Monday, June 20, 2011

MAALIM SEIF SHARIFF HAMAD AKIWA OFISINI KWAKE AKIZUNGUMZA NA VIONGOZI WATENDAJI

 
MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka viongozi na watendaji wa Ofisi yake, kuwa waadilifu na kufanyakazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuleta ufanisi mahala pa kazi.
Maalim Seif ametoa changamoto hiyo leo, Ofisini kwake Migombani wakati alipokutana na Kamati ya uongozi ya Ofisi hiyo,iliojadili mapendekezo ya marekebisho ya sheria Nam 9 ya 2009, ya udhibiti wa madawa ya kulevya Zanzibar.
Amewataka viongozi na watendaji hao kuwa makini katika usimamizi wa majukumu yao, kuwa waadilifu kwa wanaowasimamia, pamoja na kutilia mkazo suala la nidhamu.
Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa viongozi hao kujiheshimu binafsi kabla ya wao kuheshimiwa na wanaowaongoza na kuwataka kusimamia vyema majukumu yao bila ya upendeleo, chuki au kumuonea mfanyakazi kwa kuamini kuwa wafanyakazi ni binaadamu kama watu wengine.
Alisema kuna ukweli kuwa nidhamu imeshuka katika maeneo ya kazi, hali inayotokana na usimamizi usioridhisha kutoka miongoni mwa viongozi na watendaji.
Maalim Seif alisema Serikali inalenga kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kuzingatia sifa, muda wa utumishi na utendaji wao wa kazi za kila siku.
Alisema lengo la utaratibu huo ni kuweka tofauti kati ya watumishi waliolitumikia Taifa kwa kipindi kirefu na wale wanaoanza kazi, sambamba na kuwapandisha vyeo wafanyakazi kutokana na utendaji wao uliotukuka.
Aidha aliwataka watendaji hao kujenga ushirikiano wa karibu kati ya taasisi moja na nyingine kwa kuzingatia kuwa mashirikiano ndio njia pekee katika kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, Dk. Omar Dadi Shajak alisoma madhumuhi ya waraka huo na kuainisha mapendekezo ya marekebisho katika baadhi ya vifungu vya sheria Nam 9 ya 2009 ya uratibu wa madawa ya kulevya Zanzibar.
Mapendekezo yaliojadiliwa na wajumbe hao yalikuwa ni juu ya matatizo yatokanayo na mapungufu ya sheria husika pamoja na matatizo yatokanayo ni usimamizi wa sheria (ya kiutawala).Hiki ni kikao cha kwanza cha Kamati ya Uongozi ya Ofisi hiyo, kinachopaswa kukaa kila baada ya miezi mitatu.

No comments:

Post a Comment