Thursday, April 28, 2011

WANA NCHI WA ZANZIBAR WAGOMA KUUZWA KWA MAJENGO YA NCHI YAO KWA KEMPISKI HAPA ZANZIBAR

 

mji_mkongwe_1
Salma Said,
WATU 1,500 wamefunguwa pingamizi ya kupinga ukodishwaji wa ufukwe eneo la Shangani na majengo yaliyomo katika Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar maarufu ‘Mambo Msige’.
Pingamizi hiyo imefunguliwa na wazanzibari 150 kutoka wilaya 10 za Zanzibar, wakiongozwa na Juma Ali Khatib ambaye kiongozi wa Chama Cha Tadea na tayari wamewasilisha kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo leo asubuhi Khatib alisema majengo hayo yamekodishwa kwa mwekezaji Zamani Zanzibar Kempiski, kinyume na sheria namba 9 ya mwaka 2005 ya ununuzi wa mali ya umma.
Alisema kwamba majengo hayo yamekodishwa kwa muda wa miaka 99 kwa thamani ya dola milioni 1.5 wakati majengo hayo yamo katika hifadhi ya uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar.
“Majengo haya yamekodishwa kinyume na sheria, hakuna zabuni yoyote iliyotangazwa na Serikali Oktoba mwaka jana mambo yote yamefanywa kienyeji jambo ambalo halkubaliki katika ulimwengu huu wa wenye kufuata misingi ya demokrasia ya utawala bora”, alisema Khatib.
Alisema kwamba wananchi hao wameamuwa kupinga ujenzi wa hoteli ya kitalii katika eneo hilo kwa vile eneo hilo limekuwa likitumiwa na wananchi kama bustani ya kupumzika na majengo ya mambo Msige, yamo katika uhifadhi ya Mji Mkongwe.
Alisema kwamba iwapo Mamlaka ya Mjimkongwe itamruhusu muwekezaji huyo kuendelea na mradi huo watafunmguwa kesi mahakama Kuu Zanzibar ya kusimamisha mradi huo na tayari wamekwisha wasilisha barua kwa Katibu Mkuu Kiongozi kuhusu andhari ya kuishitaki Serikali (Notice).
Aidha alisema kwamba kuna kitendo cha udanganyifu kimefanyika kuhusu tangazo lililotolewa na Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe linalotoa ruhusa kwa wananchi kuwasilisha maoni yao kuhusu mradi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Alisema tangazo hilo linaonesha limetolewa April 8 mwaka huu, lakini limebandikwa katika eneo la Mradi April 20 mwaka huu wakati muda wa kuweka pingamizi ni April 29 mwaka huu.
Alisema kwamba kitendo hicho kimewanyima haki wananchi wa Makunduchi na Pemba kujitokeza kwa vile tangazo hilolimetolewa wakati wapo katika mapumziko ya Pasaka na maadhimisho ya Muungano, kitendo ambacho ni kinyume na misingi ya utawala bora.
“Kwa tangazo hili mwananchi yeyote mwenye maombi kuhusiana na ujenzi huu, anaomba awasilishe kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mjimkongwe kwa muda wa wiki tatu kuanzia April 8 mwaka huu”, lilieleza tangazo lililobandikwa na Mamlaka hiyo.
Khatib ambae ni katibu Mkuu wa TADEA amesema uchunguzi walioufanya umegunduwa lililokuwa jengo la Wizara ya Elimu pia limeuzwa na baadhi ya viongozi wa Serikali ya awamu ya sita kwa dola za Marekani milioni 2.5 kwa mfanyabiashara mzawa wa Zanzibar.
“Haiwezekani mali za Serikali ziendelee kuuzwa kienyeji tayari tumeshajipanga vizuri tutafunguwa mahakama kuu, lengo letu kufika hadi mahakama za Kimataifa kama wanasheria wetu wa ndani watashindwa kutenda haki katika suala hili”, alisema.
Wananchi hao wanapinga Kampuni hiyo kujenga Hoteli ya Daraja la tano yenye urefu wa ghorofa tano kwa vile sheria za uhifadhi Mji Mkongwe zimeeleza hairuhusiwi kujengwa zaidi ya ghorofa tatu na thamani ya majengo na ufukwe haulingani na mali iliyokodishwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe, Issa Makarani Sariboko amewaambia waandishi wa habari leo ofisini kwake kwamba suala la kwenda mahakamani ni haki ya kila mmoja na iwapo mahakama itaamua basi mamlaka yake itatii sheria za mahakama.
Aidha alisema kubandikwa kwa mabango katika ukuta uliozungushiwa mabati eneo linalotaka kujengwa hoteli hiyo kubwa ya kitalii alisema ni sheria na taratibu ndizo zinazoelekeza kwamba mabango hayo yabandiwe ili wananchi waweze kutoa maoni yao juu ya ujenzi wa hoteli eneo hilo.
Akijibu madai ya kuondolewa jengo la Mambo Msige alisema jengo hilo halitabomolewa bali litafanyiwa ukarabati na kuahidi kuendana na ruhusa na mamlaka ya uhifadhi ya mji Mkongwe kwa kuwa ndio sheria inavyosema kwamba majengo yote yasizidi na kupindukia kile kiwango na kipimo kilichowekwa.
Alisema jengo la Mambo Msige litaendelea kuwepo na halitavunjwa kama wengi wanavyofikiria bali litafanyiwa ukarabati mkubwa ambao hautoathiri majengo yake na kuharibu uhalisia wa jengo hilo huku akiwataka wananchi kufahamu kwamba hatua hiyo imezingatia masharti na sheria zote za mikataba

No comments:

Post a Comment