Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewatoa hofu askari Polisi watakapokuwa chini ya Serikali ya nchi ya Zanzibar kwamba maslahi yao yatakuwa mazuri zaidi kuliko ilivyo sasa chini ya Muungano na kwamba watafurahi.Maalim Seif amesema hayo katika viwanja vya Kambini Mchanga Mdogo, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CUF kwa ajili ya wananchi wa mikoa miwili ya Pemba, maalum kuchambua rasimu ya awali ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Maalim Seif alisema baada rasimu ya awali kutolewa na kupendekeza Polisi lisiwe jeshi la Muungano, baadhi ya askari hao wamekuwa na hofu juu ya hatma na maslahi yao chini ya nchi ya Zanzibar, hofu ambazo alisema wanapaswa kuziondoa kabisa kabisa.
Maalim, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi ya Zanzibar alisema, Zanzibar ina uwezo mkubwa wa kuzidi kujiimarisha kiuchumi, na pale itakapokuwa na Mamlaka kamili ya kujiamulia mambo yake itazidi kujijengea uwezo mkubwa kiuchumi na kukuza maendeleo ya wananchi wake.
Alieleza kuwa hivi sasa ambapo imebwana katika sera za uchumi na fedha wastani wa makusanyo yake kwa mwezi ni kati ya shilingi bilioni 13 na wataalamu wanasema bado inaweza kufanya vizuri zaidi ya hapo.
Alieleza kuwa Zanzibar ina uwezo mkubwa wa kuimarisha uchumi wake pale itakapokuwa inadhibiti sera zake za kiuchumi na fedha na itaweza kujijengea uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha ya Wazanzibari, ikiwemo kuwalipa vizuri watumishi wake, wakiwemo Polisi na askari wa vikosi vyote vilivyopo hapa nchini Zanzibar.
“Polisi msiwe na wasi wasi juu ya maslahi yenu chini ya Zanzibar, tutakulipeni vizuri kuliko mnavyolipwa kwenye Muunganao, pia vikosi vyote vya Serikali ya Zanzibar mambo yenu yatakuwa mazuri”, alisema Maalim Seif huku akishangiliwa na wananchi waliojazana katika viwanja hivyo.
Aidha, Maalim Seif alisema madai ya Wazanzibari walio wengi kutaka Mamlaka Kamili ni ya msingi kabisa na amewataka wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuyazingatia na kutetea msimamo huo kwa maslahi ya Wazanzibari wote.
Alisema kwamba Muungano uliopo umeonesha wazi kuibana sana Zanzibar katika kila nyanja na kutoa mfano kuwa hadi sasa miaka 49 ya Muungano inasikitisha kuona ni Mzanzibari mmoja tu, Dk, Salim Ahmed Salim aliyewahi kushika wadhifa wa Uwaziri wa Mambo ya Nje.
“Ni Mzanzibari mmoja tu Dk. Salim Ahmed Salim aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje tangu Muungano huu uasisiwe, kwani Zanzibar hakuna watu wenye uwezo”, alihoji Maalim Seif.
Alisema pia Zanzibar imekuwa ikinyimwa nafasi za Mabalozi wa nchi za Nje ndani ya Muungano, alitoa mfano kati ya Mabalozi 29 wanaoiwakilisha nchi ya Tanganyika ((Tanzania)) Zanzibar nchi za nje, Wazanzibari hawazidi watatu, jambo ambalo alisema si kuwatendea haki Wazanzibari.
Aidha, Katibu Mkuu wa CUF, alisema Katiba mpya lazima iainishe mipaka ya Zanzibar, ili kuepusha kutokea utata kati ya pande mbili za Muungano, kama hali ambayo imeanza kujitokeza kuhusiana na kisiwa cha ndege, ambacho kwa miaka yote kinajuilikana ni sehemu ya Zanzibar.
Alisema kwamba katiba mpya lazima itaje wazi wazi mipaka ya Zanzibar, upande wa Kusini, Magharibi na Kaskazini, ambapo alisema kwa upande wa Mashariki wa Zanzibar kuna bahari kuu.
“Kama kweli kuna nia njema, kuna ugumu gani wa kutaja mipaka, sisi tunasema Katiba hii lazima itaje mipaka”, alisema Maalim Seif.
Mapema, Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alisema kwamba ni vyema ieleweke wazi kwamba madai ya Zanzibar kuwa na Mamlaka kamili si ya CUF, bali ni ya Wazanzibari walio wengi wanaojali maslahi ya nchi na wananchi wa Zanzibar.
Jussa ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi CUF, alisema rasimu ya awali iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo wananchi wanaendelea kuijadili inakasoro nyingi, zinazo kwamisha azma ya Wazanzibari kuwa na Mamlaka yake Kamili, hivyo ni wajibu wa Wazanzibari kuzidi kushikamana na kukataa vikwazo vyote vitakavyo sababisha Zanzibar ikose Mamlaka ya kamili ya kujiamulia mambo yake yenyewe.
No comments:
Post a Comment