KADIRI siku zinavyo sogea kufikia 25 Oktoba, siku ya uamuzi wa kupata rais mpya au kubaki na yuleyule, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinazidi kuvurugikiwa. Shein anaimarisha ahadi ya kuendeleza anachoita “mafanikio” ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ukweli, ipo ipo tu juu badala ya kushushwa ngazi ya chini hadi mitaani waliko Masheha. Anarudia rudia kusema, na Balozi mdogo wa nchi ya Tanganyika Baloteli Ali Iddi akimsaidia, serikali haitamvumilia mtu yeyote hata awe na pembe kiasi gani, anayechochea uvunjifu wa amani, na wasaidizi wake katika CCM wakizidisha kauli za matusi na kutisha wananchi. Mgombea mshindani mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye ndiye Makamo wake wa kwanza, yeye anazidisha upole na kujenga watu matumaini kwa kutumia lugha nzuri. Ninavyofuatilia hutuba za viongozi hawa nathibitisha zaidi nilichopata kukieleza, wapo wagombea wawili wenye dhamira tofauti. Rais anajikaza kisabuni eti amesimama imara na anajaza imani wafuasi kuwa ushindi kwao ni lazima, ingawa katika vikao vyake vya ndani na makada, kikiwemo alichokifanya hivi karibuni kijijini Makunduchi, anakiri “mgonjwa yuhali mbaya na anatiwa maji.”
Tayari ameahidi mshahara wa Sh.300,000 kima cha chini, ambao haujawahi kufikiriwa serikalini ingawa kimekuwa kilio cha miaka mingi cha vyama vya wafanyakazi. Leo wanapo ahidiwa kiwango hiki, unajiuliza kwa uchumi upi....? Uchumi wa nchi ya Zanzibar wa kijungu mwiko usiomudu kulipa fedha hizo kila mtumishi wa chini, ikiwa na maana utaongezeka kwa wafanyakazi wa kada ya kati na juu. Rekodi zote za serikalini hazioneshi hilo litawezekana iwapo Shein atachaguliwa. Kiwango hicho kinawezekana tu iwapo kutakuja uongozi mpya wa serikali ambao utakuwa na utashi wa kukusanya kila senti inayopasa kukusanywa, itafuta misamaha ya kodi na kuziba mianya ya ufisadi. Serikali italazimu kuwa ndogo si kama ilivyo mawaziri wasio wizara, unaongeza wilaya na majimbo kwa sababu za kutafuta ushindi wa kutunga, na unazembea kukusanya kodi huku ukiachia watendaji kuiba watakavyo. Serikali itahitaji angalau mwaka kupata uwezo wa kulipa kiwango hicho, na hapo italazimu ikomeshe upotevu wa mamilioni ya shillingi kupitia wizi wa mishahara hewa na ununuzi wa huduma na vifaa serikalini usiofuata Sheria ya 2003. Pia iwe imezuia mtindo wa fedha za serikali kuchukuliwa katika mifuko ya rambo (badala ya kupelekwa benki) na zikalala majumbani kwa maofisa fisadi maswahiba wa viongozi.
Serikali ya viongozi walioamua hasa kuitumia Tume ya Kudhibiti Rushwa na Uhujumu wa Uchumi ambayo haijafanya la maana tangu ianzishwe kwa mbwembwe na 2013. Kama vile hakuna wala rushwa wala wahujumu wa uchumi hapa nchini Zanzibar; kama vile hakuna washenzi waingizaji wa ‘unga’ na kama vile hakuna wanaofisidi miradi ya maendeleo. Mabaya yote haya yameshamiri kutoka Novemba 2010 licha ya ahadi ya Shein kuahidi kuwa mlinzi mzuri wa raslimali za Wazanzibari kwa lengo, pamoja na mambo mengine, la kujenga uchumi. Sasa unapomsikia mtetea kiti akiahidi kupambana na mafisadi huku nchi ikiwa inazidi kutegemea chakula kutoka nje kwa sababu serikali haijasimamia ipasavyo mpango wa kukuza sekta ya kilimo hasa uzalishaji wa mpunga, ujue itabaki hivyo hivyo kwa mfumo uliopo chini ya CCM. Ukiambiwa changanya na zako, amesema Jayaka Kikwete, rais wa jamhuri ya Tanganyika anayestaafu baada ya Oktoba 25. Ahadi za Dk. Shein ni zilezile za uchaguzi wa 2010, nyingi kwelikweli na ukizisikia tamu kuliko; tatizo kubwa ni usimamiaji wa mipango ili kuleta tija. Juzi nikamsikia anaahidi vijana ajira za kutosha. Hivi kufikia tu Oktoba hii, vijana wangapi wameajiriwa....? Kwa kazi zipi na wapi wakati vijana wa nchi ya Zanzibar, kwa kukosa uwezo wa ada, wanashindwa kusoma Chuo cha Utalii Maruhubi ili watembeze watalii katika nchi iliyojaaliwa fukwe mwanana...? Hakuna vijana katika kilimo wala uvuvi ukiacha wa kuhisabu walioko vijijini wakirithi kazi walizofanya wazazi kwa kijembe kongoroka (kilimo) na uvuvi wa juya. Kipindi hiki nchi ya Zanzibar haina umeme wa kutosha. Wiki ya pili inaingia shirika la umeme – ZECO – linatoa umeme kwa mgao wa saa tano kwa siku.
Menejimenti imesema umeme umekuwa haba kwa sababu Shirika la Umeme kwa Masultani Weusi Tanganyika – Tanganyika Electric Supply Company (TANESCO) – linaingiza umeme kwa upungufu kwenye Gridi ya Taifa kutokana na hitilafu katika mitambo inayozoea kuendeshwa kwa kutumia gesi. Wala hili halina ukweli wa asilimia 100 maana taarifa za serikalini zinashawishi kuwa uzalishaji kwa nguvu ya maji unaofanywa Kidatu umezorota kutokana na mabwawa ya Mtera na Kihansi kupungua maji. Shein ameshindwa kuelekeza serikali kubuni mkakati wa nchi kupata umeme wake ili kuepusha gharika kama iliyotokea mwaka 2003 Tanesco waliposimama kuipatia umeme ili kushinikiza walipwe deni sugu la mabilioni. Nchi iliishi gizani kwa miezi mitatu mpaka suala hilo lilipotatuliwa kisiasa kwa maafikiano ya ratiba mahsusi ya nchi ya Zanzibar kulipa kwa awamu. Heko Wazungu wa Afrika Kusini kupitia Net Group Solution. Bila ya umeme wa kutosha na wa uhakika, huwezi kuahidi viwanda hata vidogo, achilia mbali kilimo cha kisasa na kukuza utalii, sekta ya pili kwa mchango bora katika Pato la Taifa (GDP). Hutazungumzia kamwe utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta pasipo umeme wa uhakika. Chini ya uongozi wa Shein, makada na askari wa SMZ wanaruhusiwa kuichezea amani kwa kaulimbiu ya “kutesa kwa zamu.” Askari wasio nidhamu wa vikosi maalum vya SMZ wanadhalilisha wananchi kwa vipigo na hawadhibitiwi; rushwa na ufisadi vinakua, ubaguzi serikalini ukishamiri.
Leo sitaji haja ya kuimarisha mfumo wa siasa ili ulete tija kwa maendeleo ya nchi. Eneo hilo ambalo nitalijadili wiki zijazo, lina maana kubwa katika kuilea demokrasia ya nchi ya Zanzibar, halkadhalika kuifanya siasa ichochee maendeleo makubwa ya kiuchumi. Nitagusa kwa undani ulazima wa kubadilishwa mfumo wa Muungano feki ambao ungali mfumo-dume usioisaidia hata kwa nukta nchi ya Zanzibar na watu wake, bali ukweli ukiendelea kuinyima fursa za kujijenga kiuchumi na kuacha kutegemea huruma ya Masulti Weusi wa Kitanganyika iliyovaa koti la Muungano feki. Kitu kibaya katika mfumo wa muungano wa serikali mbili, ni kuendelea kukandamiza mamlaka ya serikali yaliyopatikana kwa umwagaji wa damu ya wananchi wema kupitia mapinduzi ya 12 Januari 1964. Nitakapojadili hili, sitadharau umuhimu wa kuhusisha suala la Katiba mpya iliyotarajiwa iwe msingi wa kuivua nchi ya Zanzibar mnyororo unaoibana isifurukute mbele ya Masultani Weusi wa Tanganyika. Hili nalo ni eneo ambalo Shein pamoja na tambo zote na kauli laghai za viongozi wenzake wa CCM, amepotea kabisa njia. Kule kuamini kwa kutamka hasa kuwa kwake CCM hutangulia ndipo aifikirie nchi ya Zanzibar na Wazanzibari kwa ujumla, kumethibitishwa na kuridhia Katiba Inayopendekezwa inayodanganya Wazanzibari ila washachelewa Wazanzibari hawadanyiki tena.
KILA MZANZIBARI ATAKAE IPIGIA KURA CCM ILI IBAKI MADARAKANI AJUWE NA YEYE ANACHANGIA KUFUNGWA KWA MASHEIKH NA KUTHALILISHWA KWAO NA KUENDELEZA DHULMA KATIKA NCHI YA ZANZIBAR UKAE UKIJUWA UTAULIZWA SIKU YA KIYAMA NA MWENYEZI MUNGU ULIPOSIKIA WAZANZIBARI WENZIO WANADHALILISHWA,KUDHULUMIWA NA KULAWITIWA NA HAWA JE ULIFANYA NINI TAFUTA JIBU LAKO MAPEMA KWA SIKU HIYO YA KIYAMA SIKU AMBAYO MALI NA WATOTO WAKO WALA CHEO CHAKO HAVITAKUFAA SIKU HIYO.
No comments:
Post a Comment