Wanawake wanachukuliwa kama ni watu wa kubaki katika ndoa kutii amri za mume hata kama amri hizo siyo za haki na usawa basi mume atajidai yeye ndio yeye wala hasemezeki, heshima zinavunja utu wa mwanadamu.
Kwa mfano, gwiji la fasahi ya Kiswahili, marehemu Sheikh Shabaan Robert katika kitabu chake “Maisha yangu na baada ya miaka hamsini” katika ukurasa wa kumi anatoa wasia kwa bintiye kwa kumwambia;
“Fanya kila hali, la mume kulikubali, ila lisilo halali, kukataa si hatia” Hapa anampa ujasiri mwanawe wa kike kutokubali mambo ya ovyo kutoka kwa mume, ana mjengea uwezo wa kuwa mwanamke na mama shupavu katika maisha ya ndoa yake na kuweza kukabiliana na familia.
Matukio ya kutendewa isivyo wanawake wetu siyo mageni, wanawake wamekuwa wakipata vipigo, kuteswa na wengine kufikia hata kujeruhiwa hapa nchini Zanzibar.
Wanawake wetu hapa nchini Zanzibar wamekuwa wakifanya kazi ngumu kama punda, wana mzigo wa kuhudumia familia, wanafanya biashara, wanafanya kazi ofisini huku wakisubiriwa kupika, kuchota maji, wanabeba mimba na kujifungua na wakati mwingine hata hayo matunzo ya mama mjamzito hayapati hasa wanawake wa vijijini. Wakati mwanamume au mume yeye anacheza bao,karata,keraam,mpira usio na mshahara N.K.
Katika sehemu za mashamba Unguja na Pemba, hapa nchini Zanzibar wanawake wanalima, wanapanda, wanapalilia, wanachuma karafuu huku wengine wakianguka na wasipofikisha vyakula vinavyotakiwa katika meza au mkeka basi, anapata matusi na hatimaye kuambulia kipigo cha nguvu je hivi ndivyo tunavyo wapenda wake zetu...? je hivi ndivyo ulivyo muambia wakati unamuowa kuwa utatafuta kila kitu na kama hukuleta utapata kichapo cha nguvu...??
Katika utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanganyika (TAMWA) katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kati ya Novemba hadi Desemba mwaka jana, nchini Zanzibar kuna matukio kadhaa ya wanawake kupata vipigo kutoka kwa waume zao.
Ijapokuwa TAMWA katika utafiti huo wanasema kwamba hulka ya kuwapiga wanawake siyo matukio maarufu sana, ukweli ni kwamba wanawake wengi wa nchini Zanzibar ni wasiri mno, hata akipigwa au kuteswa hawi wazi kutangaza.
Mathalan mmoja ya wanawake aliyehojiwa Mtaa wa Kwamtipura, analalamikia hulka ya mumewe ya kumpiga mara kwa mara hasa pale anapodai huduma muhimu kama chakula na ikiwa akimweleza upungufu basi inakuwa nongwa na sababu ya kuanza kupokea vipigo..!!!!
Mwanamke huyu hivi karibuni alipokea kipigo pale aliposema kiwango cha chakula alichoachiwa ni kidogo na hakiwezi kumtosha, ndipo mume wake alianza kumfokea kwa maneno machafu na kuanza kumpiga jambo ambalo lilimfanya mwanamke huyo kukimbilia kwa Sheha (jina kapuni) kwenda kujisalimisha.
Wanawake wanaopata vipigo kwa hakika ni wengi, lakini wamekuwa wakitofautiana kutokana na sehemu hadi sehemu. Wapo wanaopigwa kwa madai ya kudai haki za msingi za mke ikiwamo kupatiwa huduma za mahitaji ya chakula, mavazi,usaidizi wa kulea watoto na hata kufanya kazi.
Miongoni mwa sababu za kushamiri kwa vitendo vya kupigwa wanawake na waume zao ni pamoja na wivu wa mapenzi, ulevi, kugombania watoto na mali na kuporomoka kwa maadili katika jamii. Akizungumzia hilo, Sheha (jina kapuni) anasema mara nyingi chanzo cha kipigo ni wanaume ambao wanawapiga wake zao wanapolalamikia haki zao.
Lakini anakitaja chanzo chengine ni ulevi, na hili limejitokeza sana katika Shehia yake ambapo amekuwa akilalamikiwa mara nyingi na wanawake kupigwa kwa sababu ya ulevi wa waume zao
Maelezo hayo yanasadikiwa pia na Makadhi wa Mahakama za Kadhi wilaya, Afisa wanawake na watoto wilaya na hata Polisi ambao wote kwa nyakati tofauti wanaeleza sababu za wanawake kupigwa katika ndoa na hata wale wasiokuwa katika ndoa.
Sababu kubwa inayozifanya kesi hizi zisiripotiwe ni wanawake kuona aibu, na upigaji huo kuchukuliwa kama adabu ya kawaida tu anayopewa mwanamke kwa sababu ya kukosea.
Pia wanawake licha ya kuwa wanaumizwa vibaya lakini wanakataa kutoa taarifa kwa kuogopa kuvunjika kwa ndoa zao. Hapa hatupaswi kuwatupia lawama wanawake kwani ni mfumo ndio uliowafikisha hapo walipo wanawake kuonekana kuwa hawana sauti katika jamii.
Katika utafiti huo wa TAMWA, ripoti inasema kwamba katika kipindi cha kuanzia mwezi Juni mwaka 2011 hadi Machi mwaka 2012 kuna matukio matano ya wanawake kupigwa na waume zao na kuripotiwa Polisi lakini wanawake waliofikwa na mkasa huo wapo wengi isipokuwa hawafiki katika vyombo vya kisheria na kutowa habari hizo za upigwaji.
Mbali ya hao wanaokwenda vituo vya Polisi na baadhi ya wakati kesi hizo kumalizwa kienyeji, wengine wanakwenda katika Mahakama ya Kadhi kudai talaka baada ya kuchoshwa na vipigo na janadume levi.
Kuna kesi 10 zimeorodheshwa katika mahakama hizo ambapo walalamikaji(wanawake) wanataka kuvunja ndoa wakiepusha miili yao kugeuzwa ngoma na waume zao.
Wakizungumzia kadhia wanayopata wanawake hapa nchini Zanzibar kwa mtazamo wa kidini, viongozi wa dini tafauti wanasema kwamba dini haijatoa ruhusa kwa wanaume kumpiga mkewe bali wanaume wanapaswa kuishi na wake zao kwa mapenzi na huruma kwani wao ndio walinzi na walezi wa familia.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dk. Sheikh Issa Ziddy r anasema “Uislamu haujaruhusu kwa hali yoyote udhalilishaji ingawa suala la kumpiga mwanamke limetajwa katika Quraan na mafunzo ya Mtume kuna hadithi zinazokataza mtu kumdhuru mwenzake”
Anasema kuna masharti yamewekwa kabla ya mume kufikia hatua ya kumwadabisha mkewa, lakini kabla ya kufikia hatua ya kumpiga kipigo kisichodhuru mume anatakiwa kutimiza mambo matano ambayo ni kuwa mume haruhusiwi kumpiga mkewe kwa kosa lolote hadi kosa hilo liwe kubwa na uzito wa pekee.
Pia kabla ya hatua ya kumpiga anapaswa kwanza kumpa nasaha mkewe kwa kosa alilotenda na sharti la pili ni kumpa mawaidha amma yeye mwenyewe au atafute mtu aje kumpa mawaidha. Sharti la tatu ni kumkumbusha mara kwa mara huku sharti la nne kumhama malazi yaani kumuacha akalala peke yake sio mume utoke nyumba ukalale kwengini laaa nyumba hiyo hiyo ila usilale nae kitanda kimoja, sharti la tano kwenda kushitaki kwa wazee au katika vyombo vya sheria ikiwemo kwa Kadhi na viongozi wa dini na la sita ndio kumpiga, lakini kipigo ambacho hakitomdhuru huku sharti la kumpiga mwanamke hutakiwi kumpiga ukiwa na hasira.
“Ukishawekewa masharti kama hayo matano sharti la mwisho ikiwa mke hasikii ndio umeruhusiwa kumpiga lakini unatakiwa usimpige ukamuumiza wala usimpige ukiwa na hasira lakini hapo hapo unaambiwa hupaswi kumdhuru mwengine basi ndio baadhi ya wanazuoni husema kupiga haijaruhusiwa kwa mantiki hiyo” aliongeza Sheikh Ziddy.
Hakuna mwanamke ambae amehojiwa akasema kuwa mumewa kabla ya kufikia kumpiga amefuata maagizo hayo ya dini kwa upande wa waumini wa kiislamu zaidi ya kujiona wao ndio wenye uwezo wa kufanya watakalo kwa kumpiga mwanamke kwa nguvu na kumuumiza vibaya.
Kwa upande wa dini ya Kikristo, Father Emmanuel Masoud wa Kanisa la Anglikan anasema kuwa hakuna andiko linalofundisha kwamba mwanamme ampige mke wake bali wanaume wanahimizwa kuwapenda na kuwatunza wake zao kama wanavyojipenda wao wenyewe na kumpa mke heshima ili maombi yao yakubalike kwa Mola.
Father Emmanuel anasema tatizo la kupiga wanawake ndani ya wakristo lipo kutokana na mapokeo ya kimila hasa mfumo dume na mfumo jike, kuna baadhi ya makabila kama mume hampigi mkewe anaonekana hampendi au anaambiwa ametawaliwa na mkewe.
Father Emmanuel anasema wakristo wanaungozwa na kitabu kitakatifu cha Biblia na wamekatazwa kuwapiga wanawake na wamesisitizwa kuishi nao kwa wema ili waombi yao yakubaliwe.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, moja ya mambo ambayo yanawaumiza wanawake karibu kote duniani ni ukiukwaji wa haki za binadamu wanazofanyiwa na matokeo ya hayo ni maumivu ya kimwili na kisaikolojia wanayopata wanawake.
Wanawake wanateseka katika vita, katika matukio ya nchi nyengine serekali haziwajali wanawake kama nchi yetu ya Zanzibar haiwajali wanawake kabisa, wengine wanakufa kwa njaa, kwa kukosa maji na huduma nyengine. Inakisiwa kuwa asilimia 80 ya wakimbizi wote ni wanawake waliokimbia machafuko ya kisiasa, vita na matukio mengine.
Huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC) Mapigano yameacha athari kubwa kwa jamii, wakina mama na watoto ndio wanaopatwa na majanga kama hayo yanayosabishwa na vita wengi wao hivi sasa wanaishi katika maisha ya dhiki wakiwa wakimbizi, huko nchini Somalia nako pia Mapigano yanaendele kuathiri kukubwa kwa jamii, wakina mama na watoto ndio wanaopatwa na majanga kama hayo yanayosabishwa na vita wengi wao hivi sasa wanaishi katika maisha ya dhiki wakiwa wakimbizi.
Nchi ya Zanzibar nayo haikuwa nyuma katika masuala ya kuathirika kwa wanawake na matukio ya machafuko ya kisiasa. Mwaka 2001 wanawake kadhaa walifanyiwa vitendo vya kikatili, wengine walikimbia nchi kwenda Shimoni Mombasa nchini Kenya kunusuru maisha yao.
Ni Wanawake hao hao wanaowapa vipigo hapa nchini Zanzibar ndio wanaokuwa mstari wa mbele katika kuwachagua viongozi mbalimbali wa kisiasa na matumbo yao makubwa kama majungu ya biriyani ya tausii, kwenye mikutano ya vyama vya kisiasa ni wanawake ndio wanaojaza uwanja.
Wanawake wa nchi ya Zanzibar walijitolea mali na maisha yao kuunga mkono, juhudi za kisiasa na kijamii, wengi wao ama hawajulikani kabisa au wamewekwa kwenye kapu la sahau kwa makusudi au kwa bahati mbaya iwapo viongozi wakishaingia madarakani basi huwapiga mateke. Hawakuwa wanaume tu waliosimama mstari wa mbele katika mapambano ya kudai uhuru, bali kulikuwa na wanawake shupavu, hodari na mahiri ambao walikuwa sehemu ya kuanzishwa kwa vuguvugu la madai ya kisiasa, lakini mambo yanapokuwa mazuri wanawake wanaelezwa kazi yao ni jikoni.....!!!!!
Wengi wetu tunafahamu kwamba historia ya mapambano ya wanawake inakwenda mbali zaidi, wakati wa kutafuta uhuru ni wanawake waliojitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya vyama vya ukombozi, wengine wakasimama kwenye majukwaa kupaza sauti za ukombozi wakiwashinda wanaume woga hata hivi sasa katika kudai mamlaka kamili ya nchi yetu ya Zanzibar wangaliye wanawake wanavyo jaza viwanja na maholi au mahali popote panapofanywa mkutano wa kutaka kuikombowa nchi ya Zanzibar katika makucha ya mkoloni mweusi Tanganyika ni wanawake huku midume mejoga ikibanza pembeni.
Katika matukio mengi ya kisiasa husikii kabisa kutajwa kwa mchango wa wanawake katika harakati za mapambano ya kudai uhuru. Hili linafanywa kwa makusudi kwani ni aina ya wanaume wanaowapiga wanawake ndio hao hao wengine wanajitumbukiza katika masuala ya kisiasa na kuhodhi madaraka.
Jambo la muhimu kwa kila mwana jamii ni kuhakikisha haki, maslahi na wajibu wa kila mmoja unatimizwa na kuheshimiwa. Elimu zaidi inahitajika kwa ngazi zote kuona kwamba wanawake waishi katika dunia ya amani na yenye kuwaheshimu Wanawake wa nchi yetu ya Zanzibar na kwengineko ulimwenguni.