Tuesday, June 25, 2013

RAISI UHURU KENYATTA ZIARANI NCHINI URUSI, CHINA NA JAPAN WIKI HII.


Nairobi. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, anatarajiwa kuanza ziara ya wiki tatu katika mataifa ya Ulaya Mashariki na Asia, katika kile kilichoelezwa kwamba ni kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi hizo na Kenya.
Uhuru anatarajiwa kuondoka mjini Nairobi wiki hii kuelekea Moscow, Russia kabla ya kuzuru China na hatimaye Japan.
Uhuru anafanya ziara hiyo na huku  Rais Barack Obama wa Marekani anayetarajiwa kutua nchini Tanganyika wiki ijayo.
Kiongozi huyo wa Marekani anakuja nchini Tanganyika akiwa katika ziara yake ya pili katika bara la Afrika.
Uhuru  itakuwa ni safari yake ya kwanza kuzuru nchi za mataifa ya Ulaya Mashariki na Asia katika mabara hayo.
Hata hivyo ziara hiyo haitamfikisha katika nchi ya asili yake, Kenya raisi Obama.
Katika siku ambazo Obama atakuwa nchini Tanganyika, Uhuru atakuwa nchini China, moja ya mataifa hasimu ya Marekani, akitokea Russia, taifa hasimu kwa Marekani pia.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wasaidizi wake wakuu, Rais Uhuru anahitaji kutumia fursa ya umuhimu wa mataifa ya mashariki katika kukuza uchumi wa Kenya kwa kuimarisha zaidi uhusiano wa kibiashara.
Akiwa nchini Urusi, Uhuru atatembelea viwanda vya silaha na kukutana na maofisa wa juu wa Serikali, kisha kutia saini makubaliano yanayohusu biashara baina ya nchi yake na Urusi.
“Ziara hii ilipangwa mahususi kwa Rais Uhuru Kenyatta kutembelea nchi rafiki na haikuwa na uhusiano wowote na ziara ya Obama nchini Tanganyika,” alisema mhadhiri Profesa Munene Macharia.
Alisema nchi hiyo kwa sasa inajaribu kutoa kipaumbele kwa nchi marafiki zinaonyesha utayari wa kushirikiana na Kenya, akizitaja kuwa ni Urusi na China.
Kuhusu ziara hiyo, wasaidizi wa Rais Uhuru wamekanusha taarifa kwamba imenuia kujenga himaya mpya na nchi mahasimu wa Marekani katika kipindi ambacho Obama anatembelea bara la Afrika.

No comments:

Post a Comment