TAREHE: 28 OKTOBA, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Chama Cha Wananchi (CUF) kimepata taarifa kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, ametangaza mwenyewe binafsi bila ya kuwashirikisha Makamishna wenzake wa Tume ya Uchaguzi, kwamba eti ameufuta uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015.
Mwenyekiti huyo amefanya hivyo baada ya kutoonekana tokea asubuhi katika kituo cha majumuisho ya matokeo ya uchaguzi wa Rais kilichopo Hoteli ya Bwawani. Mkurugenzi wa Uchaguzi, Salim Kassim Ali, naye hakuonekana tokea asubuhi na haijulikani yuko wapi.
CUF pia imepata taarifa kwamba Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Abdulhakim Muhsin Ameir, naye alichukuliwa kwa nguvu na vikosi vya ulinzi vilivyokuwepo kwenye kituo hicho cha majumuisho.
CUF imeshtushwa na hatua hii inayokwenda kinyume na Katiba na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar na inaichukulia kauli ya Mwenyekiti huyo ni yake binafsi hasa baada ya kujiridhisha kwamba hakukuwa na kikao chochote cha Tume kilichofikia maamuzi hayo. Mwenyekiti kwa nafasi yake hana mamlaka ya kufuta uchaguzi huo.
Inaonekana kuna njama za makusudi kutaka kuvuruga demokrasia Zanzibar na kuingiza nchi katika machafuko.
Kwa upande mwengine, Mwenyekiti huyo hakutafakari kwamba kuufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar kunaathiri pia uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu wapiga kura walikuwa ni wale wale waliomo kwenye Daftari la Wapiga Kura la ZEC. Na katika kusimamia uchaguzi huo, ZEC hufanya kazi ya uwakala wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Hali hii inaitia Jamhuri ya Muungano katika taharuki pasina sababu yoyote ya msingi kwa sababu Rais wa Jamhuri ya Muungano hawezi kupatikana kwa kupigiwa kura na wananchi wa Tanzania Bara pekee.
Sisi tunatambua kwamba hatua hii imekuja baada ya majaribio yote ya kutaka kulazimisha ushindi usiokuwepo wa CCM kushindikana. Uhakiki wa matokeo ya uchaguzi wa majimbo yote 36 ya Unguja na majimbo 4 ya Pemba uliokuwa umekamilika kabla ya zoezi hilo kusitishwa umethibitisha matokeo ambayo CUF ilikuwa imeyakusanya. Tunatambua kwamba zilikuwepo njama za kutaka kumtangaza mgombea Urais wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa nguvu lakini njama hizo zimeshindikana kutokana na ukweli uliokuwa ukiibuka kupitia uhakiki wa matokeo ya uchaguzi.
Tunatamka wazi kwamba CUF hatuutambui uamuzi huo binafsi wa Mwenyekiti wa Tume na tunaitaka Serikali na CCM kuiacha Tume iendelee na kazi yake ya uhakiki wa matokeo ya uchaguzi na kisha kutangaza mshindi.
Tunaiomba jumuiya ya kimataifa na marafiki wa Tanzania kuingilia kati suala hili hasa kwa sababu waangalizi wa kimataifa wameshuhudia hatua zote hizi pamoja na uhakiki wa matokeo ulivyokuwa unakwenda. CUF imeonekana wazi kwamba ni mshindi wa uchaguzi wa Rais pamoja na majimbo yote 18 ya Pemba na majimbo mengine 9 ya Unguja. Tunaiomba jumuiya ya kimataifa kutoiruhusu CCM kukandamiza haki za kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar kwa mara nyengine tena.
Wakati CUF inafuatilia hatua hizi na kuendelea kuwasiliana na wahusika mbali mbali, viongozi wa ndani na nje ya nchi ili kupata ufumbuzi wa mgogoro huu unaotengenezwa, tunatoa wito na kuwaomba sana wanachama wa CUF na Wazanzibari wote kutochokozeka na kuendelea kubaki watulivu na kuitunza amani iliyopo. Tunawahakikishia kuwa uvumilivu wao utawapa wanachokitaka, na sisi viongozi wao tutaisimamia haki yao kwa njia za amani lakini za uhakika.
HAKI SAWA KWA WOTE
SEIF SHARIF HAMAD
MGOMBEA URAIS WA ZANZIBAR KWA TIKETI YA CUF
MGOMBEA URAIS WA ZANZIBAR KWA TIKETI YA CUF
KILA MZANZIBARI ATAKAE IPIGIA KURA CCM ILI IBAKI MADARAKANI AJUWE NA YEYE ANACHANGIA KUFUNGWA KWA MASHEIKH NA KUTHALILISHWA KWAO NA KUENDELEZA DHULMA KATIKA NCHI YA ZANZIBAR UKAE UKIJUWA UTAULIZWA SIKU YA KIYAMA NA MWENYEZI MUNGU ULIPOSIKIA WAZANZIBARI WENZIO WANADHALILISHWA,KUDHULUMIWA NA KULAWITIWA NA HAWA JE ULIFANYA NINI TAFUTA JIBU LAKO MAPEMA KWA SIKU HIYO YA KIYAMA SIKU AMBAYO MALI NA WATOTO WAKO WALA CHEO CHAKO HAVITAKUFAA SIKU HIYO.
No comments:
Post a Comment