Arusha. Watu wanaoaminika kuwa ni magaidi nchini Tanganyika, wamemjeruhi kwa kumpiga risasi Mtawa wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Shobana Synd na kumpora kiasi kikubwa cha fedha.
Habari kutoka kwa wenzake zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas zinasema kuwa mtawa huyo raia wa India kutoka Shirika la Notre Dame, alishambuliwa kabla ya kuporwa fedha hizo.
Kwa mujibu habari hizo, mtawa huyo aliyekuwa akitoka benki, alijeruhiwa kwa risasi mbili wakati akisubiri kufunguliwa geti la kuingia katika Shule ya Msingi Notre Dame.
Ingawa Watawa hao hawakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha zilizoporwa, habari zinasema ni zaidi ya Sh60 milioni zilizochukuliwa benki kwa ajili ya malipo na shughuli mbalimbali za shule hiyo.
Shule ya Msingi ya Notre Dame iliyoko eneo la Njiro, jijini Arusha inamilikiwa na shirika hilo la Watawa ambao wengi wao wana asili ya Asia ambako mtawa huyo, Shobana ndiye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo. “Alipigwa risasi mbili, moja kwenye mguu wa kushoto uliovunja mfupa na nyingine ilipenya kwenye nyama za mkono wa kushoto ambako kwa bahati haijagusa mfupa...Tunamshukuru Mungu anaendelea vizuri,” alisema mmoja wa watawa kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
Akizungumza katika wodi ya Hospitali ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), alikolazwa, mtawa huyo alisema: “Ninamshukuru Mungu kwa kuninusuru katika kifo...Walinirushia risasi kadhaa wavamizi hao.
“Ninamshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea, si ujanja wala uwezo wangu kuendelea kuwa hai hadi leo baada ya mashambulizi yale ya risasi. Ninawaombea msamaha na rehema wahusika ili waache uovu na kurejea katika njia ya haki.”
Kamanda Sabas mbali na kukiri kutokea kwa tukio hilo alishindwa kulizungumzia kwa undani kwa maelezo kuwa muda huo alikuwa akiendesha gari na kuahidi kulitolea ufafanuzi leo.
Kumekuwa na matukio kadhaa ya wateja wanaochukua fedha kutoka benki mjini Arusha kuvamiwa na kuporwa fedha, matukio ambayo yanazua hisia ya kuwapo mtandao wa uhalifu unaoshirikisha baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo.
Mwaka jana, wafanyakazi wawili wa Shirika la Here’s Life Africa Mission linalomilikiwa na Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, Stanley Hotay waliochukua fedha katika moja ya benki hizo walivamiwa na kuporwa zaidi ya Sh40 milioni.
Tayari uongozi wa benki zilipochukuliwa fedha hizo umeanza uchunguzi kuhusu jambo hilo kwa nia ya kubaini kwa nini taarifa za wateja wanaochukua fedha zinafika kwa majambazi ambao huwapora njiani au baada ya kufika ofisini kwao.
No comments:
Post a Comment