Tuesday, June 21, 2011

KWA MARA YA KWANZA SMZ YAONYWA KUHUSU KUJINUNULIYA MAGARI YA KIFAHARI


SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeshauriwa kuacha kutumia fedha nyingi kununua magari ya kifahari kwa viongozi na badala yake fedha hizo zitumike katika mambo muhimu yanaowahusu wananchi.

Ushauri huo ulitolewa jana katika kikao kinachoendelea cha kujadili bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2011/12 na Mwenyekiti wa kamati wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma alipokuwa akiwasilisha ripoti ya kamati yake.
Alisema Serikali katika mipango yake ilitangaza mapinduzi ya kilimo na kuimarisha sekta hiyo kwa kujitosheleza kwa chakula na inatakiwa kujikita katika kilimo na kuepuka matumizi mengine makubwa yasiyokuwa na ulazima.
“Serikali isione tabu kutumia pesa kwani tunataka kujenga taifa la vijana wenye moyo wa kujitegemea ndio maana tukashauri Serikali iwe ndogo ili pesa nyingi ziende kwenye kazi na sio kununulia magari ya bei ghali ‘mashangingi’ hili kila mwenye akili analiona mantiki yake” alisema mwenyekiti huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi katika awamu iliyopita.
Aidha aliishauri Serikali kuimarisha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) ili kuwapa fedha za kutosha na kuwachukua vijana wote wanaomaliza shule kuacha kukaa vibarazani tu bila ya kazi kwa lengo la kwenda kujenga taifa.
Sambamba na hilo alisema kwamba vijana hao wanatakiwa kupatiwa ujuzi wa ufundi na kuwashirikisha katika kilimo mbalimbali kikiwamo cha mbogamboga ambapo kilimo hicho ni muhimu sana hasa kutegemea soko kubwa la utalii lililopo Zanzibar .
Alisema kilimo kama kitapewa nafasi kubwa kinaweza kuwa mkombozi kwa maendeleo ya wananchi na kuishauri Serikali kuwa na udhati wa dhamira yake ya kuwasaidia wananchi.
Alisema wakulima wengi wanafanya kazi kubwa ya kilimo, lakini wanavunjwa moyo na wataalamu wa kilimo kwa kushindwa kuwapatia ushauri wa kitaalamu.
“Bajeti hii tunataka iwasaidie wakulima kupata ushauri wa kitaalamu katika kuimarisha kilimo ili wakulima wajisikie kwamba Serikali yao inawajali na inafanyia kazi malalamiko yao ya muda mrefu” alisema Juma.
Alisema hali ya chakula hapa Zanzibar sio nzuri sana na sio kama hakuna chakula, lakini bei ni kubwa mno huku wananchi wakiumia kutokana na bei hizo kwani kila kukicha bei huongezeka na kwamba mwaka 2005 bei cha mchele ilikuwa Sh450 mwaka 2010 ilikuwa Sh900 na hivi sasa Sh1,200.
Juma alisema iwapo hali itaendelea kuwa hivi hivi ifikapo mwaka 2015, bei itafika Sh1,500 hivyo kamati yake ikaishauri Serikali kupitia Shirika lake la Biashara (ZSTC) kuagiza mchele na kuingiza kwenye soko ili kupunguza bei na pia kuhamasisha wakulima kulima mpunga kwa wingi, kununua na kuuhifadhi maghalani baada ya kuingiza katika soko ili kupunguza bei zilizopo.

No comments:

Post a Comment