MWENYEKITI Mao, kiongozi wa Mapinduzi ya China ya mwaka 1949, aliwahi kusema kwamba ‘Mapinduzi si karamu ya chai.’Ithibati kuwa aliyoyatamka yana ukweli si taabu kuupata. Unatukodolea macho tukiyaangalia Mapinduzi ya Ufaransa, Mapinduzi ya Urusi na hata tukiyaangalia Mapinduzi ya China.
Mapinduzi ya Ufaransa yaliyoanza mwaka 1789 yanasemekana kuwa ndiyo mapinduzi ya mwanzo duniani katika karne za hivi karibuni. Yalifyetuka kutokana na njaa na utapiamlo. Siku hizo Wafaransa wa kawaida walikuwa wakifa kwa njaa kwa vile hawakuziweza bei za kuruka za mkate, chakula chao kikuu.
Sababu kubwa iliyoifanya mikate iwe ghali mno ilikuwa mavuno duni ya nafaka ya miaka nenda miaka rudi. Sababu nyingine ilikuwa ni ya miundombinu. Hakukuwa na barabara za kutosha za kuwezesha usafirishaji wa vyakula kutoka mashambani hadi mijini ambako watu wengi wakiishi.Madeni ya taifa la Ufaransa yaliyotokana na gharama na vita pia nayo yalichangia kuifanya jamii ya Ufaransa isambaratike vikubwa hasa miaka michache kabla ya Mapinduzi.Juu ya njaa na hali za kudhalilisha za wananchi wa kawaida, mamwinyi na makabaila wa Ufaransa hawakuiona hatari iliyokuwa inawakabili. Wala hawakuwa wakitambua jinsi wananchi hao walivyokuwa wakijifia kwa kukosa rizki.Watawala walikuwa hawaoni, hawasikii wala hawatambui yaliyokuwa yakiwasibu mabwanyenye na watu wa tabaka la kati seuzi yaliyokuwa yakiwafika walala hoi.Malkia wa Ufaransa wa wakati huo, Mary Antoinette, alipoendewa na kuambiwa kwamba wakulima wadogo na walala hoi hawamudu mkate na wanakufa kwa njaa alijibu kwa kusema: ‘Waacheni wale keki.’Matamshi hayo yaliughadhibisha umma wa Ufaransa ambao tayari ulikuwa umechemka kutokana na njaa na jinsi aila ya Kifalme ilivyokuwa ikifanya itakavyo na jinsi mamwinyi na wale waliokuwa wakijiona kuwa ni waungwana pamoja na wakuu wa Kanisa walivyokuwa wakipatiwa marupurupu na fadhila nyingine kwa upendeleo.Yote hayo yalichangia kupinduliwa kwa ufalme, ufalme ambao uliporomoka katika kipindi cha miaka mitatu tu.Kwa muda wa miaka 10 kuanzia 1789 kulitokea mageuzi makubwa na ya kimsingi nchini Ufaransa na barani Ulaya. Mageuzi hayo yalikuwa ya kijamii na kisiasa. Zile fadhila walizokuwa wakizipata mamwinyi na makabaila zilimomonyoka kwa vile zilikuwa zikipingwa na makundi ya kisiasa ya mrengo wa kushoto pamoja na umma wa Wafaransa uliokuwa ukimiminika barabarani kila siku kuupinga mfumo wa utawala uliokuwapo.Hatima ya Mary Antoinette ni kwamba alikatwa kichwa, na mamia ya watu ambao wanamapinduzi walisema kuwa ni maadui, waliuliwa.Wanamapinduzi wa Ufaransa walikuwa mastadi katika kuua kiasi cha kuwafanya wavumbue zana maalum ya bamba la kukata kichwa waliyoiita ‘guillotine’ (gilotini).
Hicho kilikuwa kipindi cha machafuko makubwa Ufaransa na ilichukuwa muda wa miaka 15 kabla ya nidhamu kurejea tena nchini humo.Labda ni machafuko hayo yaliyowafanya wengi wa Wafaransa wa leo wasiyatamani tena mapinduzi. Wanaona kheri wayasalize mapinduzi yao katika kumbukumbu za kihistoria.
Wengi wanayaona Mapinduzi ya Urusi ya mwaka 1917 kuwa ndiyo ‘mama wa mapinduzi ya kisasa’. Mapinduzi hayo yalifuatiwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Urusi na kuanzishwa kwa mfumo wa Kikomunisti katika Muungano wa Kisovieti na Ulaya ya Mashariki.Mapinduzi hayo ya Urusi yalifikia kikomo mwaka 1991 pale Muungano wa Kisovieti ulipoporomoka. Huo, kadhalika, ulikuwa mwisho wa utawala mkali wa kidikteta, hasa chini ya Joseph Stalin.Ulikuwa mwisho pia wa adhabu za KGB, ile idara ya ujasusi na upelelezi ya Urusi, ambayo iliwatesa mamilioni ya watu. Wale waliokuwa wakishukiwa kuwa ni ‘waasi’ na ‘wapinga mapinduzi’ walipelekwa kuishi uhamishoni huko Siberia ambako hali za maisha zilikuwa mbaya sana. Baadhi yao waliuawa.Leo kuna mfumo tofauti wa kisiasa Urusi. Mfumo huo si wa kimapinduzi wala si wa kikomunisti, itikadi ambayo ikitakiwa na Mapinduzi ya Urusi. Hivyo, huko Urusi pia tumeshuhudia kwamba mapinduzi si tukio la kudumu. Na wala huwasikii Warusi wakinadi: ‘Mapinduzi daima’.
Mfano wa tatu na wa mwisho nitaoutoa ni wa Mapinduzi ya China ya mwaka 1949. Baada ya mapinduzi hayo China ilikuwa ikitawaliwa kimabavu na Chama cha Kikomunisti cha China.Jamii ya China ilizidi kugawika katikati ya miaka ya 1960 pale Mwenyekiti Mao alipoyaanzisha ‘mapinduzi ya utamaduni’. Nguvu nyingi mno zisizohitajika zilitumika ‘kuwafyeka’ waasi. Polepole lakini na bila ya vishindo mfumo wa kikomunisti ukawekwa kando na badala yake China ikaanza kuukumbatia ubepari.Hivi sasa China ina uchumi wenye nguvu duniani unaopikuliwa na ule wa Marekani tu. Tunayakumbuka matamshi ya Deng Xsiaoping, adui wa zamani wa Mao na ambaye baadaye alisamehewa na Mao na akaja kumrithi. Deng aliwahi kusema: ‘Haidhuru paka awe mweusi au mweupe ilimradi aweze kukamata panya.’Huko China pia hatuwasikii wenye kupayuka: ‘Mapinduzi daima’. Hiyo ni kwa sababu taifa hilo limesonga mbele na limethibitisha kwamba limeikanusha ile nadharia ya ‘mapinduzi ya kudumu’. Taifa hilo si tena lile taifa la kimapinduzi ambalo baadhi yetu tulikuwa tukilihusudu na tukishikilia tuliige ili nasi tupate maendeleo.Hii leo mfumo wa kiuchumi wa China ni sawa na ule wa Ufaransa na Urusi. Ni mfumo wa ubepari wa kiliberali. Mfumo huo umechukua nafasi ya ule wa kimapinduzi na umewezesha kuzuka kwa tabaka jipya la mamilionea na mitajiri mikubwa.
Deng Xsiaoping akipenda kusema kwamba ufukara si usoshalisti, si ujamaa na kwamba ni jambo adhimu, la kupendeza mtu kuwa tajiri. Akipenda pia kusema ya kuwa mageuzi ya kiuchumi yaliyofanywa ni mapinduzi ya pili ya China.Bila ya shaka tunasikitika kwamba siku hizi hatuzisikii tena zile nadharia au fikra za ‘usawa’ na ‘haki kwa wote’ zilizokuwa zikipigiwa mbiyu na vyama vya kikomunisti vya China na Urusi. Na wala hatusikii sana ukomunisti ambao katika kilele chake ukifuatwa na zaidi ya watu bilioni mbili.Labda ukomunisti umewatumbukia nyongo kwa vile walikuwa wakilazimishwa kuufuata kwa nguvu. Hii leo zimebaki nchi mbili tu zenye kuufuata rasmi ukomunisti. Nazo ni Korea ya Kaskazini na Cuba, na huko Cuba tumekwishakuanza kushuhudia mageuzi ambayo muda si mrefu yataibadili sura ya ukomunisti wa huko.Sifa moja iliyo bayana katika mapinduzi yote, ikiwa pamoja na yale ya Zanzibar ya mwaka 1964, ni kuibuka kwa tabaka aali la watu wenye nafasi nzuri katika jamii. Tabaka hilo ndilo linalohodhi madaraka bila ya kujali kanuni za kidemokrasia, kanuni ambazo hayo mapinduzi yamekuwa yakizipigania.Tena wapinduzi, vibarakala vyao na wafuasi wao wanajinyakulia haki ya kutawala kwa mtutu wa bunduki. Isitoshe, wanaanza kuishi maisha ya raha, ya anasa na ya kupendeleana. Muda si muda wanasahau zile haki na usawa waliokuwa wakiupigania. Si wanasahau tu lakini wanazikandamiza haki za kimsingi za kibinadamu za wananchi wenzao.Tukiangalia na kupima kwa makini tutaona kwamba mifumo ya kikomunisti na ya kimapinduzi iliporomoka zaidi kwa sababu ilikuwa ikikandamiza haki za kibinadamu.Hali hiyo iliwafanya wananchi wa hizo nchi za kikomunisti zitokwe na imani na mifumo hiyo na kuzipa nafasi Marekani na madola mingine ya kimagharibi zizishinde nchi za kikomunisti katika mchuano wa kutaka kuziteka nyoyo za waliokuwa wakitawaliwa na serikali za kikomunisti huko Ulaya ya Mashariki.Katika siasa hakuna nadharia za kudumu, marafiki wa kudumu wala maadui wa kudumu. Itikadi yoyote ile ya kisiasa isiyosimama juu ya misingi na kanuni za kidemokrasia, za haki na usawa lazima itaporomoka.Wale wenye kuipigia mbiu nadharia ya ‘mapinduzi daima’ kwa kawaida huwa ni watu wa safu ya mbele wenye kuneemeka kutokana na mfumo waliouanzisha.Hata familia zao, ambazo huitwa familia za ‘mababa wa taifa’ nazo pia hujitawalia uhalali wa kuwatawala wengine na hata kuwakalia vichwani na kuwakandamiza mpaka kufikia kuwa hawana chakula na kathalika.Hakuna mapinduzi — si ya Urusi, si ya China, si ya Cuba, si ya Zanzibar — yenye kuungwa mkono mia fil mia na wananchi wa nchi hizo.
Yale ya Zanzibar yaliungwa mkono na wafuasi wa chama cha Afro-Shirazi Party na wa Umma Party. Yalipingwa na wafuasi wa Zanzibar Nationalist Party na wa Zanzibar and Pemba Peoples Party.
Katika hali hiyo kuifanya sera ya ‘mapinduzi daima’ iwe kanuni ya kimsingi ya sera ya Taifa haikuondosha ukinzani uliopo miongoni mwa Wazanzibari.Kuifuata sera hiyo, kwa marefu na mapana yake, kumechangia pakubwa katika kuifanya jamii yetu iwe nyuma katika mambo mengi.Tafsiri ya mkato ya ‘mapinduzi’ ni ‘kuondolewa kwa nguvu kwa serikali au utangamano wa kijamii na badala yake kuwekwa mfumo mpya.’ Hivyo, mapinduzi hayawezi kuwa ya daima.Mapinduzi yanaigawa jamii na kwa wakati huu Wazanzibari hatuwezi tena kugawanyika. Tunahitaji kuutilia nguvu huu umoja wetu tulionao wenye kutufanya walio Visiwani na ughaibuni tuwe na lengo moja la kufanya kila njia ili nchi yetu isimame na isonge mbele
No comments:
Post a Comment