Tuesday, July 2, 2013

JAJI MARK BOMANI-WATU WAULIZWE WANAUTAKA AU HAWAUTAKI-KAMA HAWAUTAKI TUPEYANE MKONO WA KWA HERI NA TUISHI KWA AMANI


MWANASHERIA Mkuu wa zamani nchini Tanganyika, Jaji Mark Bomani amesema Muungano hautakufa iwapo Tanganyika na Zanzibar na serekali ya Muungano  itakuwa hivyo kwa mfumo wa serikali tatu.
Aidha, Jaji Bomani alisema adui wa Muungano wa mfumo huo ni kuwepo watu wenye tamaa kwa maslahi yao: “Serikali tatu ni kuimarisha Muungano isipokuwa kwa kuwepo watu wenye tamaa na maslahi yao binafsi,” alisema Jaji Bomani.
Jaji Bomani, alitoa kauli hiyo mjini Magharibi nchini Zanzibar, juzi. Na alisema kwamba mfumo wa Muungano wa muundo wa serikali tatu, hauna gharama yoyote zaidi ya kupunguza gharama ambazo zipo:
“Muungano hautakufa kwa sababu ya serikali tatu lakini unaweza ukafa kwa sababu ya watu wenye tamaa na kwa maslahi yao bila kuwajali wananchi,” alisema na kufafanua:
“Sikubaliani na hoja za gharama kama inavyoelezwa na baadhi ya watu…Serikali ya Muungano itakuwa na mambo machache  Bunge lake litakuwa na wabunge wachache  Kwa hivyo hakuna suala la gharama,” alisema Jaji Bomani.
Kwa upande wa mfumo wa serikali moja, alisema mfumo huo hakuna uwezekano: “Serikali tatu zitatoa nafasi kwa kila nchi mwanachama kuendesha mambo yake kwa kadiri ya mahitaji ya wananchi wake,” alisema Jaji Bomani.
Mwanasheria Mkuu mstaafu huyo, alisema ni vigumu kuendelea kuwa na mfumo wa Muungano ambao muundo wake, unamfanya mdogo kuwa na hofu ya kumezwa na mkubwa.
Alisema kwa kuondoa shaka hiyo ziwepo serikali tatu: “Tuwe na serikali ya Zanzibar  Tuwe na serikali ya Tanganyika na zote zikiwa na MADARAKA kamili ,” aliongeza:
“Sisi ni wamoja lazima tuwe na kitu kinacho tuunganisha kuwa wamoja…nacho ni serikali ndogo ya Muungano,” alisema Jaji Bomani.
Alishauri mjadala wa kupata Katiba mpya uwe huru, wananchi wafungue mioyo yao, wasifungwe na mawazo au itikadi fulani. Kila mmoja atoe alichonacho moyoni.
Kuhusu serikali ya MKATABA alisema: “Serikali ya mkataba inawezekana ikiwa watu wanataka hilo  si la ajabu  kitu muhimu watu wakae kitako kuamua wanataka nini  wasiburuzwe wala kufungwa midomo,”.
Jaji Bomani alisema uwepo mjadala huru ili kila upande utoe dukuduku lake na muwafaka huru upatikane. Na alipendekeza:
“Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Tume ya uchaguzi ya Tanzania (NEC) zisimamie mchakato ili kupata maoni huru ya wananchi,” alisema Jaji Bomani.
Alisema Tume hizo zitafute maoni ya wananchi kwa kuwauliza maswali mawili pekee ambayo ni: ‘Je unautaka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’ au hautaki muungano wa Tanganyika na Zanzibar..???
Swali la pili: Iwapo jibu ni ndiyo, aulizwe anapendelea Muungano wa mfumo gani. Serikali  moja, serikali mbili au serikali tatu..???
Kongomano hilo ambalo lilitayarishwa na Kamati ya maridhiano ya Zanzibar, lilikuwa chini ya Mwenyekiti wake, Bwana Hassan Nassor Moyo.
pia Jaji Mark Bomani alisema watu wasilazimishwa kuwa na Muungano kama wanautaka waulizwe wa aina gani na kama hawautaki basi watu wapeyane mkono wa kwaheri na kila moja abaki kuwa na nchi yake kwa amani.

No comments:

Post a Comment