukuki wa Kizanzibari walokuwa na nafasi kubwa duniani, na chamani hapa nchini, walifanya lipi kuikoa Zanzibar..? Na chakushangaza wote ni wasomi. Dokta Salim Ahmed Salim, kaifanyia lipi Zanzibar..? Dokta Bilal, kafanya lipi kuinusuru Zanzibar..?
Tuendelee na mlolongo huu, Muhammed Seif Khatibu, habithi l’amal, ndio huyo mpini wa jiti katika shoka linalotumiwa kuikata miti mengineyo ya kwao. Amina Salum Ali, yuko Magharibi huko anakula maisha akikaa kichwa wazi kama vile hatakufa na kujinasibu kuwa ni muislamu mawe. Kaifanyia lipi Zanzibar..? Sasa katika hali kama hii ambapo viongozi wakuu wa Zanzibar wasomi, wenye mvuto na ushawishi kitaifa na kimataifa kuwa hawasemi wala hawasimamii haki ya nchi yao, munategemea nini..?
Tatizo la Muungano kwa Zanzibar ni sugu mithili ya kansa au donda ndugu la mguu kwa sasa. Na ili lipone ni kukubali kuukata mguu tu. Lakini hili haliwezekani kwani viongozi wanaotuwakilisha hawako tayari kuyasema wala kuyasimamia yale tunayoyataka. Hivi tuone Wabunge wetu wako tayari kuuvunja Muungano ilhali wakijua kuwa kuvunjika kwa Muungano ni kuwavunjia kula yao ya Bure kweli unafikiri watauvunja mawee. Bungeni kuna shibe ya bure bwana usifanye masikhara. Unalala na kupiga kofi unaondoka na milioni 12 kwa mwezi umesikia wapi ulimwenguni...?  Kwa hali kama hii, ni mbunge yupi wa Zanzibar alie tayari kuuvunja Muungano...? yagujuuu
Tukiangalia Viongzoi walioko madarakani hivi sasa wote ni vibaraka wa Muungano na ni vitumwa vya Watanganyika. Tunategemea atayosema Mansour kule Chukwani watayafanyia kazi. Hapana, ndio hivyo tunaona sasa kila aliekuwa na uhusiano na Karume, anatolewa katika nafasi yake na kuwekwa bonge la pandikizi la kibaraka wa Watanganyika na Muungano ili limalize kutula. Leo pandikizi hilo likija Zanzibar hujifanya liko pamoja nasi na likifika bara ndio adui namba moja wa nchi hii. Huu ni unafiki ambao pia unachangia kuvunja uwezekano wetu wa kujikomboa.
Sababu nyengine zinazoashiria kuwa sisi Wazanzibari hatujawa tayari na wala hatuthubutu kuukataa Muungano, zinaonekana katika maoni yaliyoko hivi sasa ya Tume ya ‘Kichwa cha Nazi’. Maoni yetu yote tunayoyatoa licha ya juhudi ya Uamsho ya kututaka tuseme bayana kuwa hatuutaki au hatuwebu, kila anaesimama kutoa maini pale, husema ‘Mkataba’ akishasema hivi ‘Kidazi’ humsakama kwa masuali magumu ya kumuuliza ameona wapi aina hio ya Muungano..? Hapo mtu hujikanyaga na asijulikane maoni yake yalipo.
Kuna wengi wadai Serikali tatu. Ni hayo kwa hayo maji ya futi na nyayo. Wenzetu wa bara hawako tayari kujiita watanganyika maana wanajuwa ni jina la kitwana walilo piwa na wakoloni wao wakijarumani miaka ile walivyokuwa watumwa wa wajarumani. wala hawapo tayari kuacha kuimba wimbo wao wa Mungu ibariki. Na hili linajionesha wazi kule Uganda kwenye kombe la Chalenji. Timu yao inaimba wimbo wa Taifa la Tanzania, na pia inaitwa Tanzania. Hili kwao ni jambo kubwa wasiloweza kuliacha kwani ndio lililowapa heshima duniani. Hawakubali kwa hili hata wakisema Serikali tatu, bado watatufundia kunvini (watatulalia) tu.
Pia, kwa bahati mbaya sana kuna ndugu zetu ambao si haba wanataka Muungano ubakie hivi hivi ila urekebishwe wengi wao wakiwa viongozi wa juu Serikalini na wanachi wa majimbo ya Kusini. Hili ni jambo gumu na la kuumiza kichwa sana kwani linakwamisha kwa nguvu zote ukombozi wa Zanzibar ambayo kwa sasa sio taifa Huru, tusidanganyane. Wenzetu wanatuchezesha ukindu kama paka vile wala hapana panya wa kukamata. Tumeghafiilika.
Ukweli ni kwamba Muungano chini ya wavamizi wetu, bara, hauwezi kukatika wala kurekebishwa. Mfano mzuri ni suali la kodi mara mbili. Tulisema kule Chukwani mpaka tukatoka vipovu. Leo hii pitisha tivii bara iwe inatoka Zanzibar. Ni kifo. Utaiuza pale pale pale au utaivunja tu kwa ushuru mpya unaozidi thamani ya Tivii yenyewe. Leo hii tunabaki na Imani kuwa utarekebishwa. Huo ni upofu wa mawazo na kufilisika kuliko pitiliza mipaka. Wenzetu wa bara si majuha kiivyo. Wako macho.na kila mwaka tunaletewa mipolisi ya kibara kuhamia hapa na vijana wetu wanakula maunga tu na mabangi.

Labda kwa kuhitimisha tu niseme, uwezekano wa Zanzibar kujikwamuwa na mkoloni mweusi Tanganyika ndani ya Muungano upo iwapo tu tutashikamana, tuwe wakweli, na tupambane kwa nguvu moja, wakubwa kwa wadogo, wa dini na siasa, wazalendo na viongozi wote, hapo tutafika. Hofu yangu niliyonayo ni kuwa katika mgawanyiko mkubwa ulioko baina yetu juu ya mtazamo wetu wa Muungano, nahofia kuwa mafanikio hayapo kwani aliekuwa Waziri mkuu wa Uingereza Sir Winston Churchil alisema ‘Nyumba iliyogawika yenyewe haiwezi kusimama’.

No comments:

Post a Comment