Wednesday, March 20, 2013

RAISI WA PILI WA NCHI YA ZANZIBAR ABOUD JUMBE ILIKUWAJE AKAPINDULIWA NA CHAMA CHAKE CHA CCM..???


Rais Aboud Jumbe: Ilikuwaje Chama Kikampindua? 

imeandikwa na Joseph Mihangwa.

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya, tuliona namna Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichoshika hatamu zote za uongozi wa nchi wakati huo, kilivyoweza kumpindua Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi, Januari 1984; na jinsi hatua hiyo ilivyozua makundi mawili yenye uhasama visiwani.

Makundi hayo yalikuwa ni kundi la “Wanamstari wa mbele” (Frontliners), lililofurahishwa na mapinduzi hayo na lililotaka kuona Zanzibar mpya. Kundi la pili, lililoitwa “Wakombozi” (Liberators), lilichukizwa na mapinduzi hayo na kujenga chuki na uhasama mkubwa dhidi ya Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere, aliyesimamia na kufanikisha mapinduzi hayo; na likaapa kumpa ‘kibano’ na kumdhalilisha nafasi ikitokea. Je, nafasi hiyo ilitokea? Endelea na sehemu hii ya pili na ya mwisho kupata jibu.

Wakati akijiandaa kung’atuka urais, Mwalimu Nyerere aliwauma sikio marafiki na wasiri wake wa karibu kwamba, safari hii (mwaka 1985) angependelea Rais wa Muungano atoke visiwani. Hata hivyo, chini ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union), Sheria ya Muungano ya 1964 na Katiba ya Muungano, utaratibu huo haukuwepo wala kutambulika. Kwa hiyo, hayo yalikuwa mawazo ya Mwalimu Nyerere pekee na kutumia ushawishi ili wengine nao wakubaliane naye.

Ilivyotokea ni kwamba, CCM kilipeleka Kamati Kuu, majina matatu tu ya wagombea. Hao walikuwa ni Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti CCM taifa wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi, Rashid Mfaume Kawawa, na aliyekuwa Waziri Mkuu, Dk. Salim Ahmed Salim. Kati ya hao watatu, ni Rashid Kawawa pekee ambaye hakuwa Mzanzibari.

Mwinyi, licha ya kuzaliwa Kisarawe, mkoani Pwani -Tanzania Bara na kukulia Zanzibar alikuwa Mzanzibari kwa sababu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Mzanzibari ni Mtanzania yeyote aliyeishi kwa miaka sita mfululizo visiwani. Lakini si Mzanzibari aliyeishi Tanzania Bara kwa kipindi hicho kuweza kuitwa Mtanzania Bara; yeye huyo, anabakia “Mzanzibari” tu.

Ili kumpata mrithi wake kati ya hao watatu, Mwalimu Nyerere alianzisha mchezo wa karata za kisiasa kwa “kuwashika” wajumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM. Kwa bahati mbaya sana, vyombo  hivi - CC na NEC, vilisheheni makundi yenye uhasama, yaani kundi la “Wanamstari wa mbele” na kundi la “Wakombozi”; kila kundi likiwania kumwangamiza mwenzake. Miongoni mwa kundi la “Wanamstari wa mbele” walikuwemo ni Dk. Salim Ahmed Salim, Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu wa CUF sasa), Hamad Rashid Mohamed (Mbunge wa Wawi-CUF) na Khatib Hassan.

Wengine walikuwa ni Kanali Adam Mwakanyuki, Isaac Sepetu, Shabaani Mloo, Ali Salim na Ali Haji Pandu.


Kundi la wakombozi, ambalo lilijiona kama warithi halali wa sera za Karume na ASP, lilikuwa na Brigedia Abdullah Said Natepe (kiongozi wao), Ali Mzee, Hassan Nassoro Moyo, Muhamed Seif Khatib na Salmin Amour.

Walikuwamo pia maofisa wastaafu wa jeshi  na wa Idara ya Usalama wa Taifa kama Brigedia Ramadhan Haji ambaye pia alikuwa Waziri Kiongozi wakati wa Jumbe; Mkuu wa Jeshi la Zanzibar mstaafu, Brigedia Jenerali Khamis Hemed na wengineo.

Tangu mwanzo, “Wakombozi” hawakumtaka Dk. Salim. Itakumbukwa, kwa mfano, mwaka 1982, pale Dk. Salim alipoteuliwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Muungano, Natepe (wakati huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais wa Muungano, mwenye dhamana ya Usalama wa Taifa) na Ali Mzee (aliyekuwa na wadhifa kama huo kwa Serikali ya Zanzibar), walikwenda kwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine, kumwambia kwamba, walikuwa na mamlaka kutoka kwa Rais Jumbe na Seif Bakari, kuwataka Sokoine na Mwalimu, wafute uteuzi wa Salim.

Walitoa sababu kuu mbili:  moja ni kwamba, kulikuwa na makubaliano ya siri ya kudumu tangu utawala wa Karume, kwamba wanachama wote wa vyama vya siasa vya zamani mbali na ASP, wasishike nyadhifa zozote za uongozi wa kichama na kiserikali visiwani na kwenye Muungano, bali watumike kwa kazi za kitaaluma tu. Salim alikuwa mmoja wa viongozi wa Chama cha Kikomunisti cha “Umma Party”, kilichosimamia kishujaa Mapinduzi ya Januari 12, 1964, kwa kushirikiana na vijana wenye siasa za mrengo wa Kikomunisti ndani ya ASP, akiwamo Kassim Hanga na wengine.

Kwa mantiki hiyo, walengwa wa makubaliano hayo ya siri walikuwa Wazanzibari wote, ndugu na koo zao, waliowahi kuwa wanachama wa vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP), Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) na Chama cha Umma Party (UP) cha Abdulrahman Babu.

Uhasama huu wa kihistoria umedumu kwa zaidi ya nusu karne mpaka hivi karibuni, ilipoundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani. Baadaye katika uhasama huo, nafasi ya ASP ilichukuliwa na CCM Zanzibar; na ile ya ZNP/ZPPP/UP ilichukuliwa na CUF Zanzibar. Ni kwa sababu hii, kulikuwa na msuguano mkali wa CCM na CUF Zanzibar, na si hivyo kwa vyama hivyo Tanzania Bara.

Pili, walidai kuwa, Wazanzibari wanapoona mtu suriama wa Kiarabu na Kiafrika kama Salim akishika nafasi za madaraka, inawakumbusha chuki kubwa ya utawala wa Sultani aliyepinduliwa.

Lakini pamoja na uongo huo wa kizandiki, “Wakombozi” hao walisahau kwamba, kufuatia Mapinduzi ya Januari 12, 1964, Karume alimteua Salim Ahmed Salim, Balozi wa Zanzibar nchini Misri.

Sokoine, Waziri Mkuu ambaye hakuvumilia mizaha, majungu na uzandiki, aliwafukuzia mbali wazushi hao, na nyota ya Salim ikazidi kung’ara kiasi kwamba, Sokoine alipofariki Salim alirithi nafasi yake.

Wakombozi hawakukubali kushindwa; walibadili staili kwa kuanzisha kampeni Tanzania Bara dhidi ya Salim, safari hii kwa kudai kwamba alikuwa hakubaliki visiwani, na pia kwamba kama angepewa madaraka, angeshirikiana na nchi za Kiarabu kurejesha ubepari nchini.

Hapo tena, hawakujua kuwa nchi yetu ilikuwa mbioni kupata Ubalozi wa Saudi Arabia nchini, na pia ilitarajia kufungua Ofisi za Ubalozi kwenye nchi nyingi za Kiarabu.

Kisha wakaja na tuhuma nzito zaidi, kwamba Salim alihusika na kifo cha Karume mwaka 1972, wakati huo akiwa Balozi nchi za nje. Karume aliuawa kwa kupigwa risasi, Aprili 7, 1972 na mwanajeshi, Luteni Hamud, kulipa kisasi kwa uhasama wa kisiasa.


Nassoro Hassan Moyo, ndiye alikuwa kiunganishi kikubwa kwa kundi la visiwani na kundi la Tanzania bara katika kuhakikisha kwamba jina la Salim halipiti; akisaidiana na Ramadhan Haji, Ali Mzee na Aboud Talib, wote wa Visiwani.

Kiunganishi mkubwa kwa Bara kwenye CC na NEC katika kampeni hizo, alikuwa Waziri wa Mali asili na Utalii, Paul Bomani. 

Ali Hassan Mwinyi alionwa na “Wanamstari wa mbele” siku ya uteuzi, wakiamini kwamba walikuwa wamemshawishi kikamilifu na vya kutosha kuweza kukubali kutogombea. Hata hivyo, mambo hayakuwa hivyo Agosti 12, 1985, pale CC ilipoketi kupendekeza jina la mgombea, wakati ahadi ya Mwinyi ya kujitoa ilipoota mbawa.

Mwalimu Nyerere alielewa fika jinsi mchezo huo mchafu wa kupakana matope na kubomoana, ulivyokuwa ukichezwa. Licha ya kumpendelea Salim, lakini hakutaka kuonyesha, wala kuegemea upande wowote.

Rashid Kawawa, kama ilivyotarajiwa, alijiengua; wakabakia Mwinyi na Salim, kisha wakaombwa watoke nje ya chumba, ili wajadiliwe.

Kilichotawala mjadala pekee ni sifa za Mwinyi, kiasi kwamba Salim hakujadiliwa. Wakombozi walitumia vyema muda huu, huku Moyo na Natepe wakitawala mazungumzo.

Mjumbe mwingine wa CC wa Kambi ya Bomani aliyezungumza kwa kirefu, alikuwa Mama Getrude Mongela. Hoja yao ilikuwa kwamba, kumruka Mwinyi ambaye alikuwa Makamu wa Rais na Makamu wa chama tawala na kumteua Salim, kungetafsiriwa vibaya ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kwamba, Watanzania hawakuwa na mipango thabiti ya kuandaa watawala na kurithishana madaraka. Isitoshe, Mwinyi angejiona vibaya kwa kurukwa. Kwa njia hii, Mwinyi akaibuka mshindi kama pendekezo la CC kwenda NEC kwa uteuzi wa mwisho.

Mwinyi angeweza kujitoa kutekeleza ahadi yake kwa Nyerere na kwa kambi ya Wanamstari wa mbele, lakini hakufanya hivyo, badala yake alisema:  “Kama haya (uteuzi) ni mapenzi ya wananchi, nakubali”.  Mwalimu Nyerere, aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao, hakupinga, pengine kwa kutarajia kwamba NEC ingemwinua Salim.

Kambi ya Wakombozi ilitamba kwa kulamba dume kwa mara nyingine kwenye kikao hicho, ilipofika uteuzi wa mgombea kiti cha Rais wa Zanzibar, baada ya kupendekeza kwa sauti moja, jina la Idrisa Abdul Wakil, ambapo Wanamstari wa mbele walimpendekeza Seif Sharrif Hamad.

Mapendekezo ya CC yaliwasilishwa NEC Agosti 15, 1985 kwa uteuzi wa mwisho.  Kwenye kikao hicho, kambi ya “Wanamstari wa mbele” ilipata mtetezi kwa jina la Mzee Thabit Kombo, swahiba mkubwa wa Nyerere; aliyewasilisha hoja kwamba, kumtoa Mwinyi Zanzibar ili awe Rais wa Muungano, kungevuruga hali ya amani na utulivu aliyosaidia kujenga na kusimika katika uongozi wake wa miezi 18 tu Visiwani.


Kauli ya Kombo ilimezwa kwa sauti za kupinga za wajumbe wa NEC kutoka Bara, kuonyesha kwamba Bomani na Mongela walikuwa wamefanya kampeni yao vyema. Nyerere akaahirisha kikao kwa muda, akawaita pembeni wasiri wake wachache, wakiwamo Mwinyi, Kawawa na Kombo; wote hao, wakateta jambo.

Kikao kiliporejea, Kombo alikuwa amegeuka, alimuunga mkono Mwinyi; na kwa mara ya kwanza alimuunga mkono Wakil, kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar. Kura zilipopigwa, ni kura 14 tu kati ya 1,746 zilizomkataa Mwinyi.

Kwa upande wa Zanzibar, ambapo ni wale wajumbe 163 tu wa NEC kutoka Zanzibar waliokuwa na haki ya kupiga kura kwa uteuzi wa Rais wa Zanzibar, Wakil alipata ushindi mdogo wa kura 85 dhidi ya 75 za Seif Sharrif Hamad.

Ushindi huo kwa nafasi zote mbili uliwapagawisha kambi ya wakombozi, wakaonekana kuchezesha maungo yao dhahiri hadharani, huku Getrude Mongela akipiga mbiu kwamba ni wao, waliopendekeza jina la Mwinyi na la Wakil, kwenye CC; na kupigana kufa na kupona kwenye NEC kuokoa jahazi.

Kwa kambi ya “Wakombozi” kutoka Bara, ushindi wa Mwinyi uliwafanya wapumue kwa matarajio, kwamba angalau sasa nchi ingetawaliwa  na mtu (Mwinyi) asiye na makuu, asiye na msimamo, msikivu lakini rahisi kuyumbishwa; kuliko kama angetawala Salim, kiongozi mwenye kujiamini, mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kujenga hoja, mchangamfu lakini mwenye tahadhari daima.

Shamra shamra za “ushindi” wa “Wakombozi” zilivyozidi kuwa adha kubwa hata wakati wa Kampeni za Urais Zanzibar, ilibidi Nyerere, Mwinyi na Kawawa wavae njuga kuzikabili, ili kufuta dhana kwamba “Wakil amepona kutoswa” kwa nguvu na Wakombozi na kuanza kuwasafisha Wanamstari wa mbele ili wasidhalilishwe bila sababu za msingi.  Mwalimu, huku akimlenga Natepe na kundi lake alisema:

“Nataka mjue kwamba, nawaelewa vyema vijana (Wanamstari wa mbele) hawa. Ni vijana wakweli makini na si wasaliti.  Sitavumilia kuona wakichukuliwa kuwa maadui (wa Zanzibar na Wazanzibari). Na hilo ndilo agizo langu”.

Katika uchaguzi wa Rais wa Zanzibar mwaka 1985, mgombea pekee, Abdul Wakil Nombe, alipata ushindi duni wa asilimia 58.6 tu, ambapo kwa Pemba pekee, alipata chini ya asilimia 25.

Pamoja na kinyang’anyiro cha madaraka miongoni mwa Wana-CCM Zanzibar kufikia kikomo, bado mpasuko kwa njia ya vikundi hivyo vyenye uhasama uliendelea chini kwa chini. Na kwa sababu CCM kilikuwa Chama cha kitaifa, migongano yote ya Zanzibar ililetwa kwenye NEC Tanzania Bara (Dodoma) kwa usuluhishi na uamuzi.

Hata hivyo, hali ilipoendelea hivyo, miaka miwili baadaye, yaliandaliwa mashitaka toka CCM Zanzibar, dhidi ya “Wanamstari wa mbele” saba, maarufu kama “the magnificent seven”, kisha NEC ikakaa Kizota, Dodoma na kuwafukuza uanachama Seif Sharrif Hamad, Shabaan Mloo, Ali Haji Pandu, Khatib Hassan, Soud Yusuf Mgeni, Hamad Rashid na Ali Salim.

Kundi hili la waliofukuzwa, lilijikusanya na kuanzisha Chama cha upinzani kwa siri, kwa jina la “Kamati ya Mwelekeo wa Vyama Huru” (KAMAHURU) ambacho, miaka minne baadaye juu yake, pamoja na vyama vingine, palimea na kukua Chama cha Wananchi – CUF, chenye nguvu kubwa karibu sawa na CCM Visiwani.

Leo, CUF Zanzibar na CCM Zanzibar vimefunga ndoa kuwa mwili mmoja chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Je, ndoa hiyo itaweza kuondoa au kufuta kabisa minyukano ya chini kwa chini miongoni mwa “Wakombozi” na “Wanamstari wa mbele” ndani ya Serikali hiyo?.  Muda, kama ilivyo ada, ni shahidi wetu mzuri.
(Mwisho).

No comments:

Post a Comment