MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Maalim Seif Sharif Hamad amewataka Wazanzibari wasomi walio nje ya nchi kuwa wazalendo kwa kurudi kuitumikia nchi yao ili kukuza maendeleo ya kiuchumi.
Alisema Zanzibar imejizatiti na kujipanga kikamilifu katika kuongeza ajira na kuboresha mishahara ya watumishi, pamoja marekebisho ya stahiki kulingana na taaluma zao.
Alitoa rai hiyo mjini Morogoro wakati wa mahafali ya jumuiya ya wanafunzi wa Kizanzibari wanaosoma Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro.
Alisema, Wazanzibari wasomi na wafanyabiashara wakubwa waliopo nje ya nchi wanao wajibu wa kutambua kuwa wanahitajika kujitokeza kutoa mchango wao kwa misingi ya kujali zaidi uzalendo wa nchi yao.
“Ndugu zangu wasomi bila kuwa na uzalendo kwenye nchi yako kwa kurudi kuwatumikia wananchi hamtakuwa mmewatendea haki pindi mtakapoamua kukimbilia kikubwa zaidi nje ya nchi yenu, hamuifanyii haki Serikali yenu,” alisema.
Alisema SMZ imedhamiria kuboresha sekta ya elimu, afya, maji, kilimo na uwezeshaji wananchi kiuchumi hususan vijana.
Aliwashauri Wazanzibari kuwashawishi watoto wao kupenda kusoma masomo ya sayansi kuanzia ngazi ya chini hadi vyuo vikuu, ili waweze kutumika katika ajira zitakazohusu fani hiyo ikiwemo udaktari.
Kwa mujibu wa risala hiyo, kati ya wanafunzi 600 wanaosoma katika Chuo Kikuu hicho, zaidi ya asilimia 40 ni kutoka Visiwani Zanzibar , ambapo kwa Julai mwaka huu wanafunzi 93 wanatarajia kuhitimu masomo yao.
No comments:
Post a Comment