Mheshimiwa Spika, Tangu tuanze Mkutano huu wa Bajeti mwaka 2016 kumekuwa na malalamiko kutoka kwa Wabunge na hasa wabunge wa kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu ukiukwaji wa Sheria mbalimbali za nchi katika masuala ya Bajeti.
Jana jioni Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Andrew Chenge alitoa Changamoto kuwa Wabunge tuseme ni sharia gani zimekiukwa katika mchakato mzima wa Bajeti ya Nchi hivi sasa. Kwa maoni yangu, kuna ukiukwaji kadhaa wa sharia ya Bajeti, sharia namba 11 ya mwaka 2015 katika mchakato wa Bajeti ya Mwaka huu. Nitaeleza kwa ufupi.
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 8 cha sheria ya Bajeti kinaeleza namna ambavyo mfumo wa Bajeti ya Serikali unapaswa kuwa.
Vifungu cha 8(1)(b) na 9(1)(a) na 19(1) vinaeleza namna mchakato wa Bajeti unavyopaswa kuwa. Vifungu hivi vinataka “Planning and Budget Guidelines” zipitishwe na Bunge katika mkutano wake wa Mwezi Februari kila mwaka. Sheria inataka “budget ceilings” ziidhinishwe na Kamati ya Bajeti na baadaye Bunge linapokaa kama Kamati ya Mipango.
Mheshimiwa Spika, Bunge lilikaa kama Kamati ya Mipango na kupitisha Mpango wa Bajeti uliokuwa na Bajeti ya Tshs 23.7 trilioni kama ulivyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango. Hata hivyo Bajeti inayojadiliwa sasa ni Tshs 29.5 trilioni tofauti kabisa na sio tu viwango vilivyopitishwa na Bunge mwezi Februari bali pia hata vipaumbele vyake ni tofauti.
Hili ni suala la Utawala bora (governance issue) kwani taratibu za utungaji wa Bajeti zimeainishwa na sheria na kama sheria hazifuatwi ni vigumu sana hata Bajeti yenyewe kutekelezwa.
Ili kurekebisha hali hii ni lazima Bunge likae tena kama kamati ya Mipango na kupitisha upya viwango vya juu vya bajeti kabla ya mjadala wa Bajeti kuendelea au angalau kabla ya kupitisha Bajeti Kuu mwezi wa Juni 2016.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais Ikulu inapasa kuzingatia sana sheria na taratibu tulizojiwekea kwani madhara ya kutofuata sheria ni makubwa mno.
Kwa mfano hivi sasa Bajeti za Taasisi hazimo kwenye vitabu vya Bajeti ya Serikali kinyume na Sheria ya Bajeti ambapo hivi sasa Bajeti za Taasisi zote za Umma zinakuwa ni sehemu ya Bajeti ya Serikali na Wabunge wanapaswa kuwa na nyaraka za bajeti hizo.
Ofisi ya TR kwa mujibu wa kifungu cha 17(a) cha Sheria ya Bajeti ilipaswa kuunganisha Bajeti za Mashirika yote ya Umma na kutoa kitabu chake kwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapaswa kutoa maelezo ya kina kwa Wabunge kuhusu masuala haya ili kuzuia ukiukwaji wa Sheria tulizojitungia wenyewe.
TAKUKURU na kesi za Ufisadi Mkubwa Nchini
1. Ufisadi wa Hati Fungani ya Tshs 1.2 trilioni Standard Bank ya Uingereza
Mheshimiwa Spika, Tarehe 8 Machi mwaka 2013 Serikali ya Tanzania ilikopa fedha $600 milioni ( 1.2 trilioni) kutoka nje kwa msaada wa Benki ya Standard ya Uingereza ambayo sasa inaitwa Standard Bank ICIC Plc. Mkopo huo wenye riba yenye kuweza kupanda (floating rate) umeanza kulipwa mwezi Machi mwaka huu ( kama Serikali imeanza kutekeleza mkataba).
Mkopo huu utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo 9 inayolingana. Ifikapo mwaka 2020, Tanzania italipa deni pamoja na riba jumla ya $897 milioni ( takribani tshs 2 trilioni ).
Mkopo huu umegubikwa na ufisadi na kwa kuwa baadhi ya Watanzania wamefikishwa mahakamani kuhusiana na sehemu ya mkopo huu, sitapenda kueleza upande wa waliopo mahakamani.
Kesi iliyopo mahakamani inahusu $6 milioni ambazo inasemekana ( kwa mujibu wa nyaraka za mahakama) kuwa zilitumika kuhonga maafisa wa Serikali ili Benki hiyo ya Uingereza iweze kupata biashara iliyopata.
Jambo la kushangaza ni kwamba wanaosemekana kula rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa. Vile vile waliotoa rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa. Waliopo mahakamani ni wanaosemekena kutumika kupeleka rushwa.
Mjumbe kashtakiwa, lakini aliyemtuma hajashtakiwa na aliyepelekewa kilichotumwa hajashtakiwa. Hapa kuna tatizo la msingi ambalo tukilitatua Serikali yetu itaepuka masuala kama haya siku za usoni.
Mheshimiwa Spika, Hapa mbele yangu nina barua ambayo kundi la Watanzania zaidi ya 2000 kutoka kona zote za dunia wamesaini kutaka Benki ya Standard ya Uingereza ichunguzwe kwenye suala hili la HatiFungani.
TAKUKURU walitumia taarifa ya Taasisi ya Uingereza ya SFO katika kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya Watanzania wanaotajwa katika sakata hili.
SFO haikufanya uchunguzi dhidi ya Benki ya Uingereza ya Standard Bank. Hatujui ni kwa maslahi mapana ya Uingereza au ni kwa kupitiwa. Sisi Tanzania tumejikuta tunafuata matakwa ya Uingereza katika jambo hili, kiasi cha hata kutumia ushauri wa kitaalamu wa Waingereza katika jambo hili.
Leo hii TAKUKURU inasaidiwa katika kesi hii na wataalamu kutoka Uingereza katika kesi inayohusu Benki ya Uingereza! Watanzania walioandika petition kutaka Benki ya Standard kuchunguzwa wanataka ukweli wote kujulikana – Standard Bank walihusika kwa kiwango gani katika kutoa rushwa ili kupata biashara? TAKUKURU wanapaswa kufanyia kazi jambo hili kwa kuwafungulia mashtaka Standard Bank, mashtaka ya kutoa rushwa ili kupata biashara nchini.
Hata hivyo TAKUKURU inaogopa wazungu, inaogopa kuwaudhi watu wanaowapa ushauri wa kitaalamu kuhusu kesi za rushwa!
Mheshimiwa Spika, maslahi ya Tanzania hapa ni makubwa mno. Iwapo tutafanikiwa kuonyesha kuwa Benki ya Standard ilihonga kupata biashara nchini kwetu Tanzania itafaidika kwa namna mbili.
Moja, itakuwa ni fundisho kubwa kwa makampuni ya kimataifa kwamba Afrika sio mahala pa kuhonga na kupata kazi na kutoadhibiwa. Mbili, Tanzania haitalipa mkopo huu na riba zake.
Tutakuwa tumeokoa zaidi ya tshs 2 trilioni katika Deni la Taifa na kuelekeza fedha tulizokuwa tulipe riba kwenda kwenye kuhudumia wananchi wetu kwenye Afya na Elimu.
TAKUKURU waongozwe na maslahi mapana kwa Taifa badala ya kutafuta sifa ndogo ndogo za ‘wangapi wamefikishwa mahakamani’. Ni lazima taasisi zetu sasa zianze kutazama mambo kwa picha kubwa.
Mheshimiwa Spika, hii sio mara ya kwanza SFO kufanya ilichofanya dhidi ya Tanzania. Mnakumbuka kesi ya rada na Shirika la BAE la Uingereza. Safari hii Tanzania isikubali kubeba tu makubaliano ambayo SFO inafanya na makampuni ya kimataifa.
Ni lazima tufanye uchunguzi wetu na tufungue kesi dhidi ya makampuni haya. Haiwezekani wawe ni Watanzania tu wanaoshtakiwa kwa rushwa na kuwaacha wanaotoa rushwa hizo wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Mheshimiwa Spika, Taarifa zilizopo sasa kwenye vyombo vya habari ni kwamba Benki hii kupitia tawi lake la Tanzania ( Stanbic Bank ) siku ambayo walipata ‘deal’ la Bond ndio siku hiyo hiyo walipewa kazi na Serikali ya kufungua akaunti ya Escrow kuhusu fedha za Bomba la Gesi kutoka Mtwara.
Kimsingi biashara hii ya Escrow akaunti katika Benki hii ni kubwa zaidi kutoka ile ya mkopo kwani ni biashara ya kutunza fedha za Bomba kwa miaka 20! Benki hii ilipata biashara kubwa kama hii bila ya kuwepo kwa zabuni yeyote ile na kuleta ushindani.
Lakini pia kama kulikuwa na umuhimu wa kufungua akaunti hii ni kwanini Shirika la TPDC halikufungua akaunti hii katika Benki Kuu ya Tanzania? Haya ndio mambo TAKUKURU wanapaswa kuchunguza katika kulinda maslahi ya nchi yetu dhidi ya makampuni makubwa kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, Vile vile kuna taarifa kwamba hata fedha ambazo zilipatikana kutokana na mkopo huu hazikufika kule kunakotakiwa.
Nimewasilisha maswali Wizara ya Fedha kutaka kujua miradi ambayo fedha hizi zilikwenda. Hata hivyo kutokana na orodha ya miradi niliyonayo na kutokana na habari za hivi karibuni za Serikali kudaiwa na wakandarasi, mradi wa Kinyerezi na hata mradi wa Kiwira, ni dhahiri kuwa sehemu ya fedha zilizopatikana katika mkopo huu hazikupelekwa huko. Uchunguzi wa kina unatakiwa kwenye eneo hili ili kupata ukweli na kuzuia mambo kama haya kutokea siku za usoni.
Mheshimiwa Spika, nitatumia kanuni ya 120(2) kutaka Bunge tako tukufu kuunda Kamati Teule kuichunguza Benki ya Standard ICBC ya Uingereza na kampuni yake dada ya Stanbic Tanzania kuhusiana na Mkopo wa Hatifungani $600m, matumizi ya mkopo huo na ufunguzi wa Akaunti ya Escrow ya Bomba la Gesi la Mtwara – Dar es Salaam.
Kwa sasa ninawasilisha mezani nyaraka zote nilizonazo kuhusiana na Mkopo huu kwa ajili ya Bunge kupitia kabla ya kuwasilisha Hoja ya Kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuichunguza Standard Bank ICBC na Stanbic Tanzania
2. Uchunguzi wa IPTL Tegeta Escrow Account
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2014 TAKUKURU waliijulisha Kamati ya Bunge ya PAC kwamba ilikuwa inachunguza na kumaliza uchunguzi kuhusu miamala ya kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow Benki Kuu ya Tanzania kwenda Benki ya Stanbc Tanzania.
Katika taarifa zote ambazo TAKUKURU inatoa kuhusu kesi za ufisadi, hakuna hata siku moja wanasema kuhusu uchunguzi huu na lini wahusika waliochota fedha za umma watafikishwa mahakamani. Naomba tupate kauli ya Serikali kuhusu jambo hili kwani ni moja ya JIPU kubwa ambalo tunadhani Serikali inalikimbia.
Serikali inaogopa nini? Serikali inamwogopa nani? Kwanini kesi ya ufisadi wa IPTL unakaliwa kimya? Kwa maslahi ya nani?
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kigoma Mjini