Walisomewa mashitaka ya kufanya hujuma kwa kutoa maneno ya uchochezi katika mihadhara mbalimbali katika maeneo ya miji ya Unguja kuanzia Mei 26 hadi Oktoba 19 mwaka jana na kuwachochea wananchi kuvunja amani na kuharibu mali zilizogharimu sh. 500 milioni.
Akisikiliza kesi hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Mkoa, Yessaya Kayange alikataa kutoa dhamana kwa washitakiwa kwa vile kuna hati ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) inayozuia kupewa dhamana kwa washitakiwa hao.
Hakimu Kayange kuhusu ombi la washitakiwa la kutaka kesi yao isikilizwe Mahakama Kuu alisema ombi hilo tayari limeshapelekwa na yasubiriwe maamuzi. Wakili wa upande wa utetezi, Abdallah Juma alidai washitakiwa hao hawapaswi kushitakiwa kwa sheria ya Usalama wa Taifa na wakaongezewa mashitaka mengine na kuongeza kuwa washitakiwa wote wanaweza kupewa dhamana.
“Wateja wangu wamefungwa midomo katika mahakama hii. Kila siku wanaletwa hapa na hawatakiwi kusema chochote, kwa hiyo naomba wapelekwe Mahakama Kuu mbele ya Jaji ili waweze kupewe haki ya kusema kwani huenda wenyewe wakakiri wote makosa yao,” alidai Wakili Juma.
Wakili Juma alidai kwa vile Mahakama ya Mkoa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo basi haina haki pia ya kuwapeleka rumande na kuwataka wateja wake waachiwe na kurudi nyumbani. Upande wa mashitaka ukiongozwa na Rashid Abdallah na Raya Mselem walikataa madai ya wakili wa utetezi wa kesi hiyo kusoma upya kwa vile wameongezwa washitakiwa wawili na kwamba hawana pingamizi na suala la dhamana lakini waendelee kushitakiwa kwa sheria hiyo hiyo ya Usalama wa Taifa.
Kesi hiyo inasikilizwa chini ya ulinzi mkali na polisi wamekuwa wakiwanyanyasa waandishi wa habari kwa kuwazuia na mwandishi mmoja jana alipigwa virungu viwili na askari mmoja. Washitakiwa wa zamani katika kesi hiyo ni Sheikh Farid Hadi Ahmed (41), Msellem Ali Msellem (52), Mussa Juma Issa (37), Azzan Khalid Hamdan (48), Suleiman Juma Suleiman (66), Khamis Ali Suleiman (59), Hassan bakar Suleiman (39) na Gharib Ahmad Omar (39). Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Januari 14 mwaka huu
No comments:
Post a Comment