Kalamu ya Jabir Idrissa
WALA sishangai ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Zanzibar kufichua kitendo cha ofisa wa serikali kuidhinisha malipo ya Sh. 20 milioni kwa kazi iliyogharimu Sh. milioni mbili tu.Sishangai kwa sababu kabla ya kuingia serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) Novemba 2010, sikuwahi kusikia hata mara moja viongozi wakuu wa serikali iliyopita wakikemea ufisadi.
Twende kwa lugha nyingine. Ukweli, viongozi hawa walikana wizara au taasisi ya serikali ilipotuhumiwa kwa ufisadi. Alianza kiongozi mkuu.Amani Abeid Karume alipozungumza na waandishi wa habari kwenye sehemu ya viongozi mashuhuri (VIP) ya Uwanja wa Ndege wa Zanzibar mwaka 2006, alisema:
“Ndani ya serikali yenu ninayoiongoza, hakuna ufisadi (huo); labda ipo ‘rushwa ndogondogo tu… na hii tunaichukulia hatua.”Alikuwa amewasili nyumbani kutoka ziara ya nchi za Uarabuni na Ujerumani. Akijua fika namna gani alisimamia wizara ya fedha na uchumi ambayo kwa miaka yote kumi ya uongozi wake, aliishikilia.
Alijua viongozi wa chini yake, mawaziri na manaibu wao, walivyokuwa wakijihusisha na miradi ya kifisadi kwa kutumia madaraka aliyowapa.Akijua pia wazi namna wateule wake kadhaa wa chini ya mawaziri – makatibu wakuu, manaibu wao, wakurugenzi, makamishna na wakuu wa taasisi – walivyokuwa wakitumia vibaya ofisi za umma.
Wengi wao wakijihusisha na mipango ya kuhujumu fedha na mali za serikali. Mbele ya macho ya jamii, wakijitahidi kuonesha ni viongozi wema; bali nyuma ya pazia wakivuna kisicho chao.Lililokuwa muhimu zaidi kwao, ni kuchuma kwa ajili ya maslahi binafsi. Hawakuamini kamwe kiitwacho “maslahi ya watu” na “maslahi ya nchi.”
Ni wakati huu serikali ilinunua bidhaa na huduma kwa njia za rushwa; hakukuwa na utangazaji wa zabuni ili kuruhusu watu na taasisi binafsi kuomba. Maana yake hakukuwa na ushindani japo ni kinyume na hata sheria aliyoakisi mwenyewe rais itungwe.Sheria ya Manunuzi ya Umma ilikuwa ni miongoni mwa sheria za kwanza kutungwa na Baraza la Wawakilishi muda mfupi baada ya Karume kuingia madarakani kutokana na uchaguzi mchafu kihistoria wa Oktoba 2000.
Utungaji wa sheria hiyo ilikuwa ni utimizaji wa ahadi aliyoiweka wakati wa kampeni za uchaguzi. Nilikuwa uwanja wa Mzalendo, jimbo la Magomeni, Unguja, alipoahidi kumaliza alichoita “tatizo sugu la serikali kununua bidhaa au huduma kiholela.”Aliahidi kuweka utaratibu utakaoruhusu uwazi na ushindani katika eneo hilo.
Mambo yaligeuka hata mwaka haujesha. Kumbe alikuwa anaahidi pepo wakati hajajua raha ya kukalia kiti cha enzi pale jumba jeupe. Alipotangaza kusimamia wizara ya fedha, badala ya kumteua mtu muadilifu, alitoa fursa kwa watu kurudisha kumbukumbu nyuma. Walimfikiria baba yake.
Mzee Abeid Amani Karume alishikilia wadhifa huo. Kwa miaka mingi ya utawala wake wa miaka minane, alishikilia uwaziri wa fedha kama hatua ya kudhibiti fedha za serikali – fedha za wananchi.Alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuilinda hazina ya Zanzibar. Bali muda ulivyopita huku akitaka kuhifadhi madaraka, naye alijisahau.
Akaanza kutapanya. Ikaja njaa wakati anatekeleza sera zake za kujenga nyumba bora badala ya vibanda vya makuti na tope. Mengine yaliyotokea baadaye ni historia leo.Kitu kimoja tofauti: Angalau mzee alijenga nchi na jamii. Yapo mazuri leo wananchi wanayaona na kuyaenzi kama urithi alioucha. Hapana shaka aliipenda sana nchi.
Wakati Karume mdogo anazungumzia kutokuwepo kwa ufisadi katika serikali anayoongoza, serikali hiyo ilikuwa haijaleta majibu ya kueleweka kuhusiana na mtandao balaa wa kufisidi mamilioni ya shilingi za umma kupitia mpango wa kulipa mishahara kwa wafanyakazi hewa.
Wala siamini kuna wafanyakazi hewa. Kila mfanyakazi ni halali. Kilichopo ni mpango wa maofisa wakubwa wa serikali kudhulumu wananchi kwa kula fedha zinazotokana na kodi zao. Viongozi hao walibuni mpango wa kuibia wananchi.Karume, hadi anamaliza kipindi cha uongozi, hakuwahi kuamuru ofisi yake kutoa taarifa mpya ya mafanikio ya kudhibiti wizi wa mishahara tangu pale alipomkabidhi kazi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, Ramadhan Muombwa, ya kufuatilia tatizo hili.
Bila ya kutaja majina, nilifichua mtandao ule. Hakuna kilichofanywa maana umma haukuelezwa hatua zaidi ya kukamata maofisa wachache wadogo kama makarani wa fedha na maofisa utumishi.Serikali iliweka utaratibu mzuri wa kulipisha malipo yote kwenye ofisi moja pale Hazina. Lakini, kwa kuwa mafisadi hubadili mbinu, hiyo haikusaidia kudhibiti wizi; ilichochea ubunifu mpya wa mbinu za kuendelea kufisidi hazina.
Tangu wakati huo, viongozi hao wakiwemo mawaziri walipanga, kutekeleza na kunufaika na ufisadi.Walinunua gari kongwe kwa bei ya gari mpya; walinunua bidhaa na huduma kinyume cha sheria ya manunuzi na kanuni za fedha. Na cha kusikitisha, hata Ofisi ya Rais ilishiriki.
Kwa mfano, ilifunga mtandao wa kompyuta zenye intaneti kwa kupata huduma kwa kampuni ya kifamilia tena bila ya kutangazwa zabuni ili waombaji washindane.Ndiyo haya anayoyathibitisha CAG kupitia ripoti za ukaguzi za kila mwaka. Ushahidi gani tena tuupate?
Wafanyakazi wanalalamikia viongozi wao wanavyotumia vibaya madaraka na kujitajirisha. Kiongozi anakutwa na utajiri katika mwaka mmoja tu wa kuteuliwa kwake.
Anakutwa na gari nyingi zikiwemo zinazosubiri kuuzwa. Tayari amejenga nyumba mbili za thamani kubwa katika kipindi hicho. Baadhi yao waliwekeza mpaka Bara na nje ya jamhuri.
Uliza mashirika na taasisi za umma vituko vya wakubwa. Utajuta. Kwa mfano, mashine za maji, vipuri, mipira ya maji, nyaya za umeme na transfoma, vikinunuliwa kinyemela.
Ni nini kama si ufisadi waziri kushughulikia ununuaji vifaa hivi? Yuko wapi mtunza ghala au mhandisi? Hutashangaa kusikia mashine zilikutwa zimeshaharibika wakati zinafungwa.
Wakubwa walishirikiana na wamiliki wa hoteli za kitalii kugawa umeme kwa mikataba bandia. Hii ikafanikisha mamilioni ya shilingi kuibwa huku shirika likiporomoka.
Viongozi wakajimilikisha mali za serikali ikiwemo mitambo ya kujengea barabara iliyonunuliwa na serikali na mengine ambayo serikali iligaiwa na makampuni yaliyokamilisha ujenzi wa barabara.
Leo malalamiko yanaendelea kwani viongozi wengi wale wameendelezwa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein.Sasa lipo suala la umeme na mashine zilizofungwa dakika za mwisho kabla ya uchaguzi mkuu, linaigharimu serikali mpya. Nafuatilia suala hili ili niliweke wazi.
Ni hadi pale viongozi wakuu watakapoamini kuiba ni dhambi kwa wananchi na kwa mola wao, ndipo watashiriki kulinda mali za serikali kama walivyoahidi kwenye viapo.
Hili laweza kuchukua miaka kufikiwa, bali linaweza kufikiwa kesho tu wakiamua. Kufuta ufisadi lazima kuanze juu kuja chini.Ujumbe muhimu: Kiongozi akiibia serikali; akihujumu mali ya umma, wasaidizi wake watamuiga
No comments:
Post a Comment