USAFIRISHAJI DAWA ZA KULIVYA KUPITIA NCHINI TANGANYIKA WABAINIKA NA MAKACHERO WA KIMATAIFA.
*Makachero wa kimataifa wabaini ni kituo cha dawa za kulevya*Inapokea shehena ya zaidi ya dola bil 2 kila mwaka
*Wasichana wa Kitanganyika watumika kama makontena ya kubeba dawa hizo, Serikali ya Tanganyika yakiri.
IMEBAINIKA kuwa Tanganyika ni miongoni mwa nchi tatu kubwa duniani zinazotumika kama kituo cha usambazaji wa dawa za kulevya katika nchi za ukanda wa maziwa makuu na zile zilizoko kusini kwa jangwa la sahara.
Utafiti wa uliofanywa na taifa moja kubwa la Ulaya Magharibi, kuhusu biashara ya dawa za kulevya barani Afrika tulidokezwa, umethibitisha pasipo shaka kuwa nchi za Amerika ya Kusini na zile za Bara la Asia zinazojihusisha na uzalishaji na uuzaji dawa za kulevya, zimekuwa zikiitumia nchi ya Tanganyika kama kituo chake muhimu kusambaza dawa hizo sehemu mbalimbali duniani.
Kubainika kwa ukweli huo, kunathibitishwa na idadi kubwa ya makachero wa mataifa makubwa ya Magharibi waliopo nchini Tanganyika wanaoendesha uchunguzi wa siri wa mwenendo wa biashara ya dawa za kulevya na namna ambavyo Watanganyika wanatumika kufanikisha biashara hiyo, kama wasafirishaji wakuu kwa nchi za jirani hususani zilizo kusini mwa Afrika.
Vyanzo mbalimbali vya habari vilivyofikiwa vimeeleza kuwa wafanyabiashara wakubwa wa mihadarati kutoka mataifa ya Bara la Asia yanayostawisha mimea inayozalisha aina ya dawa hizo, katika miaka ya karibuni wamekuwa wakitumia Pwani ya Tanganyika kama kituo kikuu cha kusafirishia bidhaa zao.
Mataifa ambayo wafanyabiashara wake wamebainika kuitumia zaidi Pwani ya Tanganika katika biashara hiyo haramu ni Pakistani na Afghanistan ambayo yanafahamika zaidi kwa uzalishaji wa dawa za kulevya aina ya Heroin na Opium.
Mataifa mengine ni yale ya Amerika Kusini ya Columbia na Bolivia ambayo ni maarufu kwa uzalishaji wa Heroin ambayo pia yameigeuza Pwani ya Tanganyika kuwa kituo chake kikuu cha usafirishaji dawa za kulevya.
Mawakala wa dawa za kulevya kutoka mataifa hayo wamekuwa wakisafirisha bidhaa zao kwa njia ya maji hadi karibu na Pwani ya Bahari ya Hindi kwa upande wa Tanganyika na kutia nanga kati kati ambako boti za wavuvi zimekuwa zikitumika kwenda kuchukua mzigo na kisha kuipitisha katika bandari bubu zaidi ya 30 zilizoko Pwani na Dar es Salaam na nyingine nyingi katika maeneo ya Tanga, Bagamoyo, Mtwara na Lindi.
Utafiti katika maeneo hayo ya bandari bubu umeonyesha kuwa mawakala wa dawa za kulevya husafirisha mizigo yao kwa njia ya maji hadi Dar es Salaam.
Habari zaidi zinaeleza kuwa wakiishafikisha mizigo yao Dar es Salaam ambako wafanyabiashara za mihadarati kutoka sehemu mbalimbali duniani huinunua na kuisafirisha kwenda nchi za Ulaya Magharibi kwa kutumia ndege ndogo zinazotumika kubeba watalii ambako si rahisi kukamatwa.
Baadhi ya watu waliohojiwa kuhusu usafirishaji wa dawa hizo walieleza kuwa baada ya kufikishwa Dar es Salaam na kununuliwa na wafanyabiashara wakubwa, hukodisha ndege ndogo zinazotumiwa na watalii hususan wanaotoka Italia ambazo huruka moja kwa moja pasipo kusimama njiani. Usafiri huo unaaminika kuwa salama zaidi kwa kusafirisha dawa za kulevya kwa sababu ndege zinazotumika hazipiti kituo chochote na hivyo hazina ukaguzi wa kutosha.
Utafiti mwingine umeonyesha kuwa kama wauzaji wanataka kusafirisha mzigo kwenda sehemu nyingine wanawatumia wasichana wa Tanganyika ambao wanasafirisha dawa za kulevya wakitokea Dar es Salaam na Bagamoyo kwenda nchini Afrika Kusini wakitumia usafiri wa basi.
Taarifa zinaonyesha kuwa wasichana hao hupakizwa dawa za kulevya tumboni na kusafiri kwa njia ya basi hadi mji mkuu wa Pretoria Afrika Kusini ambako baada ya kuupakua kwa njia ya haja kubwa, mzigo unaotakiwa kubaki Afrika Kusini utabaki na ule unaotakiwa kusafirishwa kwenda nchi nyingine taratibu nyingine hufanywa nchini humo.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, ili kuondoa mashaka wasichana hao hulazimika kukaa nchini humo kwa kipindi cha miezi miwili hadi mitatu wakifanya biashara ya ukahaba ili kuondoa mashaka kwa vyombo vya ulinzi vya nchi hiyo kisha hurudi katika vituo vyao vya Dar es Salaam na Bagamoyo ambako hupakizwa mzigo mwingine.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, ambaye ofisi yake inahusika na udhibiti wa dawa za kulevya alipoulizwa kuhusu habari hizi alitaka atafutwe Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa dawa za kulevya Christopher Shekiondo.
Shekiondo alikiri Meli hizo kubwa kuleta madawa ya kulevya zikitokea katika nchi za Afghanistan na Pakistani lakini alisema hafahamu kuhusu makachero wa kimataifa kuendesha uchunguzi huo hapa nchini.
“Ni kweli katika harakati zetu za ukamataji tumegundua meli kubwa zimekuwa zikija hadi maeneo ya karibu na pwani katikati ya maji, ambako boti ndogondogo za wavuvi zimekuwa zikifuata na kuja kupitisha kwenye bandari bubu za Dar es Salaam, Bagamoyo, Lindi na Mtwara”
Alisema kiasi chote cha dawa za kulevya kinachozalishwa nchini Afghanistan asilimia zaidi ya 82 kinasafirishwa kwenda katika nchi za Iran, Pakistani na Tanganyika (Tanzania)
Kamishna Shekiondo alipoulizwa ni kiasi gani cha dawa za kulevya kinaletwa na meli hizo, alisema si rahisi kufahamu lakini akasema ni kingi ukilinganisha na kile kinachopitishwa kwa njia ya kumeza.
“Wanaopitisha kwa meli ndio wanaoingiza kiasi kingi kama kilogramu 100-200 lakini wanaomeza wanaweza kumeza kama kilogramu moja kasoro” Alisema Shekiondo.
Kuhusu wasichana wa kitanganyika kutumika, Shekiondo alikiri na kusema kuwa si Afrika Kusini tu bali hata katika maeneo mengine duniani wamekuwa wakitumika.
Shekiondo alisema wapo wasichana wa kitanganyika wengi tu katika magereza ya nchi mbalimbali duniani, huku akitolea mfano Brazil ambako kuna Watanganyika takribani 100.
“Marekani, Argentina, Perue, China mpaka Japan na Australia Watanganyika wako wengi tu huko wamekamatwa na sisi hapa tunaendelea kupata taarifa juzi tu tumekamata kilogramu 3, Lindi tulikamata kilo 81 za Cocaine, kilo 92 tulikamata Tanga” alisema
Alisema wanachofanya wao kwa sasa ni kuendelea na mchakato wa kupata taarifa zaidina kuwafahamu watu wanaoingiza dawa za kulevya ili waweze kuchukuliwa hatua na kukomesha biashara hiyo.
No comments:
Post a Comment