GAMAL ABDEL NASSER WAKATI WA UHAI WAKE ALIYEKUWA RAISI WA MISRI
YALIYOJIRI Misri tangu Jumatano iliyopita ni maafa makubwa. Ni maafa kwa Misri. Ni maafa kwa Afrika. Ni maafa kwa nchi zote zenye kuulea mfumo wa demokrasia uliomchanga katika nchi hizo. Michirizi ya damu imeonekana na itaendelea kuonekana katika sehemu mbalimbali za jiji hilo. Damu hiyo ni ya Wamisri na walioimwaga na wataoendelea kuimwaga ni Wamisri wenyewe. Wamekuwa wakitwangana risasi wenyewe kwa wenyewe usiku kwa mchana.
Wengi wetu barani Afrika tumeshika tama; twaililia Misri iliyomzaa Gamal Abdel Nasser, mmoja wa wana majumui wa Kiafrika aliyekuwa adhimu.
Wakati nchi nyingi za Kiafrika zilipokuwa zikitawaliwa na wakoloni, Nasser alikuwa pekee miongoni mwa viongozi wa nchi za Kiafrika aliyeufanya mji mkuu wa nchi yake uwe makao ya vyama vya ukombozi vya Kiafrika.
Vyama vingi vya Kiafrika vilivyokuwa vikiwania uhuru wa nchi zao vilikuwa na ofisi jijini Cairo. Kutoka kanda ya Afrika ya Mashariki kulikuwa ofisi za vyama vya Eritrea na Somalia. Kulikuwako pia ofisi za vyama vya Kenya African National Union (KANU), Uganda Peoples’ Congress (UPC) na Zanzibar Nationalist Party (ZNP).
Ingawaje, vyama vya Afro-Shirazi Party (ASP) na Tanganyika African National Union (TANU) havikuwa na ofisi Cairo. Mwanzoni Julius Nyerere, kiongozi wa TANU,hakuwa akimchangamkia Nasser. Alikuwa na wasiwasi kuhusu ushawishi wake Visiwani Zanzibar, hasa usuhuba wake na Ali Muhsin Barwani, kiongozi wa ZNP. Pia alikuwa na shaka kuhusu umaarufu wake miongoni mwa Waarabu waAfrika ya Mashariki.
Misri nayo kwa upande wake, ikiungwa mkono na wawakilishi wa vyama vingi vya ukombozi, mwanzoni ilikuwa haikupendezewa na sera za awali za Nyerere hasa baada ya Tanganyika kupata uhuru. Ikihisi kuwa sera hizo za Nyerere hazikuwa za kimapinduzi vya kutosha na zikipingana na wito wa Kwame Nkrumah wa Ghana wa kutaka bara la Afrika liungane.
Mahusiano kati ya Nasser na Nyerere yalitengenea baadaye Tanganyika ilipopata uhuru na zaidi baada ya kutolewa Azimio la Arusha.
Nasser na serikali yake waliviunga mkono kwa hali na mali hata vile vyama vilivyoamua kuchukua silaha na kupigana na wakoloni ili nchi zao ziwe huru. Kwa hivyo vyama hivyo navyo pia vilikuwa na ofisi zao Cairo.
Baadhi ya nchi zilikuwa na zaidi ya chama kimoja.Lengo la kwanza la chama chochote kipya lilikuwa ni kuelekea Cairo ili kiweze kuwapatia msaada watoto waweze kusoma bure Misri, kikubaliwe kuleta watu nchini humo kwa mafunzo ya kijeshi na kipatiwe nafasi ya kuwa na matangazo ya redio yatayorushwa hewani na Sauti ya Afrika kutoka Cairo.
Ofisi za vyama vyote hivyo, ambavyo wakati mmoja havikupungua 22, zilikuwa katika jengo moja la Rabta Afriqiyya (Jumuiya ya Kiafrika) lililokuwa katika njia ya Ahmed Hishmat Street katika mtaa wa Zamalek huko Cairo.
Katika jengo hilo uliwakuta watu kama akina Odhiambo Okello, aliyekuwa katibu wa Oginga Odinga wa KANU, Suleiman Malik mwakilishi wa chama cha ZNP, Amilcar Cabral kiongozi wa PAIGC cha Guinea-Bissau na Cape Verde, Agostinho Neto kiongozi wa chama cha MPLA cha Angola, John Kaley wa UPC, Felix Moumie, kiongozi wa chama cha UPC cha Cameroon, Sam Nujoma wa Swapo cha Namibia, Alfred Nzowa ANC cha Afrika Kusini au Joshua Nkomo wa ZAPU cha iliyokuwa Rhodesia ya Kusini.
Kadhalika, mji wa Cairo ndio uliokuwa makao makuu ya Sauti ya Afrika kutoka Cairo, ile stesheni ni ya redio niliyokwisha itaja ya kupigania uhuru na ukombozi wa Afrika. Stesheni hiyo ya redio ilikuwa ikitangaza kwa lugha 30 za Kiafrika, Kiswahili ikiwa mojawao.
Baada ya Patrice Lumumba wa Congo-Kinshasa kuuawa na Wabelgiji wakishirikiana na Waingereza pamoja na CIA, shirika la ujasusi la Marekani, Nasser aliagiza kwamba wana balozi wa Misri nchini Congo wafanye kila njia za kumkimbiza mjane wake Lumumba na wanawe hadi Cairo ambako waliishi.
Kwa hivyo Cairo, uliibuka kuwa mji mkuu wa kwanza duniani, kuipaza sauti yake kwa niaba ya Afrika nzima dhidi ya ukoloni.
Hivyo ndivyo ulivyokuwa mji wa Cairo katika miaka ya 1950 na 1960. Cairo pamoja na miji mingine nchini humo ili kuwa ni miji iliyojivunia uvumilivu na ustaarabu wao.
Hivyo ndivyo ulivyokuwa mji wa Cairo katika miaka ya 1950 na 1960. Cairo pamoja na miji mingine nchini humo ili kuwa ni miji iliyojivunia uvumilivu na ustaarabu wao.
Sio leo ambapo miji hiyo inawashuhudia Wamisri wakiuana kinyama wenyewe kwa wenyewe kwa sababu za kisiasa.
Hakuna aliyetarajia hali kama hiyo kuwa itatokea nchini humo kama tusivyoitarajia kutokea nchini mwetu. Na Mungu atuvue salama, atupishe mbali na hayo.
Pande zote mbili zilizoingia vitani nchini Misri zina makosa. Mohamed Morsi, Rais aliyepinduliwa, na vuguvugu lake la Moslem Brotherhood wamefanya makosa kadhaa.
Kosa moja ni kudhani kwamba wanaweza kufanya watakalo kwa vile wameshinda uchaguzi. Julai 2, Morsi alilihutubia taifa bila ya kujua kwamba hiyo ilikuwa mara yake ya mwisho kufanya hivyo kwani alipinduliwa siku mbili baadaye.
Katika hotuba hiyo Morsi alikariri mara chungu nzima kwamba yeye amechaguliwa na watu na hivyo ana uhalali wa kutawala. Yeye na wafuasi wake walisahau kwamba ushindi wao haukuwa wa kishindo na kwamba nchi iligawika takriban nusu nusu.
Kwa hakika mahasimu wake walimshambulia kwa namna alivyokuwa akishikilia kuwa uchaguzi ndio pekee wenye kumpa uhalali wa kutawala.
Lakini hawa pia wamekosea kwa kufikiri kuwa nguvu zao za kijeshi na mtindo wao wa kutawala kimabavu utawawezesha kuendelea kutawala nchini humo na kuyapindua mapinduzi yaliyompindua Rais wa zamani Hosni Mubarak.
Majeshi ya Misri yanaweza yakaendelea kuwaua wananchi wa kawaida wenye kuwaunga mkono akina Morsi na yanaweza yakaendelea kuwaminya na kuwakandamiza wananchi hao lakini iko siku — na siku hiyo haiko mbali — ambapo majeshi hayo yatashindwa na nguvu za umma.
Kila wananchi wanapodhalilishwa ndipo wanapozidi kusimama kidete kupamba na wanaowadhalilisha. Historia mara kwa mara imetufunza kwamba hayo yakijirudia ni majeshi huwa ndio yanayoshindwa.
Iwapo kuna majeshi kwingineko Afrika yanayotamani kuyaiga yanayotendwa sasa na majeshi ya Misri basi na yafikirie tena. Badali ya kutuletea kheri na ufanisi ukatili huo wa majeshi daima huleta nakama na huyarudisha nyuma maendeleo.
Iwapo kuna majeshi kwingineko Afrika yanayotamani kuyaiga yanayotendwa sasa na majeshi ya Misri basi na yafikirie tena. Badali ya kutuletea kheri na ufanisi ukatili huo wa majeshi daima huleta nakama na huyarudisha nyuma maendeleo.
No comments:
Post a Comment