Saturday, January 4, 2014

JUSSA NA EDDY RIAMY WAWATETE MASHEIKH WETU WA UAMSHO


Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe nchini Zanzibar (CUF), Ismail Jussa Landu amesema ikiwa kweli serikali ya umoja ya kitaifa inataka kuonekana kuwa inaheshimu utawala bora na haki za binaadamu itende haki kwa kuwapa dhamana na kuwaachia Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) waliowekwa ndani zaidi mwaka sasa.
Masheikh hao waliwekwa ndani tokea mwezi wa 10 mwaka jana bila ya kupewa dhamana kwa madai atii ya kuhatarisha usalama wa taifa ambapo Mkurugenzi wa Mshtaka nchini Zanzibar (DPP mashuzi) alitumia kifungu cha sheria ya usalama wa taifa katika kujenga hoja ya kuwanyima dhamana masheikh hao 10.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Chama Cha Wananchi (CUF) uliofanyika huko Chaani, Mkoa wa Kaskazini Unguja nchini Zanzibar, Jussa alisema Tanganyika (Tanzania) ni miongoni mwa nchi ambazo zimesaini mkataba wa kimataifa wa kuheshimu haki za binaadamu na hivyo inapaswa kuheshimu haki hizo bila ya kubagua.

Alisema katika katiba zote mbili ya Tanganyika (Tanzania) na ile ya Zanzibar katika kifungu cha 18 cha katiba hizo kinampa mtu uhuru wa kutoa maoni yake na kupokea kwa mujibu wa sheria bila ya kuadhibiwa.
Jussa ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa alisema Masheikh wa Uamsho wamewekwa ndani zaidi ya mwaka sasa bila ya kupewa dhamana wakati sheria inaipa mahakama uwezo wa kutoa dhamana kwa watuhumiwa wa makosa yote isipokuwa mauaji na uhaini.
Ikiwa nchi ya Zanzibar inataka ionekane kwamba inaheshimu haki za binaadamu basi iwape dhamana Masheikh hawa maana hata huko kuwaweka ndani bila hata kuwapa dhamana ni kinyume na haki za binaadamu muda umeshakuwa mwingi wamewekwa ndani bila ya kuzingatia athari za huku katika jamii” alisisitiza Jussa na kuungwa mkono wa wananchi waliohudhuria katika mkutano huo.
Katika kitu ambacho kinaonekana kuitia doa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Jussa alisema ni huko kuendelea kuwaweka ndani Masheikh hao na kuwanyima dhamana bila wakati sheria inasema huwezi kutiwa hatiani mpaka kuwepo na ushahidi uliokamilika hivyo kuendelea kuwaweka ni kwenda kinyume na sheria ambazo nchi ya Zanzibar wamezipitisha wenyewe.
Mjumbe wa Baraza Kuu huyo alisema Masheikh hao wanapaswa kupewa dhamana kwani ikiwa wamefanya kosa wahukumiwe kihaki na haki itendeke kila mmoja aweze kuona na kuridhika na isiwe kwa Masheikh tu bali sheria hiyo iwakamate pia wale wenye kufanya ubadhirifu wa mali ya umma na kujirimbikizia mali ambapo kamati za zilizoundwa na Baraza la Wawakilishi zimeonesha kumekuwepo na wizi mkubwa lakini hakuna aliyetiwa hatiani wala kuwekwa ndani licha ya ushahidi kamili kupatikana.
Tunasema wapo watu ambao wanaiba na ushahidi upo lakini hawakamatwi wala hawawekwi ndani na wala hakuna sheria iliyowagusa wapo nje wanatembea bila ya kuchukuliwa hatua yoyote sasa tunasema mahakimu wa mwisho ni wazanzibari wenyewe wakiona hakuna haki inayotendeka kwa Masheikh wao basi wazanzibari wataamua ifikapo 2015” alisema na kushangiriwa na wananchi wengi kwa kupigiwa makofi.
Kauli hiyo ya Jussa imeungwa mkono na aliyekuwa Mkereketwa wa Chama Cha Mapinduzi Mohammed Ahmed Sultan (Eddy Riamy) ambaye ametoa wito kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwapa dhamana Masheikh kwani imekuwa kero kubwa kwa wananchi kila unapopita mitaani.
Eddy alisema kuendelea kuwekwa ndani na kunyimwa dhamana Masheikh hao kunaleta kero kwa wananchi walio wengi ambao wamekuwa wakifuatilia habari za Masheikh hao ambao wana mchango mkubwa kwa jamii hasa ukizingatia Masheikh hao ni walimu wa vyuoni na wengine ni Maimamu wa Misikiti.
Eddy ambaye alifuatana na Kamati ya watu sita ya Maridhiano iliyoongozwa na Mzee Hassan Nassor Moyo, alisema kwamba mbali ya kukosekana darsa na kusalisha kwa Masheikh hao lakini pia familia zao zimeathirika kiuchumi na kisaikolojia kutokana na kuwa waume ndio waliokuwa wakitizama familia na sasa kuwekwa ndani kumeathiri familia hizo.
Tusiwatizame wao peke yao lakini tutizame wale akina mama waliopo majumbani mwao ambao wanaa watoto wadogo watakuwa wameathirika kiasi gani kwa waume zao kuwekwa ndani muda wote tokea mwezi wa 10 mwaka jana mpaka leo kesi inakwenda na kurudishwa nakuna linalokuwa sasa mimi natoa wito kwa Waziri wa Sheria, Makamo wa kwanza wa Rais ambao mpo hapa katika mkutano nyinyi ni miongoni mwa serikali tunasema suala hili tunaomba mlizingatie suala la kuendelea kuwaweka ndani Masheikh wananchi wamechoka” alisema Eddy huku akishangiriwa na umma uliofurika uwanjani hapo.
Kauli za kutetewa Masheikh hao zimeonekana kuvuta hisia za wananchi wengi ambapo baadhi yao walikuwa wakisema ni wakati mwafaka sasa Serikali kushughulikia kama ni kuwatia hatiani au kuwapa dhamana lakini kuendelea kuwaweka rumande kunawanyima haki zao kikatiba na hakuwatendeya haki wao na familia zao.
Katika mkutano huo wajumbe wa Kamati ya Maridhiano wakiongozwa na Mzee Moyo waliungana na Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuwataka wazanzibari kuungana na kuacha kusikiliza maneno ya chokochoko ambayo mwisho wake ni kuumizana na kujenga hasama miongoni mwao.
Maalim Seif alisema ni wakati mwafaka sasa wazanzibari kukataa kufitinishwa kwani ni muda mrefu wamekuwa katika mifarakano isiyokuwa na maana na sasa wameungana kwa maslahi ya nchi na wananchi wote bila ubaguzi hivyo alitoa wito kuendelea kushikamana ili kufikia lengo la kuitetea nchi ya Zanzibar na Mamlaka yake. 

No comments:

Post a Comment