SERIKALI imetangaza rasmi kuwa Katiba mpya itazinduliwa
Aprili 26 mwaka 2014, siku ambayo itakuwa ni
maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Dodoma na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, alipokuwa akifungua
Semina Elekezi kwa wakuu wa mikoa na wa
wilaya kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
Semina hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa
Hoteli ya St. Gasper, Pinda alisema mchakato
wa uundwaji wa katiba hiyo umeshaanza
ambapo wananchi wamepewa fursa ya
kutoa maoni yao.
Alisema matarajio ya serikali ni kuwa mpaka
ifikapo mwaka 2014 mchakato wa Katiba
mpya utakuwa umekamilika na Aprili 26
Katiba mpya itazinduliwa.
“Ni matarajio ya serikali kuwa Katiba mpya
itakuwa imekamilika na kuzinduliwa ifikapo
Aprili 26, 2014 katika maadhimisho
ya miaka 50 ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar,” alisema.
Pinda alisema kama mambo yote yatakwenda
kama yalivyopangwa, Muswada wa Sheria
kuhusu Mapitio ya Marekebisho ya Katiba
utawasilisha bungeni mwishoni mwa Mkutano
wa Nne wa Bunge unaoendelea hivi sasa.
Alisema iwapo muswada huo hautawasilishwa
katika mkutano wa nne basi utawasilishwa
mwanzoni mwa mkutano wa tano unaotarajiwa
kufanyika Oktoba mwaka huu.
Waziri Mkuu, aliwataka wakuu wa mikoa na
wa wilaya kutoa ushirikiano kwa Tume ya
Kuratibu na Kukusanya Maoni itakayoundwa
ili kuwezesha mikutano ya hadhara ya kukusanya
maoni kufanyika kama ilivyokusudiwa kwa
kuhamasisha wananchi kuhudhuria na kutoa
maoni yao.“Suala hili ni kubwa na la kitaifa,
ni vyema viongozi wasiingize siasa na
wajiepushe kuwashawishi wananchi katika
kutoa maoni yao, bali wawaache watoe maoni
kwa uhuru au pasipo shinikizo lolote,” alisema.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa hatua ya sasa si ya
kutunga Katiba Mpya bali ni kuunda Tume ya
Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi
kuelekea kutungwa kwa Katiba Mpya.
Mchakato huo wa kuelekea uundwaji wa
Katiba Mpya, umekwishaanza na katika
hatua ya awali, serikali imeandaa rasimu ya
Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Marekebisho
ya Katiba (The Constitutional Review Act)
ya mwaka 2011.
Hata hivyo mchakato huo ulipata upinzani
mkali kutoka kwa wadau mbalimbali
wakipinga vipengele kadhaa vilivyomo
kwenye muswada huo uliopelekwa bungeni
kwa hati ya dharura katika Mkutano wa Tatu
wa Bunge uliofanyika Aprili mwaka huu.
Miongoni mwa mambo yaliyolalamikiwa na
wadau ni kuwa muswada huo uliandikwa
kwa lugha ya Kiingereza ambayo ni watu
wachache wanaoizungumza na kuielewa.
Wadau walipinga pia vituo vya kutolea maoni
kuwa vitatu, ambavyo ni Zanzibar,
Dar es Salaam na Zanzibar.
Hata hivyo serikali ililazimika kuuondoa
muswada huo katika mkutano wa tatu wa
Bunge na kuahidi kuwa utaandikwa kwa
lugha ya Kiswahili na kuufanyia marekebisho
kulingana na maoni ya wadau
No comments:
Post a Comment