Monday, August 8, 2011

ZANZIBAR SASA KUANZISHA TAASISI YA KUDHIBITI RUSHWA NCHINI Z;BAR

 Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein Hatimaye,ameamua kuanzisha Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na kuweka maadili ya viongozi Zanzibar.Malaka hiyo ya kupambana na rushwa ilikwama kuanzishwa Zanzibar kwa zaidi ya miaka 15 kutokana na visingizio mbalimbali.Hata hivyo, Dk. Shein aliahidi kuwa ni miongoni mwa mambo atakayoyapa kipaumbele mara atakapioingia madarakani.Katika kutekeleza ahadi hiyo juzi, Serikali ya Zanzibar kupitia Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir,iliwasilisha muswada huo kwenye semina maalum kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.Kwa mujibu wa Waziri huyo, muswada wa sheria hiyo ya kupambana na rushwa na kuweka maadili ya viongozi wa serikali ya Zanzibar, baada ya hatua hiyo ya kujadiliwa na Wawakilishi na wadau wengine, utawasilishwa rasmi katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Oktoba, mwaka huu kwa ajili ya kupitishwa.Wakizungumza kwenye semina maalum kwa wajumbe wa Baraza hilo mjini hapa, wajumbe hao walisema hali ya rushwa Zanzibar hivi sasa inatisha na chombo hicho kinahitajika ili kudhibiti hali hiyo.Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Hija Hassan Hija, alisema rushwa Zanzibar imekithiri katika nyanja ya ardhi, manunuzi ya mali za serikali pamoja na matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya viongozi na kwenye utoaji huduma.Alisema kwamba kuna watu wananyimwa huduma muhimu za kijamii hadi watoe rushwa, huku rushwa ya ngono ikiendelea kujitokeza katika baadhi ya sehemu za kazi.“Inasikitisha mtu hawezi kuwa kiongozi hadi atoe rushwa, kwa hali iliyopo rushwa lazima itafutiwe mbinu za kuitokomeza,” alisema Mwakilishi huyo.Mwakilishi huyo alisema hivi sasa Zanzibar kumekuwa na ukiukwaji wa sheria ya manunuzi na kusababisha uuzwaji majengo ya serikali pamoja na viwanja bila ya kuwepo uwazi.Naye Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, alisema malengo ya kupambana na rushwa yatafanikiwa iwapo mkurugenzi atakayeteuliwa kuongoza mamlaka hiyo atapewa kinga, ikiwemo kuthibitishwa na Baraza la Wawakilishi.Alisema lazima viongozi wa serikali wawe tayari kuisimamia kwa vitendo sheria ya rushwa ili malengo ya kuondoa tabia hiyo ipatikane na kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui, kwa upande wake alisema Zanzibar haiwezi kupata mafanikio ya kiuchumi bila ya kuwa na sheria madhubuti na kuweka maadili kwa viongozi.Alisema nchi yenye kutawaliwa na rushwa huwakimbiza wafadhili na wawekezaji, hali ambayo huzorotesha ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wake.
Mazrui alisema yapo maeneo nyeti ya kiuchumi Zanzibar yana harufu ya rushwa ikiwemo bandari, viwanja vya ndege pamoja na masuala ya usafirishaji na kuagiziaji bidhaa kama vile vile karafuu.Alieleza kuwa kutokana na harufu hiyo, ndio maana maeneo hayo yana mkusanyiko mkubwa wa watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwemo na viongozi wa serikali za mitaa.Hata hivyo, wajumbe hao walisema kipengele cha kutangaza mali kwa viongozi wa serikali pale wanapoingia na kutoka serikalini kina umuhimu wa kipekee katika kufanikisha vita dhidi ya rushwa.Akitoa ufafanuzi juu ya sheria hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Joseph Abdallah Meza, aliwataka viongozi kuondosha hofu juu ya uanzishwaji wa sheria hiyo kwa vile ina nia njema.Alisema lengo kubwa ni kutaka kujua uhalali wa mali zao wanazozichuma na hakuna sababu ya kujenga hofu kuhusu kutangaza mali.Mapema, akiwasilisha rasimu ya muswada huo, Waziri Kheir, amesema lengo la kuletwa sheria hiyo ni kudhibiti vitendo vya rushwa, matumizi mabaya kwa viongozi na kurejesha maadili ya watumishi wa umma.Rasimu ya sheria ya kuanzisha mamlaka ya kupambana na rushwa Zanzibar ilikwama mara tatu kuwasilishwa Baraza la Wawakilishi, baada ya Baraza la Mapinduzi kueleza kuwa muswada huo unahitaji kuzingatia uzoefu zaidi kwa nchi nyingine zenye sheria kama hizo.

No comments:

Post a Comment