Saturday, August 17, 2013

NCHINI TANGANYIKA ULINZI MKALI KATIKA MISIKITI KARIBU YOTE WAKATI WA SWALA YA IJUMAA


Nchini Tanganyika Dar es Salaam. Ulinzi mkali jana uliimarishwa jijini Dar es Salaam baada ya kuwepo kwa tetesi kwamba waumini wa Kiislamu wataandamana kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi kumuweka mahabusu Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanganyika, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Baadhi ya waumini walikuwa wameonyesha kukasirishwa na kitendo cha polisi kumwondoa Sheikh Ponda Hospitali ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na kumuweka Gereza la Segerea.
Kiongozi huyo alikuwa amelezwa (MOI) kwa madai ya kupigwa risasi na polisi begani akiwa mjini Morogoro.
Hata hivyo, akiwa bado anatibiwa (MOI), Jumatano alisomewa shtaka ati la uchochezi akiwa kitandani na Mwendesha Mashtaka wa Serikali ya Tanganyika, Tumaini Kweka akidaiwa kutenda kosa hilo katika maneo mbalimbali ya nchi kati ya Juni 2 hadi Agosti 11, mwaka huu.
Kutokana na fununu za baadhi ya waumini kupanga kufanya maandamano, ulinzi uliimarisha maeneo mbalimbali ya jiji hususan misikiti ambayo inadaiwa wanasali wafuasi wake.
Waumini katika Msikiti wa Mtambani jana waliswali swala ya Ijumaa katika usimamizi mkali wa magari matano ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
Hata hivyo, hali katika mazingira ya msikiti huo ilikuwa ni tulivu huku waumini wakisikiliza kwa makini kila kinachosemwa na viongozi wao, huku taratibu za ibada zikiendelea kama kawaida licha ya kuwepo kwa ulinzi mkali.
Mapema kabla ya kuswali swala ya Ijumaa ambayo iliswaliwa saa saba za mchana, gari tano za kikosi cha kutuliza ghasia zenye askari waliovalia kivita na zana za kazi ikiwemo bunduki, yalikuwa yameegeshwa mbele ya lango kuu la msikiti huo, kitu kilichofanya litolewe tangazo msikitini hapo la kuwataka Waislamu kuja kuswali bila kuogopa vitisho vya magari hayo.
Saa 5:18, lilisikika tangazo kutoka msikitini hapo ambalo lilisema, “Njooni msikitini msiogope vitisho vyao, hatutafanya vurugu lakini kama wanataka kupambana na sisi waje na tutapambana nao,” ilisikika sauti ya mtoa tangazo ndani ya kipaza sauti.
Baada ya swala magari ya askari yalipungua na kubaki magari matatu ambayo hadi saa 9:45, bado yalikuwa yameweka kambi upande wa pili wa barabara kwenye eneo ulipo msikiti huo.
Wakati wa ibada waumini hao walionyesha hisia zao baada ya kusomwa dua ya zaidi ya saa moja na nusu kama ambavyo hufanya kwenye swala ya alfajiri, na kilio kikatanda msikiti mzima yaani kwa upande wanawake na wanaume. Baada ya ibada alisimama kaka mkubwa wa Sheikh Ponda, Maabadi Issa Ponda na kusema kuwa wao kama familia wapo pamoja na waumini wa taasisi hiyo na hawajahuzunishwa hata kidogo na kilichomtokea ndugu yao kwa kuwa anafanya kazi ya Mungu, huku akisisitiza akaze uzi afanye zaidi ya alichokifanya malipo yake atayakuta mbele ya haki.
Mwisho wa ibada hiyo waumini waliamrishwa na viongozi wao kuondoka eneo hilo kwa kukwepa kuonekana wanafanya fujo na kuwapa nafasi wanaotaka kuwakamata baadhi ya masheikh kupata nafasi hiyo.
Kitu kilichokuwa sio cha kawaida ni wanawake wawili waliodaiwa kuwa Usalama wa Taifa kukamatwa wakiwa wamejipenyeza msikitini humo, huku wakiwa na rangi za kucha kitu ambacho Waislamu hawafanyi na kuwa na nywele za bandia kitu ambacho pia kwa Muislamu ambaye anaswali hawezi kuingia nazo msikitini na kuzuiliwa kuendelea kuwepo eneo hilo.
Hapo awali Saa 4:00 asubuhi Msemaji wa Jumuiya hiyo, Rajabu Katimba alizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti Sheikh Juma Saidi Ally, alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko makubwa kitendo alichofanyiwa Ponda na kwa kupigwa risasi na kutolewa hospitali wakati akiwa anapatiwa matibabu na kinyume cha haki za binadamu, utawala bora na uhuru wa maisha ya mtu.
Alisema jumuiya hiyo inapinga kwa kauli moja tume iliyoundwa na polisi kuchunguza tukio hilo, na hawatatoa ushirikiano wa aina yoyote katika tume hiyo.
Katimba alisema kuwa kutokana na tukio hilo, jumuiya hiyo imeitisha mkutano wa dharura utakaofanyika Viwanja vya Nurul- Yakin siku ya Jumapili saa 9:00 alasiri, kutafakari kwa pamoja na hatimaye kuchukua hatua za msingi zitakazoleta tija ya kweli ili viongozi wa Kiislamu wasiendelee kudhalilishwa.
“Hatupingi kukamatwa, wala kusomewa shitaka kwa kuwa ndiyo sheria, tunachopinga ni jinsi alivyokamatwa na kunyang’anywa haki yake ya kutibiwa,” alisema Katimba.
Misikiti mbalimbali ya Kariakoo kama Idrissa na Mtoro hapakuwa na maandamano wala fujo zozote zile na waumini walionekana kuhudhuria wengi kwenye ibada.
Katika misikiti hiyo askari polisi walionekana wakiwa wamesimama na silaha zao tayari kwa kupambana na fujo zozote ambazo zingeweza kutokea endapo maandamano yangefanywa kama ilivyo kuwa imepangwa, lakini hali ilionekana kuwa tulivu baada ya maandamano hayo kuahirishwa.
Baada ya ibada waumini hao walionekana wakisambaratika kwenda maeneo yao ya kazi huku askari nao wakiendelea na ulinzi ili kuahakikisha utulivu na amani ya kifitina.
Kwa ujumla eneo la Kariakoo lilikuwa tulivu huku watu wakiendelea na kazi zao kama kawaida licha ya kwamba wengi walihofia pengine kungekuwa na fujo endapo maandamano yangefanywa na waumini hao wa kiislamu.
Amir Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini, Musa Kundecha amesema vyombo vya usalama na Tanganyika (Watanzania) kwa ujumla wamepotoshwa na taarifa kuwa waislamu walipanga kuandamana baada ya sala ya Ijumaa kupinga kupelekwa gerezani Katibu wa Taasisi za Kiislamu,Sheikh Ponda Issa Ponda.
Kundecha aliyasema hayo mara baada ya sala ya Ijumaa katika msikiti wa Mchangani na kuongeza kuwa wamepanga kufanya mkutano na waislamu wote utakaofanyika viwanja vya Mwembe yanga siku ya jumapili saa9 jioni na sio maandamano kama ambavyo iliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na vyombo vya usalama kuamini na kuanza kutoa vitisho.
Pia alisema serikali kupitia chama tawala haiongozi taifa katika dhana ya utawala bora, badala yake wanatumia mabavu kuwanyamazisha wananchi wanaojitambua na kudai haki zao suala ambalo kwa waislamu halikubaliki hata kidogo.
“Hakuna kiongozi aliyeitisha maandamano kwasababu tunatambua suala la katibu( shekh Ponda) ni la kisheria ila nimeshangazwa na kauli za vitisho toka kwa vyombo vya usalama.
Aliongeza kuwa, suala linalowaumiza Waislamu si kupelekwa gerezani kwa Shekh Ponda bali ni kitendo cha vyombo vya usalama kumpeleka gerezani ikiwa bado analalamikia maumivu makali ya bega pamoja na kutokubebwa kwa dawa alizoandikiwa na daktari.
Kundecha kwa kile alichokiita taarifa kwa waislamu alisema ni lazima wakutane siku ya Jumapili, na kusema kuwa vyombo vya usalama ni waalikwa namba moja katika mkutano huo ili waweze kujua ukweli wa mada watakazojadili waislamu ikiwemo suala la Shekh Ponda na sio kuchukua taarifa zisizo na uhakika na kuaza kutoa vitisho.
Katika msikiti wa Idrissa uliopo Kariakoo wilayani Ilala, baada ya ibada ya saa 7 mchana kuisha baadhi ya waumini walionekana wakiwapa wenzao waraka unaohusu tukio la Sheikh Ponda Issa Ponda.
Waraka huo ulionekana ukigombaniwa waumini wa msikiti huo huku ukiwa na ujumbe wa kulaani kitendo cha Sheikh Ponda kupigwa risasi..
Wakati huohuo, polisi waliendelea kuimarisha ulinzi katika mitaa mbalimbali ukiwamo wa Msimbazi ambao upo karibu na msikiti huo.
Polisi hao waliokuwa na mbwa huku wengine wakitumia pikipiki kufanya doria kwa kile walichodai kuwa Waislamu wamepanga kufanya maandamano licha ya kupigwa marufuku jana. Katika msikiti wa Mtambani wilayani Kinondoni, baada ya ibada kuisha baadhi ya makundi ya waumini yalionekana yakijigawa kuingia mitaani huku wengi wakirudi katika shughuli zao na biashara zao za kawaida wakiwawacha polisi wakiduwawa.

No comments:

Post a Comment