Friday, June 17, 2011

HII NDIO BAJETI YA KWANZA YA GNU AU SUKARI NCHINI ZANZIBAR


mzalendo_bajeti
Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar, Omar Yussuf Mzee jana alisoma hutuba ya bajeti ya kuhusu mpango wa maendeleo na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 katika kikao cha baraza la wawakilishi kilichoanza Juni 15 mwaka huu.
SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR
HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS
FEDHA, UCHUMI NA MIPANGO YA MAENDELEO
MHESHIMIWA OMAR YUSSUF MZEE
KUHUSU MPANGO WA MAENDELEO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA WA 2011/2012 KATIKA BARAZA LA WAWAKILISHI
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako tukufu sasa likae kama Kamati Maalum lijadili na hatimae kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012. Pamoja na hotuba hii, pia naomba kuwasilisha vitabu vinavyoelezea Mpango wa Serikali na Bajeti. Kitabu cha kwanza kinaelezea Mapitio ya Hali ya Uchumi na Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2010/2011. Kitabu cha pili kinahusu Mwelekeo wa Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2011/12 na Kitabu cha tatu ni Mswada wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2011/2012.
2. Mheshimiwa Spika, Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia kuwa wazima wa afya na kuweza kukamilisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ambao umetoa ushindi kwa Chama cha Mapinduzi na hatimae leo hii kukutana katika kikao hiki ambacho hujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/2012. Tunamuomba Mwenyezi Mungu akijaalie kikao hiki kiendeshe shughuli zake kwa utulivu, maelewano na upendo ili tuweze kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa maslahi ya nchi yetu na watu wetu. Aidha, napenda pia kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Hii ni uthibitisho tosha kwamba wananchi wa Zanzibar wana imani kutokana na uongozi wake. Vile vile, napenda kuwapongeza wote walioteuliwa na Mheshimiwa Rais.
3. Mheshimiwa Spika, Mwaka huu wa fedha ni mwaka maalum kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hii ni bajeti ya kwanza ya Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Halikadhalika, hii ni bajeti ya kwanza inayoanza kutekeleza nusu ya pili ya Dira ya Maendeleo ya 2020. Napenda kuchukua fursa hii kumpongezi kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein na Mheshimiwa Makamo wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kwa maamuzi ya busara ya kuukubali muundo wa Serikali ya pamoja ambao umeanza kufanya kazi rasmi kuanzia mwezi Novemba 2010. Aidha, pongezi za pekee nazitoa kwa Mheshimiwa Rais wa awamu ya sita, Dk. Amani Abeid Karume kwa kusimamia na kufanikisha kura ya maoni juu ya uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, utaratibu ambao ulitoa fursa ya kidemokrasia kwa wananchi kuweza kuchagua mfumo wa Serikali wanayoitaka. Vile vile nawapongeza viongozi wetu wa kisiasa pamoja na wananchi kwa busara na nia zao njema za kujenga taifa lenye amani na utulivu. Ni matumaini yetu kwamba, Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi itafanya kazi kwa umakini mkubwa na hatimae kuleta maendeleo endelevu kwa maslahi ya nchi na wananchi wetu wa Zanzibar.
4. Mheshimiwa Spika, Sina budi kutoa shukurani zangu za pekee, kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, kwa uongozi wake uliojaa busara na hekima katika kuiongoza nchi. Kwa kipindi kifupi cha kuwepo kwake madarakani ameweza kuendesha gurudumu la maendeleo kwa umahiri mkubwa. Maelekezo, muongozo na uzoefu mkubwa alionao umeanza kuleta ufanisi katika maendeleo ya Zanzibar. Aidha, napenda pia kutoa shukurani zangu za dhati kwa kuniteua nimsaidie katika masuala ya fedha, uchumi na mipango ya maendeleo. Ahsante sana Mheshimiwa Rais.
5. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein imeweka bayana dhamira yake katika kuwajengea Wazanzibari misingi imara ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini, utawala bora pamoja na kuimarisha huduma mbali mbali za jamii. Utekelezaji wa makusudio hayo unakwenda sambamba na mipango ya kipindi cha kati cha miaka mitano ijayo (2011-2015) kama yalivyoainishwa katika Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUZA II) na malengo ya Dira ya Maendeleo ya 2020.
6. Mheshimiwa Spika, Uchaguzi Mkuu umemalizika, wakati wa kampeni tumetoa ahadi nyingi kwa wananchi wetu. Kipindi kilichopo mbele yetu ni cha kutekeleza na kutimiza ahadi zetu kwa wananchi. Serikali ya Awamu ya Saba, ikiwa ni bajeti yake ya kwanza inakusudia kuweka misingi imara ya kutekeleza ahadi ilizozitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba 2010. Miongoni mwa ahadi hizo ni kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, uwezeshwaji wa wananchi kiuchumi, uimarishaji wa elimu katika ngazi zote, kufanya mapinduzi katika kilimo na uvuvi pamoja na usanifu wa mazao ya kilimo na uvuvi. Aidha, Serikali pia imekusudia kuweka mkazo zaidi katika uimarishaji wa utawala bora, uimarishaji wa huduma za kijamii kama vile afya na elimu, usambazaji na upatikanaji wa maji safi na salama, makaazi bora, kuongeza nafasi za ajira hususan kwa vijana, kujenga ustawi wa jamii kwa kuzingatia maslahi na mahitaji ya watu maalum kama vile walemavu, wazee na watoto pamoja na uhifadhi wa mazingira yetu. Vile vile, sekta ya viwanda itapewa msukumo wa kipekee pamoja na uendelezaji wa miundombinu ya kiuchumi ikiwemo nishati, barabara na ustawi wa utumishi wa umma.
7. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo na Bajeti ninaouwasilisha leo unabeba hatua mahsusi za mwanzo wa utekelezaji, hususan katika maeneo ya kuimarisha maslahi ya watumishi wa Umma, kuimarisha huduma za afya, upatikanaji wa maji safi na salama, umeme, barabara, uimarishaji wa viwanja vya ndege kwa lengo la kukuza utalii, uimarishaji wa sekta ya elimu, uhakika wa chakula pamoja na kuwajengea wazee mazingira mazuri ya kuishi. Kama inavyoeleweka kuwa, Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazoendelea ambayo ina idadi ndogo ya wakaazi wanaoongezeka kwa kasi kubwa mwaka hadi mwaka. Pamoja na mafanikio yaliyofikiwa katika sekta mbali mbali, bado tuko nyuma kiuchumi na maendeleo ya kijamii. Hivyo, jitihada za makusudi zinahitajika katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi inayolingana na kasi ya ukuaji wa idadi ya watu wa asilimia 3.1.
8. Mheshimiwa Spika, Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Serikali ilianza kutekeleza Mpango wa Muda Mrefu wa Maendeleo ulioitwa DIRA ya Maendeleo ya 2020. Lengo la DIRA ni kuwa na mwongozo ambao utatusaidia katika utekelezaji wa sekta mbali mbali katika kujenga uchumi imara unaohimili ushindani wa kimataifa na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi ambayo yatasaidia kupunguza makali ya umasikini. Pamoja na utekelezaji wa Dira hiyo, Serikali pia inatekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs), Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 ambayo inaendana na mnasaba wa malengo yote haya. Katika utekelezaji wa Dira 2020, Serikali iliandaa na kutekeleza Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUZA) kwa awamu ya kwanza ambao uliotekelezwa kuanzia mwaka 2007 na kumalizika mwaka 2010. Aidha, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini kwa awamu ya pili (MKUZA II) umeshaandaliwa na utekelezaji wake unaendelea. Vile vile, kufuatia kukamilika nusu ya kwanza ya Dira 2020, Serikali imefanya mapitio ya utekelezaji wa Dira hiyo kwa kipindi cha miaka kumi ya awali. Kwa sasa Serikali inakamilisha kuipitia ripoti na mapendekezo ya mapitio hayo ambapo mambo yaliyojitokeza yataendelea kufanyiwa kazi, lengo ni kutafuta mbinu zaidi za kupunguza umasikini kwa wananchi wa Zanzibar.

UCHUMI WA DUNIA NA KIKANDA
9. Mheshimiwa Spika, Pato halisi la Taifa (Real GDP) katika uchumi wa dunia limekua kwa asilimia 5.0 mwaka 2010, ikilinganishwa na asilimia 0.5 mwaka 2009. Hali hiyo imetokana na kukua kwa taasisi za fedha baada ya kuhamasisha wawekezaji kuchukua mikopo ikiwemo kupunguzwa kwa gharama za uwekezaji na kupelekea kukua kwa Pato halisi kwa nchi zilizoendelea kwa asilimia 1.8 mwaka 2010 baada ya uchumi wa dunia, ukuaji wake kuzorota mwaka 2009. Uchumi wa nchi zinazochipukia kiuchumi na zile zinazoendelea umekua kwa hali ya kuridhisha. Hii inatokana na kuongezeka kwa usafirishaji mkubwa wa bidhaa nje. Ukuaji halisi wa uchumi kwa nchi hizo ulifikia wastani wa asilimia 6.1 kwa mwaka 2008 na kushuka hadi kufikia wastani wa asilimia 2.7 mwaka 2009. Katika mwaka 2010 uchumi wa nchi zinazoendelea umekuwa kwa hadi asilimia 7.3.
10. Mheshimiwa Spika, Athari za msukosuko wa fedha na uchumi uliozikumba nchi za Magharibi na nchi zinazoendelea ikiwemo Zanzibar umeanza kupungua taratibu. Katika nchi ambazo zinaonekana uchumi wake kukua kwa haraka, kama vile; Brazil, Russia, India, China (BRIC) athari hizo zimeathiri zaidi sekta za usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi. Hali hii imepelekea nchi hizi kupanga mikakati mipya ya ukuzaji wa uchumi.
11. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa uchumi wa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, umeonekana kuongezeka kwa wastani wa asilimia 5.0 mwaka 2010 kutoka ukuaji wa asilimia 2.8 mwaka 2009. Aidha, uchumi katika nchi za Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) haukuathirika sana na mtikisiko wa uchumi wa dunia. Kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi hizi imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 5.1 mwaka 2009 hadi kufikia wastani wa asilimia 5.6 mwaka 2010. Kwa upande wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, uchumi umekua kwa asilimia 5.2 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 5.6 mwaka 2010. Aidha, Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, uchumi wake kwa mwaka 2009 haukuonyesha ukuaji lakini katika mwaka 2010 umekuwa kwa wastani asilimia 3.3.
MAPITIO YA HALI YA UCHUMI WA ZANZIBAR
Pato la Taifa na Ukuaji Wake
12. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2010 uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua ingawa kwa kasi ndogo ikilinganishwa na mwaka 2009. Kwa bei za kudumu za mwaka 2001, Pato halisi la Taifa la Zanzibar limekua kwa asilimia 6.5 na kufikia Shilingi za Kitanzania bilioni 385.4 mwaka 2010 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.7 mwaka 2009 ambapo Pato la Taifa lilikuwa TZS 361.9 bilioni. Kasi ya ukuaji imeonekana kuwa chini ya makadirio yaliyotarajiwa ya kufikia ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2010. Hali hii imetokana na kushuka kwa kasi ya ukuaji wa sekta ndogo za umeme, viwanda, ujenzi na utalii. Aidha, ukuaji wa asilimia 6.5 umechangiwa zaidi na sekta ya huduma ambayo ukuaji wake umefikia asilimia 8.7 mwaka 2010 kutoka asilimia 8.8 mwaka 2009. Mwenendo huo wa ukuaji wa uchumi umepelekea kutofikiwa kwa kiwango cha ukuaji cha asilimia 8 hadi 10 baina ya mwaka 2005 na 2010 kama kilivyotarajiwa katika Dira ya Maendeleo ya 2020.
13. Mheshimiwa Spika, Wastani wa Pato la Taifa kwa mtu binafsi limekua likiongezeka mwaka hadi mwaka. Wakati idadi ya watu ilikadiriwa kufikia milioni 1.21 kwa mwaka 2010 ikilinganishwa na milioni 1.18 ya waliokuwepo mwaka 2009, ongezeko hili ni ukuaji wa asilimia 3.1 kwa mwaka. Kwa wastani, Pato la mtu binafsi kwa mwaka 2010 liliongezeka kwa asilimia 7.6 kutoka TZS 728,000 mwaka 2009 hadi kufikia TZS 783,370 mwaka 2010 hii ni sawa na Dola za Kimarekani 561 kwa mwaka 2010 kutoka Dola za Kimarekani 558 kwa mwaka 2009. Ni dhahiri kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi maskini ambayo wastani wa kipato cha mtu binafsi kiko chini ya Dola za Kimarekani 950. Azma ya Dira ya Maendeleo ya 2020 ni kufikia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2020.
MWENENDO WA SEKTA ZA KIUCHUMI
14. Mheshimiwa Spika, Ukuaji wa Sekta ya huduma umeonekana kupungua kutoka asilimia 8.8 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 8.7 mwaka 2010. Hali hii imetokana na kupungua kwa shughuli mbali mbali za huduma zikiwemo hoteli na mikahawa ambazo zilikuwa kwa asilimia 3.0 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 5.0 mwaka 2009. Sekta hii ina mchango mkubwa katika uchumi wa Zanzibar ingawaje mchango wake kwenye Pato la Taifa umeshuka hadi kufikia asilimia 42.5 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 44.1 ya mwaka 2009. Sekta hii inajumuisha pia Sekta ndogo za Huduma za Usafirishaji na Mawasiliano, Utawala wa Umma, Elimu, Biashara na Afya.
15. Mheshimiwa Spika, Wananchi wa Zanzibar wengi bado wanategemea kilimo kwa maisha yao ya kila siku. Hali hii ndio iliyopelekea ukuaji wa Sekta ya kilimo uimarike mwaka 2010 na kufikia asilimia 4.6 ikilinganishwa na asilimia 4.4 katika mwaka 2009. Aidha kutokana na ukuaji huo na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa Sekta ya Huduma, mchango wa Sekta hiyo katika uchumi umeongezeka kutoka asilimia 30.8 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 32.8 mwaka 2010. Ongezeko hilo limechangiwa zaidi na shughuli za mazao na ufugaji. Mwenendo mzuri wa Sekta ya Kilimo unamaanisha kwamba juhudi za Serikali katika kuimarisha Sekta hii zimeanza kuleta matunda. Juhudi hizo ni pamoja na utoaji wa taaluma kwa wakulima, matumizi ya vifaa vya kisasa kama vile matrekta, utumiaji wa mbegu bora zenye kustahamili ukame na maradhi, mbolea, na dawa ya kuulia wadudu na umwagiliaji.
16. Mheshimiwa Spika, Sekta nyengine muhimu kwa maendeleo ya uchumi ni Viwanda. Kwa bahati mbaya kasi ya ukuaji wa sekta hiyo imeshuka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2009 hadi asilimia 1.9 mwaka 2010. Mchango wa sekta hii katika uchumi umefikia asilimia 12.6 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 13.1 kwa mwaka 2009. Sababu kubwa ya kudorora kwa ukuaji wa sekta hii ni kukosekana kwa umeme nchini kwa zaidi ya miezi miwili mnamo mwanzoni mwa mwaka (10 Disemba 2009 hadi 8 Machi 2010).
Listen
Read phonetically
Dictionary
UKUZAJI RASILIMALI
17. Mheshimiwa Spika, Uwekezaji katika raslimali nao ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi. Mwenendo wake unaonesha kuwa ukuaji wa rasilimali umeongezeka kutoka thamani ya TZS 175.88 bilioni mwaka 2009 na kufikia TZS 200.94 bilioni mwaka 2010 sawa na asilimia 14.2. Ongezeko hilo la thamani limetokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali pamoja na sekta binafsi katika maeneo ya ujenzi wa barabara na miundombinu mingine ya kiuchumi na kijamii na ujenzi wa nyumba za kuishi na za biashara. Uwekezaji wa Miradi ya Ujenzi wa barabara na madaraja, umekuwa kwa asilimia 12.7 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 14.7 mwaka 2009.
18. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa sekta binafsi, kiwango cha uwekezaji kimeshuka kwa mwaka 2010 ikilinganishwa na kiwango cha miaka ya karibuni, idadi ya miradi iliyothibitishwa kutekelezwa katika mwaka 2010 ina thamani ya Dola za Kimarekani 110.34 milioni ikilinganishwa na Dola za Kimarekani 270.92 milioni ya mwaka 2009 sawa na upungufu wa asilimia 59.2. Asilimia 95.2 ya uwekezaji kati ya miradi iliyothibitishwa mwaka 2010 ulikuwa katika hoteli na mikahawa. Upungufu huu wa uwekezaji umetokana zaidi katika maeneo ya usafiri na mawasiliano, huduma za fedha, ujenzi na ukodishwaji wa majumba ya kisasa.
MWENENDO WA BEI
19. Mheshimiwa Spika, Uchumi endelevu unahitaji zaidi utulivu wa bei za bidhaa na huduma. Kasi ya mfumko wa bei kwa mwaka 2010 ilionekana kushuka na kufikia asilimia 6.1 ikilinganishwa na asilimia 8.9 mwaka 2009. Katika mwaka 2010, kasi ya mfumko wa bei kwa bidhaa za chakula ilishuka hadi asilimia 6.2 kutoka asilimia 9.6 mwaka 2009, wakati bidhaa zisizo za chakula, kasi yake ya mfumko wa bei ilipanda kidogo hadi asilimia 6.2 mwaka 2010 kutoka asilimia 6.1 mwaka 2009. Mwenendo huo wa bei umetokana na mambo yafuatayo:
• Kuanza kushuka kwa bei za chakula hasa mchele, unga na sukari katika soko la dunia kwa mwaka 2010 ukilinganisha na mwaka 2009 na
• Kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani wa mazao ya kilimo na mifugo.
SEKTA YA NJE
20. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mwaka ulioishia Machi 2011, hesabu ya urari wa kawaida (current account balance) ilipanda na kufikia nakisi ya Dola za Kimarekani 9.1 milioni kutoka ziada ya Dola za Kimarekani 4.4 milioni iliyofikiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2010. Hali hii inatokana na kushuka kwa bidhaa zinazosafirishwa kwenda nje pamoja na kushuka kwa uhaulishaji wa fedha kutoka nje (current transfers). Jumla ya usafirishaji wa bidhaa na huduma nchi za nje ulipanda kutoka Dola za Kimarekani 130.9 milioni mwaka ulioishia Machi 2010 na kufikia Dola za Kimarekani 140.0 milioni mwaka ulioishia Machi 2011, hasa kutokana na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utoaji wa huduma.
21. Mheshimiwa Spika, Nakisi ya Urari wa bidhaa za biashara (trade balance- merchandize) iliongezeka kutoka Dola za Kimarekani 65.7 milioni mwaka ulioishia Machi 2010 hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 86.1 mwaka ulioshia Machi 2011. Hii ilichangiwa na kupungua kwa usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi kutoka Dola za Kimarekani 23.9 milioni mwaka ulioishia Machi 2010 hadi kufikia Dola za Kimarekani 15.6 milioni mwaka ulioishia Machi 2011, pamoja na kuongezeka kwa uagiziaji wa bidhaa kutoka nje na kufikia Dola za Kimarekani 101.7 milioni mwaka ulioishia Machi 2011 kutoka Dola za Kimarekani 89.6 milioni mwaka ulioishia Machi 2010.
22. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa usafirishaji wa bidhaa, thamani ya usafirishaji wa zao la karafuu, ilipungua kwa asilimia 29.1 kutoka Dola za Kimarekani 10.3 milioni kwa mwaka ulioshia Machi 2010 hadi kufikia Dola za Kimarekani 7.3 milioni mwaka ulioishia Machi 2011. Kiwango cha usafirishaji wa zao la karafuu kilishuka kutoka tani 2,900 mwaka ulioishia Machi 2010 hadi kufikia tani 2,000 kwa mwaka ulioishia Machi 2011, wakati bei ya karafuu iliongezeka kutoka Dola za Kimarekani 3,559.8 kwa tani na kufikia Dola za Kimarekani 3,591.4 kwa tani kwa kipindi hicho hicho. Hata hivyo, takwimu za usafirishaji wa zao hili pia zinaathiriwa sana na magendo. Serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 imeandaa mipango madhubuti ya kupandisha mikarafuu mipya pamoja na kuwatafutia wakulima soko la uhakika ambalo litapelekea kuwapatia wakulima bei nzuri itakayo kuwa na tija. Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi imeelekeza kuwa na mipango mizuri ya kuyaimarisha mazao ya biashara, ikiwa ni pamoja na karafuu; mipango ambayo itasimamiwa kwa pamoja na Wizara ya Kilimo, Biashara na Fedha.

23. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa zao la mwani, bei ilionekana kushuka kutoka Dola za Kimarekani 264.4 kwa tani mwaka ulioishia Machi 2010 hadi kufikia Dola za Kimarekani 255.7 mwaka ulioishia Machi 2011, wakati kiwango cha usafirishaji pia kilipungua kutoka tani 10,900 hadi tani 9,300 katika kipindi hicho.
24. Mheshimiwa Spika, Thamani ya uagiziaji wa bidhaa (c.i.f) kwa mwaka ulioishia Machi 2011 iliongezeka na kufikia Dola za Kimarekani 111.7 milioni kutoka Dola za Kimarekani 98.4 milioni mwaka ulioishia Machi 2010. Uagiziaji wa bidhaa za kudumu (capital goods) uliongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 38.6 na kufikia Dola za Kimarekani 40.3 milioni, na uagiziaji wa bidhaa za kati (intermediate goods) uliongezeka kutoka Dola za Kimarekani 38.7 milioni na kufikia Dola za Kimarekani 52.2 milioni kwa kipindi hicho. Kupanda kwa thamani ya uagizaji wa bidhaa za kati kulitokana hasa na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia. Kwa upande wa uagiziaji wa bidhaa za matumizi ya kawaida (consumer goods), thamani ya uagiziaji ilishuka kwa asilimia 9.0 kutoka Dola za Kimarekani 21.1 milioni mwaka ulioishia Machi 2010 na kufikia Dola za Kimarekani 19.2 milioni mwaka ulioishia Machi 2011. Hali hii inaonyesha kuwa Zanzibar inatumia fedha nyingi katika kuagiza bidhaa kutoka nje ukilinganisha na usafirishaji. Hata hivyo, ipo haja kubwa ya kuangalia eneo hili kwa kushajihisha wananchi wazalishe zaidi pamoja na kuwa na viwanda vidogo vidogo na vya kati ambavyo vitatoa msukumo katika usafirishaji wa bidhaa zetu za ndani.
HUDUMA ZA FEDHA
25. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Fedha ni miongoni mwa sekta muhimu kwa maendeleo ya nchi. Tathmini inaonesha kwamba ukuaji wa Sekta hii nchini unaongezeka mwaka hadi mwaka. Amana za benki za kibiashara ziliongezeka kutoka TZS 241.0 bilioni Disemba 2009 na kufikia TZS 300.9 bilioni Disemba 2010 ikiwa ni sawa ongezeko la asilimia 24.9. Hali hii ya ukuaji mzuri wa uwekaji wa amana inaashiria wananchi wengi kufahamu umuhimu wa kuhifadhi fedha zao benki, baada ya kuongezeka kwa benki za kibiashara.
26. Mheshimiwa Spika, Baada ya kukusanya amana, jukumu la benki za biashara ni kutoa mikopo kwa Sekta Binafsi. Ukopeshaji wa fedha nao umeongezeka kwa asilimia 6.9 na kufikia TZS 82.5 bilioni Disemba 2010 kutoka TZS 77.2 bilioni mwishoni mwa Disemba 2009. Bado kiwango cha ukopeshaji ni kidogo na hali hii inatokana zaidi na ukubwa wa riba. Hata hivyo, Serikali itakaa na viongozi wa benki kuangalia uwezekano wa kupunguza riba ili kuwawezesha wananchi wengi kukopa. Kadhalika uwiano baina ya ukopeshaji na Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 8.8 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 9.4 mwaka 2010. Uchambuzi unaonesha kuwa mikopo kwa matumizi binafsi (Personal loans) ndio inayoongoza na kufikia asilimia 55.8 ya mikopo yote. Aidha nafasi ya pili ya ukopeshaji ilikwenda kwenye sekta ya biashara ambayo ni asilimia 12.1, utalii asilimia 6.7 wakati usafirishaji ulifikia asilimia 5.8. Hali hii ya ukopaji haiwezi kutusaidia sana, nawaomba wananchi kubadili mitazamo yao, fedha wanazokopa wazitumie zaidi kwa kufanyia biashara badala ya shughuli binafsi. Vile vile, hadi kufikia Disemba mwaka 2010, maduka 25 ya ubadilishaji wa fedha za kigeni (Bureau de Change) yamesajiliwa Zanzibar na yanaendelea kufanyakazi.
AJIRA RASMI
27. Mheshimiwa Spika, Kiwango cha ajira katika sekta iliyo rasmi imeongezeka kutoka watumishi 47,548 mwaka 2009 na kufikia 48,701 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 2.4. Kati ya hao watumishi 31,433 ni wa Serikali ambapo 14,748 ni wanawake na 16,685 ni wanaume. Waajiriwa katika Sekta Binafsi ni 13,148 ambapo kati ya hao 9,083 ni wanaume na 4,065 ni wanawake. Kadhalika, watumishi katika Mashirika ya Umma ni 4,120. Hali hii inaonesha kwamba sekta binafsi inaendelea kukua ikilinganishwa na Sekta ya Umma.
28. Mheshimiwa Spika, Katika kukabiliana na tatizo la ajira, Serikali imeweka mikakati maalum na utaratibu wa upatikanaji wa taarifa za nafasi za ajira. Serikali imeshakamilisha ujenzi wa kituo cha kutoa taarifa za nafasi za ajira kwa wanaomba kazi na taarifa za biashara na masoko kwa wajasiriamali. Kituo hicho kimeimarishwa kwa kupatiwa vifaa, vitendea kazi na watendaji wa kusimamia uendeshaji. Aidha, watendaji wanapatiwa mafunzo ili wafanye kazi kwa ufanisi zaidi. Kwa upande mwengine, Serikali inaziimarisha Sheria za Kazi kwa kuzifanyia marekebisho kasoro zilizomo ndani ya Sheria hizo. Hatua hii itasaidia sana kuelewa wapi pana nafasi ya ajira na upatikanaji wake utakuwa wa uwazi zaidi.
29. Mheshimiwa Spika, Katika kilele cha maadhimisho ya kutimiza miaka 47 ya Mapinduzi Matukufu, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar alieleza nia ya kutekeleza mpango mkubwa wa Mageuzi ya Utumishi wa Umma kwa lengo la kuimarisha utendaji Serikalini na huduma kwa wananchi. Programu ya Mageuzi ya Utumishi wa Umma inahusisha maeneo ya miundo ya utumishi, mifumo ya utoaji huduma, kusimamia na kuendeleza watumishi wa umma, utunzaji wa kumbukumbu na Mageuzi ya Serikali za Mitaa. Kukamilika kwa Programu hii kutapelekea kuwa na muundo wa utumishi wa umma unaokidhi mahitaji na matakwa ya nchi, kupatikana kwa taarifa za mahitaji halisi ya watumishi na sifa zinazohitajika. Vile vile, kutakuwa na sheria na miongozo inayotoa ufafanuzi juu ya majukumu baina ya Sekta ya Umma na Sekta ya Binafsi, uwajibikaji kwa watumishi wa umma na utoaji huduma kwa jamii pamoja na mfumo unaoridhisha wa maslahi ya watumishi wa umma.
30. Mheshimiwa Spika, Katika utekelezaji wa Programu hii; Sera na Sheria za Utumishi wa Umma zimetayarishwa. Aidha, utafiti unaofafanua majukumu ya Serikali umekamilika. Serikali inaendelea kufanya mapitio na ukaguzi wa Watumishi wa Sekta ya Umma na uimarishaji wa Mfumo wa Taarifa za Wafanyakazi na kutoa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa Programu ya Mageuzi ya Utumishi wa Umma.
31. Mheshimiwa Spika, Kupitia kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Serikali iliahidi kuimarisha maslahi ya wafanyakazi kwa nia ya kuwapunguzia makali ya maisha pamoja na kuhakikisha kuwa wataalamu wanaofundishwa kwa gharama kubwa wanabakia nchini. Kuhusu suala la mishahara ya Watumishi wa Umma, Serikali tayari imefanya mapitio na kuandaa mapendekezo mapya ya mishahara ya Watumishi ambayo itaanza kutumika mwaka wa fedha 2011/2012. Viwango vipya na taratibu zake zitatolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Mapendekezo hayo ya mishahara mipya yamezingatia vigezo mbali mbali ikiwa ni pamoja na elimu aliyonayo mtumishi, uzoefu na muda aliofanyia kazi. Miundo ya Utumishi (scheme) imewapanga watumishi na nyongeza zao za mishahara kwa kuzingatia muda wa uajiri na kiwango cha elimu. Mbali ya hatua zinazochukuliwa, Serikali itakuwa ikiongeza maslahi ya watumishi wa umma kila mwaka pale hali ya uchumi na mapato ya Serikali itakapokuwa nzuri.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA 2010/2011
32. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2010/2011 umeanza kwa utekelezaji wa MKUZA II kwa kuzingatia maeneo yaliyopewa msisitizo ambayo ni maendeleo ya watu, ustawi wa uchumi na kuimarisha utawala bora na demokrasia. Aidha, Dira ya Maendeleo ya 2020 ya Zanzibar, Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Malengo ya Maendeleo ya Milenia yameendelea kuwa nguzo katika utekelezaji wa program na miradi ya maendeleo.
33. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2010/2011 unatekeleza program 25 na miradi 94. Jumla ya TZS 251.20 bilioni zimepangwa kugharamia program/miradi hiyo. Kati ya fedha hizo TZS 39.49 bilioni sawa na asilimia 15.7 zimepangwa kutolewa na Serikali na TZS 211.71 bilioni sawa na asilimia 84.3 zilitarajiwa kutolewa na Washirika wa Maendeleo. Kati ya fedha zilizotarajiwa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo TZS 78. 92 bilioni ni ruzuku na TZS 132.79 bilioni ni mikopo.
34. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai 2010 hadi Machi 2011, matumizi ya kazi za maendeleo kutokana na mchango wa Serikali yalifikia TZS 24.51 bilioni sawa na asilimia 62 ya makadirio ya mwaka. Kiwango hicho cha matumizi kimepungua kwa asilimia 13.36 ambapo zilitolewa TZS 28.29 bilioni ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita 2009/2010. Sababu kuu ya kushuka huko ni kutokana na kuwa na harakati za Uchaguzi Mkuu ambapo Wizara ya Fedha ilichukua hatua maalumu za kudhibiti matumizi ya Serikali.
35. Mheshimiwa Spika, Mchango wa Kazi za Maendeleo kupitia fedha za Washirika wa Maendeleo ni ya kuridhisha ikilingalishwa na mwaka uliopita. Katika kipindi cha Julai 2010 hadi Machi 2011 fedha zilizokwisha kutolewa na Washirika wa Maendeleo zimefikia TZS 117.71 bilioni sawa na asilimia 56 ya fedha zilizokadiriwa. Ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, kumekuwa na ongezeko la fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ambapo jumla ya TZS 66.98 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 75.9. Sababu kubwa ya ongezeko hilo inatokana na kuongezeka kwa ufanisi katika kupanga, kusimamia pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo. Aidha kumekuwa na ufanisi wa upatikanaji wa taarifa za matumizi ya fedha za Washirika wa Maendeleo kutokana na matumizi ya database inayotumia mfumo wa mtandao (Aid Management Platform).
¬Klasta ya I: Ukuzaji Uchumi na Kupunguza Umaskini wa Kipato
36. Mheshimiwa Spika, Ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo, Serikali imeugawa katika Klasta tatu. Klasta ya kwanza ni Ukuzaji Uchumi na Kupunguza Umaskini wa Kipato kwa 2010/2011 ilipangiwa kutekeleza programu 14 na miradi 27 ya maendeleo kwa kutumia jumla ya TZS 114.43 bilioni sawa na asilimia 45.6 ya Bajeti ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo mchango wa Serikali ni TZS 16.74 bilioni sawa na asilimia 14.6, wakati Washirika wa Maendeleo walitarajiwa kuchangia jumla ya TZS 97.69 bilioni ikiwa sawa na asilimia 85.4 ya bajeti ya klasta hii. Katika kipindi cha miezi tisa (Julai 2010 mpaka Machi 2011) jumla ya TZS 104.78 bilioni zimetolewa sawa na asilimia 92.2 ya bajeti ya Klasta ya kwanza. Kati ya fedha hizo Serikali imetoa TZS 13.1 bilioni sawa na asilimia 78.4 na Washirika wa Maendeleo wamechangia TZS 91.6 bilioni sawa na asilimia 93.7 ya makadirio.
37. Mheshimiwa Spika, Utekelezaji halisi katika klasta hii kwa baadhi ya sekta ni kama ifuatavyo:
Kilimo:
38. Mheshimiwa Spika, Sekta hii kwa mwaka 2010/2011 ililenga katika kuongeza uzalishaji wa mazao yenye ubora na tija, kuongeza ufanisi katika udhibiti wa matumizi ya maliasili na kupunguza uharibifu wa mazingira. Sekta ilipata mafanikio katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Kwa upande wa mazao ya chakula uzalishaji umeongezeka kutoka jumla ya tani 400,905 mwaka 2009 hadi kufikia jumla ya tani 440,529. Mazao yaliyoongezeka uzalishaji wake ni mpunga ambao ulitoka tani 26,980 mwaka 2009 mpaka 31,000 mwaka 2010, muhogo tani 195,674 mwaka 2009 mpaka tani 229,284 mwaka 2010, ndizi tani 100,873 mwaka 2009 mpaka 102,258 mwaka 2010 na viazi vitamu kutoka tani 53,596 mwaka 2009 hadi 58,958 mwaka 2010. Aidha, kwa upande wa mazao ya biashara uzalishaji nao pia umeongezeka kutoka jumla ya tani 14,657 mpaka jumla ya tani 15,526. Zao lililoongezeka katika uzalishaji ni mwani ambao umetoka tani 10,248 mwaka 2009 hadi tani 12,516 mwaka 2010. Mafanikio haya yametokana na matumizi bora ya pembejeo ikiwemo usambazaji wa tani 390 za mbolea, matumizi ya trekta, mashine za kuchimbia. Vile vile, Serikali ilisambaza tani 51 za aina mbali mbali za mbegu za mpunga kwa wakulima Unguja na Pemba. Aidha, Serikali iliendelea na kuimarisha miundo mbinu ya umwagiliaji maji katika mabonde ya Tunduni, Bumbwisudi, Kianga, Jendele, Machigini na Tungamaa.
39. Mheshimiwa Spika, Serikali ilitilia mkazo utafiti katika sekta hii na kufanya tafiti mbali mbali zikiwemo zile za mazao ya mpunga na mahindi. Kwa upande wa zao la mpunga majaribio ya aina mbegu ya NERICA yalifanyika kwa lengo la kutoa aina mpya za mbegu baada ya aina nne za hapo awali kuzalishwa. Mbegu ya NERICA itasaidia sana wakulima wetu kwani inaota katika maeneo ya juu badala ya kutegemea mabonde. Tukijipanga vizuri katika eneo hili, tunaweza kujitosheleza kwa mpunga baada ya kipindi kifupi pamoja na kusafirisha mbegu za mpunga. Tafiti nyengine za aina 55 za mpunga kutoka China zilifanyika zikilinganishwa na mbegu za kiasili ambapo 12 kati ya mbegu hizo zimeonyesha matokeo ya kutoa mazao zaidi ikilinganishwa na mbegu 3 za kiasili. Kwa upande wa mahindi aina 15 za mbegu zilifanyiwa utafiti, awamu ya kwanza ya utafiti mbegu 5 zimechaguliwa ambazo zimeonyesha kuwa na uzazi mkubwa na sasa zinaendelezwa kwa awamu ya pili.
Mifugo
40. Mheshimiwa Spika, Huduma za kinga na tiba zimeendelea kutolewa kwa wafugaji wanaohitaji huduma hizo na jumla ya mifugo 94,131 ilitibiwa na 68,533 kupatiwa kinga dhidi ya maradhi mbali mbali. Aidha idadi ya ng’ombe wa maziwa imeongezeka kutoka ng’ombe 9,500 mwaka 2009 hadi ng’ombe 11,409. Vile vile huduma za kupandisha ng’ombe kwa sindano zimeimarika ambapo kwa sasa Serikali inazalisha Liquid Nitrogen ya kutosheleza mahitaji Unguja na Pemba ambapo ng’ombe 459 tayari wamefaidika na huduma hiyo. Serikali imekusudia kuendeleza mifugo ili tuweze kujitosheleza kwa kitoweo na hatimae kusafirisha nchi za nje kwani soko la mifugo ni kubwa sana.
Uvuvi
41. Mheshimiwa Spika, Sekta hii imedhihirisha ongezeko la uzalishaji wa samaki na thamani yake. Jumla ya tani 25,693 zenye thamani ya TZS 61.78 bilioni mwaka 2010 zimezalishwa ikilinganishwa na tani 25,397 zenye thamani ya TZS 47.71 bilioni mwaka 2009. Mafanikio haya yamechangiwa kwa kushirikisha jamii katika uhifadhi wa rasilimali za baharini pamoja na kukabiliana na uvuvi haramu. Vile vile kuendelea kutoa mafunzo na vifaa kwa wavuvi na kushajiisha wavuvi juu ya ufugaji wa samaki na mazao mengine ya baharini. Aidha, Serikali ilitoa leseni 16 kwa wavuvi wanaovua bahari kuu. Leseni tano zilitolewa kwa mashirika ya uvuvi kutoka Seychelles na 11 zimetolewa kwa mashirika ya uvuvi kutoka Spain. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa wavuvi wetu wanawezeshwa kwa kupatiwa mikopo ili waweze kuwa na boti za kisasa zaidi na hatimae kuwa na uwezo mkubwa wa kuvua na hasa bahari kuu ambayo ina samaki wengi zaidi.
Uwezeshaji wananchi kiuchumi
42. Mheshimiwa Spika, Mfuko wa kuwawezesha wananchi kiuchumi ambao ulizinduliwa 2008 ulikuwa na lengo la kutoa fursa ya kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu wananchi wenye kipato cha chini ili waweze kujiajiri pamoja na kuwawezesha kiuchumi na hatimae kuwapunguzia wananchi umaskini wa kipato . Hadi kufikia Machi 2011, Serikali imetoa mikopo yenye jumla ya thamani ya TZS 1.4 bilioni kupitia Mfuko wa JK na AK. Mikopo hiyo imetolewa kwa watu binafsi 660, vikundi 58 na SACCOS 10 katika mikoa yote ya Unguja na Pemba. Vile vile, Serikali imetoa mikopo yenye thamani ya TZS 25.8 milioni kupitia Mfuko wa Kujitegemea.
43. Mheshimiwa Spika, Idadi ya waliopata mkopo na kima kilichotolewa ni kidogo ikilinganishwa na maombi yaliyopokelewa, ni asilimia 43 tu ya waombaji ndio waliopatiwa mikopo. Katika kipindi cha miezi sita ya awali, baada ya kuzinduliwa mikopo ulipaji ulikuwa ni mzuri. Kadiri siku zilivyokuwa zikienda ulipaji haukuwa wa kuridhisha. Hata hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika watashirikiana na Benki ya Watu wa Zanzibar na CRDB kuandaa utaratibu wa ukusanyaji wa mikopo iliyotolewa.
44. Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) unatoa mchango mkubwa katika jitihada za Serikali za kuyafikia Malengo Milenia na utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar. Programu hii inatekelezwa kutokana na mkopo wa Benki ya Dunia ambayo inatoa fedha za kutekeleza miradi inayoibuliwa na wananchi. Shughuli za Mfuko wa TASAF Awamu ya Pili zinatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 2011. Hadi kufikia mwezi March 2011, jumla ya miradi 104 ya wananchi imetekelezwa ambapo miradi 54 kwa Unguja na miradi 50 kwa Pemba. Miradi yote hiyo imetumia jumla ya TZS 1.49 bilioni kwa Unguja na Pemba. Miradi hiyo inajumuisha shughuli za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Barabara, na Viwanda vidogo vidogo. Aidha TASAF imetoa mafunzo ya ujasiri amali kwa vikundi 45 vya kuweka na kuwekeza.
Utalii
45. Mheshimiwa Spika, Utalii ni sekta muhimu katika kukuza uchumi wa Zanzibar. Vile vile ina mchango mkubwa katika Pato la Taifa. Sekta hii inahusisha uingiaji wa wageni kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ukuaji wake unaangaliwa zaidi kutokana na shughuli za hoteli na mikahawa. Kwa mwaka 2010 uingiaji wa wageni umeshuka kutoka watalii 134,954 mwaka 2009 hadi watalii 132,836 mwaka 2010. Hivyo, kusababisha kasi ya ukuaji wa shughuli za hoteli na mikahawa kupungua kutoka asilimia 5 mwaka 2009 hadi asilimia 3 mwaka 2010. Hata hivyo, Serikali bado itaendelea na lengo lake la kukuza utalii ili uwe chachu katika kuendeleza kilimo na viwanda. Sambamba na kukuza utalii, wananchi na hasa vijana watahamasishwa kushiriki katika kilimo chenye tija zaidi.
Nishati
46. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani inaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa njia ya pili ya umeme kutoka Ras Kiromoni hadi Fumba ambao unatarajia kuongeza kiwango cha umeme kufikia Megawati 100. Kampuni ya Viscas Corporation ya Japan inaendelea na utengenezaji wa waya wa kulaza baharini. Aidha, TZS 5.30 bilioni zimetumika kuwalipa fidia wananchi 843 waliopo katika eneo la mradi kutokana na fidia ya mali na mazao yao. Kati ya fedha hizo TZS 3.20 bilioni zimelipwa na Serikali ya Marekani na TZS 2.1 bilioni zimelipwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia sana kuwa na umeme wa uhakika. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi ina mpango wa kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia upepo na jua. Juhudi za kuzalisha umeme kwa kutumia upepo ziko mbioni na tayari maeneo kama Makunduchi, Matemwe na Nungwi yameonyesha kuwa na upepo ambao una uwezo wa kuzalisha umeme.
47. Mheshimiwa Spika, Chanzo kikuu cha nishati ya kupikia kwa Zanzibar ni kuni; nyumba saba kati ya nyumba 10 zinatumia kuni ikifuatiwa na matumizi ya makaa hivyo kusababisha ukataji ovyo wa miti na kuharibu mazingira. Hata hivyo, Serikali inaendeleza juhudi za kutoa taaluma ya matumizi ya nishati mbadala ikiwemo matumizi ya gesi na mafuta ya taa hadi hapo uwezo wa uzalishaji utakapokuwa mzuri na wananchi kufaidika na nishati ya umeme.
Biashara
48. Mheshimiwa Spika, Serikali ilipitisha Sera ya Biashara ya Zanzibar. Moja kati ya mikakati iliyomo ndani ya sera hiyo ni kuifanya Zanzibar kuwa Eneo Tengefu la Uchumi (SEZ) ndani ya ushirikiano wa Afrika Mashariki, ili iweze kufaidika kiuchumi ndani ya Jumuia hiyo. Serikali tayari imepata kampuni elekezi ya “Crisil Risk and Infrastructure” ya India ili kufanya utafiti juu ya suala hilo. Aidha katika kuweka mazingira bora ya biashara, Serikali imekamilisha Sheria ya kusimamia viwango na ubora wa bidhaa itakayounda taasisi ya viwango ya Zanzibar ili kusimamia na kuweka viwango vya bidhaa zinazozalishwa, zinazosafirishwa na zinazoingizwa nchini.
Usafirishaji
49. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2010/2011 Serikali imejenga jumla ya kilomita 91 za barabara kati ya kilomita 125 zilizopangwa kwa Unguja na Pemba. Kati ya hizo kilomita 25 zimekamilika kwa kiwango cha lami, kilomita 40 zimefikia kiwango cha sub-base na kilomita 36 zimesafishwa na kuwekwa kifusi cha mwanzo. Kazi za kuzifanyia matengenezo barabara za mijini na vijijini zimefanyika. Vile vile, kwa hatua za awali, Serikali imeanza ujenzi wa jengo jipya la abiria na huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, ujenzi unaofanywa na Kampuni ya Beijing Construction Engineering kutoka China. Kukamilika kwa ujenzi huo kutaongeza zaidi idadi ya watalii na hatimae kukuza uchumi.
MKUMBITA (BEST)
50. Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha mazingira bora ya Biashara Zanzibar, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa (MKUMBITA) ambao lengo kuu ni kuhakikisha kwamba kunakuwepo na mazingira ya kisheria yatakayorahisisha uendeshaji Biashara nchini. Hadi kufikia Machi 2011 kazi zifuatazo zimetekelezwa chini ya Mpango huu:
§ Kusimamia mageuzi katika uingiaji na utokaji katika Biashara, pamoja na usajili wa mikataba ya mali zinazohamishika.
§ Kupitia mfumo wa leseni za biashara.
§ Kufaya utafiti wa mahitaji ya Ofisi ya Mrajis Mkuu wa Serikali.
§ Kupitia viwango vya kodi kwa biashara ndogo ndogo na za kati.
§ Kuwapatia mafunzo watendaji kutoka Taasisi mbalimbali ambao wanashughulikia Mpango huu.
51. Mheshimiwa Spika, Kuendeleza mazingira ya kisheria na biashara nchini mwetu ni kigezo muhimu katika mkakati wetu wa kuvutia uwekezaji na kupungunguza umaskini, mwezi Machi mwaka huu tulizindua ripoti ya Urahisi wa utekelezaji wa biashara kwa Zanzibar. Ripoti hiyo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Benki ya dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC), na “Multilateral Investment Guarantee Agency” (MIGA) na imeonesha kuwa kati ya nchi 183, Zanzibar tuko nafasi ya 155 kwa urahisi wa kuendesha biashara. Hata hivyo, kwa upande wa kusimamia mikataba Zanzibar inashika nafasi ya 37 kati ya nchi 183 na nafasi ya pili tukilinganishwa na nchi 34 za visiwa zenye kuendelea kiuchumi. Hali yetu sio mbaya lakini kuna haja ya kufanya mapitio ya Sheria, Kanuni na taratibu zetu katika uanzishaji na ufungaji biashara, utoaji vibali vya ujenzi, usimamizi wa mikataba, kuwalinda wawekezaji, kusimamia biashara mipakani na kupata mikopo.
52. Mheshimiwa Spika, Baada ya kupata matokeo ya ripoti hiyo, Serikali imeandaa mpango kazi “Road Map’’ kwa ajili ya kuyafanyia miongozo mapendekezo ya ripoti hiyo. Mpango kazi huu unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka 2011/2012 baada ya kupitiwa, kujadiliwa na kukubaliwa na wadau husika.
53. Mheshimiwa Spika, Kama nilivyoeleza awali nchi yetu hivi sasa inaongozwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hali hii imeleta utulivu amani na mapenzi baina ya wananchi, hali ambayo imeletea wafanyabiashara, wawekezaji na wageni kutokwa na hofu ya kuja kufanya shughuli zao hapa Zanzibar. Bila ya shaka utulivu na amani iliopo itatuongezea wawekezaji, watalii na wafanyabiashara na hatimae kuongezeka kwa Pato la Taifa na ubora ya maisha ya wananchi wetu. Hapa napenda kuchukua fursa hii kuendelea kuwaomba sana wananchi kuendeleza amani iliopo na mapenzi miongoni mwetu kwani sisi sote ni ndugu.
Klasta ya II: Huduma na Ustawi wa Jamii
54. Mheshimiwa Spika, Klasta ya Huduma na Ustawi wa Jamii kwa 2010/2011 ambayo ni ya pili, ilipangiwa kutekeleza programu sita na miradi 37 ya maendeleo na kukadiriwa kutumia jumla ya TZS 110.88 bilioni sawa na asilimia 44.1 ya Bajeti ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo Serikali ilitenga TZS 9.48 bilioni sawa na asilimia 8.5 na Washirika wa Maendeleo walitarajiwa kuchangia jumla ya TZS 101.404 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 91.5 ya bajeti ya klasta hii.
55. Mheshimiwa Spika, Kuanzia Julai 2010 hadi Machi 2011, jumla ya TZS 27.3 bilioni zimetolewa sawa na asilimia 24.6 ya makadirio ya Bajeti ya Maendeleo kwa klasta ya pili. Kati ya fedha hizo Serikali imetoa TZS 4.8 bilioni sawa na asilimia 51.1 na Washirika wa Maendeleo wamechangia TZS 22.5 bilioni sawa na asilimia 22.2 ya makadirio ya kuchangia.
56. Mheshimiwa Spika, Utekelezaji halisi katika klasta hii ya pili kwa baadhi ya sekta ni kama ifuatavyo:
Elimu
57. Mheshimiwa Spika, Moja kati ya changamoto iliyobainika katika matayarisho ya MKUZA ni kiwango kidogo cha lugha ya kiingereza pamoja na masomo ya sayansi na hisabati kwa wanafunzi wetu na walimu. Serikali imeendelea kutoa mafunzo ya lugha ya kiingereza kwa walimu wapatao 700 wanaosomesha madarasa ya msingi ili kutumia lugha hii kwa kufundishia masomo mbali mbali kuanzia darasa la tano. Pia katika kuwashajiisha wanafunzi wa kike wa Sekondari hasa katika kupenda masomo ya sayansi na hisabati, wanafunzi hao wameendelezwa kupitia kambi za sayansi. Vitabu vya masomo ya Jiografia, Elimu ya Uraia, Dini, Biashara na Ufundi vimenunuliwa na kusambazwa katika skuli mbali mbali.
58. Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Elimu ya Juu umeendelea kutoa mikopo kwa ajili ya masomo kwa vijana wanaokwenda kusoma ndani na nje ya nchi. Jumla ya wanafunzi 1,271 wamepatiwa mikopo wakiwemo 1,058 katika vyuo vya ndani na 213 katika vyuo vya nje. Sheria mpya ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imeshapitishwa na Baraza lako tukufu ili kuufanya mfuko ujitegemee zaidi na kutekeleza kazi zake kwa ufanisi.
59. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na azma yake ya kuendelea kutoa huduma na kuimarisha ubora wa elimu kwa ngazi zote, nina furaha kuliarifu Baraza lako tukufu kuwa ujenzi wa skuli mpya 15 za sekondari za vijijini unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwisho mwa mwaka 2011. Skuli hizo ni Paje Mtule, Matemwe, Mwanda, Chaani, Uzini, Dole, Tunguu na Dimani kwa upande wa Unguja na Wawi, Ngwachani, Kiwani, Mauwani, Utaani, Pandani, Konde na Tumbe kwa upande wa Pemba. Kukamilika kwa skuli hizi kutaimarisha huduma na kupunguza msongamano wa wanafunzi katika madarasa. Aidha, skuli hizi zitatoa nafasi zaidi kwa wanafunzi kusoma masomo ya sayansi na kompyuta kwani zimejengwa pamoja na maabara.
Afya
60. Mheshimiwa Spika, Sekta ya afya inaendelea kuimarika ambapo kwa mwaka 2010/2011, jumla ya wafanyakazi 76 wakiwemo wanaume 44 na wanawake 32 wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi kuhusiana na masuala mbali mbali ya afya. Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu kama vile ujenzi wa vituo vya afya ambavyo vinasaidia sana katika kutoa huduma. Jitihada kadhaa zimeendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha kuwa dawa muhimu zinapatikana pamoja na vifaa vya matibabu vinavyokidhi haja. Vile vile ujenzi wa majengo matatu katika Chuo cha Afya Mbweni umeanza. Ujenzi wa nyumba 20 za wafanyakazi Pemba umekamilika na kukabidhiwa kwa wahusika. Halikadhalika huduma za kujifungua katika vituo vya afya zimeongezeka na jamii imehamasishwa kutumia njia za uzazi wa mpango. Vile vile, Serikali imeendelea na juhudi zake za kuhakikisha kuwa maradhi ya malaria yanaondoka kabisa Zanzibar. Elimu ya afya imeendelea kutolewa kwa maradhi yakuambukiza na yasiyo ya kuambukiza. Utoaji huo wa elimu umesaidia sana kwa wananchi kufahamu sababu kuu zinazosababisha maradhi hayo na hivyo kuanza kuchukua tahadhari.
Maji
61. Mheshimiwa Spika, Kutokana na matokeo ya Utafiti wa Matumizi na Mapato ya Kaya, usambazaji wa mabomba kwa ajili ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi umefikia asilimia 89.4 mwaka 2009/2010, ingawa upatikanaji wa maji bado unaendelea kuwa ni changamoto kubwa kwa Zanzibar na zaidi katika maeneo ya mjini ikilinganishwa na vijijini ambapo viwango vya matumizi ya maji vimeongezeka kutoka asilimia 80.6 mwaka 2004/2005 hadi 85.9 mwaka 2009/2010 katika maeneo ya vijijini.
62. Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa uhuishaji na upanuzi wa shughuli za maji Mkoa Mjini Magharibi umekamilika kwa kujenga matangi makubwa mawili, Dole na Kinuni na kuchimba visima vitano pamoja na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 21. Mafanikio ya mradi huu hayajaonekana sana kwa baadhi ya maeneo ya mjini kutokana na uchakavu uliopo wa mabomba na kusababisha maji mengi kupotea ardhini kabla ya kuwafikia watumiaji. Serikali inaendelea na jitihada za kurekebisha hali hiyo. Hata hivyo, tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama ni kubwa. Jumla ya dola za Kimarekani 123 milioni zinahitajika ili kuondokana na tatizo lililopo kwa ajili ya kuchimba visima zaidi, kununulia mabomba na pampu pamoja na kujenga matangi ya ziada. Serikali kwa kuona uzito wa tatizo hilo, upatikanaji wa maji safi na salama umepewa kipaumbele.
Vijana, Wanawake na Watoto
63. Mheshimiwa Spika, Serikali imezindua Mfuko wa Vijana unaoendeshwa na Shirika la UN-Habitat unaogharimiwa na Serikali ya Norway ambao una lengo la kuwaendeleza vijana kiuchumi. Mfuko huo umetengewa jumla ya TZS 149 milioni. Aidha mikutano ya kuwaelimisha vijana wa Zanzibar juu ya utaratibu na masharti ya kupata fedha kwenye mfumo huo tayari imeshafanyika Unguja na Pemba.
64. Mheshimiwa Spika, Mafunzo ya haki za watoto yametolewa kwa baraza la watoto yakiwa na lengo la kutoa fursa kwa watoto kujua haki zao na kuweza kutoa taaluma ya haki hizo kwa watoto wenzao ndani ya jamii. Vile vile, Sheria ya Mtoto imeshapitishwa na Baraza lako tukufu na uratibu wa mafunzo ya kuwasilisha ujumbe wa haki za watoto kwa watendaji wa shughuli za watoto umeshaandaliwa. Aidha kituo cha One Stop Centre kimeanzishwa kikiwa na lengo la kuratibu shughuli zote za udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto. Kituo hicho kipo hospitali ya Mnazi Mmoja (Unguja) na vile vile Chake Chake (Pemba). Vituo hivyo vitajumuisha watendaji kutoka Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Jeshi la Polisi, Wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Madaktari. Lengo la kuanzishwa Vituo hivyo ni kurahisisha ufuatiliaji wa kesi na matukio ya udhalilishaji wa kijinsia. Kadhalika, kumejitokeza vitendo vya ubakaji ndani ya visiwa vyetu vya Zanzibar na hali imefikia kutisha. Serikali itafanya kila liwezalo katika kuhakikisha kuwa vitendo vya ubakaji vinakomeshwa na kufikiwa mwisho.
Klasta ya III: Utawala Bora na Umoja wa Kitaifa
65. Mheshimiwa Spika, Klasta ya Utawala Bora na Umoja wa Kitaifa ni klasta ya tatu, kwa 2010/2011 ilipangiwa kutekeleza programu tano na miradi 30 ya maendeleo na ilipangiwa kutumia jumla ya TZS 25.89 bilioni sawa na asilimia 10.3 ya bajeti ya maendeleo. Kati ya fedha hizo Serikali ilitenga TZS 13.27 bilioni sawa na asilimia 51.2 ya bajeti na Washirika wa Maendeleo walitarajiwa kuchangia jumla ya TZS 12.26 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 48.8 ya bajeti ya klasta hii.
66. Mheshimiwa Spika, Kuanzia Julai 2010 hadi Machi 2011, TZS 10.1 bilioni sawa na asilimia 39 ya Bajeti ya Maendeleo kwa Klasta ya tatu zimetolewa. Kati ya fedha hizo, Serikali imetoa TZS 6.5 bilioni sawa na asilimia 49.2 na Washirika wa Maendeleo wamechangia TZS 3.6 bilioni sawa na asilimia 28.6.67. Mheshimiwa Spika, Utekelezaji halisi katika klasta hii kwa baadhi ya sekta ni kama ifuatavyo:
Utawala
68. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi ili kuongeza ufanisi na tija katika maendeleo ya nchi. Kwa mwaka 2010/2011, Serikali imeendelea na ujenzi wa baadhi ya ofisi na sasa zimo katika hatua za kukamilika. Ofisi zenyewe ni Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini (Unguja), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini (Unguja), Ofisi ya Makao Makuu ya Valantia, ujenzi wa Kituo cha Mafunzo na Utafiti wa Sheria kinachojengwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka n.k. Aidha, ujenzi wa Makao Makuu ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali umekamilika.
Utawala Bora
69. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na kuwashajihisha watendaji wa Serikali kuongeza uelewa wa Sheria ya Fedha za Umma, Sheria ya Manunuzi na Uondoshaji wa Mali za Serikali na Sheria ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Aidha, mafunzo ya msingi ya “Risk Based Audit” yametolewa kwa madhumuni ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili kuweza kuhakiki maeneo ya upotevu wa mapato ya Serikali na kutambua maeneo hatarishi ya matumizi ya fedha yanayofanywa kinyume na utaratibu. Pia watendaji hao wanapatiwa mafunzo ya ukaguzi wa mbinu za kisasa unaofanywa duniani yakiwemo ukaguzi wa thamani, ukaguzi wa kutumia kompyuta na ukaguzi wa mazingira. Serikali itaendelea kuwapatia mafunzo watumishi wake kwa lengo la kubadilika katika utekelezaji wa majukumu yao.
Maafa
70. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea pia kujenga uwezo wa Zanzibar katika kujiandaa na kukabiliana na maafa. Rasimu ya Sera ya kukabiliana na maafa imeanza kujadiliwa na wadau ikiwemo Kamati za Kukabiliana na Maafa za Mikoani na Wilaya ili kupata maoni ya kuimarisha sera hiyo. Pia vifaa mbali mbali kwa ajili ya matumizi ya wakati wa hali ya dharura vimepatikana yakiwemo mahema, vifaa vya huduma ya kwanza, maturubali na mablanketi. Ni muhimu kwa Serikali na jamii kwa ujumla wake kujitayarisha katika kukabiliana na maafa. Serikali imejipanga kutoa kila msukumo katika eneo hili.
Sheria
71. Mheshimiwa Spika, Sekta ya sheria ni muhimu sana katika kusimamia haki, usawa, kuleta ustawi na ufanisi katika jamii. Serikali kupitia Sekta hii imezichapisha Sheria za Zanzibar kuanzia mwaka 1980 hadi 2010 ambapo jumla ya juzuu (volumes) 15 zimechapishwa na kusambazwa kwa wadau, sambamba na uchapishaji wa nakala zisizopungua elfu tatu (3,000) za Katiba ya Zanzibar na kusambazwa kwa taasisi mbali mbali za Serikali, Mashirika na Taasisi Binafsi. Aidha katika kuendelea na mageuzi ya kuingia na kutoka katika biashara, Serikali imepitisha Sheria ya Usajili wa Mikataba ya Mali isiyohamishika. Kwa hatua hizi zinazochukuliwa na Serikali, wananchi nao hawana budi kuzifahamu sheria zinazosimamia maslahi yao na nchi yao. Imebainika wananchi wengi hufanya makosa kwa kisingizio cha kutokuijua sheria.
Habari
72. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2010/2011, Serikali ilikusudia kubadilisha Sekta ya Utangazaji na kuwa na mfumo wa mitambo ya kisasa ya dijitali na kuondokana na mfumo wa zamani wa urushaji wa matangazo wa analogi. Baadhi ya mitambo ya mfumo mpya wa digitali imeshawasili hapa nchini na Serikali imo mbioni kuunganisha mitambo hiyo. Zanzibar tukiwa ni sehemu ya dunia, hatuwezi kuwa nyuma katika matumizi ya mfumo mpya wa dijitali.
¬MASUALA YA MTAMBUKA
73. Mheshimiwa Spika, Masuala ya mtambuka ni miongoni mwa masuala yanayostahiki kupewa umuhimu katika utayarishaji wa Sera na Mipango. Masuala hayo yanajumuisha mazingira, jinsia, idadi ya watu, maafa, utawala bora na ukimwi. Ili kuyapa msukumo unaostahiki, masuala ya usimamizi wa mazingira, ukimwi na ulemavu yamewekwa chini ya Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais. Ni dhahiri kuwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii yanategemea kuwepo kwa Mpango madhubuti wa kusimamia matumizi bora ya ardhi na mazingira. Kukua kwa kasi kwa idadi ya watu kunachangia sana uharibifu wa mazingira yanayowazunguka, kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii. Katika kukabiliana na athari hizo utayarishaji wa Kanuni za Tathmini za Athari ya Mazingira na Maliasili zisizorejesheka uko katika hatua za mwisho kukamilika. Kukua kwa idadi ya watu ni changamoto kubwa Zanzibar ambapo juhudi za makusudi zinahitajika kwa ajili ya kutunza afya ya mzazi. Aidha elimu inahitajika kwa vijana hususan watoto wa kike. Vile vile, kuongezeka kwa harakati za maendeleo katika ukanda wa pwani, changamoto mbali mbali zimejitokeza zikiwemo kuharibiwa kwa mazalio ya kasa na samaki, ukataji wa miti kwa matumizi ya kupikia na kujengea, njia duni za uvuvi, uchimbaji wa mawe na mchanga.
74. Mheshimiwa Spika, Katika mikakati ya utunzaji wa mazingira, Serikali katika mwaka 2010/2011 iliweza kutoa elimu kwa jamii na wawekezaji nchini kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na mwenendo mzima wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Jumla ya miradi 36 ya uwekezaji ilifanyiwa mapitio na kutolewa ushauri wa kimazingira. Aidha miradi 14 imefanyiwa tathmini za athari za kimazingira katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar. Vile vile Serikali inaendelea kusimamia amri ya upigaji marufuku uingizwaji na matumizi ya mifuko ya plastiki ikiwemo kutoa elimu kwa wadau mbali mbali kuhusu athari za matumizi ya mifuko hiyo. Kwa upande mwengine, hatua maalum zinaendelea kuchukuliwa kwa kuangamiza kunguru weusi ambao wamebainika kuwa na athari kubwa kwa mazingira na jamii. Kadhalika, Serikali itahakikisha kuwa inawatafutia vijana na wananchi kwa ujumla njia mbadala za kuendesha maisha yao, badala ya uharibifu wa mazingira kama ndio njia ya kuendesha maisha.
75. Mheshimiwa Spika, Masuala ya Kijinsia yanachukua nafasi yake katika mipango ya maendeleo nchini. Kamati imeundwa ya kushughulikia vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar na inasimamiwa na Kamishna wa Polisi Zanzibar akishirikiana na Wizara ya Ustawi wa jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto. Aidha, Mpango Mkakati wa kupiga vita udhalilishaji wa kijinsia na Sera ya Uadilifu wa kijinsia zipo katika hatua za mwisho kukamilika.
76. Mheshimiwa Spika, Kuhusu mapambano dhidi ya ukimwi, Serikali inaendelea na utayarishaji wa Mkakati wa Pili wa Kupambana na UKIMWI ambao unajumuisha mashauriano ya kina kwa makundi mbalimbali katika jamii. Mkakati huo umejikita zaidi kutoa kipaumbele kwa makundi hatarishi kama vile wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono, watumiaji wa dawa za kulevya na watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja..
77. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2010/2011 katika juhudi za kutoa elimu ya UKIMWI kwa jamii, Serikali kwa kutumia vyombo vya habari, vipindi mbali mbali vipatavyo 720 vya kuwaelimisha wananchi vimerushwa hewani. Lengo nikuwaelimisha wananchi katika kujikinga na UKIMWI. Vyombo vya habari vilivyotumika kwa kurushia vipindi hivyo ni Sauti ya Tanzania Zanzibar, Micheweni Community Redio, Annur Zenj FM pamoja na Hits FM. Hata hivyo, licha ya juhudi hizo baadhi ya maeneo maambukizi ya UKIMWI yameonekana kuongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma. Hali hii ni hatari na iko haja ya kufanya uchunguzi zaidi ili kuelewa sababu za msingi.
KUIMARISHA MUUNGANO
78. Mheshimiwa Spika, Katika juhudi za kuimarisha Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupitia vikao mbali mbali vya Watendaji, Mawaziri, Vikao vya Waziri Mkuu, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar (zamani Waziri Kiongozi) vinavyoongozwa na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, juhudi mbali mbali zimechukuliwa za kuzipatia ufumbuzi baadhi ya kero za Muungano.
79. Mheshimiwa Spika, Tokea kuanza kwa vikao hivyo mwaka 2006 jumla ya vikao 6 vya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri Kiongozi/Makamu wa Pili wa Rais vimefanyika na jumla ya masuala (Kero) 7 yamepatiwa ufumbuzi. Hata hivyo mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa masuala (Kero) nyengine yanaendelea. Kwa upande wa Tume ya Pamoja ya Fedha, Serikali itaendelea na juhudi za kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa mapendekezo ya juu ya Taarifa ya Tume hiyo yaliyowasilishwa katika Serikali zetu mbili.
80. Mheshimiwa Spika, Katika suala la kuimarisha na kuibua vyanzo vipya vya mapato, Serikali inaendelea na juhudi za maandalizi ya uchimbaji wa mafuta na gesi kwa upande wa Zanzibar. Kufuatia maamuzi yaliyotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hatimae kupitishwa na Baraza lako tukufu juu ya kuliondoa suala la mafuta na gesi asilia katika orodha ya Mambo ya Muungano, Serikali ya awamu ya saba itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ili kulipatia ufumbuzi wa pamoja wa kulitoa suala la mafuta katika orodha ya mambo ya Muungano.
UTEKELEZAJI WA BAJETI 2010/11
Mapato ya Ndani
81. Mheshimiwa Spika, Kufuatia kuimarika kwa uwekezaji nchini, mapato ya Serikali yamekuwa yakiongezeka kutoka TZS 62.4 bilioni mwaka 2005/2006 hadi TZS 149.5 bilioni mwaka 2009/2010. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 139.6 katika kipindi hicho.
82. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha miezi tisa ya awali ya mwaka wa fedha 2010/11, jumla ya mapato yaliokusanywa yalifikia TZS 132.96 bilioni sawa na asilimia 100.9 ya makadirio ya kipindi hicho. Ikilinganishwa na mwaka uliopita (2009/2010) katika kipindi kama hicho, kunajitokeza ukuaji wa mapato kwa asilimia 16.7. Kati ya makusanyo hayo jumla ya TZS 126.10 bilioni zilitokana na mapato ya kodi ambazo ni sawa na asilimia 89.1 ya makadirio (sawa na ukuaji wa asilimia 16.8 kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2009/2010). Mapato yasiyokuwa ya kodi yalifikia TZS 6.86 bilioni sawa na asilimia 87 ya makusanyo ya kipindi hicho.
83. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa ukusanyaji wa mapato kitaasisi, katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka 2010/11, Mamlaka ya Mapato Tanzania imekusanya jumla ya TZS 55.73 bilioni sawa na asilimia 108 ya makadirio ya kipindi hicho. Ukuaji huo ni asilimia 27.2 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita. Bodi ya Mapato ya Zanzibar kwa kipindi cha Julai – Machi 2010/2011 nayo imekusanya jumla ya TZS 77.23 bilioni sawa na asilimia 96.3 ya makadirio ya miezi tisa, sawa na ukuaji wa asilimia 10.14 kwa mwaka uliopita katika kipindi kama hicho.
84. Mheshimiwa Spika, Mapato yasiyokuwa ya kodi kutoka katika Wizara za Serikali yameendelea kuwa madogo, jumla ya TZS 6.88 bilioni zilikusanywa ambazo ni sawa na asilimia 87 ya makadirio ya miezi tisa ya awali. Hali hii imetokana zaidi na viwango vya kutozea ada kuwa vidogo pamoja na baadhi ya sheria zetu kutoa mwanya kwa Waziri wa sekta kusamehe kodi. Serikali katika juhudi zake za kuongeza mapato hasa yale ya mawizara yakiwemo ya ardhí inaandaa utaratibu wa kurekebisha kasoro hizo.
Mapato ya Nje
85. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2010/2011, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepokea Misaada ya Kibajeti (4.5%) yenye thamani ya TZS 33.89 bilioni hadi Machi 2011 ambazo ni sawa na asilimia 60 ya makadirio ya mwaka wa fedha 2010/2011, ya TZS 55.24 bilioni. Aidha Ruzuku na Mikopo iliyopokelewa kwa ajili ya Miradi na Programu za Maendeleo imefikia TZS 117.72 bilioni sawa na asilimia 56 ya matarajio ya mwaka ya TZS 211.71 bilioni. Hali hii inatufanya tuongeze nguvu zaidi katika kujitegemea kimapato hasa kwa kuangalia fursa zilizopo.
MATUMIZI
86. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa matumizi ya Serikali ni dhahiri yatakuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka. Katika kipindi cha tathmini (Julai 2010 hadi Machi 2011), matumizi halisi ya Serikali yalifikia TZS 256.48 bilioni sawa na asilimia 76.9 ya makadirio ya kipindi hicho. Matumizi kwa ajili ya kazi za kawaida yalifikia TZS 138.76 bilioni sawa na asilimia 95.7 ya makadirio, wakati yale ya kazi za maendeleo yalifikia TZS 142.23 bilioni sawa na asilimia 75.5 ya makadirio ya kipindi hicho. Kati ya matumizi hayo ya kazi za maendeleo, TZS 24.51 bilioni zilikuwa ni fedha za ndani na TZS 117.72 bilioni ni fedha za kigeni kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
87. Mheshimiwa Spika, Napenda kuliarifu Baraza lako tukufu kuwa, muundo mpya wa kiwizara ulioanza mwezi wa Januari 2011 baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, hakukubadilisha kiwango cha bajeti ya Serikali iliyokadiriwa kwa mwaka 2010/2012. Wizara pamoja na Idara mpya zilizojichomoza ziligawiwa sehemu ya bajeti kutoka katika bajeti iliyopitishwa na Baraza lako tukufu.
Matumizi ya Kazi za Kawaida 2010/2011
88. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha miezi tisa cha mwaka 2010/2011, matumizi ya kazi za kawaida yalifikia TZS 138.76 bilioni. Matumizi hayo ni sawa na asilimia 95.7 ya makadirio. Ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita, matumizi ya kazi za kawaida yameongezeka kwa TZS 23.9 bilioni sawa na asilimia 20.8 ambapo jumla ya TZS 114.83 bilioni zilitumika. Kati ya matumizi hayo ya kazi za kawaida, TZS 62.86 bilioni zilitumika kwa ajili ya mishahara, TZS 56.79 bilioni ni matumizi mengineyo na TZS 19.11 bilioni ni ruzuku kwa taasisi mbali mbali za Serikali.
Mishahara
89. Mheshimiwa Spika, TZS 62.86 bilioni zilitumika kwa ajili ya kulipia mishahara kwa watumishi wa Serikali katika kipindi cha miezi tisa, sawa na asilimia 101.6 ya makadirio ya kipindi hicho na ni asilimia 45.3 ya matumizi yote ya kazi za kawaida. Aidha, matumizi hayo ya mshahara ni sawa na asilimia 47.3 ya makusanyo ya ndani.
Ruzuku
90. Mheshimiwa Spika, Uchambuzi wa matumizi unaonesha kwamba katika miezi tisa ya mwaka 2010/11 Serikali imetumia TZS 19.11 bilioni ikiwa ni ruzuku kwa Taasisi mbali mbali za Serikali. Matumizi hayo ni sawa na asilimia 94.9 ya makadirio ya kipindi hicho. Kwa kulinganisha na matumizi halisi katika kipindi kama hicho mwaka 2009/10, kiasi hicho cha ruzuku kinaonesha ukuaji wa asilimia 23.1. Kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha ruzuku, Serikali inajipanga kuzifanyia mapitio taasisi zote zinazopata ruzuku, lengo ni kuzijengea uwezo, ili baadae ziweze kujitegemea zaidi na hatimae kupunguwa kwa kiwango cha ruzuku kinachokwenda katika taasisi hizo.
Mfuko Mkuu wa Serikali na Mengineyo
91. Mheshimiwa Spika, Matumizi katika Mfuko Mkuu wa Serikali katika kipindi cha miezi tisa ya mwaka wa fedha 2010/11 yalifikia TZS 26.97 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 79.9 ya makadirio ya kipindi hicho. Matumizi mengineyo yaliyotumika kuendesha shughuli mbali mbali za Serikali yalifikia TZS 29.82 bilioni katika kipindi cha tathmini ambayo ni sawa na asilimia 48.1 ya makadirio katika kipindi hicho. Ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2009/2010 matumizi yameongezeka kwa TZS 4.23 bilioni sawa na asilimia 14 ambapo TZS 25.59 bilioni zilitumika katika kipindi kama hicho.
DENI LA TAIFA
92. Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi Machi ya mwaka wa fedha 2010/2011 malipo ya marejesho ya mikopo ya ndani yalifikia TZS 1.76 bilioni sawa na asilimia 29.3 ya makadirio katika kipindi hicho. Ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2009/2010 marejesho hayo yalifikia TZS 1.99 bilioni sawa na asilimia 55.5 ya makadirio. Kupungua kwa malipo hayo kwa mwaka 2010/2011 kumesababishwa na kuwa marejesho mengi yalitarajiwa kufanyika katika robo ya mwisho ya mwaka huu wa fedha.
93. Mheshimiwa Spika, Malipo ya riba ya madeni ya ndani kwa mwaka wa fedha 2010/2011 hadi kufikia Machi 2011 yalikuwa TZS 1.18 bilioni sawa na asilimia 84.4 ya makadirio kwa kipindi hicho ikilinganishwa na mwaka 2009/2010, hadi kufikia Machi 2010 malipo yalikuwa TZS 1.27 bilioni sawa na asilimia 95.5 ya makadirio ya kipindi hicho.
94. Mheshimiwa Spika, Malipo hayo ya riba kwa mwaka 2010/2011 yamepungua kwa TZS 0.09 bilioni au asilimia 7.6 ikilinganishwa na mwaka 2009/2010.
MALIPO YA KIINUA MGONGO
95. Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua juhudi za kuhakikisha kuwa wastaafu wanalipwa haki zao kwa wakati. Katika kipindi cha Julai 2010 hadi Machi 2011, jumla ya wastaafu 748 kati ya wastaafu 1,045 Unguja na Pemba waliripotiwa kulipwa haki zao. Jumla ya TZS 5.18 bilioni zimetumika kwa kuwalipa wastaafu hao kiinua mgongo.
Utekelezaji wa Hatua za Kuimarisha Mapato
96. Mheshimiwa Spika, Katika utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2010/2011, Serikali ilichukua hatua maalum ya kupunguza misamaha ya kodi, ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti wa kuangalia mianya iliyopo na kufuatilia kwa karibu na kufanya uchambuzi wa kina juu ya maombi ya misamaha. Hatua hizo zimeonesha matunda mazuri, kwani misamaha ya kodi imepungua kutoka TZS 21.02 bilioni mwaka 2009/2010 na kufikia TZS 14.76 bilioni mwaka 2010/2011 sawa na ushukaji wa asilimia 29.8. Serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali kwa nia ya kuimarisha mapato ya Serikali.
UTAYARISHAJI WA MKAKATI WA KUKUZA UCHUMI NA KUPUNGUZA UMASIKINI ZANZIBAR (MKUZA II) NA MAPITIO YA DIRA 2020
97. Mheshimiwa Spika, Kufuatia kukamilika utekelezaji wa MKUZA awamu ya kwanza, Serikali imekamilisha utayarishaji wa awamu ya pili ya MKUZA. Mwelekeo wa MKUZA awamu ya pili ni kama ifuatavyo:
i) Kuendelea kuwa na Klasta tatu; Klasta ya Kwanza ni Ukuzaji Uchumi na Kupunguza Umaskini wa Kipato yenye malengo manne; Klasta ya pili ni Huduma za Jamii na Ustawi yenye malengo saba; na Klasta ya tatu ni Utawala Bora na Umoja wa Kitaifa yenye malengo matatu.
ii) Katika kuendeleza Sekta Binafsi nchini, lengo maalum limewekwa katika Klasta ya kwanza.
iii) Klasta ya pili kuendelea kubeba malengo mengi zaidi.
iv) Utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanzibar unaendelea kuwa na umuhimu katika MKUZA II.
v) Mashirikiano ya Sekta za Umma na za Binafsi yamepewa msisitizo zaidi kwa dhamira ya kuleta ufanisi.
vi) Mageuzi ya Msingi (Core Reform) yanahitaji kuendelezwa kwa kasi zaidi. Ufuatiliaji na tathmini utaimarishwa zaidi kutokana na uzoefu uliopatikana baada ya mapitio ya MKUZA I.
98. Mheshimiwa Spika, Kama nilivyoeleza hapo kabla, kufuatia kufikia nusu ya kipindi cha utekelezaji, Serikali imefanya mapitio ya Dira 2020 na sasa iko katika hatua za kukamilisha taarifa ya mapitio hayo. Mategemeo ni kuwa mapendekezo ya taarifa hiyo yatasaidia kuimarisha mikakati yetu ya kujiletea maendeleo nchini kwa kipindi kilichobakia ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020.
MWELEKEO WA HALI YA UCHUMI, MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI MWAKA 2011/12
Mwelekeo wa Hali ya Uchumi
99. Mheshimiwa Spika, Uchumi wa dunia unaendelea kukua lakini kwa kasi ndogo, hali hii imetokana na msukosuko wa uchumi na fedha ulioikumba dunia katika miaka miwili ya 2008 na 2009 iliyopita. Uchumi wa dunia unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 4.4 kwa mwaka 2011. Ukuaji wa uchumi kwa nchi zilizoendelea unatarajiwa kufikia asilimia 2.5 wakati nchi zinazoendelea na zilizo chini kiuchumi zinatarajiwa kukua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 6.5 kwa mwaka 2011. Vile vile, nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara zinaendelea kurejea katika hali ya kawaida kutoka katika msukosuko wa kiuchumi na fedha, huku kukiwa na matarajio ya ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.5 kwa mwaka 2011. Taarifa hizi ni kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Uchumi wa Dunia ya Shirika la Fedha Duniani.
100. Mheshimiwa Spika, Athari ya kushuka kwa biashara katika soko la dunia na kupanda kwa kiwango cha ukosefu wa ajira ni changamoto kubwa kwa nchi mbali mbali duniani. Ukuaji wa biashara kati ya nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara na nchi za Asia umechukua nafasi kubwa ya kurudisha hali ya uzalishaji na ukuaji wa uchumi katika nchi hizi, ingawa tatizo la ajira litaendelea kudumu kwa kipindi kifupi kijacho.
101. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2011 mfumko wa bei duniani unatarajiwa kupanda hadi kufikia wastani wa asilimia 2.0. Bei za bidhaa mbali mbali zikiwemo za chakula na mafuta zimeonekana kuongezeka kuanzia mwishoni mwa mwaka 2010. Hali hii inatarajiwa kuendelea kwa mwaka 2011 kutokana na kasi ya ukuaji wa mahitaji na kupungua kwa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa kuliko mahitaji ya soko. Matatizo ya kijamii na kisiasa yanayoendelea katika nchi kadhaa za Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati, ambazo ndio wazalishaji wakubwa wa mafuta nayo yanachangia katika utete wa bei ya mafuta duniani.
102. Mheshimiwa Spika, Robo ya mwanzo ya mwaka 2011, bei za mafuta zimepanda kufikia wastani wa Dola 90 za Kimarekani kwa pipa ikilinganishwa na Dola 79 kwa pipa iliofikiwa mwezi wa Oktoba mwaka 2010. Bei hizo zinaonekana pia kusababisha kuongezeka kwa bei ya bidhaa mbali mbali duniani kwa asilimia 12 kwa mwaka 2011. Bei za mafuta zinatarajiwa kuongezeka zaidi hadi kufikia Dola 100 kwa pipa kwa mwaka 2012. Aidha, dalili za kuongezeka kwa madeni na kupanda kwa bei za rasilimali zimeanza kujitokeza katika nchi mbali mbali duniani.
103. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Zanzibar, mwaka 2011/12, mwelekeo wa hali ya uchumi unategemea zaidi utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUZA II), Malengo ya Milenia ya mwaka 2015, Mageuzi ya Msingi pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2010.
104. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2011/12, Pato la Taifa linatarajiwa kukua kwa kasi zaidi kutoka ukuaji wa asilimia 6.5 hadi kufikia asilimia 7.9. Kutokana na athari za mabadiliko ya bei za chakula na mafuta ya nishati duniani, kasi ya Mfumko wa bei inatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 6.1 mwaka 2010 hadi asilimia 7. Serikali inaendelea kuchukua juhudi za makusudi za kuongeza uzalishaji wa chakula na hasa zao la mpunga wa kumwagilia maji, ili kupunguza kiwango cha uagiziaji wa bidhaa hiyo kutoka nje. Aidha, matarajio ya kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa yanatokana na mategemeo ya matokeo ya kuimarika kwa miundombinu ya kiuchumi kama vile uwanja wa ndege, barabara, umeme na mfumo wa umwagiliaji maji pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji. Juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani zinatarajiwa kuongeza kigavi cha mapato ya ndani kwa Pato la Taifa na kufikia asilimia 20.2 kutoka asilimia 18 ya mwaka 2010/11.
105. Mheshimiwa Spika, Serikali imeazimia kujenga mazingira ya kiuchumi ambayo yatawezesha maeneo yafuatayo:
• Kuimarika kwa rasilimali watu, kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi na kuinua kiwango cha sayansi, teknolojia na mafunzo ya vitendo.
• Kuimarisha kwa sekta ya fedha kwa lengo la kuchangia na kujenga ukuaji uchumi ambao utategemea utekelezaji wa awamu ya pili ya Mageuzi ya Sekta ya Fedha.
• Kutekeleza Mkakati wa Usafirishaji wa Bidhaa nje ya nchi.
• Kuimarika kwa miundombinu ya kiuchumi na
• Sera za kodi na fedha ambazo zitatekeleza mageuzi ya mfumo wa kodi katika sekta mbali mbali.
MWELEKEO WA MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI KWA MWAKA 2011/12
106. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2011/12, Serikali inataraji kutekeleza jumla ya programu 27 (kati ya hizo saba ni mpya) na miradi ya maendeleo 77 (kati yake 11 ni mipya) yenye gharama ya jumla ya TZS 378.90 bilioni. Kati ya fedha hizi, Serikali itatoa TZS 37.95 bilioni sawa na asilimia 10 na Washirika wa Maendeleo watachangia TZS 340.96 bilioni sawa na asilimia 90. Kati ya fedha hizo za washirika wa maendeleo ruzuku ni TZS 124.96 bilioni na mikopo ni TZS 216 bilioni.
107. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa matumizi kwa kila klasta ni kama ifuatavyo: Klasta ya Ukuzaji wa Uchumi na Upunguzaji wa Umasikini inatarajiwa kutekeleza jumla ya programu 17 (kati yake tano ni mpya) na miradi 17 (mmoja ni mpya) katika mwaka 2011/2012 kwa gharama ya TZS 183.23 bilioni. Kati ya hizo Serikali itatoa TZS 15.76 bilioni sawa na asilimia 8.6 na Washirika wa Maendeleo watachangia TZS 167.48 bilioni sawa na asilimia 91.4.108. Mheshimiwa Spika, Klasta ya Uimarishaji wa Huduma za Jamii, inatarajiwa kutekeleza jumla ya programu sita (kati yake moja ni mpya) na miradi 33 (kati yake mitano ni mipya) katika mwaka 2011/2012 kwa gharama ya TZS 151.52 bilioni. Kati ya hizo Serikali itatoa TZS 12.89 bilioni sawa na asilimia 8.5 na Washirika wa Maendeleo TZS 138.63 bilioni sawa na asilimia 91.5.109. Mheshimiwa Spika, Klasta ya Utawala Bora na Umoja wa Kitaifa inatarajiwa kutekeleza jumla ya programu 4 (moja mpya) na miradi 27 (kati yake mitano mipya) katika mwaka 2011/2012, kwa gharama ya TZS 44.15 bilioni. Kati ya fedha hizo, Serikali itatoa TZS 9.30 bilioni sawa na asilimia 21.0 na Washirika wa Maendeleo watachangia TZS 34.85 bilioni sawa na asilimia 79.0.110. Mheshimiwa Spika, Maeneo makubwa ambayo programu na miradi hiyo itashughulikiwa ni kama ifuatavyo:
KUIMARISHA SEKTA YA UMMA
111. Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuimarisha utendaji wa sekta ya umma ili kuongeza ufanisi wa kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi. Ili kutimiza dhamira hiyo, Serikali itatekeleza Programu ya Mageuzi ya Sekta ya Umma itayohusisha maeneo ya kuimarisha miundo ya taasisi, watumishi, uwekaji wa kumbumbu na Mageuzi ya Serikali za Mitaa.
112. Mheshimiwa Spika, Kuhusu Marekebisho ya mfumo wa Serikali za Mitaa, dhamira ya Serikali ni kupeleka madaraka na huduma karibu zaidi na wananchi. Lengo ni kuharakisha ustawi wa maisha kwa kuzingatia masuala muhimu kwenye maeneo. Juhudi hizi zinakwenda sambamba na misingi ya kuimarisha Demokrasia na kujali vipaumbele na rasilimali zilizomo ndani ya maeneo ya wananchi.
113. Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2011/12, Sheria ya Mamlaka ya Utawala wa Mikoa itapitiwa na kufanyiwa marekebisho. Maeneo mengine yatakayofanyiwa kazi ni pamoja na haya yafuatayo:
a) Kufanya mapitio katika muundo wa kitaasisi;
b) Kufanya mapitio ya Sheria Nam. 3 na 4 ya mwaka 1995 za Serikali za Mitaa;
c) Muundo wa Utumishi na;
d) Kujenga uwezo wa rasilimaliwatu pamoja na fedha.
114. Mheshimiwa Spika, Sambamba na marekebisho hayo ya kisheria na kitaasisi, Serikali pia inatarajia kuchukua hatua maalum za kujenga uwezo wa Baraza la Manispaa na Halmashauri za miji ya Mkoani, Chake Chake na Wete Pemba ili kuiwezesha kutoa huduma bora zaidi na kuimarisha usafi wa mazingira ya makaazi katika miji hiyo. Kazi hii itafanyika kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Huduma za Mijini (Zanzibar Urban Service Programme – ZUSP) utakaogharimu jumla ya Dola za Kimarekani 38 milioni sawa na TZS 58.0 bilioni. Kati ya fedha hizo, jumla ya Dola za Kimarekani 31.2 milioni zitatumika kwa ajili ya Manispaa ya Unguja, Dola za Kimarekani 3.8 milioni kwa miji mitatu ya Pemba na Dola za Kimarekani 3.0 milioni kwa kazi za kiutawala. Aidha, mradi huo unalenga kutekeleza mambo makubwa yafuatayo:
i) Ukarabati na Ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua katika maeneo ya Manispaa ya Unguja yenye jumla ya urefu wa Kilomita 19.6. Maeneo yatakayonufaika na mradi huu ni ziwa la Sebleni, ziwa la kwa Mtumwa Jeni, ziwa la Binti Amrani, ziwa la Mwantenga, Kwamtipura, Kilima hewa, Karakana, Sogea, Mpendae, Jang’ombe (Botanical garden), Uwanja wa demokrasia na Shauri moyo.
ii) Uimarishaji wa huduma za ukusanyaji wa taka mjini kwa kupatiwa magari tisa, vikapu vya taka (skip) 193 na ndoo za taka (dust bin).
iii) Ukarabati na uwekaji wa taa za barabarani katika njia kuu za mjini kama ya Ikulu hadi uwanja wa ndege, Kiembesamaki hadi Amani, Amani hadi Mwembeladu, Magomeni hadi Kariakoo, Kinazini hadi Magereza, Creek road Kinazini hadi Bububu, katika maeneo ya Mji Mkongwe ikiwemo Kiponda, Vuga, Malindi na Shangani n.k.
iv) Kulipa uwezo Baraza la Manispaa katika mbinu za kukuza mapato, mafunzo ya wafanyakazi na utoaji wa huduma bora (ZMC Institutional Strengthening)
v) Ujenzi na utanuzi wa ukuta wa Forodhani ili kuweza kutumika kwa waendao kwa miguu kutoka Msikiti wa Ijumaa Malindi hadi Bustani ya Forodhani wenye urefu wa mita 340.
vi) Kuinua uwezo wa Mabaraza ya Miji mitatu ya Pemba (Institutional Strengthening) yaani Mkoani, Wete na Chake Chake.
vii) Kutekeleza miradi midogo midogo ya ujenzi ikiwemo ununuzi wa magari kwa ajili ya huduma.
115. Mheshimiwa Spika, Kwa dhamira hiyo hiyo ya kuimarisha ufanisi Serikalini, Serikali inakusudia kutekeleza Mradi wa Mfumo wa kompyuta Serikalini (e-government) unaotarajiwa kugharimu TZS 30 bilioni kupitia mkopo nafuu kutoka Serikali ya Watu wa China. Utakapokamilika, Mradi huu utarahisisha sana mawasiliano Serikalini na kupunguza gharama za mawasiliano. Aidha, inatazamiwa kwamba Mradi utakuwa chanzo kipya cha mapato ya Serikali kutokana na mauzo ya uwezo wa ziada kwa makampuni ya simu nchini.
UWEZESHAJI WA WANANCHI KIUCHUMI
116. Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya saba imetoa msisitizo maalumu katika kuwawezesha wananchi kiuchumi. Haya yamedhihirishwa na kauli mbali mbali za Mheshimiwa Rais, Dr Ali Mohamed Shein, kama vile katika uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi na katika kilele cha maadhimisho ya Sherehe za miaka 47 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar. Nia hii ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inaendana na Dira ya Maendeleo ya 2020 na MKUZA II. Programu mpya ya kuimarisha Miundombinu ya Soko, Kuongeza Thamani na Misaada Vijijini itatekelezwa katika mwaka 2011/12. Programu nyengine zitakazotekelezwa ni utafiti wa kilimo na mali asili, Programu ya umwagiliaji maji na Programu ya kuendeleza miundombinu ya ufugaji. Programu hizi zitatekelezwa kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi.
117. Mheshimiwa Spika, Utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa wananchi utaendelezwa. Mifuko mbalimbali iliyopo itafanyiwa mapitio kwa nia ya kuiimarisha ili lengo la kuanzishwa kwake liweze kufikiwa kwa ufanisi zaidi. Aidha maeneo mapya ya ukopaji yataanzishwa na kuhakikisha kuwepo kwa taratibu za mikopo zinazokuwa bora zaidi, mikopo inatolewa kwa wakati na kuimarisha huduma kwa wakopaji.
UJENZI WA RASLIMALI WATU
118. Mheshimiwa Spika, Maendeleo ya nchi yoyote yanategemea sana uwezo wa watu wake kielimu hususan wanaofanya kazi. Serikali inakusudia kuendelea kuimarisha utaalamu nchini kwa lengo la kuimarisha tija katika shughuli za kiuchumi na za uzalishaji. Programu na miradi mbali mbali ya elimu itatekelezwa ikiwemo Mradi wa Upanuzi na Uimarishaji wa Huduma za Maktaba, Mradi wa Uimarishaji wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), na Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Msingi. Miradi mingine ni pamoja na wa Chuo cha Kiislamu Micheweni Pemba, Mradi wa Uimarishaji wa Elimu Mbadala na Mali, Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Lazima, Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Ufundi na Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Maandalizi.
119. Mheshimiwa Spika, Ili kufanikisha suala la ubunifu kwa vijana, Serikali inakusudia kukamilisha ujenzi wa madarasa manne mapya katika Skuli ya Sekondari ya Ufundi Kengeja pamoja na kuipatia vifaa mbali mbali, kuendelea na ukarabati wa Taasisi ya Sayansi na Teklonojia ya Karume na kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Elimu Mbadala huko Wingwi Mtemani Pemba ikiwa ni pamoja na kukipatia samani na vifaa vya kufundishia. Vile vile, Serikali itatoa mikopo kwa vikundi vya ushirika vya wanawake na kwa wahitimu kutoka vituo vya Mafunzo ya Amali ili waweze kujiajiri na kuendeleza fani walizosomea. Hii itasaidia sana kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
120. Mheshimiwa Spika, Mkazo pia utaendelea kuwekwa katika kuimarisha elimu ya juu ili nchi iwe na wataalamu wa kutosha na kupunguza kutegemea utaalamu kutoka nje ya nchi. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa Tunguu, unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka wa fedha 2011/2012.
KUIMARISHA AFYA ZA WATU
121. Mheshimiwa Spika, Nia ya Serikali ni kuona kuwa Zanzibar inakuwa na watu wenye afya nzuri muda wote. Serikali inachukua jitihada maalum kuhakikisha uhakika wa chakula na lishe nchini. Uzalishaji wa mazao ya kilimo na pato la mkulima ni eneo linalopewa mkazo maalumu kwa kuongezwa huduma za ugani na utafiti, kuimarisha usimamizi wa uzalishaji endelevu wa mazao ya kilimo, kuimarisha matumizi ya mbegu bora na mbolea na pembejeo nyengine za kilimo. Uzalishaji wa Mpunga unaotoa chakula kikuu kwa wananchi wetu unatarajiwa kupata msukumo mpya kufuatia kupatikana mafanikio makubwa katika mbegu mpya ya NERICA ambayo imetoa matumaini mapya kwa wakulima. Serikali itaendeleza juhudi za kuimarisha uzalishaji huo wa mpunga ili hatimae usaidie uanzishwaji wa akiba maalum ya chakula ambayo inatarajiwa kuwa chachu ya kusaidia kupungua kwa mfumko wa bei nchini. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeshaanza kuzalisha kwa wingi mbegu ya NERICA ambayo kuota kwake haihitaji bonde. Vile vile, inaandaa utaratibu wa kulishirikisha Jeshi la Kujenga Uchumi ili nao waweze kuzalisha mbegu ya NERICA. Lengo ni kuisambaza kwa wakulima.
122. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na juhudi zake za kukiendeleza Kituo cha Usarifu wa Mazao ya Kilimo kwa madhumuni ya kutoa mafunzo ya usarifu kwa wananchi wanaojishughulisha na uuzaji wa mazao mbali mbali, ili waweza kuongeza kipato chao na hatimae kuwapunguzia makali ya umasikini, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya usarifu wa mazao ya kilimo Zanzibar.
123. Mheshimiwa Spika, Moja ya eneo lililoonesha changamoto kubwa katika kuhakikisha afya za wananchi ni upatikanaji endelevu wa maji safi na salama. Serikali imeshachukua juhudi mbali mbali za kuimarisha upatikanaji wa huduma hii ya lazima kwa maisha ya mwanaadamu, lakini bado mafanikio yake yamekuwa chini ya matarajio. Sababu zinazojitokeza ni pamoja na kupungua kwa kina cha maji kutokana na ujenzi wa karibu ya vyanzo vya maji unaofanywa na wananchi, kuchakaa kwa mitandao ya mabomba ya maji, na uharibifu wa mara kwa mara wa mitambo ya kusukumia maji kutokana na matatizo ya kukatika kwa umeme. Serikali itaendeleza juhudi zake za kuhakikisha kuwa huduma ya maji ambayo ni muhimu inapatikana kwa uhakika. Tayari Serikali imeshafanya mazungumzo na nchi na wahisani mbali mbali ili waweze kusaidiana na Serikali katika kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la maji. Lengo la Serikali ni kuwa ifikapo mwaka 2015, asilimia 75 ya wananchi wa vijijini na asilimia 85 wa mijini wawe wamepata maji safi na salama.
124. Mheshimiwa Spika, Pamoja na jitihada zote zinazoweza kuchukuliwa kuepusha maradhi, licha ya malaria kupungua kwa kiwango kikubwa lakini bado wananchi wataendelea kusumbuliwa na maradhi mbalimbali na hivyo kuna haja ya kuimarisha huduma za afya. Serikali itaendelea kutilia mkazo huduma za kinga na tiba. Serikali pia inakusudia kutekeleza Mkakati wa Afya ya Jamii. Aidha, mpango mzima wa kuifanya hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa hospitali ya rufaa, na kuanzisha mchakato wa kuzipandisha daraja hospitali za Kivunge, Makunduchi, Micheweni na Vitongoji, kuwa za Wilaya na hospitali za Wete na Abdalla Mzee kuwa za mikoa katika mwaka wa fedha 2011/2012 utapewa msukumo mkubwa.
125. Mheshimiwa Spika, Kwa upande mwengine, takwimu zinaonesha kuwa bado vifo vya mama na mtoto vimeendelea kuwa changamoto hapa nchini. Ili kurekebisha hali hii, Serikali inakusudia kuimarisha huduma za chanjo kwa mama na watoto katika vituo vyote vya huduma za mama na watoto nchini. Juhudi zinazoendelezwa za kusogeza huduma za uzazi salama karibu na wananchi nazo kwa kiwango kikubwa zinatarajiwa kupunguza vifo vya mama na watoto. Pamoja na hali ngumu ya maisha nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa dawa muhimu zinapatikana katika hospitali na vituo vya afya wakati wote.
KUUNGANISHA WATU KIJAMII NA KIUCHUMI
126. Mheshimiwa Spika, Maendeleo yanahitaji kuunganishwa kwa sehemu za uzalishaji na masoko na huduma nyengine za jamii. Serikali kwa mwaka 2011/12 itaendeleza uimarishaji wa miundombinu ya mawasiliano kwa njia ya barabara, bandari na viwanja vya ndege. Kwa upande wa barabara, madaraja manne ya barabara ya Mahonda-Donge-Mkokotoni yanatarajiwa kujengwa. Aidha, barabara za Mgagadu-Kiwani, Pale-Kiongele, Amani-Mtoni, Wete-Konde, Wete-Chake, Wete-Gando, Mzambarautakao-Finya, Mzambarauzikaribu-Mapofu, Bahanasa-Daya-Mtambwe, Chwale-Kojani, Kipangani-Kangagani zinatarajiwa kukamilishwa kwa kiwango cha lami. Pia tunataraji kuanza matayarisho ya ujenzi wa barabara Ole-Kengeja. Serikali pia inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bandari mpya ya Mpigaduri.
127. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa usafiri wa anga, ujenzi wa jengo jipya la abiria unaendelea vizuri katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume. Mazungumzo ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa maegesho (apron) na njia ya kupitia ndege (taxiway) yanaendelea. Inatarajiwa pia kuwa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba utapatiwa ufumbuzi hivi karibuni na kazi za ujenzi kuanza mapema iwezekanavyo. Uimarishaji wa njia za mawasiliano una faida kubwa kiuchumi na kijamii, hivyo Serikali itahakikisha kuwa juhudi mbali mbali zinachukuliwa kufanikisha suala la mawasiliano.
UTAFITI NA MAENDELEO
128. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kuelewa umuhimu wa utafiti katika maendeleo imeamua kwa kila Wizara kuanzisha Kitengo cha Utafiti ndani ya Idara za Mipango, Sera na Utafiti. Vitengo hivi vina jukumu la kubainisha na kuratibu masuala ya utafiti pamoja na kuandaa na kusimamia mipango ya utafiti kwa pamoja na kutumia matokeo ya tafiti hizo katika mipango ya maendeleo ya sekta.
129. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais imepewa jukumu maalumu la kuratibu masuala yote ya utafiti nchini. Katika kutimiza azma hiyo, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais imeshafanya mazungumzo na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC) kwa ajili ya COSTEC kufungua ofisi yake Zanzibar na hatua za kuanzisha ofisi hiyo zinaendelea kuchukuliwa.
130. Mheshimiwa Spika, Kwa sasa COSTEC inajitayarisha kufanya warsha maalumu kwa Watendaji Wakuu wa Serikali kuwaelewesha juu ya Sera na Sheria zinazohusiana na mambo ya tafiti za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, kamati zote za COSTEC zitafanyiwa mapitio ili kuwaingiza wataalamu wa Zanzibar katika kamati hizo. Uelewa huu utasaidia Serikali kuanzisha Baraza la Utafiti la Zanzibar ambalo litakuwa na wajumbe kutoka sekta mbali mbali.
MWELEKEO WA BAJETI
Mapato ya Serikali
131. Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 inatarajia kukusanya TZS 613.08 bilioni ikilinganishwa TZS 444.64 bilioni mwaka 2010/2011 ikiwa ni ziada ya TZS 168.44 bilioni sawa na asilimia 38. Hali hii inatokana na kuimarika kwa makusanyo ya ndani na kuongezeka kwa misaada ya Washirika wa Maendeleo.
Mapato ya Ndani
132. Mheshimiwa Spika, Jumla ya TZS 221.24 bilioni zinatarajiwa kukusanywa kutokana na vyanzo vya ndani. TZS 210.22 bilioni zitatokana na makusanyo ya vyanzo vya kodi na TZS 11.02 bilioni kutokana na vyanzo visivyokuwa vya kodi. Mapato ya ndani yanatarajiwa kuongezeka kwa TZS 49.55 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 28.86. Kati ya TZS 210.22 bilioni zitakazotokana na kodi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajiwa kukusanya TZS 100.58 bilioni wakati Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) inatarajiwa kukusanya TZS 120.66 bilioni. Makusanyo hayo ya ndani yanatarijiwa kuwa sawa na asilimia 20.2 ya Pato la Taifa. Ongezeko kubwa la mapato ya TRA linategemea kutekelezwa kwa makubaliano ya kukusanya Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi wa SMT waliopo Zanzibar kulipwa Zanzibar. Aidha Serikali inatarajia kukopa ndani kupitia Hati Fungani yenye thamani ya TZS 15.0 bilioni na mikopo ya kibenki ya TZS 1.6 bilioni. Vile vile, kutakuwa na bakaa ya bajeti kwa mwaka unaomalizika inayokadiriwa kufikia TZS 4.0 bilioni.
HATUA ZA KUIMARISHA MAPATO
133. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2011/12, Serikali haikusudii kupandisha kodi yoyote. Serikali imekusudia kuimarisha zaidi usimamizi na ukusanyaji wa mapato kwa vianzio vilivyopo na kuziba mianya inayotumika katika kuepuka, kupunguza au kukwepa kulipa kodi pamoja na kuendelea kufuatilia matumizi mabaya ya misamaha ya kodi nchini. Lengo ni kuona kuwa kabla ya kuongeza kodi, juhudi zinachukuliwa kwanza katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na uwajibikaji wa ulipaji kwenye vianzio vilivyopo na kuhakikisha kuwa misamaha inayotolewa inatumika kwa dhamira iliyokusudiwa.
134. Mheshimiwa Spika, Katika juhudi nyengine za kuongeza na kuimarisha mapato, Serikali katika mwaka ujao itaanza kupokea marejesho ya kodi ya mapato ya mtu binafsi kwa wafanyakazi wa taasisi za muungano wanaofanyakazi Zanzibar. Hatua hii imekuja kufuatia makubaliano yaliofikiwa kati ya SMZ na SMT katika juhudi za kushughulikia Kero za Muungano.
Mapato ya Nje
135. Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kupata Misaada ya Kibajeti (GBS) yenye jumla ya TZS 30.28 bilioni ikiwa ni asilimia 4.5 ya misaada ya kibajeti kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Ruzuku na Mikopo kwa ajili ya Miradi na Programu mbali mbali inatarajiwa kufikia TZS 340.96 bilioni. Kati ya fedha hizo, TZS 124.95 bilioni ni ruzuku na TZS 216.0 bilioni ni mikopo. Misaada ya Kibajeti ambayo ni ruzuku kupitia GBS na programu/miradi inawakilisha utegemezi wa bajeti kwa asilimia 24 kwa mwaka 2011/12 ikilinganishwa na asilimia 26 kwa mwaka 2010/11. Hali hii inatokana zaidi na juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo vyetu vya mapato ya ndani.
Maeneo ya Kipaumbele
136. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2011/12, maeneo ya kipaumbele yatajikita katika kutekeleza Mkakati wa muda wa kati (MKUZA) unaolenga ukuaji wa haraka ambao utahakikisha maendeleo ya wananchi na ukuaji wa uchumi ulio endelevu pamoja na huduma bora kwa ustawi wa jamii. Kulingana na malengo ya mkakati huo maeneo yafuatayo yatapewa kipaumbele:
i) Kuimarisha huduma za afya, msisitizo zaidi ukilenga katika ununuzi wa vifaa vya hospitali, dawa muhimu pamoja na kuimarisha huduma zinazotolewa na vituo vya afya vya wilaya/mikoa.
ii) Kuimarisha ubora wa elimu kwa kupunguza tatizo la uhaba wa madawati vifaa vya maabara, vifaa vya kufundishia na kumaliza ujenzi wa madarasa yaliyoanzishwa na wananchi katika maeneo yao.
iii) Kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama.
iv) Kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuendeleza shughuli za umwagiliaji, mbegu bora, mbolea na matumizi ya matrekta pamoja na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi ya barabara na umeme katika maeneo ya kilimo.
v) Kuanza kuweka mazingira bora ya uwezeshaji wananchi kiuchumi
vi) Kuendeleza tafiti mbali mbali kwa lengo la kuimarisha uzalishaji na utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo.
MATUMIZI
137. Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kutumia TZS 613.08 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Matumizi ya Kazi za Kawaida
138. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2011/2012, matumizi ya kazi za kawaida yanatazamiwa kuwa ni TZS 234.18 bilioni. Kwa kuwa Serikali imepanga kuongeza mishahara kwa watumishi wake, hivyo mishahara na posho kwa Wizara na Idara za Serikali pamoja na taasisi zinazopokea ruzuku itakuwa ni TZS 126.34 bilioni sawa na asilimia 53.9 ya matumizi yote ya kazi za kawaida ambayo ni asilimia 57.1 ya matarajio ya makusanyo ya mapato ya ndani. Aidha, kiwango hicho cha mishahara ni sawa na asilimia 11.5 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 9.9 kwa mwaka wa fedha 2010/2011. Serikali pia imepanga kutumia TZS 47.75 bilioni sawa na asilimia 20.3 ya matumizi ya kawaida kwa ajili ya Mfuko Mkuu. Matumizi mengineyo kwa Wizara na Idara za Serikali ni TZS 48.17 bilioni sawa na asilimia 20.1. Aidha, matumizi kwa ajili ya ruzuku kwa taasisi mbali mbali zinazojitegemea ni TZS 13.05 bilioni sawa na asilimia 5.6 ya matumizi yote ya kazi za kawaida. Serikali imechukua juhudi za kuongeza mishahara kwa watumishi wake, ili na wao waongeze tija katika utekelezaji wa majukumu yao.
Matumizi ya Kazi za Maendeleo
139. Mheshimiwa Spika, Fedha kutoka nje kwa ajili ya utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2011/2012 zinatarajiwa kufikia TZS 340.96 bilioni. Fedha za ndani zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya matumizi ya kazi za maendeleo zinatarajiwa kufikia jumla ya TZS 37.95 bilioni. Fedha hizo zinatarajiwa kutumika kwa miradi ambayo Washirika wa Maendeleo wanaiunga mkono na ile ambayo inategemea fedha za ndani pekee. Aidha kipaumbele kitawekwa kwa miradi yenye kuhitaji fedha za Serikali kutokana na kuchangiwa na Washirika wa Maendeleo.
140. Mheshimiwa Spika, Matumizi kutokana na mikopo na ruzuku kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kwa ajili ya programu na miradi ya maendeleo ni TZS 340.96 bilioni. Mgawanyo huu unategemea kiwango cha upatikanaji halisi wa ruzuku na mikopo katika mwaka ujao wa fedha. Jitihada zaidi za ufuatiliaji zitachukuliwa ili fedha zilizopangwa zipatikane kwa ukamilifu kwa faida ya wananchi na nchi yetu.
DENI LA TAIFA
141. Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi wa Machi 2011, deni la Taifa lilifikia TZS 144.79 bilioni sawa na asilimia 19 ya Pato la Taifa. Deni hilo ni sawa asilimia 84.3 ya mapato ya ndani na asilimia 74.8 ya matumizi ya kazi za kawaida kwa 2011/12. Kati ya deni hilo, jumla ya TZS 41.49 bilioni ni deni la ndani wakati deni la nje lilifikia TZS 103.30 bilioni. Kati ya deni lote, jumla ya TZS 93.50 bilioni sawa na asilimia 64.6 linadhaminiwa na Serikali ya Muungano na deni lililobakia linalipwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar moja kwa moja.
142. Mheshimiwa Spika, Ulipaji wa riba kutokana na deni la Taifa unatarajiwa kuwa TZS 2.93 bilioni kwa 2011/12. Kiwango hicho ni pungufu kwa TZS 0.07 bilioni ikilinganishwa na makadirio ya TZS 3.0 bilioni kwa mwaka 2010/11. Uwiano wa malipo ya riba za ndani na pato la ndani ni asilimia 1.3. Ukuaji wa malipo ya madeni katika mpango wa kati unatokana na kupevuka kwa hati fungani za muda mfupi na mrefu. Hata hivyo, uwiano wa deni na Pato la Taifa unaonyesha dhahiri kuwa Zanzibar inakopesheka.
Hatua za Kuimarisha Usimamizi wa Matumizi
143. Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuchukua hatua za kisera katika kusimamia matumizi ya Serikali kama ifuatavyo:
i) Kufuatilia kwa karibu Misaada ya Kibajeti (GBS) inayotarajiwa kwa mwaka ujao wa fedha ili kuepusha athari ya Kibajeti;
ii) Kusisitiza usimamizi wa ukusanyaji wa Mapato ya ndani pamoja na matumizi yake;
iii) Kuimarisha usimamizi wa mikataba baina ya Serikali na sekta binafsi;
iv) Kuimarisha utaratibu wa upatikanaji wa bajeti zenye uhalisia zaidi kutoka katika sekta;
v) Kuweka utaratibu mzuri zaidi wa kulipa mafao ya likizo kwa watumishi wa Serikali.
SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2011/2012
144. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2011/2012, jumla ya mapato yote ya ndani na ya nje yanakadiriwa kufikia TZS 613.08 bilioni. Kati ya fedha hizo, mapato ya ndani yanakadiriwa kufikia TZS 221.24 bilioni, wakati mapato kutokana na misaada (ruzuku na mikopo) ya Washirika wa Maendeleo kwa ajili ya Miradi na Programu za Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2011/12 ni TZS 340.96 bilioni. Aidha misaada ya kibajeti (4.5%) inakadiriwa kufikia TZS 30.28 bilioni. Jumla ya TZS 20.6 bilioni zinatarajiwa kupatikana kupitia mikopo na bakaa iliyoletwa kutoka bajeti itakayomalizika.
145. Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia masuala mbali mbali na changamoto nilizozieleza hapo juu, mapato hayo yanatarajiwa kugawanywa kama ifuatavyo: TZS 234.18 bilioni kutumiwa kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS 378.90 bilioni kwa ajili ya kazi za Maendeleo. Kati ya matumizi ya kawaida, mishahara na posho kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali zinazopokea ruzuku ni TZS 126.34 bilioni sawa na asilimia 53.9 ya matumizi yote ya kazi za kawaida na asilimia 57.1 ya makusanyo ya mapato ya ndani. Matumizi ya Mfuko Mkuu wa Serikali ni TZS 47.62 bilioni sawa na asilimia 20.3 ya matumizi ya kazi za kawaida. Matumizi mengineyo kwa Wizara na Idara za Serikali ni TZS 47.17 bilioni sawa na asilimia 20.8 na matumizi mengineyo kwa ajili ya ruzuku kwa taasisi mbali mbali zinazojitegemea ni TZS 13.05 bilioni sawa na asilimia 5.6 ya matumizi yote ya kazi za kawaida.
146. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa matumizi ya kazi za maendeleo mchango wa Serikali unatarajiwa kufikia jumla ya TZS 37.95 bilioni. Kipaumbele kitawekwa kwa miradi yenye kuhitaji mchango wa Serikali kutokana na kufadhiliwa na Washirika wa Maendeleo. Matumizi ya fedha zinazotegemewa kutoka nje kwa ajili ya Miradi na Programu za Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2011/12 ni TZS 340.96 bilioni. Hivyo jumla ya fedha zote kwa ajili ya kazi za maendeleo zitafikia TZS 378.90 bilioni kutoka TZS 251.20 bilioni mwaka 2010/2011 ikiwa ni ongezeko la TZS 127.70 bilioni sawa na asilimia 50.8. Makadirio hayo ya kazi za maendeleo ni sawa na asilimia 61.8 ya matumizi yote kwa 2011/2012.
147. Mheshimiwa Spika, Baada ya kuwasilisha mwelekeo wa mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2011/12, ufuatao ni muhtasari wa mapendekezo hayo:
Mfumo wa Bajeti ya mwaka 2011/2012
Maelezo Makisio Makisio Ongezeko (%)
2010/11
(TZS Bil.) 2011/12
(TZS Bil.)
Mapato
A. Mapato ya ndani 171.69 221.24 28.9
B. 4.5% Msaada wa kibajeti (GBS) 55.24 30.28 (45.2)
C. Hati fungate ya muda mrefu 3.00 15.00 400.0
D. Mikopo ya Kibenki 3.00 1.60 (46.7)
E. Bakaa iliyoletwa 0 4.00 100.0
F. Mikopo na Ruzuku 211.71 340.96 61.1
Jumla ya Mapato 444.64 613.08 37.9
MATUMIZI
G. Matumizi ya Kawaida 193.43 234.18 21.1
i) Mishahara (Mawizara) 82.46 105.78 28.3
ii) Mishahara (ruzuku) 12.31 20.56 67.0
iii) Matumizi mengineyo (Mawizara) 39.78 47.17 18.6
iv) Matumizi mengineyo (ruzuku) 13.86 13.05 (5.8)
v) Mfuko Mkuu wa Serikali (CFS) 45.00 47.62 5.8
H. MAENDELEO 251.20 378.90 50.8
i) Mchango wa Serikali 39.49 37.95 (3.9)
ii) Washirika wa Maendeleo 211.71 340.96 61.1
Jumla ya Matumizi 444.64 613.08 37.9
Chanzo: Ofisi ya Rais – Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo
SHUKRANI
148. Mheshimiwa Spika, Kwa kumalizia, napenda kuchukua fursa hii kukupongeza kwa kurudi tena katika nafasi ya kuliongoza Baraza hili tukufu katika awamu hii ya saba ya Serikali ya Mfumo wa Kitaifa. Ni matumaini yangu kwamba busara na hekima zako zitaongoza vyema katika majadiliano ya vikao vya Baraza hili tukufu. Aidha, kwa kupitia kwako napenda kumshukuru Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wenyeviti wa Baraza hili tukufu, Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Baraza lako, Waheshimiwa wajumbe wote wa Baraza lako tukufu kwa mashauriano, maoni na miongozo katika mchakato mzima wa maandalizi ya bajeti ninayoiwasilisha mbele ya Baraza lako tukufu. Ni imani yangu kuwa tutaendelea kushirikiana kwa nia ya kuwatumikia wananchi wetu.
149. Mheshimiwa Spika, Maandalizi ya bajeti hii yamehusisha wadau wengi wa ndani na nje ya Serikali. Napenda kuwashukuru wote waliochangia kwa kutoa maoni ambao ni pamoja na Watendaji Wakuu na wafanyakazi wa Wizara mbalimbali, Idara zinazojitegemea, Mikoa, Halmashauri za Wilaya, Manispaa, Asasi zote za Serikali na sekta binafsi. Michango yao ilisaidia kufanikisha utayarishaji wa bajeti hii. Aidha, napenda kuwashukuru watendaji wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha miswada na nyaraka mbali mbali za sheria ambazo ni sehemu ya bajeti hii. Kwa upande wa Ofisi ya Rais – Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, napenda kutoa shukurani za pekee kwa Katibu Mkuu ndugu Khamis Mussa Omar, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bi Amina Khamis Shaaban na Naibu Katibu Mkuu, Ndugu Abdi Khamis Faki. Aidha, napenda kuwashukuru Wakuu wa Idara na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Rais – Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha na hatimae leo hii kuiwasilisha hotuba hii.
150. Mheshimiwa Spika, Napenda kuwashukuru wananchi kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu hapa nchini kwetu hali inayopelekea kutekeleza vyema mipango yetu ya maendeleo. Sasa umefika wakati kwa Wazanzibari kujituma. Amani na utulivu upo hakuna sababu ya kuwa nyuma kimaendeleo, kila mmoja wetu atekeleza wajibu wake na hili linawezeka.
151. Mheshimiwa Spika, Napenda kutumia fursa hii adhimu kuwashukuru kwa dhati kabisa Washirika wetu wa Maendeleo katika kuchangia maendeleo ya nchi na wananchi wetu. Kwa hakika misaada yao imekuwa ni kichocheo kikubwa cha harakati za maendeleo nchini kwetu. Washirika wa Maendeleo waliochangia bajeti ya mwaka 2011/2012 ni Canada, Cuba, Denmark, Finland, India, Ireland, Jamhuri ya Watu wa China, Jamhuri ya Watu wa Korea, Japani, Marekani, Misri, Norway, Oman, Sweden, Ubelgiji, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Uturuki, ACBF, ACCRA, AfDB, AGRA, BADEA, CARE INTERNATIONAL, CDC, CHAI, CIDA, DANIDA, DFID, EGH, EU, EXIM Bank of China, EXIM Bank of Korea, FAO, FHI, GAVI, GEF, GLOBAL FUND, IAEA, ICAP, IDB, IFAD, ILO, IMF, IPEC, JICA, JSDF, KOICA, MCC, NORAD, OPEC, ORIO-Netherlands, PRAP, SAUDI FUND, Save the Children, SIDA, UN AIDS, UN, UNDP, UNESCO, UNFPA, UN-HABITAT, UNICEF, UNIDO, USAID, WB, WHO, WSPA .
HITIMISHO
152. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya 2011/2012 ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kufikia maendeleo ya MKUZA, malengo ya maendeleo ya Milenia, na hatimaye Dira ya Maendeleo 2020. Hata hivyo, ili kufikia malengo yetu mapema zaidi, kila mwananchi anapaswa kuwajibika na kushiriki kikamilifu kwa kutumia fursa zinazojitokeza kwa kuzalisha mali na kujiongezea kipato.
153. Mheshimiwa Spika, Ushiriki katika uzalishaji kwa wananchi mmoja mmoja au vikundi ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu. Aidha, sekta za kilimo, mifugo na viwanda zikiboreshwa na kutiliwa mkazo, usindikaji wa mazao ya kilimo una nafasi kubwa ya kuchangia Pato la Taifa na kukuza ajira. Bajeti hii pia inalenga kuongeza jitihada za Serikali za kuimarisha matumizi bora ya ardhi, miundombinu na mawasiliano.
154. Mheshimiwa Spika, Ili kuimarisha ukuzaji wa uchumi wetu, hatuna budi kufikiria mipango ya muda mrefu ambayo itachochea ari na ushindani katika uzalishaji kwa kutumia rasilimali zetu za ndani ambazo zitapelekea uchumi wa kisasa na tija kwa nchi. Mafanikio katika kukuza na kuendeleza mipango yetu ya kiuchumi hayawezi kupimwa kwa kuangalia upande mmoja, ni lazima miundombinu ya kiuchumi katika sekta mbalimbali iungane. Vile vile, kujituma pamoja na kuwa na maadili mema katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ni muhimu; maadili yanaweza kutokomeza umasikini uliokithiri.
155. Mheshimiwa Spika, Napenda kuchukua fursa hii kumalizia kwa kusisitiza kuwa Bajeti hii inalenga zaidi katika kuimarisha na kuleta maendeleo ya kiuchumi pamoja na maslahi ya wafanyakazi na wananchi kwa jumla. Tumeeleza changamoto zinazotukabili katika vyanzo vyetu vya ukuaji wa uchumi na ukusanyaji wa mapato. Hatuna budi kuwa na mikakati maaalum ya kukabiliana na changamoto hizo. Dhamira ya Serikali ni kujenga uwezo kwa watoto, vijana na wafanyakazi hatimae waweze kujenga uchumi wenye kuendana na ushindani katika dunia. Serikali inalengo la kufikia maendeleo ya kiuchumi ambayo yatazaa tija ya maisha tulivu na maslahi bora kwa wananchi wake. Mpango wetu wa Muda Mrefu ni Dira ya Maendeleo ya Kiuchumi ambao unatoa muongozo wa kuondosha umasikini uliokithiri, makazi bora na usalama wa chakula kwa nia ya kukuza uchumi na ustawi wa jamii. Bajeti yetu hii imeeleza kwa uwazi kuhusu malengo yetu. Mwisho namalizia kwa kusema “Kipimo cha ufanisi wa mtu si wapi amesimama wakati wa faraja, bali wapi amesimama wakati wa changamoto”.
156. Mheshimiwa Spika, Kwa heshima, taadhima na unyenyekevu naomba sasa Baraza lako tukufu lipokee, lijadili na hatimae lipitishe mapendekezo juu ya Mwelekeo wa Uchumi, Mpango wa Maendeleo na Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2011/2012, ili yawe muongozo wa utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa mwaka 2011/2012.
157. Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza mbele ya Baraza lako tukufu kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kukusanya jumla ya shilingi Mia Sita na Kumi na Tatu bilioni, na Sabiini na Sita milioni (TZS 613,076 millioni) pamoja na matumizi ya shilingi bilioni Mia Mbili na Thelathini na Nne, milioni Mia Moja na Sabiini na Tano (234.175 bilioni) kwa kazi za kawaida na shilingi bilioni Mia Tatu Sabiini na Nane, milioni Mia Tisa na Moja (378.901 bilioni) kwa kazi za maendeleo.
158. Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment